Tandala Afanya Simba Waaibike
MWAKA jana katika Afrika Kusini, swala mkubwa—tandala dume—alichukua kikao chake mbele ya hoteli ya hifadhi ya wanyama ya Lowveld yenye starehe. Sura yake ilikuwa chonjo na iliyo tayari kwa vita, kwa hiyo si ajabu kwamba tandala mwenyeji alihisi chuki kwa ajili ya uvamizi huo wa uchokozi wa eneo lake. Mtu aliyejionea aliripoti juu ya ushambulizi wa kiongozi huyo wa tandala: “Aliguna, akapiga chini kwa miguu na kuchukua kikao cha mashambulizi. Huku pembe zake zikiwa chini, yeye alishambulia. Alipompiga yule tandala mwingine, alipata mshtuko mkubwa.” Yule mvamizi hakusogea. Yule tandala wa kiume mwenyeji alishambulia tena. Akaambulia patupu. Katika kasirani yenye mfadhaiko na wingu la vumbi, kiongozi mwenyeji “alivunja miti yote iliyo karibu kabla ya kuondoka kwenda zake.” Yeye hajarudi, yaonekana akikata kauli kwamba mgeni huyo hawezi kushindwa.
Wafalme wa mwitu (simba) hawakufua dafu pia. Askari-mlinzi Carlson Mathebula aliripoti kwamba simba 12 walimzunguka yule tandala. Alisema hivi juu ya mashambulio yao: “Ghafula simba wawili jike walianza kumnyemelea. Kwa mgurumo mkubwa mmoja wao aliruka kwenye mgongo wa yule tandala hali yule mwingine alikimbia kwenye upande wake na kurukia shingo lake. . . . Wote wawili walianguka chini kwa woga na kulala hapo bila kusogea. Simba mwingine jike alijiunga katika windo hilo. Yeye alikimbia hadi mahali alipokuwa tandala na kwa kumbo kubwa la miguu, akajaribu kumwangusha chini, lakini yeye aliendelea kusimama tu.” Wale simba 12 walighadhabishwa sana na kule kushindwa kwao kumtwaa yule tandala hivi kwamba “waliharibu kipima-mvua, kinyunyiza-bustani-maji na fanicha za kuwekwa nje kabla ya kuondoka kisirisiri kwa aibu.”
Kwa kusimama tuli kabisa, tandala huyo alikuwa ameshinda kikundi cha tandala wenyeji kutoka kwa eneo lao na kufanya kikundi cha simba kitoroke. Ripoti hiyo katika Sunday Times la Johannesburg, Afrika Kusini, ilisema juu ya tandala huyu kuwa swala wa kipekee mwenye uzito wa kilogramu 300 na aliyefanyizwa kwa shaba nyeusi. Bw. Keith Calder, aliyekalibu tandala huyo kwa shaba nyeusi, alisema: “Ni sifa kwangu kwamba wale simba na tandala walimwona kuwa halisi sana.”