Marekebisho ya Uingereza Wakati wa Badiliko
“Huu ulikuwa wakati wa mabadiliko mengi na kujichanganua upya.”
NDIVYO J. J. Scarisbrick afafanuavyo jinsi hali ilivyokuwa huko Uingereza katika karne ya 16 katika wasifu wake Henry VIII. Marekebisho makubwa ya kidini katika Ulaya yalifanya wengi waitikadi kwamba dini yenye imani ya kidesturi ilihitaji kurekebishwa.
Katika Uingereza watu waliunga mkono mafundisho yenye ubishi ya Martin Luther. Na kuanzia mwishoni-mwishoni mwa karne ya 14, wafuasi wa Lollard, wahubiri wenye shauku na watetezi wa Biblia, walikuwa wamevumilia na kueneza mafundisho yao Uingereza kote.
Kufikia mwaka wa 1526, nakala za tafsiri ya Kiingereza ya William Tyndale ya Maandiko ya Kigiriki zilikuwa zimefika Uingereza, licha ya jitihada kali za maadui za kuzuia kugawanywa kwake. Mafundisho ya kidesturi ya Kikatoliki kama vile purgatori, itikadi kwamba mkate na mvinyo hugeuka kuwa mwili na damu ya Yesu, na useja wa kikasisi yalifunuliwa kuwa hayaungwi mkono na Biblia.
Lakini tatizo lililohusu mambo ya kinyumbani ya mfalme ndilo lililochochea Marekebisho ya Uingereza. Henry wa Nane alijaribu kumtaliki mke wake Mkatoliki Catherine wa Aragon kwa sababu alitaka mrithi wa kiume kwa kiti chake cha ufalme. Watoto wote sita ambao Catherine alimzalia Henry walizaliwa wakiwa wafu au walikufa utotoni, isipokuwa mmoja, binti aliyeitwa Mary. Zaidi ya hilo, Henry alivutiwa na Anne Boleyn mchanga aliyekuwa mchangamfu naye alinuia kumwoa.
Bila kujua, rafiki ya Henry mwenye mamlaka na uwezo, kadinali Thomas Wolsey, alichochea Marekebisho hata zaidi. Tangu mwanzo wa utawala wa Henry katika mwaka wa 1509, Wolsey alipata mamlaka na mali hatua kwa hatua. Hatimaye akawa na uwezo kuliko wote ila tu mfalme. Lakini Wolsey hakupendwa kwa sababu alikuwa mwonevu na aliongeza kodi. Kwa kuongezea, alijihisi kuwa juu ya sheria za kanisa lake, kwa sababu alikuwa baba ya watoto wawili haramu.
Wakuu walikula njama ya kumwangamiza Wolsey, njama ambayo ilifaulu Wolsey aliposhindwa kupata talaka ambayo Henry aliitaka sana. Aliponyang’anywa wadhifa wake, Wolsey alikufa mwaka wa 1530, kabla tu ya kupelekwa mbele ya mfalme kwa mashtaka ya uhaini.
Roho ya kupinga ukasisi ikawa yenye nguvu katika Uingereza. Mwanahistoria Scarisbrick aliandika kwamba “ilidaiwa kwamba Kanisa lilihitaji kutakaswa kabisa, kwamba jamii haingeweza kubeba tena mzigo huu usio na faida, Kanisa hili kubwa lililotumia watu sana, likanyonya mali nyingi sana, likachukua vitu vingi na kutoa vichache . . . , na kusafirisha pesa za Uingereza hadi Roma . . . liliharibu uchumi wa [Uingereza].”
Enzi ya Cromwell
Hatimaye, matatizo ya ndoa ya Henry “yalitatuliwa” kwa msaada wa mshauri wake mkuu Thomas Cromwell na Askofu mkuu mpya wa Canterbury, Thomas Cranmer. Kanisa la Uingereza likakatisha uhusiano na kanisa la Roma, na mfalme akawa kiongozi wa kanisa la Uingereza. Cranmer akavunja ndoa ya Henry na Catherine katika mwaka wa 1533. Kufikia wakati huu tayari Henry alikuwa amemwoa Anne Boleyn, ambaye alikuwa mjamzito. Kuachiliwa huku kutoka kwa mamlaka ya kipapa kulikuwa na matokeo mabaya sana.
Cromwell alipewa mamlaka kubwa sana na alipaswa kujitiisha tu kwa mfalme. Hatua kwa hatua, makao ya watawa yalibomolewa na mali zao akapewa mfalme, zikitokeza fedha zilizohitajika sana. Kwa kuongezea, Cromwell alichangia sehemu kubwa katika kuchapishwa na kugawanywa kwa Biblia katika Kiingereza, kama A. G. Dickens asemavyo katika kitabu chake The English Reformation: “Hatua ya kwanza ya kisiasa, kupangwa kwa kichapo, gharama, mkazo wa kulazimisha Kanisa la Uingereza liichukue Biblia Kubwa, mambo haya yote yalitokana na naibu wa mfalme Thomas Cromwell.”
Kadiri Biblia ilivyopatikana zaidi na umma, ndivyo ilivyoathiri sana maoni ya watu kuhusu dini ya kidesturi. Dickens asema hivi: “Usahili halisi wa maisha za Yesu Kristo na Mitume ulitofautiana kabisa na utaratibu wenye sheria nyingi za kushurutisha, mali nyingi na majengo yenye fahari sana ya mwishoni mwa enzi ya kati na Kanisa la Marekebisho.”
Henry akataka kufanya marekebisho fulani ya kidini, lakini mara nyingi sera zake ziliongozwa na manufaa za kisiasa badala ya usadikisho wenye nguvu wa kidini. Alifahamu kabisa vikundi viwili vyenye kupingana kortini, vile vilivyopendelea marekebisho na vile vilivyotaka kudumisha dini ya kidesturi visivyopendelea marekebisho. Ili kudhibiti hali, kwa werevu angefanya kikundi kimoja kipinge kingine.
Kufikia mwaka wa 1540 muhula bora wa marekebisho ulivurugwa kwa muda na kuanguka kwa Cromwell. Maadui wake wasiopendelea marekebisho walimsadikisha Henry kwamba alikuwa msaliti na mzushi, na kwa hiyo akafishwa bila kufanyiwa kesi.
Kwa muda fulani, wasiopendelea marekebisho walionekana kana kwamba walidhibiti hali. Lakini hawakuweza kusimamisha marekebisho yaliyokuwa yameanza. Ijapokuwa hivyo, Marekebisho hayakutimiza lengo lake. Waprotestanti wa Marekebisho walikosa kung’oa mafundisho mengi ya uwongo ya wanadamu na mapokeo yaliyochafua dini ya Katoliki ya Kiroma.
Henry alipomwoa mke wake wa sita na wa mwisho, Catherine Parr, mwaka wa 1543, wale waliopendelea marekebisho walitiwa moyo. Alionyesha upendezi mkubwa katika mafundisho mapya ya kidini. Lakini wasiopendelea marekebisho waliamua kuendelea na pigano lao. Njama na mbinu zao mahakamani zingechochea malkia mpya apiganie uhai wake kufa na kupona. Jambo hili litazungumziwa katika toleo la wakati ujao la Amkeni!
[Picha katika ukurasa wa 26]
Henry wa Nane na Anne Boleyn
[Picha katika ukurasa wa 26]
Catherine wa Aragon
[Picha katika ukurasa wa 26]
William Tyndale
[Picha katika ukurasa wa 26]
Thomas Cromwell
[Picha katika ukurasa wa 26]
Thomas Cranmer
[Picha katika ukurasa wa 26]
Thomas Wolsey
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 27]
Thomas Wolsey: From the book The Story of Liberty, 1878; crest, background design, and King Henry VIII with Anne Boleyn: From the book The Library of Historic Characters and Famous Events, Vol. VII, 1895; Catherine of Aragon, Thomas Cranmer, and Thomas Cromwell: From the book Heroes of the Reformation, 1904