Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Babu na Nyanya Zile makala “Vijana Wauliza . . . ” katika toleo la (Julai 8 na Julai 22, 1992, Kiingereza) zilizungumza juu ya babu na nyanya kuhamia kwetu. Nyanya yangu alihamia kwetu baada ya mume wake kufa. Alitutunza mimi na ndugu na dada zangu watano huku Mama na Baba wakifanya kazi; tulipata kuwa marafiki wa karibu sana. Sasa kwa kuwa Nyanya yangu hawezi kujitunza, nina pendeleo la kumlipa kiasi kidogo cha aliyotupatia. Haijakuwa rahisi, kwa kuwa nina familia ya kutunza, na mimi si mzima pia. Lakini nahisi vizuri juu ya kumtunza. Ndiyo, mambo mengi yenye kufaa yaweza kutukia babu na nyanya wahamapo kuishi na watoto na wajukuu wao!
B. M., United States
Kulea Watoto Asanteni kwa mfululizo wa makala “Kulea Watoto Katika Ulimwengu Wenye Ukosefu wa Adili.” (Juni 22, 1992, Kiingereza) Mlionya juu ya wenye hila wajipenyezao ndani ya kundi, wakidai kuwa Wakristo. Mwaka uliopita binti yetu mchanga alipewa dawa na akanajisiwa na kijana mmoja wa namna hiyo. Alikuwa akijifunza Biblia na mshiriki wa kundi. Ijapokuwa mahakama ilimhukumia hatia, pigo katika familia yetu limekuwa mbaya sana. Twatumaini kwamba wazazi wote Wakristo watajifunza pamoja na watoto wao makala hizo za wakati ufaao. wakiwatahadharisha wasiwe watumainifu kupita kiasi kwa wale ambao huonekana kuwa wanapendezwa na Biblia.
K. V., United States
Gazeti hilo lilinifanya nitambue ni jitihada ya kadiri gani ambayo wazazi wetu hulazimika kutia ili watulee katika hofu ya Mungu. Mimi binafsi nilinufaishwa na makala “Wasaidie Wachague Mwenzi kwa Hekima.” Nina miaka 16 tu nami sipendezwi na ndoa sasa. Hata hivyo, nina hakika shauri hilo lenye kutumika litakuwa lenye mafaa kwangu katika wakati ujao.
N. G., Italia
Muziki Wenye Mdundo Mzito Shukrani nyingi kwa ajili ya makala “‘Muziki Wenye Mdundo Mzito’—Ujumbe Ni Nini?” (Julai 8, 1992, Kiingereza) Muziki wa “Mdundo Mzito” na wa “Rapu” pia hupendwa na wengi sana katika shule yetu. Yeyote asiyependa namna hii ya muziki huchekwa. Makala hiyo ilifanya iwe rahisi kwangu kuukataa pamoja na kueleza kwa nini mimi sipendi muziki huo. Asanteni sana.
M. F., Ujerumani
Kunena Hadharani Maelezo machache tu juu ya makala “Wewe Unaweza Kunena Mbele ya Wasikilizaji!” (Julai 22, 1992, Kiingereza). Sikuzote mimi nilikuwa mwenye haya. Shuleni ni mara chache sana nilipoweza kunena mbele ya darasa, na hatimaye niliacha kwenda shuleni kwa sababu ya hofu zangu. Lakini nilipopata kuwa Mkristo, nilijiunga na Shule ya Huduma ya Kitheokrasi na ilikuwa lazima ninene mbele ya wasikilizaji. Haikuwa rahisi, lakini kwa msaada wa sala na nia ya kushinda tatizo langu, hatua kwa hatua nilifanya maendeleo. Ningali nahisi kuwa mwoga-mwoga, lakini hata nimenena mbele ya idadi kubwa za wasikilizaji kwenye mikusanyiko ya Mashahidi wa Yehova!
A. H., Brazili.
Fanya Kumbukumbu Lako Liwe Bora Kabla tu ya kusoma makala “Jinsi ya Kufanya Kumbukumbu lako Liwe Bora” (Julai 22, 1992, Kiingereza), niligundua kwamba kwa mara nyingine tena nilikuwa nimesahau kununua kitu fulani nilipokuwa nikinunua vitu dukani. Makala hiyo ilionyesha misaada kadhaa ambayo mtu aweza kutumia kuzoeza kumbukumbu lake, kama vile kufanyiza sura ya kitu hicho akilini. Mfano wa kuona picha ya ng’ombe akipiga meno yake mswaki wakati mtu anapohitaji kununua maziwa na dawa ya meno ulikuwa wenye kuchekesha hasa. Wakati ujao, nitatumia njia hizo nami natumaini sitahitaji orodha ya vitu vya kununua.
E. B., Ujerumani
Kutoka kwa Wasomaji Wetu Asanteni sana kwa makala “Kutoka kwa Wasomaji Wetu.” Tofauti sana na kuwa mchanganyiko wa taarifa zilizochaguliwa kuunga mkono maoni yenu, huo ni mkusanyo wa mambo yaliyoonwa ya kibinadamu yenye kugusa moyo sana. Ule utayari ambao kwao nyinyi huchapisha uchambuzi wa wasomaji na, pindi kwa pindi, masahihisho ya mhariri ni uthibitisho dhahiri wa unyenyekevu wenu.
C. Q., Italia