Wazazi—Mtoto Wenu Anacheza na Nini?
KAZI bila burudani kwa mtoto si kazi tena. Sikuzote mchezo umekuwa sehemu ya maana ya maisha za watoto. Ni kwa njia ya michezo kwamba watoto hupanua akili na misuli yao na kukuza stadi za maana. Hata hivyo, leo kumekuwa na biashara kubwa kuhusiana na michezo ya watoto. Ulimwengu wa vichezeo hautawalwi na watoto wala wazazi, bali na watengeneza-bidhaa, wauzaji rejareja, watangazaji, na watafiti werevu wa soko la bidhaa. Wakiwa na ufundi mpya wa kutengeneza vichezeo na kuungwa mkono na vyombo hodari vya habari, wanaleta mamboleo katika ulimwengu wa michezo—matokeo yakiwa mazito kwa wazazi na kwa watoto pia.
Bila shaka wengi katika shughuli ya kutengeneza vichezeo hupendezwa kikweli na masilahi ya watoto. Ingawa hivyo, mara nyingi sana faida wajipatiayo hutangulizwa. Suala kubwa huwa si kile kitakachoelimisha watoto au kuchochea mawazio yao, bali kile kitakachouzwa kwa wingi. Na kile kiuzwacho sana huwa mara nyingi si vile vichezeo vya sahili vya juzi vilivyotengenezwa kwa nguo, mbao, na plastiki bali ni vichezeo vya ufundi wa hali ya juu, vichezeo vilivyoundwa kihalisi sana hivi kwamba mtoto hachochewi kuwaza ili ajivumbulie mambo mwenyewe.
Kwa kielelezo, mtengenezaji mmoja hupeleka sokoni vigari vya kuchezea vyenye sanamu-binadamu zitengukanazo kwa kugongana. Vigari hivyo vigonganapo, sanamu-binadamu hizo hutapakaza mikono yao, miguu—na vichwa—nje ya dirisha la vijigari vyao. Kichezeo kingine kilichoundwa kihalisi hujaribu kuigiza mimba. Mfuko kama wa kubebea vitu ulioundwa kuzungushwa kwenye tumbo la msichana mdogo huigiza teke dogo na pigo la moyo la kijusu anayekua.[2]
Watu fulani huamini kwamba vichezeo hivyo vina thamani ya kielimu. Donna Gibbs, mkurugenzi wa mahusiano ya vyombo vya habari wa kampuni moja ya kutengeneza vichezeo, huita kiigiza-mimba “njia ya kufurahisha ya [wasichana wadogo] kushiriki mambo yanayompata mama.”[3] Hata hivyo, si kila mtu anayekubaliana na shauku ya mkurugenzi huyo. Dakt. T. Berry Brazelton, profesa wa matibabu ya watoto kwenye Shule ya Kitiba ya Chuo Kikuu cha Harvard, aita kichezeo hiki “uvamizi wa fursa ya mzazi kushiriki kitu cha thamani pamoja na mtoto.”[4] Dakt. David Elkind, profesa wa uchunguzi wa ukuzi wa watoto, ashikilia kwamba “vichezeo hivi vinaruka mipaka.” Asema kwamba mwanasesere [doli] achocheaye kijusu “amezidi mno mambo wawezayo [watoto] kuyaelewa au kuyathamini.” Kwa habari ya vichezeo viigizavyo kihalisi mauaji ya mgongano wa magari, yeye aongezea kwamba kwa kuwa tayari televisheni imetota jeuri nyingi, “kwa nini kuiongezea kichezeo cha aina hii?”[5]—The Globe and Mail, Februari 8, 1992.
Kuna ubishi pia juu ya michezo mingine ipendwayo, kama vile michezo ya vidio ya vita na bunduki za kurusha maji mbali kwa nguvu. Kwa kufikiria kwamba, kulingana na msimamizi wa shirika la Watengeneza-Vichezeo wa Marekani,[6] “sokoni kuna vichezeo vikadiriwavyo kuwa 150,000 wakati wowote ule,” wazazi wana ugumu mkubwa wa kuamua ni vichezeo vipi wapaswavyo kununua. Ni nini kipasacho kuongoza wazazi katika jambo hili? Je, kuna sababu halali ya kuhangaishwa na baadhi ya vichezeo vya leo? Makala zinazofuata zitazungumzia maswali haya na mengine yahusianayo.