Wanawake Je! Wanastahiwa Kazini?
“Iwe walikuwa waseja au walikuwa wameolewa, wanaume wengi waliwaona wanawake kuwa vyombo vya kuchezea.”—Jenny, aliyekuwa sekretari wa sheria.
“Udhia wa kingono na kutendwa vibaya kwa wanawake katika hospitali ni jambo la kawaida.”—Sarah, mwuguzi aliyeidhinishwa.
“Nilitongozwa-tongozwa daima nikiwa kazini, yaani, kubembwa ili kufanya yasiyo ya kiadili.”—Jean, mwuguzi aliyeidhinishwa.
JE! VISA hivyo huwakilisha hali zisizo za kawaida, au ni vyenye kuenea? Amkeni! lilihoji wanawake kadhaa ambao wamejionea wenyewe hali ya kazini. Je! walistahiwa na kutendewa kwa adabu na wafanya kazi wenzao wa kiume? Haya ndiyo yaliyokuwa baadhi ya maelezo yao:
Sarah, mwuguzi wa kike kutoka New Jersey, U.S.A., mwenye ujuzi wa miaka tisa katika hospitali za kijeshi za U.S.: “Nakumbuka wakati nilipofanya kazi katika San Antonio, Texas, na nafasi ya kazi ikatokea katika Idara ya Dialisisi ya figo. Niliuliza kikundi cha madaktari jambo ambalo ningepaswa kufanya ili nipate kazi hiyo. Mmoja alijibu kwa kuchekelea, ‘Lala na mkubwa wa madaktari.’ Nilisema tu, ‘Ikiwa ni hivyo sitaki hiyo kazi.’ Lakini hiyo mara nyingi ndiyo njia ambayo kupandishwa cheo na kupata kazi huamuliwa. Mwanamke analazimika kujiweka chini ya mwanamume mkuu mwenye ashiki.
“Katika pindi nyingine, nilikuwa nikifanya kazi katika wodi ya utunzaji wa dharura nikimtia mgonjwa dawa ya kutiwa mishipani wakati daktari alipokuja na kunifinya sehemu yangu ya nyuma. Nilikasirika sana nikatoka kwa kishindo hadi chumba cha karibu. Alinifuata na kuniambia jambo lisilo la adabu. Nilimpiga kwa nguvu akaanguka ndani ya pipa. Nikarudi moja kwa moja kwa mgonjwa wangu. Bila shaka hakuniudhi tena kamwe!”
Miriam, mwanamke aliyeolewa kutoka Misri ambaye hapo awali alikuwa sekretari katika Cairo, alieleza hali ya wanawake wafanyao kazi katika mazingira ya Kiislamu katika Misri. “Wanawake hujivalia kwa njia yenye kiasi kuliko katika jamii ya Magharibi. Sikuona udhia wowote wa kingono kazini mwangu. Lakini kuna udhia wa kingono katika reli za chini za Cairo hivi kwamba wanawake wamewekewa behewa la kwanza.”
Jean, mwanamke mnyamavu lakini mwenye kuazimia akiwa na ujuzi wa miaka 20 akiwa mwuguzi wa kike, alisema: “Nilifuata sera thabiti ya kutofanya urafiki na mtu yeyote kazini. Lakini udhia ulitokea iwe nilikuwa nikifanya kazi na madaktari au watumishi wa kiume. Wote walifikiri walinishinda kiakili. Ikiwa sisi wauguzi wa kike ‘hatungeshirikiana’ nao katika tamaa zao za ngono, basi watumishi hao hawangetusaidia tulipohitaji msaada wa kuinua mgonjwa kitandani na mambo kama hayo.”
Jenny alifanya kazi akiwa sekretari wa sheria kwa miaka saba. Anaelezea aliyojionea alipokuwa akifanya kazi na mawakili. “Iwe walikuwa waseja au wameolewa, wanaume wengi waliwaona wanawake kuwa vyombo vya kuchezea. Mtazamo wao ulikuwa, ‘Tukiwa mawakili tunastahili yote, na wanawake ni mojawapo mapendeleo yetu.’” Na uthibitisho waonyesha kwamba wastadi wengine wa kazi wana maoni kama hayo. Lakini mwanamke aweza kufanya nini ili kupunguza udhia?
Darlene, Mwamerika mweusi aliyefanya kazi akiwa sekretari na mkaribishaji katika mkahawa, alisema: “Mambo yanaweza kuharibika ukishindwa kujiwekea mipaka yako mwenyewe ya mwenendo. Mwanamume akianza kukutania na wewe umtanie pia, basi mambo yaweza kupita kiasi kwa urahisi. Nimelazimika kueleza msimamo wangu waziwazi katika pindi tofauti-tofauti. Nimetumia maneno kama, ‘Ningethamini ikiwa usingeniambia maneno hayo.’ Katika pindi nyingine nilisema: ‘Nikiwa mwanamke aliyeolewa, naona yale uliyosema kuwa yenye kuudhi, na sifikiri mume wangu angependa hilo.’
“Jambo la maana ni kwamba, ikiwa unataka staha, ni lazima uistahili. Na sioni jinsi ambavyo mwanamke aweza kustahili staha ikiwa anajaribu kushindana na wanaume katika yale ninayoita maongezi ya kimchezo yasiyo na adabu na madokezo ya ngono. Usipoweka mpaka wa wazi kati ya maongeo na mwenendo unaokubalika na usiokubalika, basi mtu fulani atajaribu kuuvuka.”
Yule Mwanamume Mwenye Kuonea Sana
Connie, mwuguzi wa kike mwenye ujuzi wa miaka 14, alieleza namna nyingine ya udhia iwezayo kutokea katika hali nyingi. “Nilikuwa nikifanya kazi na daktari mmoja katika kazi ya kawaida ya kufunga majeraha. Nilifuata taratibu zote za kawaida nilizokuwa nimejifunza. Najua yote kuhusu njia ya kuondoa vijidudu vyote, na kadhalika. Lakini kwa daktari huyo hakuna kilichokuwa sawa. Alinifokea na kunighadhibikia na kuchambua kila nilichofanya. Jambo hilo, la kushusha wanawake, hutukia mara kwa mara. Wanaume wengine wana tatizo la kujiona, na inaonekana wanataka kulazimisha mamlaka yao juu ya wanawake wanaofanya kazi pamoja nao.”
Sarah aliyenukuliwa awali, aliongezea yale aliyojionea mwenyewe kuhusu hilo: “Nilikuwa nikifanya matayarisho kwa ajili ya upasuaji nilipoangalia dalili kuu za mgonjwa mmoja. Rekodi yake ya EKG [elektrokadiogramu] ya kuchunguza pigo la moyo ilikuwa ikigeukageuka sana hivi kwamba nilijua hakuwa katika hali ya kupasuliwa. Nilifanya kosa la kumjulisha daktari mpasuaji jambo hilo. Alikasirika wee, na itikio lake lilikuwa: ‘Wauguzi wanapaswa kushughulikia vyombo vinavyotumika kwendea choo kitandani, si EKG.’ Kwa hiyo nilimjulisha tu daktari-nusukaputi, naye akasema kwamba chini ya hali hizo watu wake hawangeshirikiana na huyo daktari mpasuaji. Halafu huyo daktari mpasuaji akageuka na kumwambia mke wa mtu huyo kwamba ninapaswa kulaumiwa kwa sababu ya mume wake kukosa kupasuliwa! Katika hali hiyo mwanamke hawezi kushinda. Kwa nini? Kwa sababu bila kukusudia ameumiza hisia ya kiume.”
Ni wazi kwamba, wanawake mara nyingi hutendwa kwa udhia na mwenendo wa kushushiwa staha kazini. Lakini msimamo wao ni upi mbele ya sheria?
Wanawake na Sheria
Katika nchi fulani imechukua karne nyingi kwa wanawake kupata hata usawa kinadharia chini ya sheria. Na mahali ambako sheria inataja usawa huo pengo kubwa hutenga nadharia na matendo.
Kichapo cha UM The World’s Women—1970-1990 chasema: “Sehemu kubwa ya pengo hilo [pengo la sera ya kiserikali] imetiwa ndani ya sheria zinazowanyima wanawake usawa na wanaume katika haki zao za kumiliki ardhi, kukopa pesa na kuingia katika kondrati.” Kama vile mwanamke mmoja kutoka Uganda alivyosema: “Tunaendelea kuwa raia wa cheo cha chini—la, cheo cha chini kabisa, kwa kuwa wana wetu hututangulia. Hata nyakati nyingine punda na matrekta hutendwa vizuri.”
Kichapo Time-Life Men and Women chasema hivi: “Katika 1920, Marekebisho ya 19 ya Katiba ya United States yalihakikishia wanawake haki ya kupiga kura—muda mrefu baada ya wao kupewa haki hiyo katika nchi nyingi za Ulaya. Lakini kupiga kura huko hakukuruhusiwa katika Uingereza hadi 1928 (na baada ya vita vya 2 katika Japani).” Ili kupinga ukosefu wa haki ya kisiasa kwa wanawake, mwanamke Mwingereza aliyekuwa mteteaji wa haki za wanawake za kupiga kura, Emily Wilding Davison, alijitupa mwenyewe mbele ya farasi wa Mfalme katika mbio za farasi za 1913 na akauawa. Akafa kwa sababu ya haki za usawa kwa wanawake.
Uhakika wa kwamba baadaye sana kufikia mwisho wa 1990, ndipo Bunge la U.S. lilifikiria ile “Sheria Inayopinga Jeuri kwa Wanawake” huonyesha kwamba watungaji sheria ambao wengi ni wanaume wamefanya polepole kuitikia mahitaji ya wanawake.
Mambo hayo machache juu ya jinsi wanawake wanavyotendwa ulimwenguni pote yatuongoza kwenye swali, Je! mambo yatakuwa tofauti wakati wowote? Ni nini linalohitajiwa ili hali ibadilike? Makala mbili zifuatazo zitazungumzia maswali hayo.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]
Ni Nani Walio Katika Hali Mbaya Zaidi?
“Wanawake hufanya theluthi mbili za kazi ya ulimwengu. Wao hutokeza asilimia 60 hadi 80 ya chakula cha Afrika na Esia, asilimia 40 ya chakula cha Amerika ya Latini. Hata hivyo wao huchuma sehemu moja kwa kumi ya mapato ya ulimwengu na kumiliki chini ya asilimia moja ya mali ya ulimwengu. Wao ni miongoni mwa walio maskini zaidi kati ya maskini wa ulimwengu.”—May You Be the Mother of a Hundred Sons, cha Elisabeth Bumiller.
“Uhakika ni kwamba wasichana wadogo hawaendi shuleni [katika sehemu nyingine za ulimwengu] kwa sababu hakuna maji safi ya kunywa. . . . Nimeona wasichana wabalehe wakichota maji ya kunywa kutoka umbali wa kilometa ishirini hadi thelathini, jambo ambalo huchukua siku nzima. Kufikia wakati wana umri wa miaka kumi na minne au kumi na mitano, wasichana hawa . . . hawajapata kamwe kwenda shuleni, hawajapata kamwe kujifunza kitu chochote.”—Jacques-Yves Cousteau, The Unesco Courier, Novemba 1991.
[Picha katika ukurasa wa 22]
Udhia wa kingono haupaswi kuvumiliwa