Kusomea Nyumbani Je! Kunakufaa Wewe?
“JAMBO lililoonwa kuwa si la kawaida ambalo limekuja kuwa harakati ya kitaifa.” Hivyo ndivyo gazeti Time lilieleza hivi karibuni juu ya kusomea nyumbani katika United States—mwelekeo unaozidi kukua ukiongozwa na wazazi wanaoamini kwamba elimu bora zaidi ambayo mtoto aweza kupokea inapatikana katika sebule yake mwenyewe, si katika darasa la kawaida.
Ingawa bado linaonwa na wengine kuwa jambo lisilo la kawaida au hata kuwa mvuvumko, kusomea nyumbani hata hivyo kunaungwa mkono na watu wengi zaidi kila mwaka. Watafiti wanasema idadi ya wale wanaosomea nyumbani imepanda kutoka karibu 15,000 katika 1970 hadi 500,000 katika 1990. Baadhi ya wale wanaounga mkono kusomea nyumbani hudai kwamba familia zaidi ya milioni moja katika United States sasa hufunzia watoto wao nyumbani.
Vikundi vyenye kuunga mkono wanaosomea nyumbani vimeibuka pia upesi katika Australia, Kanada, Uingereza, Ujerumani, Japan, na New Zealand, ikionyesha kwamba kupendezwa na kusomea nyumbani kunaenea tufeni pote.
Kwa nini wazazi wengi wanafanya uamuzi wa kufunzia watoto wao nyumbani? Kusomea nyumbani kuna matokeo kadiri gani? Je! ni uchaguzi unaostahili kufikiriwa kwa ajili ya familia yako?
Kwa msingi, kusomea nyumbani si jambo la kupita kiasi kama linavyoweza kuonwa. “Nyumbani, wala si shuleni, ndio uliokuwa mfumo wa elimu pale mwanzoni,” adokeza Raymond na Dorothy Moore katika kitabu chao Home-Spun Schools. “Hadi karne iliyopita, watoto wengi walioenda shuleni walianza kwenda wakiwa na umri wa miaka kumi na mbili au baadaye.”
Watu mashuhuri, kama vile George Washington, Abraham Lincoln, Thomas Jefferson, Thomas Edison, na Albert Einstein, walisomea nyumbani. Kwa kweli, sheria za kushurutisha kwenda shule hazikuwapo katika United States hadi mwishoni mwa karne ya 19. Kwa hiyo, kulingana na mtungaji na mzazi aliyesomea nyumbani Kerri Bennett Williamson, kusomea nyumbani si mtindo wa hivi majuzi, bali ni “mpango wa elimu wa kale.” Kwa kweli, kusomea nyumbani kulikuwa ndio mpango wa watu wengi katika nyakati za Biblia.
Sababu ya Wao Kufanya Hivyo
Kwa kupendeza, National Catholic Reporter lakadiria kwamba kuanzia asilimia 50 hadi 90 ya wazazi wa U.S. wanaosomesha watoto wao nyumbani hufanya hivyo kwa sababu za kidini. Wazazi hao kwa msingi huhangaikia kulinda watoto wao na yale wanayoona kuwa mavutano ya kutokuamini kuwako kwa Mungu yaliyo shuleni. “Msingi wa harakati ya kusomea nyumbani ni jumuiya ya Wakristo Washupavu, inayoamini kwamba dini ama inashushiwa heshima au inapuuzwa darasani,” likasema gazeti Time.
Wazazi wengine wameondoa watoto wao katika shule za umma ili kuwalinda salama wasipatwe na mavutano yanayoharibu ya ukosefu wa adili wakiwa na umri mdogo. “Hali ilikuwa inaharibika zaidi kukiwa na ukosefu wa adili shuleni,” akasema mwanamume mmoja Mkristo aliyeamua miaka kadha iliyopita kwamba yeye na mke wake wangesomesha watoto wao nyumbani. “Tulihangaikia watoto wetu na hali za kusikitisha shuleni.”
Nyakati nyingine, wazazi huchagua masomo ya nyumbani kwa sababu za kielimu badala ya kimawazo. Wameudhiwa na madarasa yaliyojaa pomoni, viwango vya elimu vya chini, na matatizo ya usalama yanayopatikana katika shule nyingi za umma. Wakikatishwa tamaa na matokeo ya mafunzo ya kitaasisi ambayo mara nyingi hayatii moyo, wao wanaamini kwamba wanaweza kusaidia watoto wao zaidi kwa kuwapa uangalifu wa moja kwa moja ambao huwezekana kwa masomo ya nyumbani.
Kikieleza kwa nini wengine hupendelea kusomea nyumbani, kitabu Home Schools: An Alternative husema: “Wazazi [wanaofunza nyumbani] wanahusika na watoto wao kwa asilimia 100 . . . Wanaweza kutoa uangalifu wao kwa elimu ya mtoto wao.”
JE! Kusomea Nyumbani Hufanikiwa?
Wale wanaounga mkono kusomea nyumbani husema kwamba watoto hujifunza kwa matokeo zaidi nyumbani kwa sababu masomo hufungamana na kila aina ya utendaji wa kila siku wa familia. “Familia nyingi huanza kwa kitabu cha hisabati, lakini kisha wanang’amua kwamba mafunzo yanaweza kutolewa katika maono ya kila siku,” aandika Jane A. Avner katika School Library Journal. “Kwa mfano, kununua vitu na kusawazisha hundi, kwaweza kusaidia wanafunzi wao waelewe juu ya usimamizi wa pesa, na kurekebisha vitu nyumbani kunakuwa kama kitabu kizuri cha hisabati.”
Kusomea nyumbani kumekuwa na matokeo ya aina gani? Baadhi ya uchunguzi umeonyesha kwamba wasomea nyumbani kwa ujumla hupata maksi za wastani au zilizo juu ya wastani wa kitaifa katika mitihani ya kiwango kinachokubalika. Lakini matokeo hayo hayathibitishi kwa lazima kwamba wasomea nyumbani wana elimu bora zaidi ya watoto wanaosomea shuleni.
“Ithibati ya sasa haitoshi,” chasema kitabu The Home School Manual. “Tatizo la msingi katika uchunguzi huo wote ni kwamba mtafiti hapati sehemu kubwa ya maksi za mitihani kutoka kwa wasomea nyumbani.”
“Karibu hakuna ithibati halisi inayopatikana” kuthibitisha kikamili kwamba kusomea nyumbani ni njia ya uelimishaji iliyo bora zaidi, chaeleza The Home School Manual. “Ingawa wasomea nyumbani mara nyingi hufanya vema, mpango ufaao wa kutafiti ungehitaji kuonyesha kwamba tofauti yoyote hailetwi na mambo mengineyo.”
Wengi Bado Wana Shaka
Kuna wale wanaopinga kusomea nyumbani. Maofisa wengi wa shule wameonyesha hangaiko juu ya ubora usiopatana wa elimu inayotolewa katika masomo ya nyumbani. Gazeti Time linasema: “Makusudio mazuri hayatokezi elimu thabiti moja kwa moja.”
Kwa sababu hiyo, nyakati nyingine wasimamizi wa shule hawaungi mkono, au hata wanapinga, wazazi wanapowajulisha juu ya mipango yao ya kuwafunza watoto wao wenyewe. Ingawa katika miaka ya hivi karibuni baadhi ya wasimamizi wa shule wamefanya jitihada ya kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na wale wanaosomea nyumbani, wasimamizi wengine wa shule wanaendelea kutia shaka. Shirika la Kitaifa la Wakuu wa Shule ya Msingi na Shirika la Elimu ya Kitaifa (NEA) wamechukua msimamo dhidi ya kusomea nyumbani, wakihofia kwamba huenda wazazi wengine wasiweze kuandaa elimu ifaayo nyumbani. Kulingana na taarifa rasmi ya msimamo wa NEA, “programu za kusomea nyumbani haziwezi kuandalia mwanafunzi elimu inayotia ndani mambo yote.”
Wenye kutetea kusomea nyumbani wanasema kwamba wazazi hawahitaji vyeti vya chuo ili wawe walimu bora. “Wazazi hawahitaji kujua majibu yote ili kuwatia moyo watoto wao kutafuta majibu ya maswali yao wenyewe,” chasema kitabu Home Schooling—Answering Questions. Watoto waweza kuelekezwa kwenye vyanzo vya habari vinavyofaa. Wazazi na watoto waweza kujifunza pamoja. Na mazoezi zaidi au ustadi ukihitajiwa, wakufunzi wa kibinafsi waweza kuajiriwa kwa nusu wakati.
Wachambuzi pia hudai kwamba watoto wanaosomea nyumbani huwa mbali sana na hukosa hali ya kawaida ya kuchangamana na watoto wengine wa rika lao. Pia, huo ni mkataa ambao watetezi hupinga kabisa. “Watoto hao hawawi mbali na jamii,” akasema Brian Ray, mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Elimu ya Nyumbani. “Mara nyingi wasomea nyumbani hufanya ziara za nje kwenda kwenye hifadhi ya wanyama au kwenye hifadhi ya vitu vya kale. Wao hucheza katika ujirani kama watoto wale wengine. Wazo la kwamba wao hufungiwa kwenye kabati kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa nne usiku si la kweli.”
Je! Kusomea Nyumbani Kunakufaa Wewe?
Kusomea nyumbani huhitaji, “si ujasiri tu, bali pia nguvu, ubuni, na hisia zilizo imara,” chasema Christianity Today. Kwa hiyo ikiwa unafikiria kusomea nyumbani, fikiria kwa uhalisi kuhusu daraka linalohusika. Bidii-nyendelevu na utaratibu mzuri utahitajiwa kuongezea kuandaa programu ya elimu ya kila siku kwa watoto wako. “Huenda ukafanya kazi nyingi sana hivi kwamba utake kuacha,” Ray akasema. “Ni kazi ya jasho.”
Halafu, fahamu sheria za kusomea nyumbani katika eneo lako. Kwa mfano, katika United States, kusomea nyumbani ni halali katika majimbo yote 50, lakini viwango vya sheria hutofautiana sana. Katika sehemu nyingine, kufundisha mtoto wako nyumbani humaanisha tu kujulisha msimamizi wa shule ya kwenu na kujaza fomu ya ukurasa mmoja. Katika majimbo mengine, ni lazima mzazi awe mwalimu aliyehitimu ili astahili kufundisha nyumbani. Fahamu mwongozo wa kwenu ili uweze kushikamana na matakwa yote halali yanayohitajiwa.
Kisha, fikiria gharama. Kununua vitu vya kufunzia hutokeza mojawapo tatizo kuu zaidi katika kusomea nyumbani—hasa ikiwa pesa hazitoshi. “Wewe ni kama mawindo rahisi kwa wauzaji wa vitu vya kufundishia,” yaonya A Survivor’s Guide to Home Schooling.
Ingawa wauzaji wengine hawauzi bidhaa za kusomea kwa bei ya juu, programu nyinginezo za kufunzia nyumbani hugharimu mamia ya dola. Mitihani ya kiwango kinachokubaliwa, ambayo wasomea nyumbani hutakiwa wafanye kila mwaka katika majimbo fulani, yaweza kugharimu dola 50 za U.S. kila moja. Vitabu vipya, vitabu vya kuandikia, na vitu vinginevyo vitahitajiwa mwaka baada ya mwaka, kwa hiyo bajeti ya masomo ya nyumbani iliyopangwa kwa uangalifu ni ya lazima.
Bila shaka, si wazazi wote wanaotaka na wanaoweza kutoa wakati, jitihada, na pesa ambazo wastadi wanasema zinahitajiwa ili kufanya kusomea nyumbani kufaulu. “Kusomea nyumbani hakumfai kila mtu,” akasema msichana mmoja mwenye umri wa miaka 14 aliyeanza kusomea nyumbani alipokuwa na miaka 7. “Huhitaji hali zinazofaa, mitazamo inayofaa, na wazazi wanaofaa.” Kujitia nidhamu—kwa mzazi na mtoto—kwaweza kuongezwa kwenye orodha pia. Mwanamume aliyenukuliwa mapema alisema kwamba ili kufanikisha masomo ya nyumbani, “kunahitaji kujitoa kabisa.” Yeye aliendelea: “Tatizo kuu ni kuweza kutoa wakati wa kufanya hivyo na kuendelea kufanya hivyo.”
Hata waungaji mkono hodari wa elimu ya nyumbani wanakiri kwamba masomo ya nyumbani wakati mwingine hufanywa katika njia isiyo na matokeo au hata isiyo ya kujali daraka. Kwa kweli, kila mwaka kuna wale wanaojaribu kusomea nyumbani na wanashindwa, kukiacha watoto wakiwa hawajajitayarisha kukabili magumu ya kielimu ya wakati ujao.
Isitoshe, wazazi hawapaswi kujidanganya wenyewe kwa kufikiri kwamba kusomea nyumbani pekee kutalinda watoto wao na mavutano yasiyo ya adili yanayopatikana katika shule za umma. Hakuna njia ya mtu yeyote kulindwa kabisa kutokana na ulimwengu. Mambo mengi zaidi ya shule ya msingi huongoza kufikiri kwa mtoto, kutia ndani mfano wa wazazi, mashirika, vitumbuizo, na mafunzo ya kibinafsi na ya familia. Bila mazoezi ya bidii katika sehemu hizo zote, hakuna mfumo wa elimu utakaothibitika kuwa wenye kufanikiwa katika kulea watoto Wakristo.
Ni kweli, wazazi wengine wamehisi kwamba masomo ya nyumbani yamechochea maendeleo ya kiroho ya watoto wao. Lakini haipaswi kusahauliwa kwamba vijana wengi Wakristo ambao wanaenda shule za umma wanafanya maendeleo mazuri ya kiroho pia. Katika visa vingi, wazazi wamepata matokeo mazuri katika kufanya kazi kwa ukaribu na wasimamizi wa shule ya kwao ili kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata elimu bora.
Wazazi, ambao mwishowe ndio wenye daraka la elimu na mazoezi yafaayo kwa watoto wao, wanahitaji kujiamulia wenyewe aina ya shule wanayohisi itanufaisha familia yao zaidi. Kwa hiyo changanua mambo yote kwa uangalifu kabla ya kuamua ikiwa uko tayari kuhimili kazi ya kufunza watoto wako nyumbani.
[Blabu katika ukurasa wa 12]
“Watoto wanapaswa kuwa na ratiba ya wakati kana kwamba wako shuleni.”C. F. L., mzazi aliyefunza binti nyumbani
[Picha katika ukurasa wa 10]
Ni wewe tu unayeweza kuamua yale yaliyo bora kwa mtoto wako—shule ya umma au kusomea nyumbani