“Jioni Hii Utakuwa Umekufa”
Na mleta habari za Amkeni! katika Afrika Kusini
JE! UNAJUA kwamba unakufa na kwamba kufikia jioni hii utakuwa umekufa?” daktari akauliza.
Akiwa mnyonge kutokana na kupoteza damu, Wyndham Cook mwenye umri wa miaka 15 alijibu kwamba hata ikiwa ingemaanisha kupoteza maisha yake, alikuwa amepiga moyo konde kutii amri ya Biblia ya ‘kujiepusha na damu.’—Matendo 15:20.
“Je! ungeweka bunduki kichwani pako na kujipiga risasi?” daktari akabisha.
“Nisingeweza,” akaeleza Wyndham. “Lakini kukataa kutiwa damu mishipani si ujiuaji. Ni utii tu wa amri ya Mungu.” Wyndham ana vena za varikosi katika umio wake, ambazo wakati mwingine humfanya avuje damu kwa ndani. Isitoshe, wakati mwingine Wyndham huwa na ugonjwa wa kutokungama kwa damu.
Tatizo Kubwa Latokea
Kwa kueleweka, wazazi wa Wyndham walikuwa na wasiwasi, wakati alipoanza kuvuja damu tena Jumanne, Novemba 28, 1989, baada ya miaka saba isiyo na matatizo yoyote. Wyndham alipelekwa hospitalini mara moja. Baada ya kutazamwa ndani ya umio, kipimo cha hemoglobini yake kilishuka kikawa gramu 6.6 kwa kila desilita. (Kipimo cha kawaida cha hemoglobini ni gramu 14 hadi 15 kwa kila desilita.) Usiku huo, kila mtu alikuwa na wasiwasi Wyndham alipokuwa akilala na kuamka mara kwa mara.
Kufikia Jumatano mchana hesabu ya damu yake ilishuka ikawa gramu 4.3, na bado alikuwa anatokwa damu. Hilo lilianzisha mazungumzo ya kwanza kati ya mengine kadhaa pamoja na wafanyakazi wa hospitali kuhusu sababu ya Wyndham kutoweza kutiwa damu mishipani. Chris baba ya Wyndham, aeleza: “Tulisababu kirefu juu ya Maandiko. Tulifanya iwe wazi pia kwamba hatukuwa tunakataa msaada wao wa kitiba, au uhai wenyewe. Katika tatizo kubwa kama hilo, tulihitaji sana ustadi wao wa kitiba. Tulikuwa tunakataa tu damu kuwa tiba.”
Saa 8:00 mchana, mrija uliojaa hewa ungeingizwa kupitia kooni mwa Wyndham, ambao ungepuliziwa hewa ili kuwe na msongo kwenye vena zilizofura na hivyo kuzuie kuvuja damu. Mrija huo pia huenea hadi kwenye tumbo kuvuta damu yoyote ambayo imekusanyika humo kutokana na kuvuja damu kwa ndani. Kufikia hapo, wakati wazazi wa Wyndham hawakuwapo, muuguzi mmoja alisema naye hivi: “Ni kiasi kidogo tu cha damu unachohitaji na uhai wako waweza kuokolewa. Wazazi na mhubiri wako hawatahitaji kujua.”
“Yesu alikunywa damu na mitume wake 12,” daktari akatoa hoja. “Kristo alisema, ‘Hii ni damu yangu . . . inyweni.’ Wewe wajiita Mkristo na wataka kufuata mfano wa Kristo, kwa hiyo mbona usikubali kutiwa damu mishipani?”
Wyndham alieleza kwamba wakati mitume walipokunywa kutoka kwa kikombe ambacho Yesu alitoa, hiyo ilikuwa divai ambayo ilikuwa kifananisho tu na haikuwa damu halisi ya Yesu. Msimamo wa Wyndham wa kutoridhiana ulivutia sana hivi kwamba maandishi fulani yaliwekwa kwenye faili yake yakisema kwamba, akiwa mwenye miaka 15, mwenye fahamu na akili timamu, alikuwa amekataa katakata kutiwa damu mishipani. Msimamo huo imara ungekuwa wa faida kubwa siku iliyofuata.
Jua lilipochomoza Alhamisi, Wyndham alionekana kuwa amepata nafuu kidogo. Lakini hali hiyo ilikuwa ya muda tu. Yeye alianza kuvuja damu tena. Kufikia saa 3:00 asubuhi, hesabu yake ya damu ilikuwa imeshuka hadi 3.0. Hali yake ilikuwa ya dharura. Daktari mkuu aliyehusika na sehemu ya upasuaji aliuliza kama familia ya Wyndham wangeweza kuondoka chumbani kwani alitaka kuzungumza na Wyndham akiwa peke yake.
“Haikuwa rahisi kumwacha peke yake,” asema mama yake, Judy. “Tulikuwa na hofu kwamba katika hali yake ya udhaifu, ukinzani wake ungepunguka. Lakini alikuwa amebatizwa miezi sita iliyotangulia, na hivyo alikuwa na haki ya kufanya utetezi wake mwenyewe.”
Baba yake akumbuka: “Kile tu ambacho tungeweza kufanya sasa kilikuwa ni kumwomba Yehova amsaidie Wyndham adumishe uaminifu wake wa kimaadili. Tulijifunza maana yenyewe ya neno ‘kuomba dua.’” Wyndham mchanga asema kwamba kile kilichomsaidia ni kukumbuka Ufunuo 2:10. “Yale maneno, ‘jidhibitishe mwenyewe kuwa mwaminifu hadi kifo, nami nitakupa taji ya uzima’ yalizungukazunguka akilini mwangu,” yeye alisema.
Agizo la Mahakama?
Hatimaye daktari akasema kwamba angeomba agizo la mahakama la kuruhusu kutiwa damu mishipani. Kwa vile Wyndham alikuwa mchanga, kila mtu alitarajia kuwa ombi hilo litakubaliwa. Sala kwa niaba ya Wyndham zilikuwa nyingi. “Kwa kweli kundi zima lilishikamana na familia ya Cook katika kisa hicho,” akaeleza Neville, mwangalizi msimamizi wa kundi. “Wyndham alipopata nafuu kidogo, kundi zima lilipata faraja. Alipodhoofika, kundi zima lilihuzunika na kusali kuwe na matokeo mema.”
“Wakati tulipokuwa tukingoja matokeo ya mahakama,” akumbuka Judy, “wengi wa baraza letu la wazee walifika na walikuwa wanangoja katika sebule ya wagonjwa. Walidhibitika kuwa baraka kama nini! Huku mvujo wa damu ukiendelea na hesabu ya damu ikiwa 2.9, ilionekana kana kwamba hangepona.”
Katika saa hiyo hiyo, jibu lilifika kwamba agizo la mahakama la kulazimisha mtio wa damu mishipani mwa Wyndham lilikuwa limekataliwa. “Tuliambiwa kuwa,” aeleza Chris, “sababu ya kukataliwa huko ilikuwa kwamba Wyndham alikuwa mwenye fahamu kabisa na mwenye akili timamu. Yeye alikuwa anajua matokeo ya uamuzi wake, na alikuwa amefanya uamuzi uliofikiriwa kwa makini unaopatana na itikadi zake zenye msingi wa Biblia.”
Kukabiliana na Kifo
Lakini Wyndham hakuwa anapata nafuu. Kwa kweli, Alhamisi saa sita, Chris na Judy walifahamishwa: “Mwana wenu ana saa chache tu za kuishi. Ikiwa mnataka mhubiri na baadhi ya watu wa ukoo wenu wamwone kabla hajafa, ni afadhali mwaite mara moja.” Ndugu ya Wyndham, Jonathan, mwenye miaka 9, aliletwa kumwona.
Saa 7:30 mchana, wafanyakazi waliondoa mrija uliopitia kooni mwa Wyndham ili afe kwa heshima. Kwa muda wa saa chache zilizofuata, uhai wa Wyndham ulikuwa ukingoni. Ingawa alikuwa hali mahututi, hali yake ilibaki ikiwa tulivu huku akiwa na homa kali mwilini mwote. Aliendelea kuwa hai usiku huo wote.
Ndipo, wakati wa mwisho juma, akaanza kufanya maendeleo. Jumatatu iliamuliwa apelekwe nyumbani, kwani hakukuwa na mengi zaidi ambayo yangeweza kufanywa kwake hospitalini. Mara alipofika nyumbani, mambo yaligeuka vibaya. Chris akumbuka: “Tulimbeba Wyndham ndani ya nyumba na kumweka kitandani. Hata kabla ya dakika 45 kupita aliamka na akaanza tena kuvuja damu sana. Tulishindwa kabisa na hali! Tulisali kwa Mungu kwamba atusaidie kuwezana na hali hiyo katika njia ifaayo.”
Haipati dakika 30 Wyndham alikuwa amerudi kwenye hospitali ile ile, katika chumba kile kile, akiwa na daktari yule yule aliyemhudumia. Kipimo cha hemoglobini kilikuwa kimeshuka hadi 2.5. Kufikia jioni hiyo Wyndham alipewa oksijeni, kwa sababu aliona vigumu kupumua. Vita vya kuendelea kuishi vilikuwa vinaendelea siku iliyofuata wakati ambapo ziara yenye kutia moyo sana ilipofanywa. Judy aeleza: “Mwangalizi wetu wa wilaya, Sarel na mke wake Maryann, walikuja kumwona Wyndham.” “Sarel alisimama kando ya kitanda cha Wyndham, na akishika mkono wake, alitoa sala ya kuhisiwa moyoni kwa Yehova. Tulihisi tumeimarishwa baada ya ziara yake.”
Muda wote wa tatizo hilo, kundi la Kikristo liliandaa msaada wa kazi. Kulikuwako na orodha ya kundi ya wale ambao wangepeleka vyakula si kwa familia ya Cook pekee, bali pia kwa Mashahidi wengine waliofanya kazi kwa zamu pamoja nao. Vijana walisafisha nyumba, wakampa mbwa chakula, wakawasha taa, na kadhalika. Walifanya mambo yote madogo ambayo familia haikuwa na wakati kufikiria kufanya. Utegemezo na kitia-moyo kutoka kwa Wakristo wenzi wakati kama huo, haupasi kupuuzwa kamwe.
Kwa mara nyingine madaktari waliamua kwamba, zaidi ya kutia damu, hakuna kingine zaidi wangeweza kumfanyia Wyndham. Kwa hiyo, akiwa bado anapewa oksijeni na akiwa na hesabu ya damu iliyo chini ya 2, alirudishwa nyumbani.
Kupona
Ile dawa erythropoietin, aina ya homoni ya kufanyizwa ambayo huchochea uboho wa mfupa ufanyize chembe nyekundu za damu kwa kiwango cha haraka zaidi, ilipendekezwa ili kuongeza hesabu ya damu ya Wyndham.a Utibabu huo haujasajiliwa katika Afrika Kusini, lakini hati ya kisheria ilipitishwa na dawa hiyo ikatumiwa na daktari wa familia. Kwa kipindi cha majuma matatu, hesabu ya damu ya Wyndham ilipanda kufikia 6.2, na kufikia majuma sita ilikuwa 11.5. Miezi miwili baadaye, Wyndham alikuwa mwenye nguvu vya kutosha kutumia mwezi mzima pamoja na familia yake katika mahubiri ya peupe akiwa painia msaidizi.
Tokeo moja zuri la kabiliano na kifo la Wyndham lilikuwa jinsi lilivyoathiri vijana kundini. Judy aonelea: “Ninafikiri walipata kuelewa kwamba wao wangeweza kukabiliwa pia kuchukua msimamo kama huo katika kipindi kifupi. Wao walikuwako hospitalini, wakajihusisha katika kisa hicho chote, na ninafikiri walielewa ujumbe, ‘Je! tunachukua kweli kwa uzito?’”
Tangu kisa hicho, Wyndham amevumilia mivujo mingine miwili ya damu kwa mafanikio. Wyndham ang’amua kwamba huenda akapatwa na ugonjwa huo tena wakati wowote. Lakini chochote kitakachotukia wakati ujao, Wyndham Cook atazamia kwa makini wakati ambapo Yehova Mungu atakapomdhawabisha hatimaye na afya kamili katika Paradiso inayokuja duniani. Kwa wakati huu, Wyndham amepiga moyo konde kuendelea kuishi kulingana na kanuni za Biblia.b
[Maelezo ya Chini]
a Ona broshua Damu Yaweza Kuokoaje Uhai Wako?, ukurasa 15, iliyotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
b Gazeti hili lilipokuwa likienda kuchapishwa, Wyndham alikufa baada ya tukio jingine la kuvuja damu.
[Picha katika ukurasa wa 28]
Wyndham na wazazi wake