Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 9/8 kur. 7-10
  • Wazazi—Chagueni Vichezeo vya Mtoto Wenu kwa Hekima

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wazazi—Chagueni Vichezeo vya Mtoto Wenu kwa Hekima
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Miongozo Saba Isaidiayo
  • Mambo Fulani ya Maana Kuliko Vichezeo
  • Vichezeo vya Leo—Hufundisha Watoto Wetu Nini?
    Amkeni!—1994
  • Wazazi—Mtoto Wenu Anacheza na Nini?
    Amkeni!—1994
  • Vitu vya Kuchezea vya Zamani na vya Sasa
    Amkeni!—2005
  • Vitu Bora vya Kuchezea
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 9/8 kur. 7-10

Wazazi—Chagueni Vichezeo vya Mtoto Wenu kwa Hekima

WATOTO ni “urithi wa BWANA,” yasema Biblia. (Zaburi 127:3) Hivyo wazazi wahofu-Mungu hutambua daraka lao kuzoeza watoto wao “katika nidhamu na rekebisho la akilini la Yehova.” (Waefeso 6:4, New World Translation) Hawaachii watengeneza-vichezeo kuunda nyutu za watoto wao.

Vichezeo vyaweza kutimiza fungu la maana katika kuchochea ukuzi wa watoto wa kihisiamoyo na kiakili. Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba ni lazima wazazi watumie fedha nyingi kununua vifaa vya hali ya juu. Baadhi ya vitu vya kuchezea vifaavyo na kuchochea zaidi huwa vya bei rahisi sana.

Sanduku sahili la kadibodi (karatasi) laweza kugeuzwa nyumba ya kuchezea, ndege, au chochote kiwezacho kuwaziwa na akili ya mtoto yenye uvumbuzi mwingi. Ndoo na koleo huwezesha mtoto kujenga ngome za mchanga. Vibao sahili, vidude vya kuunganisha, udongo, na kalamu za kupaka rangi zaweza vilevile kuandaa muda mwingi wa tafrija ifaayo. Kwa watoto wakubwa zaidi, vifaa vya uchoraji na vya kuungwa-ungwa vyaweza kufundisha stadi zenye mafaa na kuandaa burudani yenye ubuni—yenye kuridhisha sana kuliko miwakowako ya picha za kompyuta za kufyatua risasi.[1]

Michezo fulani haihitaji vifaa maalumu kamwe. Matembezi katika mwitu yaweza kuwa tukio la kusisimua mtoto, hasa aandamanapo na mzazi mwenye upendo, mwenye kuhusika. Naam, hata stadi za msingi za kinyumbani zaweza kufundishwa kama vifurahisho. Penelope Leach (mwanamke) aandika katika kitabu chake Your Growing Child: “Kupika keki au mlo, kuchimba bustani, kusafisha gari au kupaka dari rangi, kwenda dukani au kuosha mtoto huenda kukawa ni kazi tupu kwako, lakini kwa mtoto wako huenda yakawa miongoni mwa aina za michezo itamanikayo zaidi.”[2]

Miongozo Saba Isaidiayo

Bila shaka, vichezeo vilivyotengenezwa viwandani vyaweza kuwa na mafaa. Na ikiwa fedha za matumizi ya familia zatosha kuvinunua, huenda ukataka kujiuliza maswali yanayofuata kabla ya kununua:

1. Je, kweli kichezeo hicho huchochea hamu ya kujua na akili ya mtoto wangu? Ikiwa sivyo, atakosa kupendezwa nacho upesi. Huenda kichezeo kikaonekana chema katika tangazo la kibiashara la televisheni, lakini kumbuka: Wale watoto waigizaji wamelipwa ili wasisimukie kichezeo. Huenda mtoto wako asitende ivyohivyo. Jaribu kumchungulia akicheza au akiwa katika duka la vichezeo. Aelekea kwenye vitu gani vya kuchezea?[3]

Nyakati fulani wazazi huhisi kwamba kichezeo hakina thamani kisipokuwa “cha kuelimisha.” Hata hivyo, profesa Janice T. Gibson atukumbusha: “Watoto hujifunza kutokana na vichezeo vyote wachezeavyo. Jambo la maana ni kwamba wafurahi ili wafulize kucheza kwa njia ziwafaazo.”[4]

2. Je, kichezeo hicho chafaa uwezo wa kimwili na wa kiakili wa mtoto wangu? Nyakati fulani mtoto hana kamwe nguvu za kutosha, subira ya kutosha, au wepesi wa kutosha kutumia kichezeo fulani. Ingawa hivyo, huenda mzazi akawa na elekeo la kukinunua kwa sababu chamkumbusha uvutio fulani wa zamani. Lakini je, mvulana wa miaka mitatu aweza kweli kuendesha gari-moshi la umeme—au kutumia jiti la kupigia besiboli? Kwa nini usingoje mtoto wako awe tayari zaidi kuthamini vitu hivyo vya kuchezea?

3. Je, kichezeo hicho ni salama? Watoto wanaokaribia kutembea huelekea kuingiza kila kitu ndani ya vinywa vyao na waweza kunyongwa kwa urahisi na vibao au viplastiki. Ncha kali au zilizochongoka zaweza kuwa hatari kwa watoto wa umri wowote. Ingefaa pia ujiulize kama kichezeo hicho kitaelekea kutupwa au kutumiwa kama silaha dhidi ya ndugu yake.[5]

Katika Marekani, vichezeo fulani hutiwa kibandiko kuonyesha marika hususa viliyokusudiwa. Kushikamana na mapendekezo hayo kwaweza kulinda mtoto wako asijeruhiwe. Ukiwa na shaka kuhusu kichezeo, jaribu kumwuliza karani wa duka kama kuna kiolezo cha maonyesho ili ukichunguze.[6]

4. Je, kichezeo kimejengwa vizuri na kina maisha? “Watoto wanaokaribia kutembea wapendao kuangusha, kutupa, na kuonja kila kitu waweza kuharibu-haribu vichezeo visivyo na maisha,” latukumbusha hivyo gazeti Parents.[7]

5. Je, kichezeo hicho chastahili kuzitumia fedha? Ni nadra matangazo ya biashara ya televisheni kuzungumzia bei, lakini vichezeo vina bei. Fedha nyingi hulipwa kwa sababu ya jina tu la muundo wa kitu wala si kwa vifaa kilivyotengenezwa kwavyo hasa.[8] Tena, mara nyingi matangazo ya biashara husitawisha mataraja yasiyo halisi katika watoto, yawezayo kutamausha sana.

Fundisha watoto wako kuwa wanunuzi wenye busara. Mithali 14:15 husema: “Mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.” Makala moja katika The New York Times ilisema: “Nyakati fulani waweza kuonyesha mapema kwa nini kichezeo fulani kimetengenezwa vibaya au chatangazwa kwa kupotosha.” Times liliongezea: “Watoto huwa wanunuzi wenye utambuzi zaidi fedha zitokapo katika mifuko yao badala ya wako.”[9]

Bila shaka, thamani halisi ya kichezeo si vifaa kilivyotengenezwa kwavyo au ufundi tu. Mambo ya maana ni kitatumiwa kadiri gani na mtoto wako, na kitamletea ufurahisho wa kadiri gani. Pembea ya uani huenda ikawa ghali kidogo, lakini huenda ikaandaa saa nyingi za ufurahisho kwa muda wa miaka mingi. Kichezeo rahisi kitupwacho upesi huenda kikawa kiliharibu fedha muda mwingi upitapo.[10]

6. Kichezeo hufundisha kanuni na viwango gani? Profesa wa kuchunguza watoto David Elkind atahadharisha kwamba “vichezeo vyapasa kuchochea akili za watoto kwa njia ifaayo, si isiyofaa.”[11] Epuka vichezeo vya kuogofya, viendelezavyo jeuri waziwazi, au viigavyo maovu ya watu wazima, kama vile kucheza kamari.

Namna gani vichezeo vya mazimwi maridadi yapendwayo na wengi au vya ubuni wa sayansi ya kuwazia tu? Hadithi hizo kwa jumla zahusu wema kushinda uovu. Hivyo wazazi fulani huona kwamba ‘mizungu ya kichawi’ iliyo katika hadithi hizi ni ya kusisimua tu akili ndogo ya mtoto na hawaoni dhara lolote la kuruhusu watoto wao kuzifurahia. Huenda wengine wakahofu kwamba hadithi hizo zingeweza kuchochea upendezi wa mafumbo ya kipepo. (Kumbukumbu la Torati 18:10-13) Lazima wazazi wajifanyie maamuzi katika jambo hili bila kuhukumu wengine, wakifikiria matokeo ambayo hadithi hizo—na vichezeo vyovyote vizitegemeavyo—vinayo juu ya watoto wao.

Kumbuka pia kanuni kwenye 1 Wakorintho 10:23: “Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vifaavyo.” Ingawa huenda kichezeo kipendwacho na wengi kisionekane kibaya kwako, je, kweli yafaa kukinunua? Je, kingeweza kuudhi au kukwaza wengine?

Vichezeo visemwavyo kuwa vya kuelimisha vyapasa pia kuchunguzwa sana na wazazi, hasa vigusiapo kufundisha watoto mambo ya ngono na mimba. Je, mtoto yuko tayari kwa habari hizo? Je, ingekuwa afadhali habari hizo zielezwe kupitia mazungumzo kati yako na mtoto wako?a Vichezeo fulani huenda vikaonyesha mawazo ya kimwili juu ya mambo hayo, lakini je, vyaonyesha mawazo ya mitazamo ifaayo ya kiadili?

7. Je, kweli nataka mtoto wangu apate kichezeo hiki? Huenda ukahisi kwamba tayari mtoto wako ana vichezeo vingi mno, kwamba kichezeo hiki hakifai kamwe hali zako, au kwamba kichezeo hicho kina makelele usiyoweza kuvumilia. Ikiwa matatizo hayo hayatatuliki, huenda usiwe na budi ila kukataa. Hii si rahisi. Lakini kukubalia kila msisimko na dai la mtoto hakutasaidia mtoto wako awe mtu mzima aliyesawazika. Iangalie kanuni kwenye Mithali 29:21: “Amtunduiaye mtumwa wake [au mtoto] tangu utoto, mwisho wake atakuwa ni mwanawe [“atakuwa asiye na shukrani katika maisha yake ya baadaye,” NW].”

Hii haimaanishi kwamba wewe mzazi lazima ushikilie kauli na kukosa kiasi. Hiyo ingehisisha mtoto wako hasira na uchukizo tu. ‘Hekima itokayo juu ni tayari kusikiliza maneno ya watu.’ (Yakobo 3:17) Mstadi mmoja wa utunzaji watoto alieleza hivi: “Wahitaji kuketi na mtoto ueleze kwa makini sana kwa nini hutaki kumpa vichezeo fulani.”[11a]

Mambo Fulani ya Maana Kuliko Vichezeo

Ingawa vichezeo vyaweza kuwa vyombo vya thamani kubwa kwa kuelimisha na kutumbuiza, hivyo ni vitu tu. Mtoto aweza kupenda kichezeo, lakini kichezeo hakiwezi kupenda mtoto. Watoto huhitaji uangalifu wenye upendo uwezao kutolewa na wazazi tu. “Mzazi pekee ndiye kichezeo bora zaidi kilichopata kubuniwa,” asema Dakt. Magdalena Grey.[12] Wazazi wachezapo na watoto wao, wao husaidia kuunda kifungo cha ukaribu wa kihisiamoyo na kuchangia ukuzi wa mitazamo na hisiamoyo zenye afya.[13]

Ndiyo, watoto wahitaji mchezo ufaao. Lakini la maana zaidi, wahitaji mwelekezo wa kiadili na kiroho. “Hii yamaanisha uhai udumuo milele,” yasema Biblia, “kutwaa kwao ujuzi juu yako wewe, Mungu pekee wa kweli, na juu ya yule uliyemtuma, Yesu Kristo.” (Yohana 17:3, NW) Wazazi waweza kutimiza fungu kubwa katika kusaidia watoto wao wapate ujuzi huu wenye kuokoa uhai. Familia miongoni mwa Mashahidi wa Yehova hujaribu kufanya funzo la Biblia liwe sehemu ya kawaida yao. Mara nyingi wao hufanya hivyo kwa usaidizi wa vichapo kama vile Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia, Kumsikiliza Mwalimu Mkuu, na Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, ambavyo vimeandikwa kwa ajili ya vijana hasa.b Vitabu hivi havitumbuizi tu—vimesaidia maelfu ya watoto kukuza imani thabiti katika Mungu. Watoto huthamini mirekodi ya audiokaseti za drama za Biblia pia na vichapo kama vile Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi.*

Basi Wakristo wa kweli hawachezi tu na watoto wao—pia husali nao, hujifunza nao, na huongea nao. Kutoa uangalifu huo wenye upendo huhitaji wakati na jitihada nyingi. Lakini hatimaye, hiyo huletea mtoto shangwe ya kudumu kuliko ile ambayo mchezo wowote au kichezeo kimetametacho chaweza kuleta!

[Maelezo ya Chini]

a Zione makala juu ya elimu ya ngono katika toleo la Amkeni! la Februari 22, 1992 (la Kiingereza).

b Kimechapwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Watoto hufurahia vichezeo vya kutengenezewa nyumbani—vikapu vya nguo za kufua huwa magari; visanduku vya viatu huwa magari-moshi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki