Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 11/8 kur. 20-22
  • Malkia Mwenye Busara Aliyemshinda Askofu Mwenye Hila

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Malkia Mwenye Busara Aliyemshinda Askofu Mwenye Hila
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Askofu Mwenye Hila
  • Ateswa Kwenye Chombo cha Kutesea
  • Malkia Mwenye Hekima na Busara
  • Marekebisho ya Uingereza Wakati wa Badiliko
    Amkeni!—1998
  • Sasa Wakiri Kutovumiliana Kidini
    Amkeni!—2000
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1999
  • “Sijawahi Kamwe Kuhisi Upendo Kama Huu”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 11/8 kur. 20-22

Malkia Mwenye Busara Aliyemshinda Askofu Mwenye Hila

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Afrika Kusini

AKIWA katika ushirika wa bibi wapambe, Malkia Catherine Parr wa Uingereza huhisi usalama. Ugonjwa wa Mfalme Henry wa Nane, kwa kuongezea maisha yenye hila ya nyumba ya mfalme, unamwathiri vibaya. Malkia huyo anapoongea na rafiki yake, mmoja wa wale bibi akimbia ndani, akiwa amebeba karatasi. Akiwa ameishiwa pumzi, ampokeza Catherine karatasi hiyo. Akiwa amefadhaishwa na uso uliokunjamana wa bibi wapambe, malkia huyo apokea karatasi hiyo kwa kusitasita. Yaonekana, iliangushwa kwa aksidenti na ofisa nje ya makao ya malkia.a

Anapoisoma, uso wa Catherine wabadilika rangi. Kutoamini kwake kwageuka kuwa ogofyo. Ni madai ya uzushi yaliyofanywa dhidi yake, na kutiwa sahihi na mfalme. Alia kwa sauti kubwa na kukaribia kuanguka chini lakini marafiki wamsaidia. Ajaribu kujituliza, kufikiri waziwazi, lakini amevurugika sana. Kwa rehema, bibi wapambe wamsaidia kujilaza kitandani.

Ajilaza chini, lakini ashindwa kupumzika. Akijipinduapindua, apitia matukio ya ndoa yake na Mfalme Henry wa Nane. Alikuwa na umri wa miaka 31, akiwa ameolewa mara mbili na kuwa mjane, na alikuwa akifikiria kuolewa na Thomas Seymour mwenye tabia nzuri. Lakini mfalme alikuwa na mipango mingine. Alipendekeza kumwoa. Angewezaje kukataa? Kwa kweli ilikuwa jambo la kujivunia, lakini lililojaa matatizo. Akawa mke wake wa sita mnamo Julai 12, 1543.

Henry hakuwa tena yule mtu mwenye tabia nzuri, mwenye kupenda michezo ya farasi kama alivyokuwa wakati wa ujana wake. Akiwa na umri wa miaka 52, alikuwa mnene kupita kiasi, akiwa mwenye kubadilika-badilika tabia, na alikuwa na vidonda miguuni pake ambavyo nyakati fulani vingemfanya asiweze kutembea na ahitaji kusukumwa akiwa kwenye kiti.

Na bado, Catherine alitumia akili na vipawa vyake kwa kadiri kubwa ili kufanya ndoa yao ifanikiwe. Akawa karibu na watoto watatu wa mfalme wa ndoa zilizotangulia. Alijaribu sana kuwa mama mwenye kuburudisha. Mfalme alipoumwa miguu, malkia huyo alikengeusha fikira zake kwa mazungumzo machangamfu, mara nyingi yaliyohusu mambo ya kidini. Alimpa mfalme utulivu wa kiasi fulani katika miaka yake ya baadaye.

Sasa anajaribu kukumbuka maisha yake akiwa pamoja na mfalme. Alikosea katika jambo gani? Afikiri juu ya mkutano aliokuwa nao pamoja naye hivi majuzi. Jioni hiyo baadhi ya watumishi wake walikuwepo, na alionekana akiwa katika hali yenye furaha. Kama ilivyokuwa desturi yake, malkia alizusha swali la kidini walilokuwa wamelizungumzia hapo awali. Mfalme akawa mwenye kiherehere akamkatisha kwa ghafula. Malkia alishangazwa na hali hiyo lakini akaipuuza tu kuwa tabia yake ya kubadilika-badilika. Kwa kawaida alifurahia mazungumzo hayo na hakupinga kupendezwa kwake na mambo ya kidini.

Malkia akumbuka ni nani aliyekuwako katika pindi hiyo. Mawazo yake yarudi kwa mtu mmoja mara zote—adui ajulikanaye, Stephen Gardiner.

Askofu Mwenye Hila

Gardiner, askofu wa Winchester na pia mshiriki wa baraza la mfalme ni mtu mwenye uvutano na mpinzani wa marekebisho ya kidini. Anamchukia Catherine, kwa sababu ya kupendezwa na mabadiliko ya kidini na kwa uvutano wake kwa mfalme.

Mshauri mkuu wa Henry, Thomas Cromwell, alipomng’oa Gardiner katika cheo chake cha katibu mkuu wa mfalme, Gardiner alitafuta fursa ya kulipizia kisasi. Alishiriki njama zilizomwangusha Cromwell na kumuua. Gardiner alifadhaika pia kwa sababu Henry alikuwa amempuuza na kumteua Thomas Cranmer, aliyependelea Waprotestanti, kuwa Askofu Mkuu wa Canterbury. Cranmer akaponea chupuchupu wakati Henry alipoharibu njama iliyokuwa imefanywa dhidi yake na Gardiner na wengineo.

Hatari kwa Catherine na bibi wenzake katika jumba la mfalme ilizidishwa na njama nyingine ya karibuni ya Askofu Gardiner. Mwanamke mmoja mchanga, Anne Askew, alikuwa mtetezi asiyeogopa wa marekebisho ya kidini. Alikuwa gerezani, akisubiri kuuawa kwa sababu ya uzushi. Lakini Gardiner alipendezwa naye kwa sababu tofauti. Alitaka uthibitisho wa kwamba mwanamke huyo alikuwa na uhusiano na mabibi waliokuwa na uvutano katika nyumba ya mfalme, jambo ambalo pia lingemhatarisha malkia. Mwenzi wa Gardiner, Thomas Wriothesley, mmojawapo wa washiriki mashuhuri wa baraza la mfalme, alienda kumhoji Anne Askew.

Ateswa Kwenye Chombo cha Kutesea

Wriothesley alimhoji Anne kwa muda fulani, lakini hakupata uthibitisho wa kumhusisha malkia aliohitaji. Hatimaye, aliamuru mwanamke huyo afungwe kwenye chombo cha kutesea watu,b ijapokuwa ilikuwa kinyume cha sheria kutesa mwanamke kwa kutumia chombo hicho. Mateso hayo yaliposhindwa kumfanya Anne aongee, Wriothesley na diwani mwingine walitumia chombo hicho cha kutesea wao wenyewe na kumvuta hadi kikomo, lakini bado hawakupata habari walizotaka.

Kuteseka kwa Anne Askew kwamfanya Catherine atokwe na machozi. Anajua kwamba mtu fulani ameingia chumbani. Mojawapo wa bibi hao anamfikia na kumwambia kwamba tabibu wa mfalme, Dakt. Wendy, ametumwa na mfame kumpima. Daktari huyo mwenye fadhili auliza jinsi anavyohisi na kwamba mfalme amtakia afya njema.

Daktari aeleza jinsi mfalme alivyomwambia kwa faragha njama dhidi yake na kumwambia asimwambie mtu yeyote. Hata hivyo, Dakt. Wendy amwambia mambo yote—kwamba baada ya malkia kumwacha mfalme usiku huo, mfalme alikejeli kwa kusema kwamba ilimfariji sana katika umri wake wa uzee “kufundishwa na mke [wake].”

Gardiner aliona fursa hii na kuitwaa. Alisema kwamba malkia aliwaficha wazushi na kwamba matendo yake yalikuwa ya uhaini, yakitisha mamlaka ya mfalme. Alisema kwamba akipewa muda, yeye pamoja na wengine wangetoa uthibitisho mbele ya mfalme. Mfalme aliyekasirika alikubali kutia sahihi mswada wa vifungu dhidi yake.

Baada ya kutaja matukio haya, Dakt. Wendy amhimiza aende kwa mfalme haraka iwezekanavyo na kuomba msamaha wake kwa unyenyekevu. Hii ndiyo njia pekee ya kuwashinda akili maadui wake, ambao hawatapumzika mpaka atakapofungwa jela katika Mnara wa London mpaka wawe na uthibitisho wa kutosha kumhukumia kifo.

Catherine aona shauri hili kuwa lenye hekima, na usiku mmoja, anaposikia kwamba mfalme yumo chumbani mwake, avalia kwa makini na kufanya mazoezi ya mambo atakayosema. Aandamana na dada yake na rafiki yake mmoja, Bibi Lane.

Malkia Mwenye Hekima na Busara

Mfalme ameketi na anafanya mzaha na baadhi ya watu wakuu. Amkaribisha mke wake kwa tabasamu. Kisha abadili mazungumzo kuwa mambo ya kidini. Amwomba Catherine atatue shaka alizo nazo juu ya mambo fulani. Catherine aona mtego huo mara moja. Ajaribu kadiri awezavyo kuitikia kwa weupe wa moyo na kwa unyoofu.

Asema kwamba Mungu alimwumba mwanamke baada ya mwanamume—akiwa wa hali ya chini kwake. Aendelea: ‘Kwa kuwa basi Mungu ameweka tofauti hiyo ya kiasili kati ya mwanamume na mwanamke, na wewe mtukufu ukiwa na hekima bora na mimi nikiwa wa hali ya chini sana katika mambo yote, inawezekanaje basi wewe mtukufu, katika mambo hayo ya kidini yaliyo tata, ukataka uamuzi wangu?’ Kisha akiri kwamba yeye ni kichwa chake katika mambo yote, akiwa wa pili tu baada ya Mungu.

‘Sivyo,’ ajibu mfalme. ‘Umekuwa mwalimu wa kutuagiza na si sisi kukuagiza au kukuongoza.’

Malkia ajibu: ‘Ikiwa wewe mtukufu waona hivyo, basi mtukufu umenichukulia vibaya sana, ni nani amepata kufikiri kwa njia isiyofaa, na isiyo na maana, kwa mwanamke kuchukua wadhifa wa mkufunzi au mwalimu wa bwana na mume wake; lakini badala yake kujifunza kutoka kwa mume wake na kufundishwa naye.’ Azidi kuelezea kwamba aliposema naye kuhusu mambo ya kidini na nyakati fulani akaeleza maoni fulani, haikuwa kuendeleza mawazo yake. Badala yake, kwa kuzungumza naye, alitumaini kuondosha fikira zake kutokana na maumivu aliyohisi kwa sababu ya ugonjwa wake.

‘Je, ndivyo ilivyo Mpenzi?’ asema mfalme. ‘Je, hukuelekeza hoja zako ili utimize lengo fulani bovu? Basi sasa tu marafiki wema tena, kama ambavyo hatujapata kuwa hapo awali.’ Akiwa ameketi bado, amwita aje karibu naye, amkumbatia kwa uchangamfu, na kumbusu. Asema kwamba kusikia habari hizi ni bora kuliko kupata kwa ghafula zawadi ya pauni elfu mia moja. Wanaendelea na mazungumzo yenye kupendeza mpaka anapompa idhini ya kuondoka karibu usiku wa manane.

Siku iliyofuata mfalme aenda matembezi ya kawaida katika bustani ya kifalme, akiandamana na wakuu wawili wa chumba cha kulala. Amemwita malkia ajiunge naye, na atokea kwa wakati wake pamoja na baadhi ya mabibi zake watatu. Henry amekosa kumwambia Catherine kwamba huu ndio wakati uliokubaliwa hapo kwanza wa kumkamata. Pia amekosa kumwambia Wriothesley, aliyepaswa kumkamata, juu ya upatanisho wake na malkia. Wanapojifurahisha, Wriothesley atokea akiwa pamoja na walinzi 40 wa mfalme ili kumkamata malkia pamoja na mabibi zake.

Henry ajitenga na kikundi hicho na kumwita Wriothesley, anayepiga magoti mbele za mfalme akisihi. Watu wengineo hawawezi kusikia anayosema mfalme, lakini wanamsikia akitamka kwa hasira maneno, ‘Mlaghai! Hayawani! Mpumbavu!’ Amwamuru Wriothesley aondoke mbele zake.

Mfalme anaporudi, Catherine ajaribu kumtuliza kwa maneno ya upole. Hata anazungumza kwa niaba ya Wriothesley, akisema kwamba lolote ambalo amefanya laweza kuwa limefanywa kimakosa.

Mfalme ajibu kwa kusema: ‘Nakuhakikishia, Mpenzi, amekuwa mlaghai wa kupindukia kukuelekea, kwa hiyo mwache aende.’

Basi, Catherine aliokolewa kutoka kwa maadui wake, na Askofu Gardiner akapoteza upendeleo wa mfalme. Malkia alikuwa amemshinda askofu mwenye hila. Mzozo ukaisha.c

[Maelezo ya Chini]

a Simulizi hili la kubuniwa lategemea vyanzo mbalimbali, kutia ndani Foxe’s Book of Martyrs.

b “Chombo cha kutesea chenye fremu yenye magurudumu ambayo vifundo vya mikono na miguu ya mtu vilifungwa hivi kwamba viungo vyake vilivutwa magurudumu yalipozungushwa.”—Oxford Advanced Learner’s Dictionary.

c Catherine Parr aliishi kwa muda mrefu kuliko Henry na hatimaye aliolewa na Thomas Seymour. Alikufa mnamo 1548, akiwa na umri wa miaka 36, muda mfupi tu baada ya kujifungua. Baada ya kukaa gerezani kwa muda fulani katika Mnara wa London, Gardiner alinyang’anywa uaskofu katika mwaka wa 1550. Alipata upendeleo chini ya Mkatoliki Mary wa Kwanza (1553) akafa mwaka wa 1555.

[Picha katika ukurasa wa 21]

Malkia Catherine Parr

Askofu Stephen Gardiner

Picha ya Catherine Parr: By courtesy of the National Portrait Gallery, London; Stephen Gardiner: National Trust Photographic Library/J. Whitaker

[Picha katika ukurasa wa 22]

Henry wa Nane Amshtumu Thomas Wriothesley mbele za malkia

[Hisani]

Portrait by Holbein, from the book The History of Protestantism (Vol. III)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 20]

Mandarinyuma kwenye ukurasa wa 20-22: From the book The Library of Historical Characters and Famous Events, Vol. 3, 1895

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki