Baraza la Makanisa Ulimwenguni Ushirikiano au Mvurugo?
Na mleta habari za Amkeni! katika Australia
KUSANYIKO lilianza Februari 7, 1991, kwenye uwanja wenye kuvutia wa Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia katika Canberra, Australia, ambalo ni jiji kuu la taifa. Kadirio la watu 4,000 ambao ni washiriki tu wa kanisa na viongozi wa kanisa 316 hivi kutoka nchi zaidi ya mia moja walihudhuria. Makusanyiko sita ya WCC (World Council of Churches au Baraza la Makanisa Ulimwenguni) yaliyotangulia yalikuwa yamefanywa katika nchi mbalimbali katika kipindi cha miaka 35, kuanzia 1948 katika Amsterdam, Uholanzi.
WCC ni nini? Si kanisa kubwa mno. Ni ushirika wa makanisa, baraza la kubadilishana maoni. Hotuba rasmi ya kukaribisha ya kusanyiko hilo la saba ilitolewa na waziri mkuu wa Australia, Robert J. Hawke—hata ingawa yeye amejiungama kuwa mwagnosti. Kichwa kikuu kilichochaguliwa kwa kusanyiko hilo la majuma mawili kilikuwa katika namna ya sala: “Njoo Roho Mtakatifu—Fanya Upya Uumbaji Wote!”
Hata hivyo, jinsi mambo yalivyogeuka katika mandhari ya ulimwengu yalikengeusha hisi na matarajio ya wajumbe kutoka kwa kufanywa upya kwa roho mtakatifu hadi kwenye siasa na adili ya vita ya Ghuba ya Uajemi. Mgeuko huo wa mapema kutoka kwa mazungumzo ya kiroho ulifanya Sir Paul Reeves, askofu mkuu Mwanglikana aliyekuwa msimamizi mkuu wa New Zealand, aeleze mshangao wake: “Katika makusanyiko kama haya, sisi huelekea kubishana juu ya mamlaka, isiyo na uhusiano wowote na Roho Mtakatifu.” Askofu mkuu wa Canberra alijaribu kutoa hoja kuhusu thamani ya kutoafikiana: “Umoja ni zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu. Mgawanyiko usio na chuki ni zawadi ya Roho Mtakatifu huyo huyo.”
David Gill, katibu mkuu wa Baraza la Makanisa la Australia, alionyesha pia hangaiko kwamba uaminifu wa kimaadili wa WCC wenyewe ulikuwa hatarini, akisema kwamba shirika hilo lilizidi kuwa lenye msaada kwa vikundi vyenye miradi fulani vinavyotafuta jukwaa la kutoa mahangaiko yavyo hususa.
Kuwekwa kwa Wanawake—Mtengano Zaidi
Sehemu ya wanawake katika kanisa la siku hizi ilikuwa pia kwenye ajenda, lakini wanawake hawakufurahi. Wengi wao waliliona kuwa limeongozwa na wanaume. Lois Wilson wa Kanada alimalizia vikali: “Siasa za WCC zinachukiza sana na sifikiri hilo ndilo Yesu alilotaka.” Ni nini kilicholeta mfadhaiko huo? Gazeti Canberra Times lilisema hivi: “Kumekuwako kilio kingi katika vyoo vya wanawake kwa sababu wanawake walikuwa wametishwa ili kuwazuia wasikubali kuchaguliwa kwenye halmashauri kuu ya baraza hilo. Mwanamke mmoja alikuwa ameambiwa kwamba angefukuzwa kutoka kanisa lake katika kujaribu kumvunja moyo asikubali kuchaguliwa.”
Ni Nini Kilichokipata Kile Kichwa cha Kiroho?
Wengine walihangaika kwamba kusanyiko hilo halikukazia vya kutosha kazi yalo ya hali ya Kibiblia au ya kitheolojia. Hilo halishangazi kwa kuwa mengi ya mambo makuu kwenye ajenda hiyo yalikuwa ya hali ya kisiasa. Kwa kweli, katika ripoti zilizochapishwa juu ya kusanyiko hilo, msomaji alipata rejezo moja fupi tu la Biblia.
Gazeti la kidini National Outlook lilisema kwamba David Gill “ana maoni kama yale ya wengine ambao wamehudhuria mikutano ya WCC katika siku za karibuni, na ambao, kama vile mtu mmoja alivyosema karibuni, walienda wakiwa na matumaini makubwa lakini wakaondoka huko wakihisi kuwa wakavu na watupu.”
Kwa kutofautiana, wakati wenye njaa na kiu ya kiroho walipokutana na Kristo Yesu, hawakuondoka wakihisi kuwa “wakavu na watupu.” Waliondoka wakiwa wameburudishwa: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, mzigo wangu ni mwepesi.”—Mathayo 11:28-30.