Harara ya Michezo ya Bahati Nasibu Kamari ya Ulimwengu
“KILE tu unachohitaji ni dola moja na ndoto.” Ndoto yenyewe ilikuwa ni kushinda zawadi yenye thamani ya juu kabisa ya bahati nasibu ya dola milioni 45 katika New York. Dola moja ilimwezesha mtu apate jaribio la kushinda. Mamilioni ya waota ndoto walikuja. Wakisimama katika foleni (msururu) kununua tikiti zao, walizungumza juu ya vyombo vya anasa vya kutembelea baharini na makoti ya ngozi ya wanyama wa baharini na majumba—vitu ambavyo wangenunua kama wangeshinda fedha ya tuzo. Katika kipindi kimoja, kotekote katika jimbo, walitokeza tikiti kwa kadiri ya 28,000 kwa dakika moja. Katika siku tatu za mwisho kabla ya kupiga kura, walinunua tikiti milioni 37.4.
Katika Japani huwa kuna biashara nzuri siku zote katika vibanda 10,000 vilivyoidhinishwa vya bahati nasibu ambapo watu humiminika kununua tikiti kwa ajili ya Takarakuji (bahati nasibu) iliyo Kubwa Zaidi ya Mwisho wa Mwaka. Katika kibanda kimoja cha Tokyo ambapo iliripotiwa kwamba tikiti tano zenye kushinda zawadi ya kwanza zilikuwa zimeuzwa katika miaka ya majuzi, watu 300 hivi walikuwa tayari wamesimama katika foleni wakati kibanda hicho kilipofunguliwa kwa shughuli. Mwanamke mmoja mchanga, ambaye aliamini kwamba bahati hupendelea wenye kufika mapema, alikuwa akingoja tangu saa 7 za usiku. Zawadi kuu yenye kutamaniwa ya mwaka jana: rekodi ya yen milioni 100 (dola 714,285 za U.S.)
Katika mji mmoja mkuu wa Afrika Magharibi, pale panapoitwa na wenyeji sehemu ya Lotto Koleji huwa mara zote pamejawa na watu ambao wamekuja kununua tikiti na kubahatisha juu ya nambari zitakazofuata. Orodha ndefu za nambari zilizoshinda wakati uliopita zinauzwa kwa wale wanaotumainia kupata kwazo kidalili cha mchanganyiko wa nambari za wakati ujao. Kwa wale wenye imani katika maarifa ya mafumbo, wanabii wa lotto wako tayari kuwatabiria namba watakazobahatisha, kwa mtozo wa pesa.
Matukio ya kipekee? La, hasha. Harara ya michezo ya bahati nasibu ni yenye mweneo mkubwa. Inapatikana katika kila bara. Inapatikana katika nchi tajiri na maskini. Inasisimua wachanga na wazee pia katika kila daraja ya jamii iwe ni kiuchumi, kijamii, au kielimu.
Naam, michezo ya bahati nasibu ni biashara kubwa, na biashara hiyo inapata usitawi mwingi. Katika United States pekee, michezo ya bahati nasibu ya kiserikali ilichukua dola elfu milioni 18.5 katika 1989. Miaka 27 tu iliyopita, hesabu hiyo ilikuwa sufuri. Lakini sasa michezo ya bahati nasibu ndiyo namna ya pili kwa ukubwa ya kamari katika United States, na biashara hiyo inakua kwa asilimia 17.5 kila mwaka, kwa uharaka kama ule wa biashara ya kompyuta.
Kulingana na tarakimu za hivi karibuni zaidi zinazopatikana katika gazeti Gaming and Wagering Business, uuzaji wa tikiti za bahati nasibu ulimwenguni katika 1988, zilijumlika kuwa dola elfu milioni 56.38, idadi kubwa kweli kweli. Hiyo inajumlika kuwa zaidi ya dola kumi kwa kila mwanamume, mwanamke, na mtoto duniani! Hilo likiwa katika mwaka mmoja tu!
Hali hakuna anayeweza kukana kwamba michezo ya bahati nasibu inasitawi, wengi hutoa hoja kwa nguvu dhidi yayo. Makala mbili zinazofuata zinachunguza upendezi unaozidi kukua wa michezo ya bahati nasibu na ubishi ulioko kuihusu. Unapofikiria juu ya mambo ya hakika, utaweza kuamua kama michezo hiyo ya bahati nasibu inakufaa. Ni jambo la akili kuicheza? Ni rahisi jinsi gani kushinda? Je, waweza kupoteza zaidi ya pesa?