Kuutazama Ulimwengu
Sheria ya Mitio ya Damu Mishipani Katika Italia
Kulingana na Katiba ya Italia, hakuna yeyote anayeweza kupewa aina fulani ya utibabu dhidi ya mapenzi yake. Sheria ya hivi karibuni ya Wizara ya Afya ya Italia yahakikisha kwamba utaratibu huo wa kikatiba hutumika pia kwa mitio ya damu mishipani. Kwa kweli, sheria hiyo, iliyotiwa tarehe ya Januari 15, 1991, husema kwamba “mitio ya damu, visehemu vya damu, au vitu vinavyofanyizwa kwa damu, huwa ni zoea la kitiba ambalo lina hatari; kwa hiyo, linahitaji ukubali wa mpokezi baada ya kujulishwa.” Kwa maneno mengine, wagonjwa wapaswa kujua hatari zinazohusika na wana haki ya kukataa damu. Sehemu ya mwisho ya sheria hiyo yakubali kwamba mitio ya damu yaweza kueneza “magonjwa yenye kuambukiza, kama vile mchochota wa ini na UKIMWI,” na kwamba “majaribio katika maabara hayawezi nyakati zote kutambulisha watu walioambukizwa hivi karibuni.”
Ukatili wa Tabaka
Gazeti India Today laripoti kwamba mfumo wa tabaka wa India ndio uliosababisha uuaji makusudi wa vijana watatu hivi karibuni. Katika mji mdogo wa Mehrana, mvulana wa umri wa miaka 18 wa tabaka la Jatav alikuwa na mapenzi ya mahaba na msichana wa umri wa miaka 16 wa tabaka la Jat lenye utajiri na uwezo mwingi zaidi. Wazazi wa msichana, na wengineo wa tabaka la Jat, walighadhabishwa sana. Katika baraza moja, ambalo lilikuwa na Wajat matajiri wengi, vijana hao wawili pamoja na mvulana mwingine wa Jatav aliyekuwa mpatanishi wa hao wawili walihukumiwa kifo. Wavulana hao wawili waliteswa kikatili kwa saa nyingi, halafu inasemwa kwamba baba zao walilazimishwa kuwaweka tanzi shingoni mwao. Vijana wote watatu walinyongwa katikati ya mji. India Today laripoti kwamba waliokuwa na hatia katika mauaji hayo sasa wako gerezani lakini linaomboleza: “Kilikuwa ni kikumbusha cha majonzi kwamba katika vijiji vya nchini bado tabaka ya kikale inashikiliwa sana, na hakuna kiasi chochote cha ‘kustaarabishwa’ kinachoweza kuimaliza.”
Maswali ya Watoto
Uchunguzi wa mielekeo ya watoto Wafaransa wa umri wa kutoka miaka 12 hadi 15 ulifunua kwamba idadi kubwa yao (asilimia 57) wanahisi uhakika wa kwamba Mungu yuko au kwamba labda Mungu yuko. Uchunguzi huo pia unafunua kwamba asilimia 59 yao husali. Walipoulizwa ni maswali gani wangependa sana wapewe majibu, itikio kubwa lilikuwa: “Ni nini maana ya uhai?” Maswali mengine yalikuwa: “Sisi tumetoka wapi, na tunaelekea wapi?” “Tunaweza kufanya nini ili maisha yapendeze?” “Kwa nini tujifunze kwa bidii shuleni?” “Nitafanya nini baadaye maishani?” Wasosholojia Françoise Champion na Yves Lambert, waliofanya uchunguzi huo, waliona kwamba kwa ujumla, vijana wa leo huhisi “utupu, na wasiwasi usio dhahiri.”
Uhalifu Bila Adhabu
Idara ya Utafiti na Takwimu ya Serikali ya Uingereza hivi karibuni imetoa tarakimu zinazohuzunisha kuhusu uhalifu katika nchi hiyo. Fikiria uhalifu 100. Kati ya huo, 59 huwa hauripotiwi kamwe. Kati ya ule unaoripotiwa, polisi huchunguza 26 pekee. Kati ya huo, wao husuluhisha uhalifu unaopungua theluthi moja—ni saba tu unaokamilishwa. Na kati ya huo, ni nne tu unaoongoza kwenye kuhukumiwa kwa mhalifu au hata kuonywa kwake! Hata hivyo, tarakimu hizo zinahusu uhalifu wote, kutia ndani na uharibifu wa mali na wizi. Polisi wa Uingereza husuluhisha asilimia 70 ya uhalifu unaohusisha jeuri na asilimia 90 ya uuaji makusudi.
Kutetea Mapadri Wanaovutiwa na Watoto Kingono?
Kichwa kikuu cha gazeti la hivi karibuni la U.S. liitwalo National Catholic Reporter kilisema: “Baadhi ya dayosisi bado zinawatetea mapadri wanaoshtakiwa kudhulumu watoto kingono.” Gazeti hilo lilimhoji Jeffrey Anderson, wakili ambaye ni mtaalamu wa kuchunguza visa vya watoto wanaodhulumiwa kingono. Yeye anakadiria kwamba tangu 1985, wakati watu walipoanza kuchunguza kwa makini zaidi mapadri ambao huvutiwa kingono na watoto, kumekuwako zaidi ya visa elfu moja ambapo mapadri waliwadhulumu watoto. Anderson alitumia maneno makali kwa itikio la kanisa kuhusu mkasa unaoendelea: “Ni kisa cha muda mrefu cha kuepuka daraka,” yeye ashtaki, akishutumu mwelekeo wa kanisa wa kuwatetea mapadri walioshtakiwa. “Kwa ujumla, itikio la kanisa limekuwa dogo kimakusudi katika kushughulikia wadhulumiwa na hatari zilizopo pia.”
Vizazi Vinavyoishi
Ikiwa ungegawanya Waamerika katika vizazi vitatu kutoka kati ya miaka 1800 hadi 1920, ni watu wangapi kutoka kila kizazi wangalikuwa hai katika United States leo? Jumla ya zaidi ya milioni 30, kulingana na Constitution ya Atlanta. Ilichapisha yafuatayo: Kati ya wale waliozaliwa baina ya miaka ya 1860 na 1882, kuna 3,000 walio hai leo. Kati ya wale waliozaliwa baina ya miaka ya 1883 na 1900, kuna 1,100,000 walio hai leo. Na kati ya wale waliozaliwa baina ya miaka ya 1901 na 1924, kuna 29,000,000 walio hai leo.
Mshuko Mkubwa Zaidi wa Kanisa
Uanachama katika dini kubwa zaidi Kanada, iitwayo United Church of Canada, ulipata mshuko wao mkubwa zaidi katika miaka karibu 20, ukishuka kwa watu 21,000 mwaka jana. “Uanachama ulifikia kilele katika 1965 ulipokuwa na watu 1,064,033,” yaripoti The Toronto Star, lakini kumekuwako na mshuko katika utegemezo wa kanisa tangu wakati huo. Uanachama wa kanisa sasa ni 808,441, mshuko wa zaidi ya watu 250,000. Kati ya visababishi vya mshuko huo ni “kutoafikiana kuhusu kuwekwa kwa wanaume wagoni-jinsia-moja kuwa makasisi,” yadai Star. Mtu mmoja mwenye kushikilia mambo ya kanisa alimalizia kwamba “kuna ukweli ambao unatokea kuhusu mamlaka na uongozi wa kanisa.”
Kidogo Zaidi, Kuchelewa Zaidi
Afrika inakabiliwa tena na njaa—labda njaa kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote, kulingana na gazeti la Paris Le Figaro. Watu wanaokadiriwa kuwa milioni 20 hadi 29 wanatishwa na njaa. Mkurugenzi wa Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa anasema kwamba dola milioni mia moja zahitajiwa ili kulipia uhitaji wa chakula. Hata hivyo, wito wa msaada umepata tokeo dogo kwa sababu ulitolewa wakati ambao ulimwengu ulikuwa umekazia fikira mizozano ya vita vya Ghuba ya Uajemi. Kama tokeo, msaada kidogo zaidi unafika kukiwa kuchelewa zaidi. Gazeti la Ufaransa Le Nouvel Observateur laripoti kwamba watu kwa ujumla wamezoea kuona picha za watu wanaoona njaa hivi kwamba mkasa wa njaa unaonekana kuwa kitu cha kawaida.
Mageuzi Katika Jaribu
Phillip Johnson, profesa wa sheria ya uhalifu katika Chuo Kikuu cha California katika Berkeley, United States, amevutiwa kwa muda mrefu na njia ambayo wanabayolojia hutetea nadharia ya mageuzi. Wao huonekana wenye kulinda sana na kushikilia habari hiyo sana hivi kwamba Johnson alianza kuchunguza “mambo makuu yaliyo dhaifu ambayo walikuwa wanajaribu kulinda.” Matokeo ya utafiti wake ilikuwa kitabu, Darwin on Trial, ambacho The Sacramento Bee laeleza kuwa “uchunguzi wa mwanasheria, sehemu kwa sehemu, kwa hoja zenye akili na ithibati ya nadharia ya mageuzi.” Gazeti hilo linafanya muhtasari hivi: “Darwin aanguka.” Johnson adai alipata wasomi wengi, kutia na wanabayolojia, ambao wanaogopa kusema wazi dhidi ya mageuzi. “Jambo moja ambalo nimejifunza kutokana na ono hilo,” akaambia San Francisco Chronicle, “ni kwamba kuanzisha nadharia fulani ya wasomi na kuiendeleza bila kupata uchambuzi, hauhitaji kambi za mateso na polisi wa kisiri-siri. Yale tu unayotakiwa kufanya ni kusema kwamba watu watakucheka na utapoteza heshima yako. Hilo lina uvutano mkubwa kwa maisha ya kielimu.”
Kibandiko cha Unyofu
Utangazaji wenye unyofu ulitokea hivi karibuni katika sehemu isiyotarajiwa—kwenye paketi ya sigareti. Mapema mwaka huu, katika Los Angeles, California, U.S.A., aina mpya ya sigareti ilitokea madukani, ikiwa imewekwa katika paketi nyeusi yenye picha ya fuvu la kichwa jeupe na mifupa yenye kupitana. Kwenye upande wa paketi kumeandikwa katika herufi kubwa nyeupe, jina layo: DEATH (KIFO). Kulingana na gazeti Newsweek, watengenezaji wanadai kuwa wameuza paketi 25,000 tayari, kukiwa hakuna utangazaji ila ule wa kibandiko cha bidhaa yao kisicho cha kawaida—lakini kilicho sahihi. Watengenezaji wanatumaini kuongeza uuzaji kitaifa, akivutia wavutaji ambao ni wachanga mno au wasiojali kuweza kuogopa kifo. Wateja kama hao wanaelekea kupuuza onyo lililo kwenye kila paketi ya sigareti hizo za Kifo: “Ikiwa Huvuti Sigareti, Usianze. Ikiwa Wewe Huvuta, Koma.”
Matokeo ya Useja
Kulazimisha mapadri waendelee kuwa bila wake “huongoza kwenye mashtaka ya ubaba, wanawake wenye waume wasio halali, kuongezeka kwa makasisi na wanaseminari walio wagoni-jinsia-moja, upweke na katika visa fulani unajisi wa watoto.” Kulingana na National Catholic Reporter, hivyo ndivyo visababu vilivyotajwa na Joe Sternak, aliyekuwa padri Mkatoliki wa dayosisi kuu ya Chicago katika United States, alipotoa onyo kwa habari ya useja katika mkutano wa hivi karibuni wa kila mwaka. Sternak, ambaye kwa sasa anaandika kitabu juu ya unajisi wa watoto, ashtaki kwamba dayosisi katika majimbo zaidi ya 20 hutumia upaji wa kanisa kulipia mashtaka na mapatano ya nje ya mahakama katika visa vya mapadri kunajisi watoto.
Je! Matineja Waweza Kuamua?
Je! vijana matineja wamekomaa vya kutosha kufanya maamuzi kuhusu utibabu wao? Swali hilo huzuka mara nyingi wakati wabalehe Mashahidi wa Yehova wakataapo mitio ya damu mishipani. Ingawa wastadi fulani wa kisheria na kitiba waweza kudhania kuwa jibu ni la, uchunguzi wa hivi karibuni uliofanywa na Baraza la Maendeleo ya Wabalehe la Carnegie hudokeza vingine. Kulingana na gazeti la Science, uchunguzi saba mbalimbali ulilinganisha jinsi wabalehe na watu wazima walivyoshughulika na hali za kitiba zilizo halisi na zinazokisiwa pia. Wachunguzi hao walipata kwamba kulikuwa na tofauti kidogo katika uwezo wa kufanya maamuzi wa “wabalehe wachanga wa miaka 14 au 15” kwa kulinganisha na watu wakubwa (kutoka umri wa miaka 18 hadi 25). Uchunguzi huo ulipata kwamba wao walionyesha “mkazo na ‘sifa’ ile ile ya kutumia akili” kama vile wenzao wakubwa.
Mchochota wa Ini Kutoka kwa Damu
Uchunguzi wa hivi karibuni katika Japani ulithibitisha hatari ya kuambukizwa mchochota wa ini Aina ya-C kupitia mitio ya damu. Aina hiyo ya vairasi inasemekana husababisha nusu ya visa vya kansa ya ini na mnyauko wa ini katika Japani. Kulingana na uchunguzi huo, asilimia 8.3 ya watu 962 waliokuwa wametiwa damu mishipani walikuwa na vairasi ya mchochota wa ini Aina ya-C, hali ni asilimia 0.7 tu ya watu 1,870 ambao hawakuwa wamepata kutiwa damu ndio walikuwa nayo. Kwa kushangaza, asilimia 40 ya wanaobeba vairasi hawakutambulika walipopata majaribio ya damu inayotumiwa na Shirika la Msalaba Mwekundu la Japani.