Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 5/22 kur. 3-5
  • Tatizo la Utoaji-Mimba—Je! Suluhisho Ni Kuua Milioni 60?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tatizo la Utoaji-Mimba—Je! Suluhisho Ni Kuua Milioni 60?
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Tabia Isiyofaa
  • Wanapatwa na Ujeuri au Hali?
  • Kutoa Mimba—Si Suluhisho Lisilo na Madhara
    Amkeni!—2009
  • Je, Utoaji-Mimba—Ndio Suluhisho?
    Amkeni!—1995
  • Matokeo Yenye Msiba ya Utoaji-Mimba
    Amkeni!—1993
  • Biblia Inasema Nini Kuhusu Kutoa Mimba?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 5/22 kur. 3-5

Tatizo la Utoaji-Mimba—Je! Suluhisho Ni Kuua Milioni 60?

AKIWA na wasiwasi, woga, na machozi, msichana mwenye miaka 15 atazama mpenzi wake akiondoka kwa kuchukizwa. Alimwita mjinga kwa sababu ya kupata mimba. Msichana huyo alifikiri walikuwa wamependana.

Mwanamke afadhaika sana anapong’amua kwamba ana mimba ya mtoto wake wa sita. Mume wake hana kazi, na watoto hulala njaa kila usiku. Wanawezaje kumtunza mtoto mwingine?

“Mimba hii imekuja wakati mbaya sana,” mwanamke aliyevalia vizuri aeleza daktari wake. Alikuwa amepokea shahada ya uhandisi hatimaye na alikuwa karibu kuanza kazi yake mpya ya maisha. Mume wake alikuwa amejiingiza mno katika kazi yake ya wakili. Wangepata wapi wakati wa kulea mtoto?

Maisha ya watu hao yanatofautiana sana na wanakabili matatizo tofauti, lakini wanachagua suluhisho moja: utoaji-mimba.

Utoaji-mimba ni mojapo masuala makubwa zaidi katika miaka hii, likichochea mijadala mikali katika nyanja za kisiasa, kijamii, kitiba, na kitheolojia. Katika United States, wenye kupinga utoaji-mimba huandamana wakitetea haki za watoto ambao hawajazaliwa. Kikundi cha wenye kutetea utoaji-mimba uliohalalishwa wana msingi wa sheria ya uhuru na haki ya mwanamke kujichagulia. Wenye kupinga utoaji-mimba hupambana na wenye kutetea utoaji-mimba uliohalalishwa katika uchaguzi mbalimbali, mahakamani, makanisani, na hata barabarani.

Mamilioni wamenaswa katika mzozo, wakivutwa na hoja motomoto zinazotoka kila upande. Maneno hayo “kutetea utoaji-mimba uliohalalishwa” na “kupinga utoaji-mimba” yaliteuliwa kwa uangalifu ili yashawishi wasiokuwa na uamuzi. Katika wakati huu ambao uhuru unapendwa sana, ni nani asingependelea hiari? Lakini pia, ni nani asingependelea uhai? Vikundi vinavyotetea utoaji-mimba uliohalalishwa hubeba waya za kuangika nguo za kuonyesha vifo vya wanawake waliodhulumiwa ambao hutumia njia zisizo salama na zisizo halali za utoaji-mimba (kwa kutumia waya). Wenye kupinga utoaji-mimba hubeba chupa za vijusi vilivyotolewa vikiwa ukumbusho unaohuzunisha wa mamilioni ya wafu wasiozaliwa.

Msiba huo wa kifo unaelezwa kwa usahihi sana katika kitabu cha Laurence H. Tribe Abortion: The Clash of Absolutes. “Wengi wanaoweza kutambua mara moja kwamba kijusi kwa hakika ni binadamu, wanaokiona kuwa cha maana sana na kulia machozi, mara nyingi hawaoni mwanamke yule anayekibeba na matatizo yake. . . . Wengine wengi, wanaoweza kuona mara moja mwanamke mwenye mimba na mwili wake, wanaotetea haki zake za kudhibiti wakati ujao wake, mara nyingi hawaoni kijusi kilicho ndani ya mwanamke huyo na hawaoni kuwa kingeweza kuwa na uhai wa kweli ikiwa kingepewa nafasi.”

Huku vita hii ya kiadili inapoendelea, watoto ambao hawajazaliwa milioni 50 hadi milioni 60 watakufa mwaka huu huku watu wakibishania haki.

Wewe unaunga mkono upande gani katika suala hili la kihisia-moyo? Ungejibuje maswali haya makuu: Je! ni haki ya msingi ya mwanamke kuchagua? Je! utoaji-mimba wafaa chini ya hali yoyote? Uhai huanza wakati gani? Na swali la mwisho, ambalo huulizwa mara chache sana: Muumba wa uhai na uzazi huuonaje utoaji-mimba?

Utoaji-mimba una historia ndefu. Katika Ugiriki na Roma za kale, utoaji-mimba ulikuwa zoea la kawaida. Katika Ulaya wakati wa Enzi za Katikati na wa Mvuvumko, ulikubaliwa mpaka wakati mama angehisi uhai katika tumbo lake la uzazi. Yale mapinduzi ya kingono yalikuja na matokeo mabaya—mamilioni ya mimba zisizotakikana.

Miaka ya 1960 ilianzisha ongezeko la harakati za wanawake, ambazo msingi wazo ni ile inayoitwa eti haki ya uzazi. Wengine hutetea haki za utoaji-mimba kwa wanawake waliopata mimba kutokana na kunajisiwa au ugoni wa kifamilia au wakati uhai wa mama umo hatarini. Tekinolojia ya kitiba imetokeza uwezo wa kutambua zile zinazoweza kuwa kasoro za kuzaliwa au kutambua jinsia ya mtoto aliye katika tumbo la uzazi. Mimba hutolewa kwa msingi wa matazamio mabaya ya daktari kuhusu kijusi. Wanawake wenye miaka zaidi ya 40 wanaweza kuwa na wasiwasi juu ya ulemavu wa kijusi.

Katika nchi zenye umaskini, wanawake wengi ambao hawapati kwa urahisi vizuia-mimba huhisi kwamba hawawezi kuandalia watoto zaidi. Na katika kupanua mpaka mwisho ule ufafanuzi wa kutetea utoaji-mimba uliohalalishwa, wanawake wengine wenye mimba huamua kutoa kijusi kwa sababu wanahisi kuwa wakati haufai hata kidogo kwa mimba au kwa sababu wanapata kujua jinsia ya mtoto huyo asiyezaliwa na hawataki mtoto wa jinsia hiyo.

Hoja nyingi motomoto zinazotokezwa katika pambano hilo zinashughulika na swali la wakati ambao uhai huanza. Si wengi watabisha kwamba yai lililorutubishwa linaishi. Swali ni, linaishi likiwa nini? Mnofu tu? Au ni binadamu? Je! mbegu ya mti oki ni mti huo? Basi je, kijusi ni mtu? Je! kina haki za kibinadamu? Mabishano juu ya maneno hayaishi. Inashangaza kama nini kwamba katika hospitali ileile, madaktari wanaweza kufanya kazi kwa bidii sana waokoe uhai wa mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati wake na bado wakomeshe uhai wa kijusi chenye umri uo-huo! Sheria inaweza kuwaruhusu waue mtoto aliye tumboni, lakini ni uuaji mbele ya sheria ikiwa mtoto huyo yuko nje ya tumbo la uzazi.

Madai makubwa zaidi ya kutaka utoaji-mimba uhalalishwe hutoka kwa wanawake wa kisasa “waliowekwa huru” wanaopata kwa wingi vizuia-mimba ili kwanza wazuie mimba. Wanatetea kwa bidii kile kinachoitwa haki za uzazi, ingawa kwa kweli tayari wametumia uwezo wao wa kushika mimba na kuzaa. Kile wanachotaka hasa ni haki ya kuharibu uzazi huo. Sababu yao ni nini? “Ni mwili wangu!” Lakini kweli ni mwili wao?

Kitabu Abortion—A Citizens’ Guide to the Issues chaeleza kwamba katika majuma 12 ya kwanza ya mimba, “ule mnofu kidogo sana ulioganda ni rahisi sana kuondolewa.” Je! utoaji-mimba waweza kuonwa kwa njia inayofaa kuwa “kuondolewa kwa mnofu kidogo sana” au “kukomesha matokeo ya utungaji”? Au je, maneno hayo matamu yamebuniwa ili ile kweli iliyo chungu iweze kukubalika na itulize dhamiri zinazofadhaika?

Mnofu huo kidogo usiotakwa ni uhai unaokua na kusitawi, ukiwa kamili na chembe zao za urithi. Zikiwa kama historia ya kimbele, chembe hizo zinaeleza kindani hali ya kipekee ya mtu huyo anayefanyizwa. Profesa mashuhuri wa utafiti wa vijusi A. W. Liley aeleza hivi: “Kibiolojia, hatuwezi kamwe kukubali maoni ya kwamba kijusi ni kisehemu tu cha mwili wa mama. Kiuzazi, mama na mtoto ni watu tofauti kutokea kutungwa kwa mimba.”

Tabia Isiyofaa

Hata hivyo, kwa sababu wanaweza kutoa mimba kwa urahisi, wengi hawaoni uhitaji mkubwa wa kujilinda wasishike mimba isiyotakwa. Wanapendelea kutumia utoaji-mimba kuwa jambo linalofaa la kuondoa “mimba zinazotokea kiaksidenti.”

Tarakimu zaonyesha kwamba umri wa kubalehe umeshuka katika karne hii. Kwa hiyo, watoto wachanga wanaweza kuzaa. Je! wanafundishwa daraka zito linaloandamana na pendeleo hilo? Mwamerika wa kawaida hupoteza ubikira wake kufikia umri wa miaka 16, na 1 kati ya 5 hupoteza ubikira wake kabla ya umri wa miaka 13. Theluthi moja ya wanaume na wanawake waliofunga ndoa wanaendelea na uhusiano wa kingono nje ya ndoa au walipata kufanya hivyo wakati uliopita. Utoaji-mimba hupendelewa na wengi miongoni mwa watu wanaokosa adili. Kama ilivyo na ombi la kuhalalisha umalaya ili kukomesha UKIMWI, kuhalalisha utoaji-mimba kungefanya kitendo hicho kiwe salama kadiri fulani kitiba, lakini kimechangia sana kuleta hali ambamo maradhi ya kiadili yanaweza kusitawi na hata husitawi.

Wanapatwa na Ujeuri au Hali?

Kwa kupendeza, uchunguzi mbalimbali waonyesha kwamba kushika mimba kutokana na kunajisiwa hutokea mara chache sana. Uchunguzi mmoja wa visa vya unajisi 3,500 vilivyofuatana mfululizo katika Minneapolis, U.S.A., haukutoa hata kisa kimoja cha kushika mimba. Kati ya utoaji mimba 86,000 katika ile iliyokuwa Chekoslovakia, ni mimba 22 tu zilizotolewa kwa sababu ya unajisi. Hivyo, ni sehemu kidogo sana ya wale wanaotoa mimba hufanya hivyo kwa sababu ya unajisi au ugoni wa kifamilia.

Vipi ju ya yale matabiri ya watoto waliolemaa vibaya sana wenye kasoro za kuzaliwa zisizoweza kurekebishwa? Wakiona tu ishara ya kwanza ya ulemavu, madaktari wengi hufanya haraka kupendekeza utoaji-mimba. Je! wanaweza kuwa na uhakika kabisa juu ya uchunguzi huo? Wazazi wengi wanaweza kuthibitisha kwamba matabiri hayo mabaya huenda yasiwe na msingi, na wana watoto wenye furaha na wenye afya kuthibitisha jambo hilo. Wengine wenye watoto wanaoonwa kuwa wamelemaa wanafurahi vilevile kuwa wazazi. Kwa kweli, ni asilimia 1 tu ya wale wanaotaka kutoa mimba katika United States ambao wanafanya hivyo kwa sababu ya kuelezwa juu ya uwezekano wa ulemavu katika kijusi.

Hata hivyo, kwa wakati ambao umechukua kusoma makala hii, mamia kadhaa ya watoto ambao hawajazaliwa tayari wamekufa. Jambo hilo linatukia wapi? Na maisha ya wale wanaohusika yanaathiriwaje?

[Blabu katika ukurasa wa 4]

Mama: “Ni mwili wangu!”

Mtoto: “La! ni mwili wangu!”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki