Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 3/22 kur. 16-19
  • Vitu vya Kuchezea vya Afrika Bila Malipo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Vitu vya Kuchezea vya Afrika Bila Malipo
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Vitu vya Kuchezea vya Wavulana
  • Kujenga Kigari cha Waya
  • Wanasesere wa Afrika
  • Nyakati Zinazobadilika
  • Vitu vya Kuchezea vya Zamani na vya Sasa
    Amkeni!—2005
  • Vitu Bora vya Kuchezea
    Amkeni!—2004
  • Si Vifaa vya Kuchezea Tu
    Amkeni!—2008
  • Wazazi—Chagueni Vichezeo vya Mtoto Wenu kwa Hekima
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 3/22 kur. 16-19

Vitu vya Kuchezea vya Afrika Bila Malipo

Na mleta habari za Amkeni! kutoka Sierra Leone

Akiwa amevaa tu suruali fupi ya kaki iliyochakaa, mvulana mdogo atembea, huku akivuta kigari chake cha kuchezea—mkebe wa samaki ulio na kutu. Ndani yacho mna shehena yake—rundo la changarawe.

Mbele kidogo kwenye barabara hiyo, kikundi cha wavulana wenye miguu mitupu wanacheza mchezo wa soka. Hata hivyo, mpira wao ni vitambara vilivyofungwa pamoja. Vizingiti vya goli yao ni mawe.

Pale mbele, msichana wa miaka mitatu ashika mwanasesere wake—kijiti cha hudhurungi kilichofungwa kwa nguo nyororo nyekundu.

Hayo ni mambo ya kawaida katika nchi za Afrika. Na bado, huenda yakaonekana kuwa mageni kwa wasomaji wanaoishi katika nchi zilizoendelea. Labda unaamini (kama vile biashara ya utangazaji imekutia moyo uamini) kwamba vitu vya kuchezea ni vitu vya kununuliwa. Hata hivyo, muda mrefu kabla ya enzi ya vitu vya kuchezea kutokezwa na kiwanda, watoto walitengeneza vitu vya kuchezea vyao wenyewe. Na katika Afrika desturi ya ubuni inasitawi sana.

Vitu vya Kuchezea vya Wavulana

Kutoka nyakati za kale wavulana wamevutiwa na magari. Wavulana Wagiriki na Warumi walichezea mikokoteni midogo. Na bila kushangaza, usafiri wa mashine bado huvutia na kuchochea ubuni wa wavulana wachanga.

Abraham, mvulana wa shule Mghana, hukata matawi kutoka kwa mnazi kwa kisu kirefu. Kwa matawi hayo yeye hujenga kigari cha kubebea mizigo. Magurudumu ni diski zilizokatwa kutoka kwa plastiki iliyotupwa.

Katika Lesotho kijana aitwaye Chepa hujenga kigari aina ya Land-Rover kutoka kwa mikebe ya pombe na waya. Baada ya kupasua mikebe hiyo, yeye huitandaza, anaikata kwa ukubwa ufaao, na kuikunja juu ya fremu ya waya ili kufanyiza mwili wa gari. Mikebe nusu ya pombe yafanyiza magurudumu ya gari hilo.

Ndiyo, kuanzia mikebe, vijiti, kadibodi, waya, na mianzi, wavulana Waafrika hujenga ndege, mabasi, pikipiki, malori, matrekta, magari, na mitumbwi. Na hakuna mbili kati yayo zinazofanana!

Kujenga Kigari cha Waya

Labda ustadi huo unaweza kuelezwa vema zaidi kwa yale yaitwayo vigari vya waya. Hivyo ni vigari vilivyojengwa kwa waya na mikebe mikuukuu.

Kwanza, hata hivyo, ni lazima mfanyizaji wa kigari cha waya apate vitu vya kujengea. Kwa mfano, Tamba aondoka nyumbani mapema asubuhi ili aanze kuvitafuta. Jirani mmoja ampa waya kuukuu za kuangikia makoti—zifaazo kwa fremu na mwili wa kigari. Apata waya za umeme kwenye jaa la taka. Vifuniko vya mikebe vya sentimita 8 vitakuwa magurudumu. Na akielekea nyumbani, Tamba apata ruhusa ya kuchukua waya ya urefu wa mita 1.2 kutoka kwa ua uliovunjika.

Sasa ni sehemu ya kubuni. Baada ya kuchora mchoro wa vivi-hivi kwenye kadi, Tamba yuko tayari kuanza ujenzi wenyewe. Akitumia chamburo ya baba yake, yeye akata, akunja, na kufunga waya za kuangikia makoti kulingana na mchoro. Baada ya kumaliza fremu ya juu, yeye aongeza waya za magurudumu na magurudumu ya vifuniko vya mikebe. Kisha mambo mengineyo—milango, sakafu, viti, fremu za dirisha, kifuniko cha fito, bati la mbele na nyuma, na mataa. Bila shaka, kigari cha Tamba kitakuwa na nyongeza nyinginezo, kama vile kipande kidogo cha kioo na mkeka wa sakafu. Vikaratasi vya peremende vinavyoruhusu mwangaza hutumika kuwa “vioo” vya madirisha.

Sasa ni wakati wa kuweka ufito wa usukani, ambao huenea kupitia paani na kupita kigari chenyewe hadi urefu wa kiunoni. Tamba afanyiza mwisho huo kuwa usukani, ambao utamwezesha “aendeshe” kigari chake kwa kukisukuma. Ni muda gani wa wakati unaotumiwa kujenga? Siku mbili. Lakini sasa raha yenyewe yafika—kukiendesha! Mkono wake ukiwa kwenye usukani, Tamba asukuma kigari chake na kukiendesha kwa ustadi ili kuepuka vizuizi. Na kwa habari ya kuendesha wakati wa usiku, wavulana wengine hutia mataa ya betri, yaani, mataa ya tochi.

Wanasesere wa Afrika

Wanasesere wameitwa “vitu vya kuchezea vya ainabinadamu vilivyo vya kale zaidi.” Hata hivyo, wanasesere wa Afrika ni tofauti sana na aina ile inayonunuliwa dukani. a Wazia kwa mfano, mwanasesere wa ndizi! Hao wanapendwa miongoni mwa wasichana wa Afrika Magharibi. Baada ya kuchora macho mawili, mdomo, na pua juu ya tunda hilo, wanavalisha mwanasesere ifaavyo. Watoto wengine hata hubeba wanasesere wao—kama mama afanyavyo!

Wasichana wa Afrika Kusini pia wanajua jinsi ya kutengeneza “watoto” kwa mahindi. Vijiti huongezwa ili kuwa mikono na miguu. Vipande vichache vya nguo huwa mavazi. Na nywele za maganda hufaa kwa kusukwa.

Cynthia, msichana kutoka Sierra Leone, huenda kutoka kwa mshona nguo mmoja hadi mwingine akikusanya vitambara vya nguo kwa ajili ya mwanasesere wa aina nyingine bado. Huyo ni mtoto wa vipande-vipande, au mwanasesere wa viraka. Akiazima makasi, sindano, na uzi kutoka kwa mama yake, yeye akata vipande vya nguo na kushona mwanasesere wake. Visehemu vidogo vya nguo husindiliwa ndani au hushonelewa kuwa sura ya uso.

Nyakati Zinazobadilika

Katika miaka ya hivi karibuni, Afrika imepokea shehena kubwa ya vitu vya kuchezea visivyo ghali vilivyotengenezewa Mashariki ya Mbali. Katika Afrika Magharibi, kwa mfano, wanasesere wa plastiki waweza kununuliwa kwa kiasi kidogo cha senti 40 za U.S. Kwa sababu wanadumu na wanashabihi sana watoto halisi, mara nyingi wasichana huwapendelea kuliko wanasesere wa mahindi au wa viraka.

Msichana tineja aitwaye Saffie huuza watoto wa viraka kwenye kibanda cha barabarani katika Freetown, jiji kuu lenye shughuli nyingi la Sierra Leone. Yeye huwauza kwa kiasi cha dola 2.50 (za U.S.). Wateja wake ni nani? Saffie akiri: “Sana-sana ni watalii Waamerika na Wazungu wanaotaka watoto wa viraka sasa. Watoto Waafrika hupendelea watoto wa plastiki.”

Lakini je, wavulana hupendelea vitu vya kuchezea vya dukani? Raymond mwenye miaka kumi na mitatu alikuwa tu ndio ametumia juma nzima katika kujenga kilori kikubwa cha waya. “Ikiwa mtu angekupatia kilori cha kuchezea kilichofanyizwa kiwandani kwa kubadilishana na kilori chako,” tukamuuliza, “ungekubali?” Hakupoteza wakati kujibu: “Bila shaka! Kwa sababu kinashabihi zaidi kile halisi.”

Ndiyo, huku vigari vilivyotengenezewa viwandani vikiongezeka, vigari vya kuchezea vilivyofanyiziwa nyumbani vinapoteza umashuhuri. Patricia Davison katika gazeti African Arts asema: “Inaonekana kwamba hali za umaskini wa kijamii na kiuchumi ambazo ni kawaida katika jumuiya zinazotokeza vitu hivyo vya kuchezea zimechochea aina hiyo ya uwezo wa ubuni na, hivyo, huenda ukazuiwa na wingi wa mali.”

Je! vitu vya kuchezea vilivyofanyiziwa viwandani hatimaye vitachukua mahali pa vile vilivyofanyizwa kwa mkono katika Afrika? Tutajua hayo baada ya muda. Kwa kupendeza, hesabu fulani ya mashirika kotekote Afrika yanajaribu kuendeleza desturi ya kufanyiza nyumbani vitu vya kuchezea kwa kuthamini mashindano ya kufanyiza vitu hivyo. Pia, majumba mengine ya uhifadhi yanakusanya mifano ya ufundi huo kwa ajili ya maonyesho yao. Hata hivyo, wakipewa nafasi ya kuchagua, watoto karibu siku zote hupendelea vitu vya kuchezea vilivyofanyiziwa viwandani kwa ajili ya uhalisi wavyo.

Labda hilo ni sikitiko. Kwa kuwa tofauti na aina ile inayonunuliwa dukani, vitu vya kuchezea vilivyofanyiziwa nyumbani huchochea ubuni, uasilia, umahiri, usanii, na uwazio. Kuvifanyiza kunafurahisha na hutokeza hisi ya utimizo. Na gharama ya pesa ni ya chini sana.

[Maelezo ya Chini]

a Sanamu za Afrika zilizochongwa kwa mti, ambazo zamani zilihusishwa sanasana na dini na uwasiliani-roho, mara nyingi hazitumiwi kuwa vitu vya kuchezea na watoto Waafrika. Bw. H. U. Cole, mkurugenzi wa Jumba la Uhifadhi la Sierra Leone katika Freetown, aliambia Amkeni! kwamba kwa sababu ya uvutano wa Magharibi, sanamu hizo sanasana zinazidi kutumiwa kwa makusudi ya kurembesha.

[Blabu katika ukurasa wa 19]

Muda mrefu kabla ya enzi ya vitu vya kuchezea vilivyofanyiziwa viwandani, watoto walifanyiza vitu vyao wenyewe

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki