Je! Dini na Siasa Zina Urafiki Wenye Kudumu?
SIKU moja mtawala Mrusi Vladimir wa Kwanza aliamua kwamba watu wake wa kipagani wanapaswa kuwa “Wakristo.” Yeye mwenyewe alikuwa ameongolewa mwaka wa 987 W.K. baada ya kuoa binti-mfalme wa dini ya Orthodoksi ya Ugiriki, na sasa akaagiza kuwe na ubatizo wa ujumla wa raia zake—kwa tisho la upanga ikiwa lazima. Pole kwa pole Kanisa la Urusi lilianza kujitegemea likawa mbali na “mama” yake, yaani Kanisa la Ugiriki, hata mwishowe likawa idara ya Serikali. Na ingawa watawala wa Urusi leo wanakana rasmi kuwako kwa Mungu, Kanisa na Serikali katika Urusi bado zinadumisha urafiki wenye matatizo.
Karne nyingi baadaye, Mfalme Henri wa Nane wa Uingereza alifaulu pia kufanyiza urafiki wa karibu kati ya Kanisa na Serikali, ingawa alitumia njia zilizo tofauti. Mwaka wa 1532 alikuwa na wasiwasi kwa sababu mke wake, Catherine wa Aragon, alikuwa ameshindwa kuzaa mrithi wa kiume wa kiti cha ufalme. Ili kutatua tatizo hilo, Henri alimwoa kwa siri Anne Boleyn, mpenzi wake. Askofu Mkuu wa Canterbury aliruhusu jambo hilo, akatangaza kwamba ndoa ya kwanza ya Henry imefutwa. Mwaka wa 1534, mzinzi na mkatili huyo alijitangaza kuwa kichwa cha Kanisa la Uingereza, cheo ambacho kinashikiliwa na mfalme wa Uingereza mpaka leo hii. Maamuzi yanayofanywa na Baraza la Kanisa yako chini ya wajibu wa kukubaliwa na bunge, nao maaskofu, ambao ni washiriki wa Baraza la Wabunge Wenye Daraja la Juu, wanashiriki kusimamia Uingereza. Hivyo Kanisa na Serikali zimekuwa katika hali ya kuoana katika Uingereza kwa zaidi ya miaka 450.
Ndoa za Kisasa Kati ya Kanisa na Serikali
Mwaka wa 1936 maasi katika Hispania juu ya serikali ya Jamhuri yalileta vita ya wenyewe kwa wenyewe kisha Jemadari Franco akapata mamlaka ya kutawala. Wenye kupinga Serikali walivunjika sana moyo kuona Franco akiwapa viongozi wa kidini mamlaka nyingi kwa sababu wao walimuunga sana mkono.
Mwaka wa 1983 shirika linaloitwa W.C.C. (Baraza la Makanisa Ulimwenguni) lilikusanyika katika Vancouver, Kanada. Katibu mkuu wake, Philip Potter, aliwaambia ‘waendelee kufuata siasa.’ Watu wengi wanaoenda kanisani wamehangaishwa sana na jambo la kwamba vikundi vya kisiasa vimekuwa vikipewa pesa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika nchi kadha.
Basi, hakuna shaka kwamba dini inajiingiza katika siasa. Hata hivyo, ulizo lililo la maana ni kwamba, je! inapaswa kufanya hivyo? Je! kuhusika kwa dini katika siasa kunainua viwango vya siasa katika maadili, au kunapotosha dini? Na namna gani juu ya wakati ujao? Je! dini na siasa zitaendelea kufurahia ‘mapenzi’ yazo, au mambo yatakuwa machungu yawaweke katika mwendo wa kugongana?
[Picha katika ukurasa wa 3]
Kichwa cha kwanza cha Kanisa la Uingereza