Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 11/8 kur. 7-9
  • Michezo ya Bahati Nasibu— Nani Hushinda? Nani Hupoteza?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Michezo ya Bahati Nasibu— Nani Hushinda? Nani Hupoteza?
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matokeo kwa Maskini
  • Swala la Thamani
  • Michezo ya Bahati Nasibu kwa Nini Inapendwa na Wengi?
    Amkeni!—1991
  • Harara ya Michezo ya Bahati Nasibu Kamari ya Ulimwengu
    Amkeni!—1991
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • Muono-Ndani Juu ya Habari
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 11/8 kur. 7-9

Michezo ya Bahati Nasibu— Nani Hushinda? Nani Hupoteza?

HOJA ya msingi inayounga mkono michezo ya bahati nasibu inayofanyizwa na serikali ni kwamba huwa inailetea serikali mamilioni ya dola, pesa ambazo zaweza tu labda kupatikana kwa kupandisha kodi. ‘Na jinsi ilivyo rahisi!’ wasema wategemezaji. Ni kama kodi ambayo hakuna anayetakiwa kuilipa; ni ya hiari. Kwa kweli, watu wanatamani kulipa; wanangoja katika foleni waweze kulipa!

Lakini baadhi ya mashtaka dhidi ya michezo ya bahati nasibu ni yapi?

Moja ni kwamba matangazo ya michezo ya bahati nasibu mara nyingi huwa hayatoi habari ya kutosha au ni yenye madanganyo matupu. Hayo huendeleza wazo la kwamba wewe utashinda. Mfano mmoja ni tangazo la bahati nasibu ya Kanada linalosema: “Tunaifanya iwe rahisi. . .KUSHINDA!!”

Lakini kushinda ni rahisi jinsi gani? Alie hucheza michezo ya bahati nasibu ya Ujerumani Magharibi. Tangazo hufoka: “Nafasi zako za kushinda ni nyingi ajabu.” Lakini, Alie anasikitika: “Nimecheza bahati nasibu kwa miaka kumi, na sijawahi kushinda kitu. Tena sijui mtu mwingine yeyote ambaye ameshinda kitu chochote.”

Kwa kila ashindaye zawadi kubwa, kuna mamilioni wanaopoteza kama Alie, ambao hutoa pesa zao juma baada ya juma, mwaka baada ya mwaka, lakini hawapati kitu. Katika United States, wale wanaoshinda dola milioni 1 ni asilimia 0.000008 ya wacheza kamari milioni 97 huko.

Uwezekano wa kupata nafasi ya kushinda zawadi iliyo kubwa kabisa si mmoja katika milioni moja tu (kwa kukadiria, hii ni kama uwezekano wa mtu kupigwa na radi); waweza kuwa mmoja katika milioni nyingi. Kwa mfano, ilipokuwa wazi kwamba pesa za tuzo zilipokuwa nyingi zaidi, ndivyo tikiti nyingi zaidi zilivyouzwa, uwezekano wa kushinda mchezo wa Lotto wa New York ukashuka kutoka mmoja katika milioni 6 hadi mmoja katika milioni 12.9!

Haishangazi kwamba watu hushtaki michezo ya bahati nasibu kwa kuwasisimua wanunuzi isivyofaa ambao huwa hawana hadhari na hawang’amui juu ya uwezekano mdogo sana ambao wanao wa kushinda. Dakt. Valerie Lorenz, mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Kamari ya Kipatholojia cha U.S., asema kwa urahisi: “Michezo ya bahati nasibu? Ndiyo michezo yenye kunyonya zaidi iliyopo. Nafasi za kushinda ziko ndogo sana.”

Vipi iwapo unashinda dola milioni moja? Hutazipata zote. Baada ya mtoza kodi kuchukua sehemu yake, washindi katika United States hupokea dola 35,000 kila mwaka kwa miaka 20. Hizo ni dola 700,000, zinazopunguzwa zaidi katika thamani na infleshoni kwa muda wa miaka hiyo 20.

Matokeo kwa Maskini

Uchambuzi mwingine ni kwamba wale wanaotumia pesa nyingi zaidi ni watu maskini, wale wasioweza kuzipata. Wafanyizaji wa michezo ya bahati nasibu hubisha kwamba hili si kweli, kwamba uchunguzi umeonyesha kuwa michezo ya bahati nasibu inapendwa na wengi walio na mapato ya kati. Wao wanasema michezo ya bahati nasibu ni ya hiari, na hakuna anayelazimishwa kucheza. Hata hivyo, matangazo huwasha tamaa za wachezaji kwa makusudi, na wengi ni watu maskini. Muuzaji mmoja auzaye katika mahali pa kufaa katika Florida asema hivi: “Tuna kikundi hususa cha watu ambao sisi huona kila juma. Wengine hununua tikiti 10 kila siku. Wengine hununua 100 kila juma. Wao hawana pesa za kununua chakula, lakini wanacheza ‘Lotto.’”

Katika nchi fulani zinazositawi, mara nyingi hali huwa mbaya hata zaidi. Hivi karibuni serikali ya Indonesia ilichunguza tena mchezo wa bahati nasibu wa mpira wa miguu uitwao Porka wakati waeneza habari waliporipoti kwamba vijiji vizima vizima vilikuwa vimepata “kichaa cha Porka.” Gazeti Asiaweek liliripoti: “Magazeti ya [Indonesia] yalijawa na habari za kuogofya: wanaume wakiwapiga wake zao au watoto; watoto wakiiba pesa kutoka kwa wazazi wao; watoto wakitumia pesa zenye kupatikana kwa shida zilizowekwa kando kuwa za karo ya shule—yote hayo kwa ajili ya Porka.”

Kwa sababu ya ongezeko kubwa la michezo ya bahati nasibu ulimwenguni pote, watu wengi zaidi na zaidi wanapata kuifahamu kamari. Wengine, sio maskini peke yao, wanakuwa wacheza kamari wa kawaida—wazoevu wa michezo ya bahati nasibu. Arnie Wexler huongoza Baraza la Uchezaji Kawaida wa Kamari katika New Jersey, U.S.A. Yeye asema: “Wafanyizaji sheria wanafikiri kwamba wamepata njia isiyoumiza, na iliyo rahisi ya kukusanya pesa, wakati, hasa, wanaharibu familia nyingi, na biashara nyingi, na wanadamu wengi, na uhai mwingi.”

Swala la Thamani

Jambo jingine la kufikiriwa lililo la maana ni kwamba michezo ya bahati nasibu inayoongozwa na serikali imebadilisha mtazamo wa watu kuelekea kamari. Michezo ya leo ya bahati nasibu ya “Cheza 3” au “Nambari za Bahati” zenye kuongozwa na serikali hutoa nafasi moja ya kushinda kwa kila elfu moja lakini hurudisha tu asilimia 50 hivi kwa pesa za zawadi. Kabla ya serikali kuingia katika biashara hiyo, mchezo huo ulikuwa “mwovu,” biashara haramu, upotovu. Sasa mchezo huo huo unaitwa kitumbuizo, raha, daraka la raia!

Bila shaka, tofauti ya maana kati ya mchezo wa nambari usio halali na bahati nasibu ya kiserikali ni kwamba badala ya faida kwenda kwenye mifuko ya wahalifu, faida hiyo hutegemeza miradi ya kiserikali. Hata hivyo, wachunguzi wengi wana wasiwasi juu ya tokeo la michezo ya bahati nasibu kwa thamani za kiadili za jamii ambayo zapasa kufaidi.

Hii ni kwa sababu michezo ya bahati nasibu huongezea tumaini na mbetuko wa kuwa tajiri bila jitihada. Paul Dworin, mhariri wa Gaming and Wagering Business, alisema: “Nyakati zilizopita, serikali imesema kwamba ukifanya kazi kwa bidii, utafanikiwa. Sasa, imekuwa ‘Nunua tikiti na utakuwa milionea.’ Huo ni ujumbe mgeni wa kupelekwa na serikali.” Na George Will aliandika katika Newsweek: “Watu waaminipo kwa kadiri kubwa juu ya umaana wa bahati, ajali, nasibu, mwisho ulioamriwa na Mungu, ndivyo waaminivyo kwa kadiri ndogo juu ya umaana wa mambo mema kama bidii, uwekevu, utoshelezo, juhudi, wenye bidii ya kujifunza.”

Jambo jingine, linalohusu jamii ya kibinadamu hasa, ni hili: Watu mmoja mmoja hawapaswi kupata faida kutokana na misiba ya wengine. Hata hivyo, wafanyizaji wa michezo ya bahati nasibu, huendeleza maoni ya kwamba ni haki kwa mtu mmoja mmoja kupata faida na raha kutokana na hasara ya wengine. Fikira kama hiyo ni ya kichoyo; inadharau shauri la Biblia: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”—Mathayo 22:39.

Kujapokuwako na sauti nyingi za kupinga, michezo ya bahati nasibu yaendelea kuongezeka kwa njia yenye kutokeza ulimwenguni pote. Mgeni mmoja aliyetembelea Afrika Magharibi aliona mamia ya watu wamekusanyika kuzunguka jengo moja la Serikali la bahati nasibu. “Kwa nini watu hawa wote wanaponda pesa zao kwa bahati nasibu,” yeye akauliza mwenyeji mmoja, akionelea, “na hasa wao ni watu maskini?”

“Rafiki yangu, wao hucheza bahati nasibu kwa sababu hiyo huwapatia tumaini,” mwenyeji huyo akajibu. “Kwa wengi wao, hiyo ndio tumaini pekee ambayo wanayo maishani.”

Lakini je, kushinda katika bahati nasibu ni tumaini kweli? Sana sana hiyo huwa ni mawazo yenye makosa, mazigazi, ndoto isiyowezekana. Kwa kweli, Mkristo mwenye kudhamiria hatapoteza wakati na mali yake katika kufuatilia utajiri wa kamari ulio ubatili. Ni vema zaidi jinsi gani kufuata shauri la mtume Paulo, aliyeandika kwamba watu wenye hekima ‘hawautumainii utajiri usio yakini, bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha.’—1 Timotheo 6:17.

[Blabu katika ukurasa wa 8]

“Wafanyizaji sheria wanafikiri kwamba wamepata njia isiyoumiza, na iliyo rahisi ya kukusanya pesa, wakati, hasa, wanaharibu familia nyingi, na biashara nyingi, na wanadamu wengi, na uhai mwingi”

[Sanduku katika ukurasa wa 9]

Vidokezi Bora Kabisa kwa Wacheza Kamari

“Hakuna tabasamu iliyo baridi zaidi ya ile ya mbashiri anayesalimu mteja wake aliyeshinda. . ..Ni mbashiri asiye wa kawaida azuiliaye mcheza kamari asibahatishe kwa sababu mteja wake anapoteza sana. . ..Kumbuka, pia, kwamba wacheza kamari wenye mafanikio ni wachache sana kama ilivyo na wabashiri maskini.”—Graham Rock, The Times, London.

“Pesa za tuzo dola milioni 45 zilizohakikishwa katika kura ya Lotto ya jioni hii ndiyo kiasi kikubwa zaidi katika historia ya Jimbo la New York. Lakini uwezekano wa kuzishinda ukibahatisha kwa dola moja ni 1 kwa 12,913,582.”—The New York Times.

“Mpumbavu na pesa zake hutenganishwa upesi.” Msemo wenye kutumika tangu karne 16.—Familiar Quotations, ya John Bartlett.

“Mcheza kamari, usishangilie; yeyote anayeshinda leo hupoteza kesho.”—Mithali ya Kihispania.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki