Heroe-‘Ndege Warukao Pamoja’
Na mleta habari za Amkeni! katika Hispania
AJULIKANAYE sana na hata hivyo asiyefahamika sana, asiye na umbo zuri na hata hivyo mwenye kuvutia sana, mwenye kutamani sana kuishi mahali palipojitenga na hata hivyo asiyeweza kutenganishwa na kundi la aina yake—Heroe ni ndege asiyeeleweka.
Ajulikana karibu na kila mtu, sura yake huonekana katika mwandiko wa michoro ya Kimisri (alifananisha rangi nyekundu), katika michoro ya rangi katika mapango ya kale, na katika sanaa ya ki-siku-hizi. Lakini kungali kuna mambo tusiyojua kuhusu heroe. Mahali pao pa kuzalia huwa mbali sana isivyo kawaida, na aina kadhaa za heroe wakubwa zaidi wamegunduliwa katika muda wa miaka 50 tu iliyopita. Na ndege wa kiume na wa kike wanafanana sana hivi kwamba waornithopolojia (wataalamu wa ndege) waweza kuwatofautisha kwa kutumia tu chombo cha kitiba kinachoingizwa mwilini.
Miguu hiyo mirefu myembamba na shingo hiyo ndefu—aizungushayo na kuificha ndani ya bawa lake kana kwamba ni ya mpira—huchangia umbo lake lisilo zuri. Hata hivyo, atembeapo polepole katika maji yasiyo na kina au kudokoa-dokoa chini ya maji ili kupata viumbe wadogo wa baharini wenye gamba ambao ndio chakula chake, anakuwa na uzuri ulio wazi kuona, madaha yageuzwayo kuwa uzuri wa ajabu arukapo angani.
Si tamasha nyingi za asili zionekanazo zinazoweza kulinganishwa na kundi la heroe wanaporuka angani. Ule wekundu na weusi wa mabawa yao hutofautiana kwa njia yenye kuvutia na pinki na weupe wa miili yao.a Huonekana kana kwamba vipepea-hewa vingi mno vyenye rangi nyingi vinapepea kwa umoja wakati kundi hilo liinukapo polepole kuingia angani. Na wakiisha kuwa angani umbo lao lenye uzuri na mwendo wa utaratibu huwageuza kuwa wacheza dansi ya baleti wa ulimwengu wa ndege.
Inasikitisha kwamba, si rahisi kuona tamasha kama hiyo. Heroe ni ndege wenye kupenda kukaa pamoja makundimakundi, lakini wao hupendelea kukaa na wa aina yao wenyewe—wao ni mfano mkamilifu wa ‘ndege warukao pamoja.’ Daima wao huepuka maeneo yenye kukaliwa na kwa kawaida hukusanyika pamoja wakiwa idadi kubwa katika maziwa ya chumvi tu au mahali tambarare penye matope.
Tabia Zenye Kutokeza
Ili kujifunza zaidi kuhusu ndege hao wenye kusisimua, Amkeni! lilimhoji Manuel Rendón, mkurugenzi wa Hifadhi ya Fuente de Piedra, katika Málaga, Hispania.
Je! heroe ni dhaifu kama waonekavyo? “Sivyo kwa kweli. Wao husitawi katika maziwa yenye chumvi yenye baridi sana juu ya milima Andes ambapo hakuna ndege mwingine angethubutu kukaa. Katika maziwa ya Afrika wazoeako kwenda, maji ni yenye moto sana na yenye kuumiza hivi kwamba yangeweza kuchoma ngozi yako, lakini ile ngozi ngumu ya miguu ya heroe huikinga isipatwe na dhara.”
Tatizo lao kubwa ni nini? “Bila shaka ni lile la kupata mahali pafaapo pa kuzalia. Wanahitaji ziwa tulivu lisilo na kina lenye chumvi ambapo pana visiwa vidogo wawezapo kujenga viota vyao. Siku hizi ni vigumu sana kupapata mahali kama hapo. Kwa kweli, katika [eneo] lote la magharibi mwa Mediterranea, sasa tuna mahali pawili tu kama hapo: pamoja katika Hispania na pamoja katika Ufaransa.b
“Hapa katika Fuente de Piedra, wana ugumu mwingine. Ziwa ambamo wao huzalia hukauka upesi sana chini ya jua kali la Andalusia—kabla ya vifaranga kuwa wenye umri wa kutosha kuweza kuruka.”
Inakuwaje ziwa likikauka kabisa? “Miaka fulani tunalazimika kutoa ugavi wa maji kwa ubunifu wetu wenyewe ili kundi lote lenye kuzaa lisife. Tumeona kwamba tukimwaga maji hekta zipatazo 6, hiyo yatosha, hata ingawa hiyo yamaanisha kwamba heroe wazima watalazimika kula karibu wakati wote katika nyangwa zilizo umbali wa kilometa nyingi. Heroe watatumia wakati wao mwingi wakiruka kwenda malishoni mwao na kurudi, huku wakiachia ndege wazima wachache vifaranga wawatunze—kwa kweli kama vile nasari.”
Umegundua nini jingine? “Kwa sababu ya kuwafungia ndege vitambulisho, tumejifunza mengi zaidi juu ya tamaa yao ya kuhama-hama. Heroe hawahami-hami hasa, bali wao husafiri kutoka lisho moja hadi jingine, popote watakapo kwenda. Hivyo, ndege mmoja aweza kutumia wakati wa kiangazi katika Hispania na wakati wa kipupwe katika Afrika Kaskazini, hali mwingine atafanya kinyume kabisa. Ungeweza kuwaita watalii, ijapokuwa kuhama-hama kwao kwa wazi kwahusiana zaidi na ugavi wa chakula si kutafuta raha.
“Jambo lililo wazi ni kwamba wakipewa msaada na ulinzi kidogo, heroe husitawi. Kabla ya miaka ya 1980 walizalia hapa mara kwa mara na kwa idadi ndogo kwa kulinganisha. Kwa kuzuia wanadamu wasiwaingilie sana na kudumisha kiwango fulani cha usawa wa maji unaohitajiwa katika ziwa mpaka vifaranga viweze kuruka ili viishi, tumeona ongezeko kubwa katika idadi yao. Katika 1988 tulikuwa na karibu vifaranga elfu kumi vilivyolelewa.”
Ajabu ya Uumbaji
Si wengi ambao wameona heroe katika makao yao ya asili watasahau jambo hilo. Na kwa sababu ya wao kupenda maeneo ya mbali na kujitoa kwa wahifadhi, kungali kuna sehemu za ulimwengu zilizo na pendeleo ambako makundi makubwa yaweza kuonwa katika mazingira yao ya asili.
Dunia ingekuwa mahali palipopungukiwa zaidi bila maajabu kama hayo ya uumbaji ili kupendeza macho na kuchangamsha roho. Kwelikweli, inaweza kusemwa kwamba hao ‘ndege warukao pamoja’ huongeza sauti yao kwa “ndege wenye mbawa” wasifuo jina la Yehova.—Zaburi 148:10, 13.
[Maelezo ya Chini]
a Heroe wa Karibea (Phoenicopterus ruber ruber) ana rangi ya pinki yenye kutokeza sana, hali heroe mkubwa zaidi (phoenicopterus ruber roseus) ana rangi hafifu zaidi, ikitegemea ulaji.
b Mahali hapo ni: Fuente de Piedra, (Málaga), Hispania, na Camargue (Bouches-du-Rhône), Ufaransa.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Picha juu na chini: Zoo de la Casa del Campo, Madrid