Kutoka Kuwa Shujaa wa Vita Hadi Kuwa Askari-Jeshi wa Kristo
KAMA ILIVYOSIMULIWA NA LOUIS LOLLIOT
Agosti 16, 1944, nilikuwa miongoni mwa majeshi ya Muungano yaliyotua kwenye fuo za kusini mwa Ufaransa wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili. Baada ya juma moja la mapambano kwenye Pwani ya Mediterania, kikosi chetu cha vifaru kiliingia kwenye bandari ya Marseilles na kupigana hadi mlimani kuelekea Notre-Dame-de-la-Garde Basilica. Tulikuwa na lengo la kutwaa ngome za Wajerumani zilizoko huko.
PIGANO lilikuwa kali. Kifaru kimoja katika kikosi chetu kilipigwa, na wenzangu watatu waliokuwamo wakauawa. Ndipo bomu la ardhini likalipua mmojawapo wa minyororo ya kifaru chetu, na kukiharibu. Tukiwa tumeazimia kutoshindwa, tulipigana kwa muda wa saa kadhaa zilizofuata.
Nikiwa nimebeba bunduki kwa mkono mmoja na bendera ya Ufaransa kwa mwingine, niliitumia nafasi iliyotokezwa na kutulia kwa pigano nikatembea kwa miguu pamoja na mpiganiaji mmoja wa Ukombozi wa Ufaransa. Nikiwa nimechoka na kuwa mweusi kwa baruti, niliichomelea bendera ya Ufaransa penye lango la basilika.
Ukombozi
Majuma yaliyofuata, tulielekea kaskazini tukiyaandama majeshi ya Ujerumani yaliyokuwa yakitoroka. Kwa sababu ya majeshi ya kuvizia pamoja na waya zilizopitishwa barabara kwenye kimo cha mtu, ilitubidi kusonga mbele tukiwa tumefunga milango ya vifaru vyetu.
Mwezi wa Oktoba kikosi chetu kilifika Ramonchamp, mji mdogo ulio katika Milima ya Vosges kaskazini-mashariki mwa Ufaransa. Mji huo ulionekana kama mahame. Nikiwa nimesimama sehemu ya juu ya kifaru chetu nikiyachunguza mazingira, kwa ghafula kombora lililorushwa kupitia dirisha likaingia ndani ya kifaru chetu, likalipuka na kuwaua wenzangu watatu papo hapo. Mimi na mwanajeshi mmoja tukajeruhiwa vibaya sana, na kifaru chetu kikaharibiwa. Licha ya kuwa na vipande 17 vya kombora mguuni mwangu, nilishika usukani wa kifaru huku kifaru kingine kikitukokota.
Kutokana na kisa hiki nilipokea pongezi kupitia ujumbe uliotumwa haraka. Siku chache baadaye, wakati Jenerali de Lattre de Tassigny, kamanda wa Kikosi cha Kwanza cha Ufaransa, alipokuwa akinitunukia nishani kwa yale niliyotimiza katika Marseilles, alisema: “Tutaonana tena hivi karibuni.”
Muda mfupi baadaye, niliteuliwa kuwa katibu wa kibinafsi wa huyo jenerali. Baada ya muda fulani, nikaandamana naye hadi Berlin, alikowakilisha Ufaransa wakati Ujerumani ilipokubali kushindwa Mei 8, 1945. Kwa miaka minne iliyofuata, nilimtumikia.
Lakini, ilikuwaje nikaja kuhusika na matukio muhimu ya Vita ya Ulimwengu ya Pili?
Nilifunzwa Dini na Vita Pia
Nililelewa nikiwa Mkatoliki mchaji mwenye tamaa ya kumtumikia Mungu na nchi yetu. Agosti 29, 1939, siku chache tu kabla ya Ufaransa kuingia katika Vita ya Ulimwengu ya Pili, nilijiandikisha katika kikosi cha vifaru. Nilikuwa na umri wa miaka 18 tu. Baada ya mafunzo ya miezi mitano katika École Militaire huko Paris, nilitumwa kuwa ofisa mchanga wa cheo cha chini katika eneo la vita mashariki mwa Ufaransa.
Hiki ndicho kipindi kilichoitwa vita bandia, kwa sababu hatukufanya lolote ila kuyangojea majeshi ya Wajerumani ambayo yalikuwa yakipigana katika maeneo mengine. Mnamo Juni 1940, Wajerumani waliposhambulia hatimaye, nilitekwa na kufungwa. Miezi miwili baadaye nilitoroka, na mwishowe nikajiunga na vikosi vya Ufaransa katika Afrika Kaskazini.
Kwenye mapambano dhidi ya majeshi ya Ujerumani huko Tunisia yakiongozwa na Jenerali Erwin Rommel, aliyebandikwa jina Mbweha wa Jangwa, asilimia 70 ya mwili wangu ulichomeka nikapoteza fahamu kwa siku tisa. Nililazwa hospitalini miezi mitatu katika Sidi-bel-Abbès, kaskazini-magharibi mwa Algeria, ambako makao makuu ya Kikosi cha Kigeni cha Ufaransa yalikuwa. Huko Afrika Kaskazini, nilipokea nishani ya Msalaba wa Kijeshi wa Croix de Guerre.
Makasisi Wakatoliki walituhimiza tutekeleze wajibu wetu wa “Kikristo.” Nilikuwa tayari kudhabihu uhai wangu kwa ajili ya Ufaransa kwa kutii mahimizo yao. Wakati wowote ilipowezekana, nilishiriki Komunyo Takatifu kabla ya vita. Na vita ilipopamba moto, nilisali kwa Mungu na kwa Bikira Maria.
Niliwaheshimu wanajeshi maadui, ambao wengi wao walikuwa Wakatoliki wachaji pia. Baadhi yao walivaa mshipi wenye kishikizo kilichoandikwa Gott mit uns (Mungu yuko pamoja nasi). Je, si ni jambo la ajabu kufikiri kwamba Mungu angejibu sala za makundi mawili ya wanajeshi wa dini moja yanayopigana baina yao?
Mabadiliko Baada ya Vita
Baada ya vita, Aprili 10, 1947, nilimwoa Reine, msichana kutoka mji wa Mouilleron-en-Pareds, Vendée, alikotoka Jenerali de Lattre de Tassigny. Jenerali huyo alinisimamia kwa arusi yangu. Kufuatia kifo chake, Januari 1952, nilibeba bendera yake wakati wa mazishi yake ya kitaifa.
Ndipo, asubuhi moja Jumapili mwishoni mwa 1952, wakati ambapo mimi, mke wangu, pamoja na binti yetu mchanga tulipokuwa tunajiandaa kuhudhuria Misa, Mashahidi wa Yehova wawili walibisha mlango wetu. Yale waliyosema kuihusu Biblia yaliamsha udadisi wetu. Ijapokuwa mimi na mke wangu tulikuwa watu wa kidini sana, hatukujua Biblia sana, kwa vile kanisa lilikuwa limetukataza kuisoma Biblia. Shahidi aliyejitolea kutufundisha Biblia ni Léopold Jontès, aliyekuwa wakati huo mwangalizi wa ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Ufaransa. Kutokana na funzo letu la Biblia, hatimaye niliweza kupata majibu kwa maswali yasiyojibiwa tangu utotoni.
Kwa mfano, nyakati zote nilivutiwa sana na Baba Yetu, au Sala ya Bwana. Nikiwa Mkatoliki, niliamini kwamba watu wazuri wote huenda mbinguni wanapokufa, kwa hivyo sikuelewa ni kwa nini tulisali kwa Mungu: “Mapenzi yako yafanywe duniani.” (Mathayo 6:9, 10, Douay Version; italiki ni zetu.) Wale makasisi nilioongea nao ama walihepa swali langu kuhusu jambo hili ama walisema kwamba sala hii itajibiwa wakati kila mtu atakapokuwa Mkatoliki. Lakini jibu hilo halikuniridhisha.
Wala makasisi hawakutoa majibu yenye kuridhisha kwa maswali yangu kuhusu Utatu. Fundisho hili la Kikatoliki husema, kulingana na maneno ya imani ya kanisa, kwamba ‘Baba ni Mungu, Mwana ni Mungu, na Roho Mtakatifu ni Mungu, na bado hao sio Miungu watatu bali Mungu mmoja.’ Kwa hiyo mimi na mke wangu tulifurahi sana kugundua fundisho la Biblia lililo wazi kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu na si Mungu Mweza Yote.—Marko 12:30, 32; Luka 22:42; Yohana 14:28; Matendo 2:32; 1 Wakorintho 11:3.
Sisi wawili tuliona kwamba macho yetu yamefumbuliwa kwa mara ya kwanza na kwamba tulikuwa tumepata lulu ya thamani isiyoweza kukadiriwa, kuipata hiyo lulu kulistahili dhabihu yoyote. (Mathayo 13:46) Tuling’amua kwamba ni lazima tufanye uamuzi ili tuipate hazina hii. Upesi tukawa na maoni kama ya mtume Paulo, aliyesema kwamba aliviona “vitu vyote kuwa hasara kwa sababu ya thamani iliyo bora zaidi ya ujuzi wa Kristo Yesu.” Basi tukafanya mabadiliko katika maisha yetu ili tumtumikie Mungu.—Wafilipi 3:8.
Nafanya Uamuzi
Aprili 1953, miezi michache tu baada ya Mashahidi kuanza kutufunza Biblia, niliamrishwa nijiunge na kikosi cha kijeshi cha Ufaransa walichotaka kukipeleka kupigana huko Indochina. Wakati huo, nilikuwa katibu wa kamanda mkuu wa Baraza Kuu lililoko Paris. Kwa kuwa kufikia wakati huo nilikuwa nimeelewa ile kanuni ya Biblia ya kutokuwamo, niling’amua kwamba napaswa kufanya uamuzi. (Yohana 17:16) Niliwaarifu wakubwa wangu kauli yangu ya kukataa kutii amri ya kwenda kupigana huko Indochina, nikitaja tamaa yangu ya kutoshiriki katika vita tena.—Isaya 2:4.
“Je, unatambua kwamba utashutumiwa na hutapata mapendeleo yoyote wakati ujao?” wakubwa wangu wakaniuliza. Kutokea wakati huo na kuendelea, nikapuuzwa. Lakini huu ulikuwa ulinzi, kwa vile sikuitwa tena kufanya mazoezi ya kijeshi. Watu wengi wa ukoo na marafiki hawakuelewa ni kwa nini nilikataa kile walichokiona kuwa cheo kilichotukuka katika jamii.
Kutokana na rekodi yangu ya jeshi, nilitendewa kwa staha na wenye mamlaka, walioniheshimu licha ya itikadi zangu. Kwa miaka miwili iliyofuata, nilipewa likizo ndefu kwa sababu ya afya, na haikuwa lazima nirudie tena kazi yangu. Wakati huohuo, mimi na mke wangu tulikuwa tukihudhuria mikutano katika kutaniko la Mashahidi wa Yehova la kwetu na hata tukawaeleza wengine juu ya imani yetu mpya.
Mwishowe—Askari-Jeshi wa Kristo!
Hatimaye, mapema mwaka 1955, niliondolewa wajibu wa kijeshi. Siku 15 baadaye, Machi 12, mimi na mke wangu tulionyesha wakfu wetu kwa Yehova Mungu kupitia ubatizo wa maji kwenye kusanyiko huko Versailles. Hali yangu ya kikazi ikiwa imebadilika, ilinibidi nitafute kazi tofauti ili nitunze mahitaji ya familia yangu. Kwa miaka minne iliyofuata, nilikuwa mhudumu katika soko la Halles (soko kuu), lililoko Paris. Ingawa kufanya badiliko kama hilo hakukuwa rahisi, Yehova alibariki jitihada zangu.
Kwa miaka mingi, mimi na mke wangu tumeweza kuwasaidia watu wengi kukubali ujumbe wa Biblia. Nimekuwa na fursa ya kuwaeleza wenye mamlaka mbalimbali wa jeshi na wa serikali juu ya maoni ya Mkristo kuhusu kutokuwamo. Kazi yangu ya zamani ya uanajeshi mara nyingi imenisaidia kushinda maoni mabaya ya wengi dhidi ya Mashahidi wa Yehova. Imenipa fursa ya kueleza msimamo wetu wa kutokuwamo kwa Kikristo kuhusu vita vya mataifa, nikionyesha kwamba huu ndio msimamo ambao wafuasi wa mapema wa Kristo waliuchukua. Kwa mfano, Profesa C. J. Cadoux aliandika katika kitabu chake The Early Church and the World: “Hadi kufikia utawala wa Marcus Aurelius angalau [161-180 W.K.], hakuna Mkristo angekuwa mwanajeshi baada ya kubatizwa.”
Moja ya majaribu magumu zaidi niliyokabili ni kifo cha mke wangu mwaka wa 1977. Alikufa baada ya ugonjwa wa mwaka mzima, akidhihirisha imani yake kwa ujasiri hadi kifo. Tumaini zuri ajabu la ufufuo lilinitegemeza. (Yohana 5:28, 29) Jambo jingine lililonisaidia kushinda huzuni yangu ni kujiandikisha kuwa painia wa kawaida, kama wahudumu wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova wanavyoitwa. Nilifanya hivyo mwaka wa 1982 baada ya kustaafu kazi ya kimwili. Baadaye, mwaka wa 1988, nilikuwa na furaha iliyoje kuwa mfunzi katika shule ya kufundisha mapainia!
Tangu mke wangu afe, imenilazimu kupambana na mshuko-moyo wa ghafula wa mara kwa mara. Lakini marafiki wa karibu, wenye nguvu kiroho wamenisaidia kupata nafuu. Kupitia majaribu hayo yote, siku zote nimehisi nguvu na fadhili zenye upendo za Yehova, ambaye huwatunza wote wanaomtumaini yeye. (Zaburi 18:2) Pia ninaona kwamba majaribu ambayo tunayavumilia yanaweza kutuzoeza kuendeleza vita vyetu vya kiroho. (1 Petro 1:6, 7) Nikiwa mzee kutanikoni, mimi nami nimeweza kuwasaidia wengine ambao wameshuka moyo.—1 Wathesalonike 5:14.
Nilipokuwa mvulana, nilitamani kuwa mwanajeshi, nami, kwa namna fulani, nimekuwa mwanajeshi hadi wakati huu. Niliacha jeshi moja na kujiunga na jingine, nikawa ‘askari-jeshi wa Kristo Yesu.’ (2 Timotheo 2:3) Leo, licha ya afya yangu inayozorota, najitahidi kadiri niwezavyo kuendelea kupigana nikiwa askari-jeshi wa Kristo katika “vita bora” ambayo mwishowe itatokeza ushindi, kwa heshima na utukufu wa Mungu wetu, Yehova.—1 Timotheo 1:18.
Louis Lolliot alikufa Machi 1, 1998, wakati makala hii ilipokuwa ikitayarishwa ili ichapishwe.
[Picha katika ukurasa wa 13]
Arusi yetu, iliyohudhuriwa na Jenerali de Lattre de Tassigny
[Picha katika ukurasa wa 15]
Louis Lolliot na mke wake, Reine, mwaka wa 1976