Kuokolewa kwa Dunia Kwakaribia Sana
STEPHEN M. WOLF, mwenyekiti na ofisa mkuu mtendaji wa shirika la United Airlines, alisema hivi katika tahariri moja: “Iwe mtu ni mhifadhi mazingira au la, haiwezi kukanwa kwamba matazamio yenye kutisha kuhusu wanyama wanaohatirishwa na makao yao ni huzuni kwa dunia yote—na mwishowe, hutisha kuwako kwa spishi zote, kutia ainabinadamu. Kama vile imesemwa, ‘Si sisi tuliofuma utando wa uhai; sisi ni uzi mmoja tu katika huo. Lolote tufanyalo kwa utando huo, twajifanyia wenyewe.’” Alinena kwa usahihi.
Pia alisema katika tahariri hiyo hivi: “Sisi ndio kisababishi cha matatizo. Na sisi ndio utatuzi pekee.” Katika hilo alikuwa sahihi nusu tu. Ni sisi kisababishi; si sisi utatuzi. Hatuonyeshi ishara za kuwa hivyo. Maendeleo hufanywa, lakini ni kidogo kwa kufikiria dhara linaloendelea duniani kote.
Mwaka jana Al Gore aliandika kitabu Earth in the Balance—Ecology and the Human Spirit. Ni kitabu kinachoonya juu ya hatari ya kimazingira inayokua ulimwenguni pote, na ndani yacho alitoa taarifa hii yenye umaana: “Kadiri nizidivyo kuchunguza mashina ya hatari ya kimazingira ya kitufe, ndivyo nizidivyo kusadikishwa kwamba ni udhihirisho wa njenje wa hatari ya ndani ambayo ni, kwa kukosa neno bora zaidi, hali ya kiroho.”
Kwelikweli ni hatari ya asili ya kiroho. Ni kuharibika kwa roho ya kibinadamu. Ni nia ya kudhabihu uzuri wa asili wa dunia na maliasili yayo, uhai wa maelfu ya spishi za mimea na za wanyama, na hata afya na uhai wa watu. Zaidi ya hilo, ni kutojali kabisa watoto na wajukuu ambao lazima wawezane na dunia iliyoharibiwa wanayoachiwa. Pia ni kutojali kikatili shukrani kwa Yeye aliyeumba dunia na aliyeibuni iwe makao ya ainabinadamu.
Isaya 45:18 humtambulisha Yehova kuwa “aliyeziumba mbingu, yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu.” Mwanzoni alimweka mwanadamu duniani ili aitunze: “BWANA [Yehova, NW] Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.” (Mwanzo 2:15) Ijapokuwa aliumbwa akiwa mkamilifu, Adamu aliacha ukamilifu aende njia yake mwenyewe. Aliacha kazi yake ya ‘kuitunza dunia.’
Kushindwa huko kwaendelea mpaka siku yetu, na kuangamiza dunia kwa sasa kumekuwa hatari. “Mungu amemfanya mwanadamu mnyofu, lakini wamebuni mavumbuzi mengi.” (Mhubiri 7:29) “Wametenda mambo ya uharibifu, hawawi watoto wake, hii ndiyo ila yao; wao ni kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka”! (Kumbukumbu la Torati 32:5) Hata hivyo, dunia itaendelea kukaliwa, lakini haitakaliwa na kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka. Mtunga zaburi alisema kwamba katika wakati wa Mungu ufaao, ni ‘wenye haki tu watakaoimiliki.’—Zaburi 37:29.
Hangaikio la Yehova kwa Dunia
Yehova alipokamilisha kuumba dunia, yeye ‘aliona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana.’ Yeye alitaka ikae hivyo. Alikuwa amepanda bustani nzuri sana katika Edeni na alikuwa amemweka mwanamume Adamu humo aitunze. Mimea iliyokuwa humo haikuwa ya matumizi ya mwanadamu pekee. Mungu alisema hivi: “Chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu.”—Mwanzo 1:30, 31.
Sheria ya Musa ilipotolewa baadaye kwa Waisraeli, ilikuwa na uandalizi kwa ajili ya kutunza nchi. Kila mwaka wa saba ungekuwa “Sabato ya kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi.” Kilichojikulia chenyewe wakati huo hakingevunwa bali kingefanywa kipatikane kwa ajili ya watu maskini na kwa hayawani wao, na kwa wanyama walio katika nchi yao.—Mambo ya Walawi 25:4-7.
Hangaikio la Yehova kwa ajili ya kuhifadhiwa kwa spishi lilionyeshwa kwa kuagiza wanyama hai wawiliwawili wachukuliwe ndani ya safina wakati wa Furiko la siku ya Noa. Hangaikio hilo pia lilidhihirishwa katika agano la Sheria. Kwa mfano, fahali aliyekuwa akipura nafaka hangefungwa kinywa. Alikuwa na haki ya kula baadhi ya nafaka hizo. Fahali na punda hawangefungwa nira pamoja kulima kwa plau. Hilo lingemuumiza yule mnyama mdogo zaidi, mnyonge zaidi. Hayawani wa jirani alipasa kusaidiwa ikiwa alikuwa katika taabu, hata kama mwenyewe alikuwa adui ya mtu na hata kama ingemaanisha kufanya kazi katika siku ya Sabato. (Kutoka 23:4, 5; Kumbukumbu la Torati 22:1, 2, 10; 25:4; Luka 14:5) Mayai au kifaranga angeweza kutwaliwa kutoka katika kiota cha ndege, lakini si ndege mama. Ilikuwa lazima aachwe aendeleze spishi hiyo. Na Yesu alisema kwamba hata ingawa shomoro alikuwa wa thamani ndogo, ‘hata mmoja wao haanguki chini bila Mungu kujua.’—Mathayo 10:29; Kumbukumbu la Torati 22:6, 7.
Mtunga zaburi aliyepuliziwa alisema hivi: “Mbingu ni mbingu za BWANA [Yehova, NW], bali nchi amewapa wanadamu.” (Zaburi 115:16) Yesu alisema kwenye Mathayo 5:5 hivi: “Heri wenye upole; maana hao watairithi nchi.” Je! wewe wafikiri kwamba urithi huo kutoka kwa Yehova utakuwa dunia iliyochafuliwa? Kama ungekuwa na makao mazuri uliyotaka kuwaachia watoto wako, je, ungeruhusu wapangaji wanaoharibu nyumba na nyua waendelee kukaa humo? Badala ya hivyo, je, hungewaondosha na kuitengeneza kabla ya kuiachia watoto wako?
Ndivyo alivyofanya Yehova kabla ya kuingiza Waisraeli katika bara alilokuwa amewaahidi. Kwa ukosefu wao wa adili mbaya sana, Wakanaani walikuwa wamechafua bara, na kwa sababu hiyo Yehova aliwaondosha. Wakati huohuo, aliwaonya Waisraeli kwamba kama wangechafua bara kama Wakanaani walivyokuwa wamefanya, wao pia wangeondoshwa. Masimulizi hayo yamerekodiwa kwenye Mambo ya Walawi 18:24-28:
“Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote; na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa. Kwa hiyo mtazishika amri zangu na hukumu zangu, wala msifanye machukizo hayo mojawapo; yeye aliye mzalia, wala mgeni aketiye kati yenu; (kwa kuwa hao watu wa nchi wameyafanya machukizo haya yote, hao waliotangulia mbele zenu, na hiyo nchi imekuwa najisi;) ili kwamba hiyo nchi isiwatapike na ninyi pia, hapo mtakapoitia unajisi, kama ilivyoitapika hiyo taifa iliyotangulia mbele yenu.”
Hata hivyo, Israeli walichafua bara kwa kufanya ukosefu wa adili huohuo mbaya sana ambao wakanaani walikuwa wameufanya. Kupatana na neno lake, Yehova aliwaondosha Israeli kwa kupeleka Wababuloni wawachukue mateka na kuwapeleka Babuloni. Muda mrefu kabla hilo halijatukia, onyo lilitolewa kwa Waisraeli na nabii wa Yehova Isaya: “Tazama, BWANA [Yehova, NW] ameifanya dunia kuwa tupu, aifanya ukiwa, aipindua, na kuwatawanya wakaao ndani yake. Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele. Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu.”—Isaya 24:1, 5, 6.
Uharibifu kwa Wale Wanaoiharibu Dunia
Leo sisi tumo katika hali inayofanana na hiyo. Vitabu, majarida, magazeti, televisheni, video, na vyombo vya habari kwa ujumla huonyesha jamii ambayo imepotoka kingono, yenye jeuri ya kinyama, na yenye ufisadi kisiasa. Mashirika ya kibiashara yenye pupa huchafua mazingira bila maadili, hata kupeleka vitu vilivyopigwa marufuku kwa kuwa ni hatari kwa afya katika mataifa yao wenyewe yenye utajiri kwenye nchi zinazositawi ambako hakuna sheria kama hizo za usalama zinazofuatwa. Wakristo wanaonywa waepuke mwendo kama huo:
“Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao; ambao akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao; ambao wakiisha kufa ganzi wanajitia katika mambo ya ufisadi wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani.”—Waefeso 4:17-19; 2 Timotheo 3:1-5.
Roho ya kibinadamu na mazingira vimechafuliwa pia. Dunia ina vidhibiti vya kiasili nayo husawazisha kila kitu. Kwa sababu ya mwanadamu kuangukia dhambi, dhamiri ya kibinadamu, kidhibiti chake mwenyewe cha kiasili, kimefisidiwa, kikiongoza kwenye uchafuzi wa dunia. Sasa, ni Mungu tu awezaye kumdhibiti mwanadamu. Ni Mungu tu awezaye kuiokoa dunia. Tuna uhakikisho kwamba yeye atafanya hivyo kwenye Ufunuo 11:18, ambapo Yehova Mungu huahidi “kuwaharibu hao waiharibuo nchi.”