Kuutazama Ulimwengu
Vifo vya Kileo Katika Japan
The Daily Yomiuri yaripoti kwamba visa vya kutiwa sumu sana na kileo vimeongezeka kwa kutazamisha katika Japan hivi karibuni. Jambo moja lenye kutokeza hilo: kuanzishwa tena kwa ikkinomi, au kukugumiza—yaani, kunywa kileo kwa pupa bila kituo. Mara nyingi hilo hutukia chini ya msongo au hata kwa kulazimishwa na umati wa watazamaji wanaochochea na kumshangilia mnywaji aendelee. Mtindo huo ulikuwa ni kama umekwisha, kisha ukatokea tena mwaka jana. Miyako Omoto, profesa msaidizi katika shule ya tiba ya Chuo Kikuu cha Toho, analinganisha kule kumlazimisha mtu agugumize kileo na kujaribu kumwua kimakusudi. Yeye alisema: “Ikkinomi ni hatari kwa sababu mtu hunywa kileo zaidi ya kiasi ambacho mwili wake waweza kushughulikia kabla ya mwili wake kuanza kutoa ishara ya kuonya.” Idara ya Wazima-Moto ya Tokyo inasema kwamba ilibidi watu 9,122 wapelekwe kwenye hospitali wakiwa wametiwa sumu sana na kileo katika 1991—ongezeko la asilimia 8 kupita mwaka uliopita. Sita kati yao walikufa.
Majirani Wasiovumilia
Ni nani ambaye hungependa awe jirani yako wa karibu? Kikundi cha Utafiti wa Mifumo ya Tabia ya Ulaya kilizusha swali hilo kwa watu 20,000 katika nchi 14 katika jitihada ya kujua hofu na chuki za kawaida. “Nchi yenye uvumilio zaidi ni Denmark,” lasema The European, hali Ureno iliripotiwa kuwa yenye uvumilio mdogo zaidi. Kuhusu majirani wenye UKIMWI, watu katika nchi zenye Wakatoliki wengi kama Italia, Uhispania, na Ailandi walionyesha chuki sana hali Wabelgiji walionyesha kutovumilia rangi na dini tofauti. Wajerumani walichukia kuwa na majirani wenye siasa kali. Wanaume na wanawake walionyesha tofauti ndogo kwa habari ya kutovumiliana. Lakini jambo moja lilionekana kuwa likishirikishwa na kutovumiliana katika nchi zote—umri. Watu wazee kwa kawaida walikuwa wateuzi zaidi kuhusu wale waliopenda wawe majirani wao.
Hesabu ya Simba-Marara Inapungua
Mojawapo hifadhi mashuhuri ya wanyama ya India inapoteza simba-marara wake wa Bengal walio wachache, laripoti gazeti New Scientist. Hesabu ya hivi karibuni katika hifadhi ya Ranthambhor ilipata simba-marara 15 pekee—kutoka kwa 44 miaka mitatu tu iliyopita. Bila kushangaza, tatizo ni uwindaji haramu. Lakini siku hizi wawindaji haramu wanataka zaidi ya ngozi zenye kuvutia. Mifupa ya simba-marara hutumiwa kutengenezea “divai ya mfupa wa simba-marara,” ambayo inapendwa na wengi ikiwa dawa katika nchi fulani za Esia. Wawindaji haramu kwa kawaida huua simba-marara kwa chambo chenye sumu, nyakati nyingine wakifagilia mbali wanasimba pamoja na mama simba-marara. Jambo lililo kinyume ni kwamba, hapo mbeleni hifadhi ya Ranthambhor ilikuwa wonyesho wa Mradi wa Simba-Marara—jitihada ya uhifadhi iliyofanyizwa ili kuokoa simba-marara wa Bengal asiangamie. Wote pamoja, kuna kadirio la wanyama hao wenye kupendeza 6,000 hadi 9,000 tu waliobakia duniani.
Kuvuta Sigara na Mifupa Iliyovunjika
“Siku imefika ambapo hata wataalamu wa mifupa watawaagiza wagonjwa wao waache kuvuta sigara,” laripoti gazeti la Brazili Folha de S. Paulo. Uchunguzi wa watu 29 waliovunjika mifupa ulifunua kwamba nikotini kutoka kwa moshi wa tumbaku ilifanya mishipa ya damu ya wavutaji wazoevu idhoofike zaidi. Kwa kutofautisha, wale wasiovuta sigara na wale ambao hawakuwa wamevuta kwa zaidi ya miaka miwili walikuwa na mishipa ya damu iliyokuwa na uwezo bora wa kupungua na kutanuka, jambo linalosaidia mivunjiko ipone upesi. Kwa wastani, mivunjiko ya wale wasiovuta sigara ilipona kwa asilimia 28 upesi zaidi ya wale walio wavutaji wa muda mrefu. Pia, kuvuta kaboni monoksaidi wakati wa kuvuta sigara hupunguza kuenea kwa oksijeni, hivi kwamba mfupa uliovunjika hupokea lishe ndogo.
Ugonjwa wa Chaga Waenea
Shirika la Afya Ulimwenguni laripoti kwamba watu milioni 18 hivi katika Amerika ya Latini wameambukiwa kimelea kinacholeta ugonjwa wa Chaga, unaoweza kuleta ugonjwa mbaya wa moyo na hata kifo. Jumla ya watu milioni 90—asilimia 25 ya watu wote—katika nchi 17 za Amerika ya Latini wamo katika hatari ya kuambukiwa ugonjwa huo, kulingana na gazeti la Bolivia El Diario. Mdudu anayejulikana sana kuwa mdudu kibusu mara nyingi hueneza ugonjwa huo. Notícias Bolivianas hupendekeza kupaka kuta zote chokaa, kuweka wanyama wote katika mazizi ya nje badala ya ndani ya nyumba, na kusafisha sana nyumba ili kuondoa wadudu wenye kubeba ugonjwa. Kuhusu mitio ya damu mishipani, jarida ilo hilo lasema kwamba asilimia 47.6 yayo huwa na hatari ya kuambukiza ugonjwa wa Chaga. Linamalizia hivi: “Kujiepusha na damu kunapendekezwa kupatana na amri ya Kibiblia.”
Ndege Walio Hatarini
Kati ya aina za ndege 273 wanaotaga mayai Ujerumani, 166 wamo hatarini, Shirika la Uhifadhi la Ujerumani ladai. Sababu zinasemwa kuwa ni kumalizwa kwa ardhi iliyoko kwa kujengwa barabara, viwanda, ukulima mwingi, na utalii. Gazeti Frankfurter Allgemeine Zeitung laripoti kwamba hata ingawa maziwa mengi ya maji, mito, na sehemu zenye unyevu katika Ujerumani zimetangazwa kuwa sehemu zinazolindwa, hatua hizo hazitoshi kusaidia aina ya ndege kama sha-kwe mweusi, ngojamaliko mdogo, na koho wa baharini. Kuhifadhi sehemu wanakotaga mayai hakutimizi mengi isipokuwa ikiwa sehemu za makimbilio ya ndege wakati wa kipupwe, kama yale ya Afrika, yanalindwa pia. Hivyo, gazeti hilo linasema: “Katika visa vingi, uhifadhi waweza tu kuleta matokeo baada ya ushirikiano wa kimataifa.”
Manufaa za Kumkanda (Kumsugua) Mtoto
“Uwezo wa kufahamu mambo na maono ya binafsi hutuambia kwamba mguso wa mtu kwa mtu ni wenye afya,” lasema Stress & Health Report. Kanuni hiyo ilitumiwa kwenye utunzi wa kikundi cha vitoto vilivyozaliwa kabla havijakomaa, na gazeti hilo, lililochapishwa na Hospitali ya Enloe katika California, laonyesha uchunguzi wa kisayansi wa vitoto 40 kama hivyo. Ishirini kati yavyo vilikandwa kwa wororo mara tatu kwa dakika 15 kila siku. Vitoto vingine ishirini visivyokomaa vilipokea utunzi wa kawaida. Wale 20 waliokandwa walifanya vizuri katika mambo kadhaa kuliko wale 20 wengineo. Nyongeza ya uzito wao wa kila siku ilikuwa asilimia 47 zaidi kwa wastani, matokeo ya majaribio ya tabia zao yalikuwa ya juu zaidi, na walionekana wakiwa watendaji na walio chonjo zaidi. Stress & Health Report lamalizia: “Kile kinachofaa vitoto vidogo sana labda kinatufaa sote.”
Ziwa Linalosongwa
Baadhi ya wanasayansi wanaamini kwamba Ziwa Viktoria linalovutia sana la Afrika, ambalo ni ziwa la pili kwa ukubwa duniani lisilo na chumvi, linakabiliwa na kifo cha ukosefu wa hewa. Inaonekana kwamba miani inasitawi chini ya ziwa na kufyonza oksijeni kutoka majini. Kisababishi? Kwa neno moja, mwanadamu, kupitia uharibifu wa misitu, ukulima, na idadi ya watu inayopita kiasi. Kiasi kikubwa cha lishe kutoka kwa udongo unaomomonyoka, maji machafu, na moshi wa kuni unalisha miani. Pia, maofisa wa uvuvi waliamua miaka 30 iliyopita kuongeza biashara ya uvuvi kwa kuzalisha samaki wa Naili wa maji yasiyo na chumvi. Hao walisitawi, na biashara ya uvuvi ikafanikiwa kama ilivyopangwa. Hata hivyo, samaki wa Naili alikula samaki wadogo-wadogo ambao walikuwa wameweka usawaziko kwa muda mrefu kwa kula miani. Zaidi ya nusu ya aina hiyo ya samaki wadogo wametoweka. Sasa, kwa sababu ya uvuvi wa kupita kiasi na ukosefu wa oksijeni, huenda samaki wa Naili akawa yumo hatarini pia. Watu wapatao milioni 30 hutegemea Ziwa Viktoria kwa biashara ya uvuvi.
Mazoezi ya Ubongo
“Bongo Timamu.” Hilo ndilo jina la kampeni ya Finlandi inayokazia kutumia ubongo. Hoja ni rahisi. Kadiri tutumiavyo sana ubongo wetu—kwa kutafakari, kubuni, kujifunza mambo mapya—ndivyo unavyofanya kazi vizuri zaidi. “Katika ubongo tuna uwezekano usiokwisha wa kutatua matatizo, lakini kwa kusikitisha, kwa wastani mwanadamu hutumia sehemu moja tu kwa kumi ya uwezo wa ubongo,” akazia Juhani Juntunen, mtafiti wa ubongo na msimamizi wa hospitali anayetumika akiwa meneja wa mradi wa kampeni hiyo. “Kuza ubongo wako, jifunze mambo mapya, na utakuwa na uwezo mwingi zaidi wa kuutumia,” yeye ahimiza. Yeye huudhika kwamba watu wengi hukweza ujana na kushusha uwezo wa ubongo wa watu wazee, kwa sababu anaamini kwamba bongo nzee huelekea kufanya kazi vizuri hata zaidi ya zile changa katika mambo fulani. “Si jambo la kutukia tu kwamba vyeo vikubwa hushikiliwa na wazee wa zamani,” asema Juntunen. “Huenda ubongo ukawa chombo chenye kudhoofika, lakini watu wazee huutumia kwa ustadi zaidi kuliko vijana.”
Unamna-Namna Unaopungua
Kulingana na gazeti la Brazili Superinteressante, aina kadhaa za matikiti katika Uhispania na unamna-namna wa vitunguu katika Esia ya Kati vinatokomea, na katika Brazili kuna aina za muwa na mahindi ambazo tayari hazipatikani tena. “Wa kulaumiwa ni wakuzaji na wanunuzi, ambao wakati wote hupendelea bidhaa zilezile,” Edouard Saouma, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la UM, alinukuliwa akisema. Gazeti hilo linaongeza: “Kwa kuwa wakulima hujaribu kuridhisha soko, upungufu wa aina za mimea unakuwa mbaya zaidi kila siku.” Kwa sababu ya kufuata kanuni hizo, ainabinadamu huenda ikapoteza aina 40,000 za mboga katika miongo ya miaka ijayo, aonya Saouma. Wanasayansi wanahofia kwamba bila unamna-namna wa kibiolojia, mavuno yataelekea zaidi kupatwa na tauni.
Kitu Hatari Zaidi Chenye Kukuza Uzoevu
Si kwamba tu sigara zimo miongoni mwa dawa za kulevya zenye kukuza uzoevu zaidi bali pia hizo ni “zenye hatari zaidi sana,” aonelea aliyekuwa mkurugenzi wa Taasisi ya Uchunguzi wa Tabia na Mwongozo wa Uvutaji, Thomas C. Schelling. Yeye asema katika toleo la gazeti Science la Januari 24, 1992, kwamba kuacha ni vigumu. Kiasi cha wanaofanikiwa kuacha kwa miaka miwili au zaidi ni 1 kati ya 5 katika kila jaribu. Kwa nini ni vigumu sana kuacha? Schelling aorodhesha sababu hizi: Sigara zina bei rahisi, zinapatikana kwa urahisi, zinabebeka, na zaweza kuhifadhiwa; hazilemezi kiungo chochote; na kuvuta sigara hakuhitaji vifaa vyovyote. “Madhara yanakuja polepole,” yeye asema. “Kwa kawaida, watu wanaopata kansa na magonjwa ya mapafu na moyo kutokana na kuvuta sigara wameivuta kwa miongo mitatu au zaidi kabla ya dalili kutokea.” Ingawa nikotini ndicho kitu hasa kinachokuza uzoevu katika moshi wa sigara, Schelling anashuku pia kwamba ladha ya moshi wa tumbaku na udhibiti wa hali ya moyoni unaoletwa na kuvuta sigara kwaweza kuongezea uzoevu. Kwa nini ni kawaida sana kurudia kuvuta? “Wavutaji wengi wanaoacha huwa mara nyingi hawako mbali kwa zaidi ya dakika 5 kutoka kwa sigara iliyo karibu zaidi, na kukosa kujidhibiti hata kidogo tu hufanya mtu atimize tamaa ya kuvuta sigara,” yeye asema.