Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 4/22 kur. 9-13
  • Maoni Yangu Nikiwa Mwanahistoria wa Kijeshi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maoni Yangu Nikiwa Mwanahistoria wa Kijeshi
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maswali Yaliyozushwa na Vita
  • Vita na Maashirio ya Vita
  • Kuelekea Visiwa vya Uingereza
  • Uvamizi wa Ulaya
  • Vita ya Bulge
  • Sala ya Patton
  • Kushindwa kwa Ujerumani na Ujerumani ya Baada ya Vita
  • Shughuli za Jumba la Hifadhi la Kijeshi
  • Kustaafu na Fadhaiko
  • Njia Mpya ya Maisha
  • Kutoka Kuwa Shujaa wa Vita Hadi Kuwa Askari-Jeshi wa Kristo
    Amkeni!—1998
  • Wafalme Washindani Waingia Katika Karne ya 20
    Sikiliza Unabii wa Danieli!
  • Jinsi Watu Wawezavyo Kuishi Pamoja kwa Amani
    Amkeni!—1994
  • Kutoka Jeshi la Hitler Hadi Kwenye Huduma Katika Hispania
    Amkeni!—1991
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 4/22 kur. 9-13

Maoni Yangu Nikiwa Mwanahistoria wa Kijeshi

Ilikuwa siku ya Agosti 25, 1944. Mahali: Paris, Ufaransa. Gari letu la aina ya jeep lilipokuwa likipitia barabara pana ya Champs Élysées, ilitubidi turuke nje mara nyingi na kujikinga milangoni huku risasi za walengaji shabaha wa Nazi zikipita kwa kasi hadi upande mwingine wa barabara.

KUKOMBOLEWA kwa Paris kutokana na majeshi ya Hitler wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, kulianza siku hiyo, na mimi nilikuwa miongoni mwa Waamerika wa kwanza kuingia jiji hilo. Wanaume na wanawake wengi Wafaransa wenye kushangilia walimiminika barabarani kutukaribisha sisi tukiwa wakombozi. Tulilala katika hoteli moja starehe ambayo maofisa wakuu wa Ujerumani walikuwa wameiondoka kwa haraka asubuhi hiyo.

Nilikuwa nimeenda Ulaya nikiwa mshiriki wa kikundi cha historia ya vita kilichokuwa kikishughulikia utendaji wa Jeshi la Tatu la U.S., lililoongozwa na Jenerali George S. Patton, Jr.

Maswali Yaliyozushwa na Vita

Siku chache kabla ya kuingia Paris, tulipitia barabara nyembamba ambazo zilikuwa zimeondolewa hivi karibuni magari ya vita ya Ujerumani yaliyokuwa yamechomwa. Tulitua katika ngome fulani penye miti mingi iliyopitiwa karibuni na majeshi ya U.S. Miili ya majeshi ya Ujerumani ilitapakaa huku na kule, ikiwa imepindika na kukatika-katika. Vifungo vya mishipi yao vilikuwa vimeandikwa ishara hii, “Mungu yu pamoja nasi.” Hata hivyo, kwenye ukuta wa mawe uliokuwa karibu, mwanajeshi wa Ujerumani alikuwa ameandika sihi hii, “Kiongozi [Hitler], utusaidie!”

Taarifa hizo mbili ziliniingia akilini sana. Kwa upande mmoja, utawala wa Nazi ulikazia kwamba Mungu alikuwa pamoja nao, lakini kwa upande mwingine, mwanajeshi mmoja alimsihi kiongozi, Hitler awaokoe. Nilitambua kwamba tamathali hiyo haitokani na Wajerumani tu. Hiyo ilikuwa kawaida kwa pande zote mbili zilizokuwa zikipigana vibaya sana. Kwa hiyo nilijiuliza, ‘Je! Mungu huunga mkono upande wowote vitani? Mungu anaunga mkono upande gani?’

Vita na Maashirio ya Vita

Nilizaliwa Butte, Montana, katika 1917, mwaka ambao Amerika iliingia katika vita ya ulimwengu ya kwanza. Baada ya kuhitimu katika shule ya binafsi katika 1936, niliingia Chuo Kikuu cha Stanford katika Kalifornia. Hata hivyo, niliona masomo ya waliokuwa wapya kuwa hayafurahishi yakilinganishwa na matukio yenye kusisimua yaliyokuwa yakitokea ulimwenguni pote. Japan ilikuwa imevamia Uchina, Mussolini alikuwa ameshinda Ethiopia, na Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe ya Uhispania ilikuwa ikiendelea. Katika ile vita, Wanazi, Wafashisti, na Wakomunisti walikuwa wakijaribu silaha na mbinu zao kwa kujitayarishia Vita ya Ulimwengu 2, huku Ushirika wa Mataifa ukiwapo tu usiweze kufanya kitu.

Baada ya vipindi viwili vya masomo, niliacha chuo kwa kibali cha baba, nikichagua badala yake, kutumia pesa zilizokuwa zimewekwa kando kwa ajili ya masomo yangu kusafiri hadi Ulaya na Afrika. Nilivuka Atlantiki mwisho-mwisho wa 1938 nikiwa katika meli ya Ujerumani Deutschland, na nikawa na mazungumzo marefu pamoja na maofisa wachanga wa Ujerumani waliokuwa ndani ya meli hiyo juu ya nguvu za Ujerumani ya Hitler zikilinganishwa na za milki za Uingereza na Ufaransa. Katika Paris watu walizungumzia matisho, majisifu, na ahadi za karibuni zaidi za Hitler, na bado maisha yaliendelea tu kama kawaida. Nilipokuwa nikizuru Tangier, katika Afrika, mara kwa mara ningesikia kelele za vita ng’ambo tu ya Mlango-Bahari wa Gibraltar katika Uhispania iliyokumbwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Niliporudi United States katika 1939, nilibashiri mambo mabaya kwa nyakati zetu. Wakati Wajapan walishambulia Pearl Harbor katika Desemba 1941, hivyo ikileta United States katika Vita ya Ulimwengu 2, nilijiunga na Huduma ya Uchukuzi ya Jeshi nikiwa raia. Katika 1942, nilipokuwa Alaska, niliitwa na halmashauri ya kijeshi.

Kuelekea Visiwa vya Uingereza

Baada ya kutembelea nyumbani, niliingizwa Jeshini na kukaa katika States kwa mwaka mmoja. Kisha nilipelekwa Uingereza, msafara wetu ukiondoka kutoka Pwani ya Mashariki mwa United States katika masika ya 1944. Nilionja vita kwa mara ya kwanza katika Atlantiki ya Kaskazini wakati sabmarini ya Ujerumani ilipozamisha meli iliyokuwa kando yetu. Msafara wetu ulitawanyika, na ikawa kila meli ishike njia yake kutoka hapo mpaka Liverpool.

Nikiwa ninangojea mgawo wangu katika depo moja katika Uingereza, wanajeshi walikusanywa ili wazungumziwe na kasisi wa Jeshi. Iliniudhi kwamba makasisi waliwahimiza watu waende vitani dhidi ya washiriki wa dini zao wenyewe waliokuwa upande mwingine wa vita, na bado sikuzote walidai kwamba Mungu anaunga mkono upande wao katika vita. Bila shaka Mungu hangeunga mkono pande zote.

Kufikia masika ya 1944, Visiwa vya Uingereza vilijaa majeshi ya Amerika na Uingereza pamoja na vifaa. Jenerali Patton, (chini) aliyejulikana sana kwa mbinu zake za ujasiri katika vita vya Sicily na Afrika Kaskazini, alitoa hotuba kali-kali zilizowaacha wanajeshi bila shaka yoyote juu ya kuwapo kwao huko—kuua maadui wengi kadiri ilivyowezekana kwa kila silaha inayopatikana mpaka ushindi upatikane. Patton alikuwa mfano wa mpiganaji wa kisasa: mrefu, mwenye silaha na kofia ya vita, nguo za vita nadhifu—jaketi yake ya vita iling’aa kwa nyota na mapambo mengi. Pia alikuwa mwenye bidii, mkatili sana, na mtu wa kidini—angesali kabla ya kuenda vitani.

Katika “Sala ya Majeshi” aliyotoa Januari 1, 1944, Patton alikuwa amesihi hivi: “Mungu wa Baba zetu, ambaye umetuongoza tukashinda katika bara na bahari, tafadhali endelea na uongozi huo unaovuvia katika pambano hili kuu zaidi ya yote. . . . Tupatie ushindi, Bwana.”

Uvamizi wa Ulaya

Katika Juni 6, 1944, majeshi ya Muungano yalivuka Bahari ya Uingereza katika kikundi cha manowari za vita kilichokuwa kikubwa zaidi ambacho ulimwengu ulipata kuona, wakitua katika ufuo wa Normandy huku wakishambuliwa vikali na Wajerumani. Sehemu ya ufuo iliyokuwa imeshikiliwa bado ilikuwa ndogo wakati Jeshi letu la Tatu lilipofika siku 30 baadaye. Usiku tulilala katika mashimo huku ndege za Ujerumani zikilipua mabomu kwelikweli.

Katika Julai 25, majeshi ya Muungano yaliondoka katika ile sehemu ndogo waliokuwa wameteka, na juma moja baadaye Jeshi letu la Tatu liliachiliwa livamie Peninsula ya Brittany. Kisha tukaelekea upande wa mashariki kupitia majeshi ya Ujerumani yaliyokuwa yakirudi nyuma hadi Mto Seine karibu na Paris. Kufikia Septemba, vifaru vya vita na majeshi ya Patton yalikuwa ndani sana katika mashariki mwa Ufaransa, baada ya moja ya mapambano yenye kuvutia zaidi katika historia ya kisasa. Kwa shangwe, tulifikiri mwisho wa vita ulikuwa karibu.

Hata hivyo, uwezekano huo uliondoshwa wakati vifaa vingi na majeshi mengi yalipopelekwa kwa majeshi ya Amiri Mkuu wa Uingereza Montgomery katika mapambano ya kaskazini. Huko, mashambulizi makuu yalifanywa kwa vikosi vya Ujerumani vilivyokuwa Uholanzi. Lakini msiba ulifuata wakati kikosi cha hewa kilitua bila kutazamia miongoni mwa vikosi vya Ujerumani vyenye silaha na vilivyokuwa na nguvu na kumalizwa. Sehemu iliyobaki ya vikosi vya majeshi ya Muungano vilikwama, na shambulizi hilo likashindwa.

Vita ya Bulge

Hitler na majenerali wake walitwaa fursa hiyo kujipanga upya, wakisajili wanajeshi wapya na kutayarisha kisiri kikosi kikubwa sana cha Panzer karibu na mahali majeshi ya U.S. yalikuwa machache zaidi. Mashambulizi ya Nazi, yaliyoitwa Vita ya Bulge, yalianza katika usiku wa Desemba 16 kukiwa na mawingu mazito. Yalikusudiwa yafungue njia kwa vikosi vya Ujerumani mpaka Bahari ya Kaskazini, yakigawanya majeshi ya Muungano mara mbili na kuiteka bandari ya ugavi wao mkuu.

Majeshi ya Ujerumani yalipitia sehemu hiyo ndogo na punde si punde wakateka majeshi ya Amerika katika Bastogne. Kwa haraka Jeshi la Tatu chini ya Jenerali Patton likabadilisha mwendo walo, na baada ya kutembea kwa muda mrefu, hatimaye tulifika na kushambulia vikali vikosi vya Panzer. Hata hivyo, kwa sababu ya mawingu mazito na mvua iliyoendelea karibu juma zima, mashambulizi ya ndege hayangewezekana.

Sala ya Patton

Katika Desemba 22, kitu kilitendeka kilichogusa kiini cha kutatanika kwangu kiroho. Majuma kadhaa yaliyopita, Jenerali Patton alikuwa amemwagiza mkuu wa makasisi wa vita atayarishe karatasi ya sala ambayo ingetumiwa baadaye katika ngome za Mstari wa Ujerumani na Siegfried uliokuwa umenyooka upande wa magharibi wa Mto Rhine. Lakini sasa Patton aliagiza nakala 350,000 zigawanywe kwa saa chache, kila moja kwa kila mwanajeshi wa Jeshi la Tatu. Ilisihi Baba Mweza Yote “azuie mvua hii inayonyesha kupita kiasi” na “atupatie hali ya hewa inayofaa vita” ili majeshi ya U.S. “yaharibu kabisa uonevu na uovu wa maadui zetu, na kuweka haki Yake miongoni mwa watu na mataifa.”

Kwa kustaajabisha, usiku huo mawingu yakatoweka ghafula na anga ikabaki bila mawingu kwa siku tano zilizofuata. Jambo hilo liliwezesha ndege za kivita za majeshi ya Muungano kufikia vikosi vya Nazi, zikiviharibu na kuvimaliza kabisa. Shambulizi hatari la mwisho la Hitler likakomeshwa, na majeshi yake yaliyokuwa yamepigwa yakaanza kurejea.

Patton alichachawa. “Nadhani nitaagiza sala nyingine 100,000 zichapishwe,” akasema. “Bwana yuko upande wetu, na ni lazima tujulishe Yeye juu ya mahitaji yetu.” Lakini nikajiuliza, ‘Je! mawingu hayangetoweka Desemba 23 iwe ile sala iligawanywa au la?’ Idara ya hali ya hewa ilieleza kwamba upepo baridi kutoka nyanda za Urusi ulikuwa umekuja na kutawanya mawingu mazito.

Kushindwa kwa Ujerumani na Ujerumani ya Baada ya Vita

Mashambulizi ya majira ya masika ya majeshi ya Muungano yalimaliza milki ya Hitler, ikijisalimisha katika Mei 7, 1945. Siku hiyo ilinipata katika kijiji kimoja cha Ujerumani kilichokuwa Rhineland mahali nilipokutana na yule ambaye angekuwa mke wangu mwema, Lilly, aliyetoroshwa Ubelgiji. Mnamo Novemba 1945, nilijiondoa jeshini na kujiunga na sehemu ya historia, jeshi la U.S. lililokaa Ujerumani. Mnamo Desemba, meya wa Frankfurt alitufunganisha ndoa na Lilly.

Sehemu hiyo ya historia ilikuwa na utume wa kushughulikia historia ya kukaliwa kwa Ujerumani. Ilitumia mamia ya majenerali wa Ujerumani waliotekwa katika kuandika historia ya vita kwa upande wa Ujerumani. Nilibaki Ujerumani kwa miaka mitano nikiwa mkuu wa matukio yaliyorekodiwa. Kisha, tukiwa na watoto wetu wawili, Gary na Lizette, tukahamia United States.

Baada ya kuzuru wazazi wangu, nilijiandikisha katika Chuo Kikuu cha Montana. Nilidhania kwamba ushirika wangu na jeshi ulikuwa umekwisha. Hata hivyo, katika masika ya 1954, nilipokuwa karibu kupata digrii ya elimu ya historia ya binadamu, wenzi wangu wa zamani wawili walinijulisha kwamba nafasi ya kazi ya mkurugenzi/mwangalizi wa Kituo cha Jumba la Hifadhi la Silaha za Jeshi la U.S. katika Oklahoma ilikuwa wazi. Niliomba kazi hiyo na nikakubaliwa, basi tukahama.

Shughuli za Jumba la Hifadhi la Kijeshi

Mara nyingine tena nilikuwa nikishughulikia historia ya kijeshi. Nikajiingiza katika utafiti, kupata sanii, vitu vya kuonyeshwa, matembezi, mihadhara, uchimbuzi wa akiolojia, na sherehe za kijeshi na za kihistoria. Nilipanga mchezo wa kizamani wa kikosi cha kuendesha farasi kilichoshiriki katika sherehe ya kutawazwa kwa rais katika Washington, D.C., katika 1973. Pia nilianzisha jumba la maonyesho ya bendera, ili kuonyesha historia na mapokeo ya bendera ya taifa na za vikosi vya jeshi. Kwa muda wa miaka jumba la hifadhi la silaha limepanuka kutoka kuwa jengo moja hadi kuwa jumba la hifadhi la kijeshi kubwa zaidi nchini.

Wakati uo huo watoto wetu walikuwa wakikua. Mwana wetu Gary, baada ya kuhitimu kutoka shule ya sekondari, alijisikia hana tumaini lolote. Alijiunga na Kikosi cha Wanamaji na kutumika katika Vita ya Vietnam. Baada ya kutumia miaka miwili ng’ambo, tulishukuru kwamba alirudi tena nyumbani akiwa salama. Kwa wazi, vita hushindwa kudumisha amani. Badala ya hivyo, tumeona ono lenye kuendelea la mataifa yaliyo washiriki wa Umoja wa Mataifa yakipigana yenyewe kwa yenyewe huku njaa kali na maradhi yakikumba watu wao.

Kustaafu na Fadhaiko

Hatimaye, baada ya kushirikiana na jeshi kwa miaka 33, niliamua kustaafu. Jenerali aliyekuwa akiongoza na wanajeshi walifanya sherehe maalumu ya kustaafu kwa ajili yangu, na gavana wa jimbo la Oklahoma alitangaza rasmi siku fulani kwa jina langu, Julai 20, 1979. Nilipokea barua za pongezi juu ya michango yangu katika nyanja za historia za kijeshi na majumba ya hifadhi.

Kikombe changu kilipaswa kiwe kimefurika. Lakini nilipofikiria maisha yangu, sikufurahi. Badala ya kufunua mambo hakika ya vita yanayosikitisha, kazi-maisha yangu ilikuwa imetumiwa kwa utukuzo wayo, ikikazia mapokeo, yunifomu na medali, silaha na mbinu za vita, desturi na sherehe, fahari na tamasha. Hata Jenerali Dwight D. Eisenhower, aliyekuwa baadaye rais wa 34 wa U.S., alisema hivi: “Uhalisi wa vita ni moto, njaa kali na magonjwa ya kipuku . . . nimekuja kuchukia vita. Vita haisuluhishi chochote.”

Baadaye nikajua kwamba mama ya Eisenhower alikuwa amekuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova—imani iliyokuwa tayari inanivutia kupitia funzo la Biblia la mke wangu pamoja na Mashahidi. Akawa Shahidi aliyebatizwa katika 1979, miezi sita kabla ya kustaafu kwangu. Alionekana amebadilika. Alikuwa na furaha na tamaa ya kushiriki yale aliyokuwa amejifunza hivi kwamba mwana wetu na mke wake, Karin, walianza kujifunza Biblia, na kwa muda wa mwaka mmoja wao pia wakawa Mashahidi waliobatizwa.

Hata hivyo, nilikuwa na shaka. Jambo la kwamba Mungu hasa angeingilia mambo ya kibinadamu na kuuharibu ulimwengu huu na kuleta ulimwengu mpya, usio na vita lilionekana kuwa haliwezekani. Licha ya hayo, mimi nami nikaanza kujifunza na Mashahidi, hasa ili nitambue ikiwa masadikisho yao ya kidini yalikuwa na msingi mzuri. Kwa ajili ya malezi yangu na uwezo wangu uliozoezwa wa kufanya utafiti, nilidhani kwamba nisingechukua muda mrefu kabla sijatambua makosa na kupingana kwa itikadi zao.

Njia Mpya ya Maisha

Hata hivyo, kadiri funzo langu la Biblia lilivyoendelea, upesi nilitambua jinsi nilivyokuwa nimekosea. Shaka zangu zikakwisha wakati magamba ya ujinga wa kidini yalipotoka machoni pangu. Niliweza kuona kwamba kwa kweli kuna msingi mzuri wa kuwa na hakika katika ahadi ya Mungu ya ulimwengu mpya wa uadilifu. (2 Petro 3:13; Ufunuo 21:3, 4) Na ilituliza kama nini kujifunza kwamba maovu na ukosefu wa haki ambao umejaa miongoni mwa wanadamu upo kwa sababu Shetani, bali si Mungu Mweza yote, ndiye mtawala wa mfumo huu wa mambo! (Yohana 14:30; 2 Wakorintho 4:4) Kwa hiyo, Yehova Mungu haungi mkono upande wowote katika vita vya mataifa, lakini yeye hujali wanadamu.—Yohana 3:16.

Nilibatizwa mwaka wa 1983 katika mkusanyiko mmoja wa Mashahidi wa Yehova uliokuwa Billings, Montana, hivyo nikifananisha wakfu wangu kwa Yehova. Mwana wangu Gary, nami tunatumikia tukiwa wazee katika makundi yetu mbalimbali. Lilly pamoja nami ni wenye shukrani sana kwamba Yehova, kupitia Neno lake na Mashahidi wake, amefungua mioyo yetu kwa kweli za Biblia ili tuelewe maana ya matukio yenye msiba yanayotia alama kizazi hiki. (Mathayo 24:3-14; 1 Yohana 2:17)—Kama ilivyosimuliwa na Gillett Griswold.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]

Wakazi wa Paris watawanyika wakati walengaji shabaha wa Ujerumani wanapofyatua risasi, Agosti 1944 (Picha ya U.S. National Archives)

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 10]

Picha ya U.S. National Archives

[Picha katika ukurasa wa 11]

Silaha za Ujerumani zilizoharibiwa na kuchomwa, Ufaransa, 1944

[Hisani]

Idara ya Ulinzi ya U.S.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Nikiwa pamoja na mke wangu na binti yangu katika 1947

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki