Michezo ya Bahati Nasibu kwa Nini Inapendwa na Wengi?
KWA nini watu wengi hucheza mchezo wa bahati nasibu? “Unapendeza, unafurahisha,” akasema mwanamke mmoja aliye mwakilishi wa baraza la michezo ya bahati nasibu. Labda ndivyo, lakini kivutio halisi kwa kweli ni pesa za tuzo. Karibu kila mtu angeweza kutumia pesa za ziada. Nayo michezo ya bahati nasibu hutoa tumaini la rundo la pesa. Katika ulimwengu wa leo usio yakini wenye bei zinazopanda, soko la hisa zenye kuanguka, na kazi zenye kufikia mwisho, mamilioni ya watu wanaamini kwamba kushinda bahati nasibu ndiyo njia pekee inayoweza kuwaziwa ya wao kuja kuwa matajiri sana.
Likiongezea uvutio, bahati nasibu huwa haitatanishi na ni rahisi kucheza. Kuna unamna-namna mwingi, kama vile Lotto, nambari, na michezo ambapo unasugua karatasi kufunua namba zilizofichwa, lakini michezo yote hiyo ina sehemu mbili zinazotumika kwazo. La kwanza ni kwamba wachezaji hushinda wakati nambari zilizo katika tikiti zao zinapofanana na zile zenye kupigiwa kura na watengenezaji. La pili, tofauti na namna nyingine za kamari, ufundi wa kipekee au maarifa hayahitajiki ili kushinda. Kushinda au kupoteza ni jambo la kujaribia tu.
Watu pia hucheza bahati nasibu kwa sababu ni rahisi kununua tikiti. Waamerika wengi huzinunua katika maduka ya kwao. Kwingineko, ikiwa kibanda cha bahati nasibu hakipo karibu, wachezaji wanaweza kubahatisha kupitia kwa barua, simu, teleksi, au faksi.
Ni Jambo Gani Jipya Kuhusu Bahati Nasibu?
Je, michezo ya bahati nasibu ni jambo jipya? La, hasha. Kwenye sherehe za Rumi ya kale, maliki Nero na Augusto walipeana watumwa na mali kama zawadi. Moja ya zawadi ya kwanza ya pesa iliyorekodiwa labda ililipwa katika mwaka 1530 kwa bahati nasibu katika Florence, Italia. Katika karne zilizofuata, bahati nasibu ilisitawi katika Ulaya. Bahati nasibu ilifanikiwa katika Amerika ya mapema pia, ikileta pesa ambazo zilisaidia kulipia gharama ya Jamestown, Jeshi la Bara, na ujenzi wa vyuo vikuu vyenye sifa, kama vile Harvard, Dartmouth, Yale, na Columbia.
Hata hivyo, katika karne ya 19, biashara hiyo iliingia matatani. Wapingamizi walilalamika dhidi ya kamari ya watu wengi na wakashtaki kwamba kura zilifanyiwa ulaghai. Bahati nasibu ilijawa na hongo, ufisadi, na uhalifu ndani yake. Wafanyizaji wa kibinafsi walipata faida kubwa. Kama tokeo, michezo ya bahati nasibu katika United States, Ufaransa, na Uingereza ilipigwa marufuku.
Mwisho wa hadithi? Bila shaka sivyo. Michezo ya bahati nasibu ilikuwa imeendelea kusitawi kwingineko—kwa mfano, Italia na Australia. Carlos wa 3 wa Hispania alianzisha michezo ya bahati nasibu katika 1763; namna yake ya ki-siku-hizi ikianzishwa kisheria katika 1812. Nchi baada ya nchi zilifuata mkondo huo. Katika 1933, Ufaransa iliondoa marufuku na kuanzisha Loterie nationale. Pia katika miaka ya 1930, Ailandi ilianzisha michezo ya bahati nasibu yenye kufana sana ijulikanayo kama Irish Hospitals’ Sweepstake. Ile ya Japan Takarakuji ilianzishwa katika 1945. Uingereza ilikubali mashindano ya fedha za watu wengi katika mpira wa miguu na kura za dhamana ya pesa zinazolipwa kimbele, bahati na sibu hasa ikiwa si kwa jina. Katika 1964, United States ilianzisha tena biashara hiyo.
Halafu katika miaka ya 1970, mavuvumko mawili yalibadilisha njia ya kuendesha michezo ya bahati nasibu. La kwanza lilikuwa ni kuanzishwa kwa kompyuta zilizounganishwa na vituo vidogo vidogo vya biashara. Sasa ingewezekana kupanga michezo yenye sauti kubwa, na yenye marudio ya juu ambapo wachezaji wangeweza kuchagua nambari zao wenyewe. Haingehitajika tena kungoja kwa majuma au miezi kuona kama wameshinda; wachezaji wangejua matokeo kwa muda wa masiku, masaa, au hata madakika.
Vuvumko la pili lilikuwa ni kuanzishwa kwa Lotto, mchezo ambao nafasi za kushinda ni duni. Katika Lotto, wakati pesa za tuzo hazishindwi, zinawekwa kwenye michezo itakayofuata. Baada ya wakati, zawadi ya pesa yaweza kukua iwe mamilioni ya dola. Kwa mchezo wa Lotto, uuzaji ulipanda, na biashara ikawa kubwa, kubwa kweli kweli.
Uvutio kwa Wafanyizaji
Kwa nini serikali hufanyiza michezo ya kamari? Kwa sababu ni njia rahisi ya kupata pesa bila kupandisha kodi. Hali mashine za kutumbukizia pesa na mchezo wa kamari wa kizungushi duara hurudisha pesa kama zawadi kwa kadiri ya asilimia 95 ya kiasi kile zinazochukua, michezo ya bahati nasibu hulipa kiasi kilicho chini ya asilimia 50. Kwa mfano, katika United States katika 1988, senti 48 hivi kwa kila dola ya bahati nasibu ililipwa kama zawadi na senti 15 zilitumika katika kufanyiza michezo, uuzaji, na usimamizi. Senti 37 zinazobakia zilitumiwa katika kulipia maendeleo ya umma, elimu, utunzaji wa afya, na msaada kwa wazee-wazee. Kwa taifa lote, hilo lilijumlika kuwa dola elfu milioni 7.2.
Lakini serikali huwa hazipangi michezo ya bahati nasibu ili tu kufanyiza pesa. Ikiwa hazijiingizi katika biashara hiyo, zaweza kupoteza pesa. Raia zao wanaweza kucheza kwingineko. Hivyo basi nchi moja ianzishapo bahati nasibu, jirani zake huja chini ya mkazo wa kufanya vivyo hivyo. Tokeo hili lenye kuambukiza liko wazi katika United States. Katika 1964 kulikuwako na mchezo mmoja tu wa Kiserikali wa bahati nasibu; katika 1989 kulikuwako na 30.
Ndoto za Utajiri
Bila shaka, kuna watu wengi sana wanaojaribu kupata kipande cha dola ya ununuzi. Kwa hiyo wafanyizaji wa michezo husadikishaje umma watumie fedha zao katika michezo ya bahati nasibu? Utangazaji! Wanatumia mafundi hasa wa utangazaji!
Je, matangazo hukazia kwamba sehemu (ingawa ni ndogo) ya mapato itasaidia kugharimia elimu au iandae utunzaji kwa ajili ya wazee-wazee? Hasha! Hilo huwa halitajwi mara nyingi. Badala yake, matangazo hukazia juu ya furaha nyingi ambayo hupatikana kutokana na kushinda mamilioni ya dola. Hapa pana mifano kadhaa:
◻“Mtindo-maisha Ulio wa Ajabu wa Walio Matajiri na Wenye Umaarufu Waweza Kuwa Wako Papo kwa Hapo. . . Unapocheza Mchezo Wenye Utukuzo wa Kanada, LOTTO 6/49 wa Mamilioni ya Dola.”
◻“BAHATI NASIBU YA FLORIDA. . . Kuwa Tajiri katika Bahati Nasibu Iliyo Kubwa Zaidi Amerika.”
◻“Pesa Zafanyiziwa Ujerumani—PATA UTAJIRI uwe milionea mara moja.”
Uuzaji wa bidii? Ndivyo ilivyo! Jitihada za kupunguza utangazaji kwa kawaida hupunguka tikiti zinapokosa kununuliwa. Kwa hakika, wafanyizaji hugeukia michezo mikubwa zaidi na uuzaji mkubwa zaidi ili kushawishi wachezaji wapya na kuendeleza wale wa zamani wakiwa wamependezwa bado. Inawabidi wafanyizaji kutoa mara kwa mara jambo lionekanalo kuwa jipya. Mkurugenzi wa michezo ya bahati nasibu ya Oregon James Davey alisema: “Tunazo hoja za kamari, huwa tunafanya Olimpiki. Wakati wa Krismasi huwa tunafanya Pesa za Sikukuu. Kwa Nyota za Bahati huwa tunacheza na ishara za watu za unajimu. Tunapata kwamba ukiendesha michezo miwili au mitatu, minne au mitano kwa wakati ule ule mmoja, utauza tikiti zaidi.”
Lakini chenye kuvutia zaidi ya yote ni pesa za tuzo zilizo nyingi ajabu. Katika Lotto, pesa za zawadi zinapopanda sana, kama zilivyofanya zilipofika dola milioni 115 katika Pennsylvania katika 1989, hufanyiza habari za maana. Watu hung’ang’ania kununua tikiti katika kile mwandikaji mmoja alichokiita “ulaji wenye kichaa wa mcheza kamari.” Kati ya mchocheo huo, hata wale ambao kwa kawaida hawachezi bahati nasibu hutoa pesa zao.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Harara ya Kamari na Dini
“Kanisa la Katoliki limenifundisha kucheza kamari. Mchezo wa kamari wa kutumia kadi (bingo) na wa kupigia pesa kura si tofauti hata kidogo na bahati nasibu. Kama Kanisa la Katoliki lingechukua mwongozo na kuacha kamari ya aina yote, basi ningefikiria tena wazo la kutokucheza bahati nasibu. Ikiwa mimi ni mwenye pupa, ni kwa sababu hilo ni karibu kuwa sakramenti Kanisani.”—Msomaji kwa gazeti la U.S. Catholic.
“Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Notre Dame, kuhusu parishi (parokia) za Katoliki, baada ya Misa ya Jumapili, mwadhimisho wa pili unaohudhuriwa na wengi katika makanisa ya Katoliki ni michezo ya kila juma ya kamari kwa kutumia kadi (bingo).” Hata hivyo, mapadri kadhaa wanadai kwamba wengi wa wale wanaohudhuria michezo hiyo ya kamari huwa hawaendi kanisani.—The Sunday Star-Ledger, New Jersey, U.S.A.
“Mtakatifu Pancras Alileta Bahati Madridi” ndicho kilikuwa kichwa kikuu cha gazeti la kila juma la Kihispania ABC, toleo la kimataifa. Makala hiyo iliendelea hivi: “‘Ilikuwa ni Mtakatifu Pancras’ wakasema tena na tena wafanyakazi wawili wa duka la michezo ya bahati nasibu. . . mahali walipokuwa wameuza tikiti mwendelezo pekee ya 21515, iitwayo ‘gordo’ [kubwa] yenye thamani ya milioni 250 [peseta, au leo, dola 2,500,000, za U.S.], ambayo ilikuwa imeenezwa katika Madridi. [Wafanyakazi hao] waliungama kwamba walikuwa wametoa sala kwa mtakatifu huyo, ambaye sanamu yake waliokuwa wameiwekelea kitawi cha mboga ya kizungu ilikuwa juu ya kibanda chao, ili kupata bahati njema ya kuuza ‘gordo’ ya Krismasi.”
“Wakijaribu kufikiri njia za kueleza bahati yao njema, washindi wa zamani walielekea kuamini kwamba Mungu pamoja na ajali aliwachagua wao kushinda pesa hizo. . ..‘Sisi tunataka kuamini kwamba bahati njema na bahati mbaya huwa kwa sababu ya kitu fulani, si ajali,’ akasema Dakt. Jack A. Kapchan, profesa wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Miami. ‘Na ni kitu gani kingine kipo cha kuileta isipokuwa Mungu?’”—The New York Times.
Biblia inasema nini kuhusu bahati njema? Kwa wasio waaminifu katika Israeli, Yehova alisema: “Lakini ninyi watu ndinyi wale wanaomwacha Yehova, wale wanaosahau mlima wangu mtakatifu, wale wanaoandaa meza kwa ajili ya mungu wa Bahati Njema na wale wanaojaza sana divai iliyochanganyika kwa ajili ya mungu wa Ajali.”—Isaya 65:11, NW.
Ni wangapi wa washindi hao wachache wanaotulia na kufikiria kwamba bahati njema yao iliyo ya peke yake imepatikana kukiwa na mamilioni ya wapotezaji wenye bahati mbaya? Je, kamari inaonyesha ‘upendo wa jirani’ kwa njia yoyote? Je, ni jambo la akili au la Kibiblia kufikiri kwamba Bwana mwenye Enzi kuu aweza kujiingiza mwenyewe katika mambo ya kichoyo kama kamari?—Mathayo 22:39.