Kiajabu Chekundu-Cheupe
Ndege anayewaka miali ya moto! Hivyo ndivyo Wagiriki wa kale walieleza juu ya finiksi, ndege wa kihadithi tu aliyemalizia maisha yake katika miali ya moto na baadaye akatokea katika majivu. Karne zilizopita, jina la finiksi lilihamishwa likawa la ndege halisi, heroe (flamingo). Yeye anatimiza maana ya jina hilo kwa njia nzuri kuliko vile hekaya ingeweza kulitimiza. Kuona kundi lao likiruka juu ni ajabu ya maajabu—ule mlio wa papara-papara, honihoni, “kishindo cha moto” kilicho chekundu-cheupe, cheusi, na chekundu-kiangavu kikijaa angani.
Naye heroe mmoja tu ni ajabu ya ubuni, kuanzia kichwani mpaka mguuni. Fikiria mdomo, ambao ni sanduku la umbo mstatili, lenye kifuniko, likiwa limeinamishwa chini mwishoni ili liende sambamba na sehemu ya chini ya kidimbwi cha maji wakati kichwa kinaporushwa-rushwa nyuma na mbele kutafuta chakula katika yale maji yasiyo na kina kirefu. Ndani, kinywa kimepangiliwa vinywele vinavyozuia vitu vikubwa zaidi viwe nje huku kikinasa vijipande vyenye kulika vya mimea midogo na vitu vya namna hiyo, huku ulimi ukipiga maji bomba la kuyaingiza ndani na kuyapeleka nje. Ni nyangumi peke yao wanaokula kwa njia kama hiyo, wakichunga uduvi wadogo sana kupitia kichungi chao.
Shingo na miguu ya heroe ni mirefu kuliko ya ndege yeyote, kulinganishwa na mwili ule mwingine. Heroe anaweza kuwa na urefu wa zaidi ya meta 1.8. Miguu yake iliyo kama mikongojo ya kutembea juu-juu inafaa kwa maisha katika maziwa ya maji yenye chumvi yasiyo na kina kirefu. Hata yeye anapumzika akiwa amesimama ndani ya maji, salama kutoka kwa wenye kumwinda, na akiwa katika msimamo usioelekea kufaa sana—kusimama kwa mguu mmoja! Wastadi wanasema kwamba heroe anasimama kwa mguu mmoja ili apumzishe ule mwingine. Uzi wa mnofu wa pekee unawezesha ndege huyu kuufungia mguu mahali pamoja kwa nguvu sana, kama kiguzo cha mti. Hisia nzuri ajabu ya usawaziko inasaidia pia.
Wanamageuzi wanapata magumu ya kueleza chanzo cha heroe. Kwao, yeye anafanana na bata kwa njia fulani-fulani, kwa njia nyinginezo ni kama korongo, na bado katika nyinginezo ni kama kulasitara. Tungeweza kuongeza kwamba yeye anakula kama nyangumi na kulala kama taa yenye kusimama. Lakini hatuhitaji kushangaa ametoka wapi. Ni Mbuni mwenye akili tu ambaye angeweza kubuni kiajabu cha jinsi hiyo.