Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 8/8 kur. 16-17
  • Mjue Tandala Mwenye Kuepa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mjue Tandala Mwenye Kuepa
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uchanga na Kuwa na Mipaka ya Eneo
  • Ithibati ya Ubuni Wenye Akili
  • Mwondoko wa Kushtua
  • Tandala Afanya Simba Waaibike
    Amkeni!—1993
  • Tandala Huyu Alikumbuka
    Amkeni!—1996
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1994
  • Kula Majani Katikati ya Miiba
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 8/8 kur. 16-17

Mjue Tandala Mwenye Kuepa

Na mleta-habari za Amkeni! katika Kenya

‘NINI chenye kuepa?” unauliza. Tandala mwenye kuepa! Paa mwenye kupendeza anayeishi katika hifadhi za kitaifa na za wanyama wa pori katika Afrika Mashariki. Na neno kuepa ndilo bora zaidi katika kueleza mnyama huyu mwenye haya sana. Ebu na twende kwenye hifadhi ya Kitaifa ya Tsavo katika Kenya na tuone kama tutaweza kumwona mmoja.

Ni asubuhi katikati tunapoingia sehemu ya magharibi ya hifadhi hiyo. Mlima Kilimanjaro, ulio mrefu zaidi katika Afrika, waamkua macho yetu. Kilele chao kitukufu chenye theluji ni mojapo mandhari tunazofurahia tunaposafiri kupitia sehemu hii ya kupendeza iliyo na mipaka. La, sasa hatutaona tandala wowote. Wao hula na kuzurura-zurura mapema sana asubuhi, jioni-jioni, au usiku. Wakati wa joto la mchana, wao hupumzika kwenye vichaka vilivyosongamana. Kwa hiyo ili tuwaone, inatubidi kuwa katika mahali panapofaa baada tu ya maawio au muda wa saa chache kabla ya machweo.

Giza linapoanza kuingia, tunapiga hema letu kwenye sehemu ya kambi iliyo juu ya jabali linaloelekea Mto Tsavo. Tunaamka mapema asubuhi, na baada ya kiamsha-kinywa kidogo, tunaondoka, tukiendesha gari polepole kwenye kijia kimoja. Tazama pale! Ni tandala wa kiume, amesimama bila kujongea.

Loo, jinsi mwangaza wa asubuhi unavyommulika kwa uzuri! Ni dume mwenye rangi nzuri ya kijivujivu na sura ya kuvutia. Mwili wake una mistari 13 au 14 myembamba myeupe, yenye kusimama wima. Alama nyeupe yenye kujikunja kama “V” inapamba koo lake, na mstari mweupe sehemu ya chini ya shingo yake. Mstari mweupe kati ya macho yake na sehemu nyeupe mdomoni mwake inaainisha uso wake mweusi. Upepo wa asubuhi wenye baridi unafanya viwimbi kwenye nywele fupi nyeupe zinazoteremka kutoka shingo yake, mabega, na mgongo. Kichwa chake kimevikwa kwa pembe mbili zilizopindika mara tatu na kuinuka juu kwa madaha na kuelekea nje.

Tandala tunayemtazama ni mmoja wa aina mbili zinazopatikana katika Afrika. Anajulikana kama tandala mdogo. ‘Binamu yake mkubwa,’ tandala mkubwa, huzoelea kaskazini mwa Kenya na ni mara chache huonekana Tsavo. Zaidi ya kuwa mkubwa zaidi, tandala mkubwa anaweza kutofautishwa kwa kidevu chake kizito cha rangi ya kahawia na nyeupe ambacho huenea mpaka kwenye kifua chake kwa ukingo wenye kuvutia shingoni. Pembe zake ni nene zaidi, na masikio yake ni makubwa zaidi kwa kuwiana. Yeye hawi kamwe na mistari myeupe zaidi ya minane mwilini mwake.

Uchanga na Kuwa na Mipaka ya Eneo

Mtoto wa tandala anapozaliwa, mama yake anamramba kuwa safi mara hiyo ili asiwe na harufu ambayo kwayo adui watamtambua. Halafu, wakati mama aendapo kujilisha, yule paa mchanga atakaa pale pale kwa utii, akijilaza bila kelele mahali ambapo mama yake alimweka. Mama yake atamwosha mwana wake kwa ukawaida kwa mwosho wa “kurambwa” ili kuondoa harufu mbaya na hivyo amlinde na maadui. Lakini karibu na siku ya kumi hivi, mtoto wake aanzapo kutafuna mimea, harufu ya mwili inaanza kutokeza. Kwa kuwa ulinzi wake maalumu wa kutovumbuliwa umetoweka, kuanzia wakati huo na kuendelea, anaandamana na mama yake kila mahali.

Tabia moja ya tandala iliyo wazi ni ile ya kuimarisha mipaka ya eneo. Tabia hiyo ni ya madume wa jamii hiyo kuchagua na kulinda sehemu hususa ya ardhi. Katika kudai sehemu fulani, yule dume huweka alama mipaka yake kwa kuweka kinyesi chake juu ya nyasi na vichaka. Halafu analinda sehemu yake kwa kufukuza dume yeyote anayejipenyeza kupitia mipaka hii iliyotiwa harufu. Namna gani wapenyezaji wa kike? Wao si wapenyezaji! Wao ni wageni wanaokaribishwa kukaa. Kwa hakika, huenda wakakazwa kufanya hivyo!

Ithibati ya Ubuni Wenye Akili

Tabia hii ya kisilika ya kuweka alama ya mipaka ya eneo huweka vikundi vya tandala vikiwa vimetawanyika na huwa ulinzi dhidi ya kulisha kupita kiasi katika mahali pamoja. Hivyo, tandala wanaolisha wana uhakika wa kuwa na wingi wa vichaka vyenye majani ambayo huwa wanapenda. Lakini hutukia nini wakati ukame utokeapo?

Mhifadhi Daphne Sheldrick aeleza katika gazeti Swara la Sosaiti ya Wanyama wa Pori Afrika Mashariki: “Hata hivyo, wakati hali ni ngumu na chakula na maji ni haba, Asili hutokeza hatua tofauti kabisa ambayo huwa ni kinyume kabisa na ile ya kuwa na mipaka . . . , na hiyo ni Mhamo. Kuwa na mipaka huelekea kuwa na mtengano na utayari wa kupigana na kuzaa; kuhamahama huzuia mambo haya mawili ya asili kwa jinsi uhitaji wa kuwa pamoja zaidi unavyoongezeka. Kuokoka kunakuwa ndilo jambo la maana la kushughulikiwa na wote, na hivyo tandala wa kiume na wa kike wanakuja pamoja . . . katika changamano la amani. Halafu, siku moja, kana kwamba kwa Amri ya Kimungu, wataondoka sehemu hiyo wote kwa ujumla na ondoko la kawaida linatukia.” Ndiyo, wanashika njia, kutafuta sehemu mpya za malisho ambapo majani ni mengi!

Je, nguvu fulani isiyo na akili na isiyoongozwa iitwayo Asili ingeweza kufanya na kuendeleza miendo hiyo miwili inayotofautiana hivyo? Bila shaka, ni Mfanyizi Mkuu mwenye akili tu ambaye angeweza kupangilia programu hii iliyotatanika ya kuwa na tabia ya silika ndani ya tandala.

Mwondoko wa Kushtua

Sasa, je, wewe hufurahi kwamba udadisi wako kuhusu tandala ulikufanya ukaja nasi? Tunapomtazama pale, akitafuna majani kwa bidii, haonekani mwenye kuepa hata kidogo! Lakini ametuona! Kwa ghafula, mianzi ya pua yake na masikio yake makubwa yanatetema. Kwa mbweko wa kukohoa, anaruka vichakani na kukimbia. Tunapotusha pumzi, tunashtuliwa tena! Kutoka mahali pasipotazamiwa, jike mwenye rangi ya hudhurungi-nyeupe yenye kijivu aruka kumfuata. Wakati huo wote, alikuwa amesimama katika kichaka kilichoko karibu! Rangi yake na kutojongea kwake kuliificha sura yake asionekane kabisa.

Hivi ndivyo tandala mwenye amani huokoka katika pori za Afrika. Ulinzi wake ni ule uwezo wa silika wa kusimama bila kujongea na kulandana na mazingira yake. Si ajabu kwamba tandala ni mwenye kuepa sana! Uhai wake wategemea hilo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki