Jinsi Televisheni Imebadili Ulimwengu
KIANGAZI kilichopita, televisheni ilibadili ulimwengu kuwa uwanja wa michezo wa tufe lote. Katika Roma, Italia, barabara zilikuwa hazina watu. Waitalia wapatao milioni 25 walikuwa wakitazama michezo ya mpira ya Kombe la Dunia. Katika Buenos Aires, Argentina, barabara hali kadhalika zilikuwa tupu, tena kwa sababu ile ile. Katika Cameroon, Afrika Magharibi, mwangaza uo huo wa rangi nyeupe-buluu uliangaza kwa njia ya kutisha kwenye madirisha huku mamilioni wakishangilia kwa umoja. Katika Lebanoni yenye vita, askari waliegemeza televisheni zao juu ya vifaru vyao visivyotumiwa ili kuitazama. Kufikia wakati michezo hiyo ilipofikia upeo wake, watu wanaokadiriwa kuwa sehemu moja kwa tano ya idadi ya dunia walikuwa wakitazama, wakivutwa kwenye sanduku hilo kama nondo kwenye miali ya moto, nyuso zao zikimulikwa kwa mng’ao walo mweupe-mweupe.
Tukio hilo kubwa katika televisheni halikuwa la namna ya peke yake. Katika 1985 karibu theluthi moja ya idadi ya watu duniani—watu 1,600,000,000 hivi—walitazama mchezo wa rock uitwao Live Aid. Setelaiti kumi na mbili zilieneza kipindi hicho kwenye nchi 150 hivi, toka Iceland mpaka Ghana.
Televisheni—sanduku hili lenye kupatikana kila mahali limeshiriki sana kuleta mabadiliko makubwa yaliyofanyika bila kuonekana wazi sana. Tekinolojia hiyo ilikua kuanzia na televisheni zisizoonyesha vizuri za miaka ya 1920 na 1930 hadi kwenye televisheni za kisasa, zenye rangi za waziwazi na picha zenye kutokeza, wakati ule ule hilo likichochea ongezeko kubwa katika tufe lote. Katika 1950 kulikuwako na televisheni chini ya milioni tano ulimwenguni. Leo, kuna kama 750,000,000 hivi.
Matukio kama vile michezo ya mpira wa Kombe la Dunia yanatoa kielezi juu ya uwezo wa televisheni wa kuunganisha tufe kwa mfumo mmoja tu wa usambazaji habari. Televisheni imebadili njia ambayo watu hujifunza juu ya ulimwengu unaowazunguka. Imesaidia kusambaza habari na mawazo, hata utamaduni na thamani, kutoka bara moja hadi nyingine, ikisambaza habari hizo bila kuzuiwa na mipaka ya kisiasa na kijiografia ambayo hapo zamani ilizuia habari kama hizo. Televisheni imebadilisha ulimwengu. Wengine husema kwamba yaweza kukubadili.
Johannes Gutenberg anafikiriwa kuwa alivuvumua uwasiliano wa kuwafikia watu wengi alipotoa Biblia ya kwanza kwa matbaa yake ya kuchapia katika 1455. Sasa habari moja tu ingeweza ghafula kufikia watu wengi zaidi kwa muda mfupi zaidi wa wakati, na kwa gharama zilizopunguzwa sana. Upesi serikali zilitambua uwezo wa kueneza habari kwa matbaa na zikajaribu kuidhibiti kwa kuweka sheria za kupata leseni. Lakini habari zilizochapwa zilifikia watu wengi zaidi kulipo hapo kwanza. Katika miaka ya mapema ya 1800, mwanahistoria Alexis de Tocqueville alisema kwamba magazeti yalikuwa na uwezo usio wa kawaida wa kutia wazo lile lile moja akilini mwa watu 10,000 kwa siku moja.
Sasa fikiria televisheni. Hiyo yaweza kutia wazo lile lile moja akilini mwa mamia ya mamilioni ya watu—wote kwa wakati ule ule mmoja! Na tofauti na kurasa zilizochapwa, watazamaji wayo hawahitajiki kuwa wenye elimu ya ufundi tata wa kusoma, wala haiwahitaji kufanyiza picha zao wenyewe akilini wala maoneleo yao wenyewe. Hiyo hutoa habari kwa njia ya picha na sauti pamoja na uvutio wote ziwezao kutoa.
Haikuchukua muda mrefu kwa wanasiasa kuyatambua makubwa yawezayo kufanywa na televisheni. Katika United States, Dwight D. Eisenhower alitumia televisheni kwa werevu katika kampeni yake ya urais ya 1952. Kulingana na kitabu Tube of Plenty—The Evolution of American Television, Eisenhower alishinda kura kwa sababu alijidhibitisha kuwa mgombea uchaguzi “mwenye kununulika zaidi” katika vyombo vya usambazaji habari. Kitabu hicho kinaonyesha kwamba huenda ikawa televisheni ndiyo iliyochukua sehemu kubwa katika ushindi wa John F. Kennedy dhidi ya Richard M. Nixon katika uchaguzi wa 1960. Wakati wagombea uchaguzi hao waliposhindana kwa maneno katika televisheni, Kennedy alipata upendeleo wa watazamaji wengi kuliko Nixon. Na bado, watu waliosikiliza mashindano hayo hayo kwenye redio walihisi kwamba yalikuwa na matokeo ya sawa kwa sawa. Kwa nini tofauti hiyo? Nixon alionekana mwenye sura ya kufifia na hafifu, hali Kennedy alikuwa na sura thabiti yenye kunawiri kwa rangi ya hudhurungi, akionyesha uhakika na uhai. Baada ya uchaguzi, Kennedy alisema hivi kuhusu televisheni: “Sisi hatungalifua dafu kamwe bila chombo hicho.”
“Chombo hicho” kiliendelea kufanyiza uwezo wacho uhisiwe ulimwenguni pote. Wengine walianza kukiita serikali iliyo ya tatu ulimwenguni kwa uwezo. Tekinolojia ya setelaiti iliwezesha watangazaji habari kusambaza habari kupita mipaka ya kitaifa na hata bahari. Viongozi wa ulimwengu walitumia televisheni kama baraza ili kupata utegemezo wa kimataifa na kushutumu washindani wao. Baadhi ya serikali ziliitumia kueneza propaganda katika nchi zilizo adui. Na kama vile serikali zilivyokuwa zimejaribu kudhibiti uvumbuzi wa Gutenberg baada ya kufahamu uwezo wake, serikali nyingi zilidhibiti sana televisheni. Katika 1986 karibu nusu ya mataifa yote yalikuwa yakionyesha vipindi vyenye kudhibitiwa na serikali tu.
Hata hivyo, tekinolojia imefanya iwe vigumu zaidi na zaidi kuidhibiti televisheni. Setelaiti za kisasa hupisha habari ambazo zaweza kunaswa hata katika nyumba zenye vipapasi vidogo zaidi vya kupokelea habari. Kamera ndogo za video zenye kubebeka na video-kaseti, pamoja na umayamaya wa wapiga picha wasio stadi, wametokeza rekodi nyingi zisizozuilika za kila aina ya tukio linalostahili kusambazwa.
Shirika moja la habari la U.S., Turner Broadcasting’s CNN (“Cable News Network”), hukusanya ripoti za habari kutoka nchi 80 hivi na kuzisambaza kote kote ulimwenguni. Mwenezo wake wa habari ulio wa tufe lote na wa wakati wote unaweza kufanya tukio lolote liwe jambo kuu la kimataifa karibu kwa wakati ule ule mmoja.
Kwa kiasi chenye kuongezeka, televisheni imebadilika kutoka kuwa chombo cha kurekodi matukio ya ulimwengu mpaka kuwa chombo cha kuelekeza matukio ya ulimwengu. Televisheni ilihusika kwa sehemu kubwa katika msururu wa mapinduzi yaliyotetemesha Ulaya Mashariki katika 1989. Halaiki za watu katika Prague, Chekoslovakia, walipiga kelele kwenye barabara, wakidai vipindi vya televisheni vyenye “kuonyeshwa wakati ule ule kama vinavyotukia.” Na ingawa wakati mmoja wanamapinduzi walimwaga damu ili kujipatia jumba la kiserikali, mji wenye boma, au ngome ya polisi, wanamapinduzi wa 1989 waling’ang’ania kwanza kabisa kupata utunzi wa stesheni ya televisheni. Kwa kweli, utawala mpya wa Romania ulianza kuongoza nchi hiyo kutoka kwenye stesheni ya televisheni! Kwa hiyo, kuiita televisheni kuwa mamlaka kuu ya tatu huenda kusiwe kutia chumvi mno.
Lakini televisheni imefanya mengi zaidi ya kuathiri uwanja wa siasa. Sasa inabadilisha tamaduni na thamani za ulimwengu. United States hushtakiwa mara nyingi kwa ‘kueneza utawala wa kitamaduni,’ yaani, kutumia hila katika kueneza utamaduni wao kwa ulimwengu kupitia televisheni. Kwa sababu United States ndiyo iliyokuwa nchi ya kwanza kurundika programu za kibiashara zenye faida, katika miaka ya mwisho mwisho ya 1940 na miaka ya 1950, wafanyizaji wa Kiamerika waliweza kuuzia mataifa mengine programu kwa kiasi kidogo kuliko kile kingewagharimu kufanyiza vipindi vyao wenyewe.
Katika miaka ya mwisho mwisho ya 1980, Kenya ilikuwa ikiingiza nchini kufikia asilimia 60 ya vipindi vyayo vyote vya televisheni; Australia, asilimia 46; Ecuador, asilimia 70; na Hispania, asilimia 35. Vingi vya viingizwa hivyo vilitoka United States. Kipindi kimoja cha Kiamerika, Little House on the Prairie, kilionyeshwa katika nchi 110. Kipindi Dallas kilitazamwa katika nchi 96. Wengine walilalamika kwamba ladha ya kienyeji ilikuwa ikitoweka kwenye televisheni ulimwenguni kote, na kwamba ununuzi na mali za Kiamerika zilikuwa zinaenea.
Mataifa mengi wanalalamika kwa fujo juu ya ‘ubeberu wa kitamaduni.’ Katika Nigeria, watangazaji wamelalamika kwamba kuingizwa kwa vipindi vya kigeni kunamomonyoa utamaduni wa kitaifa; wao wana wasiwasi kwamba watazamaji wa Nigeria wanaonekana kuwa wamefahamishwa vema zaidi juu ya United States na Uingereza kuliko juu ya Nigeria. Wazungu wanahisi vivyo hivyo. Katika mkutano wa hivi karibuni wa baraza kuu la U.S., mtangazaji mkwasi Robert Maxwell alisema hivi kwa ghadhabu: “Hakuna taifa linalopaswa kuvumilia kutiishwa kwa utamaduni walo na ulio wa kigeni.” Kufuatia hilo, mataifa mengine yameanza kuweka vizuizi juu ya hesabu ya vipindi vya kigeni ambavyo vyaweza kuonyeshwa na stesheni za televisheni.
‘Mwenezo wa utawala wa utamaduni’ si kwamba waweza kuharibu tamaduni tu. Waweza hata kuathiri sayari vibaya. Ununuzi wa jamii ya Magharibi wa kuvipata vyote sasa umekuwa na sehemu katika kuchafua hewa, kutia maji sumu, na kukumba dunia kwa angamizo kubwa. Kama vile mwandikaji mmoja wa The Independent, gazeti la London, alivyosema: “Televisheni imeletea ulimwengu mataraja yenye kumetameta ya uhuru wa kuwa na mali—ufanisi wa Magharibi—ulio wa kudanganya, kwa sababu yaweza kupatikana tu kukiwa na madhara makubwa kwa mazingira kwa kiwango kisichoweza kurekebishwa.”
Kwa wazi, televisheni inabadili ulimwengu leo, na badiliko haliwi jema sikuzote. Lakini pia ina matokeo hususa kwa mtu mmoja mmoja. Je, wewe waweza kudhuriwa?
[Blabu katika ukurasa wa 4]
Magazeti yaweza kutia wazo moja akilini mwa watu kumi elfu kwa siku moja
[Blabu katika ukurasa wa 5]
Televisheni yaweza kutia wazo moja akilini mwa mamia ya mamilioni ya watu mara ile ile