Krismasi Mambo ya Kweli au Ngano?
“UKIULIZA Wakatoliki waaminifu kwa nini Krismasi husherehekewa Desemba 25, angalau tisa kati ya kumi, wengine wakishangaa na wengine wakichekeshwa, watajibu: ‘Hiyo ndiyo siku Yesu alizaliwa!’ Hata hivyo, ukiuliza mmoja wa Mashahidi wa Yehova sababu kwa nini yeye haadhimishi sherehe hiyo, yeye kama kawaida atakujibu: ‘Ni kwa sababu haijatajwa katika Gospeli.’”
Hivyo ndivyo makala moja kuhusu Krismasi ilivyoanza katika gazeti la kila siku la Naples, Italia, liitwalo Il Mattino. Lakini ni maoni gani yaliyo sahihi? “Lile unalohitaji kufanya,” gazeti hilo liliongezea, “ni kufungua-fungua tu kurasa za Mathayo na Luka nzima (ndio waevangeli wawili tu wanaozungumzia Uzaliwa wa Kristo) na kutambua kwamba jibu la pili ndilo sahihi.”
Makala kama hizo si jambo lisilo la kawaida tena. Vyombo vya habari mara nyingi hufunua itikadi za Krismasi zinazoshikiliwa na wengi kuwa ni ngano. Kwa mfano, katika Desemba 1990, gazeti The Press, la Christchurch, katika New Zealand, lilikuwa na makala “Ngano Sita za Krismasi.” Hilo lilisema:
“NGANO YA 1. Baba Krismasi, anayeishi katika Ncha ya Kaskazini mwa dunia, huenda huku na huku duniani katika Mkesha wa Krismasi ili kutoa zawadi kwa wasichana na wavulana wazuri. Hakuna yeyote anayependa kuharibu jambo lenye kufurahisha, lakini jambo hilo si kweli, ama sivyo? Nyumba nyingi hivyo kwa usiku mmoja, keki ya matunda na divai nyekundu nyingi hivyo? Na hutukia nini iwapo hakuna bomba la kutokea moshi? La, hadithi hiyo si ya kweli. . . .
“NGANO YA 2. Desemba 25 ndiyo siku ya kuzaliwa kwa Kristo. Haiwezekani. Gospeli ya Luka husema kwamba Yesu alipozaliwa Bethlehemu, wachungaji walikaa nje na kulinda mifugo yao usiku. Katika sehemu hiyo ya Palestina hali-joto katika Desemba huwa wastani wa digrii 7 Sentigredi wakati wa mchana na baridi zaidi wakati wa usiku. Kunakuwako mvua ya baridi ya mara kwa mara, wakati mwingine barafu kwenye sehemu za milimani. Wachungaji hao wangalikuwa pale ambapo kondoo zao huwa nyakati zote wakati huo wa mwaka—nyumbani. . . .
“NGANO YA 3. Krismasi ya kwanza ilikuwa Bethlehemu, Kristo alipozaliwa. Kwa kweli mwanzo wayo unaonekana ulikuwa Roma, rekodi ya mapema zaidi ya mwadhimisho wayo ikiwa katika mwaka 336. Ilienea kotekote Mashariki na Magharibi hadi ilipoingizwa kwenye Kanisa la Yerusalemu katikati ya karne ya 5.
“Kwa njia fulani, mwanzo wa Krismasi kwa kweli ulikuja kwa viwango vidogo-vidogo na ilikuwa tu kubadilika kwa jina la mwadhimisho huo: sherehe na karamu za kipagani zinazofanana nayo zilikuwa zinafanywa mwishoni mwa Desemba kwa karne nyingi kabla ya Kristo zikiwa sehemu ya sherehe za kipupwe ambapo jua limefikia ukomo upande wa kizio cha kaskazini . . .
“Kukubaliwa kwa uzaliwa wa Kristo katika sherehe hizo zenye msingi wa kipagani hakukupata upinzani kutoka kwa viongozi wa makanisa, walioonekana kuwa hawapendezwi sana na ukweli au usafi wa mafundisho kuliko uwezekano wa kuongeza wafuasi wao na hivyo waongeze uwezo wao pia. . . .
“Haishangazi sana basi kwamba Wapuriti wa Skotlandi, Uingereza na New England walijitahidi kukomesha Krismasi wakati wa karne ya 17, wakiishutumu kuwa mwendelezo wa ‘ubatili na kukosa kiasi ambako wasiojua Mungu hufuatilia.’
“Kwa hiyo vilio hivyo vya kila mwaka vya ‘kumrudisha Kristo kwenye Krismasi’ huwa kwa kweli havina maana: ukweli ni kwamba, yeye kwa hiari yake hakuwa kamwe sehemu yake.
“NGANO YA 4. Desturi ya kupeana zawadi wakati wa Krismasi hufuata zoea lililoanzishwa na zawadi alizopewa Yesu za dhahabu, uvumba na manemane. Kwa kweli watu walikuwa wamekuwa wakibadilishana zawadi Desemba 25 na 26 kwa karne nyingi kabla ya Kristo zikiwa sehemu ya sherehe hizo za jua. Warumi wa kale walibadilishana zawadi kama sehemu ya sherehe ya ibada ya jua, iitwayo Saturnalia.
“Kwa vyovyote Wanajimu walimpa Yesu zawadi, si wao wenyewe, kulingana na desturi ya wakati huo, wakati mtu alipotembelea watu mashuhuri. Kwa vyovyote, gospeli ya Mathayo inaonyesha kupendezwa kwao na Yesu kulikuwa ni yeye akiwa mfalme wa Wayahudi wa wakati ujao.
“NGANO YA 5. Wale ‘wanajimu watatu’ na wachungaji walimsujudia Yesu akiwa katika hori. Wowote wanaochora picha za mandhari za kuvutia za uzaliwa wa kristo zikionyesha wachungaji na wanajimu wakiwa pamoja kwenye zizi la ng’ombe huwa hawasomi Biblia zao vizuri.
“Gospeli ya Mathayo inasema wazi kwamba kufikia wakati ‘wanajimu’ walipompata Yesu, yeye alikuwa nyumbani—na inafaa hivyo, kwa sababu huenda ilikuwa miaka miwili hivi baada ya kuzaliwa kwake.
“Isitoshe, Mathayo anapoelezea ziara ya Wanajimu, anazungumzia Yesu kuwa mtoto, si kitoto. Alikuwa amekwisha acha kutumia nguo za kitoto na wachungaji walikuwa wamerudia mifugo yao zamani.
“Fikiria, pia, kwamba wakati Herode alipotafuta kumwua Mesiya, alitumia tarehe aliyopewa na Wanajimu na akaagiza kwamba watoto wote wanaume wa kufikia umri wa miaka miwili wauawe.
“Je! angelitoa agizo hilo [la] kukirihisha—licha ya kwamba halikupendwa na wengi—kama angelijua kuwa yule aliyewinda alikuwa mwenye umri wa majuma machache tu? . . .
“Kwa kweli Biblia haidokezi mahali popote ni wanajimu wangapi waliokuwako. Neno la Kigiriki katika gospeli ni magoi, ambalo jina [la Kiingereza] ‘magic’ [‘mizungu’] linatokana. . . .
“NGANO YA 6. Krismasi ni wakati wa amani duniani na hali njema kwa watu wote. Ni wazo zuri kweli kweli, lakini Biblia haisemi hivyo. . . .
“Tafsiri za Interlinear za gospeli ya Luka katika Kigiriki cha awali huonyesha kwamba yale hasa yaliyosemwa na halaiki ya malaika waliowatokea wachungaji ni: ‘na duniani iweko amani miongoni mwa watu wa nia njema’.
“Na hiyo ndiyo tofauti iliyoko. Siku moja kwa mwaka ya kulewa pombe chakari, na kula kupindukia inayofanyiwa biashara nyingi sana haimfanyizi Mkristo; amani, Biblia husema, haiji kwa wale wanaosherehekea siku ya kuzaliwa kwa Yesu isiyo ya kweli, hiyo huja kwa wale wanaofuata mafundisho yake—mwaka mzima.”