Matokeo Yenye Msiba ya Utoaji-Mimba
WATOTO ambao hawajazaliwa tokea milioni 50 hadi milioni 60 hufa kila mwaka kutokana na utoaji-mimba. Je! unaweza kuwazia idadi hiyo? Ingekuwa ni kama kufutilia mbali idadi yote ya wakazi wa Visiwa vya Hawaii kila juma!
Ni vigumu kupata hesabu kamili kwa sababu serikali nyingi haziweki kwa uangalifu rekodi za utoaji-mimba. Na katika sehemu ambazo utoaji-mimba umedhibitiwa au ni kinyume cha sheria, wataalamu wanaweza kukisia tu. Lakini utoaji-mimba wa duniani pote unakaribia mambo haya yanayofuata:
Katika United States, utoaji-mimba hutokea mara nyingi sana hivi kwamba ni wa pili tu kwa upasuaji wa kuondolewa tezi ya kooni. Kila mwaka, utoaji-mimba zaidi ya milioni 1.5 hufanywa. Wengi sana wa wanawake hawa hawajaolewa—4 kati ya 5. Wanawake waseja hukomesha mimba zao mara mbili kushinda walivyozaa, hali, kwa wastani, wanawake walioolewa huzaa mara kumi kushinda walivyotoa mimba.
Katika Amerika ya Kati na Kusini—ambazo sana ni za Kikatoliki—sheria za utoaji-mimba ni kali zaidi ulimwenguni pote. Hata hivyo, utoaji-mimba wa kinyume cha sheria ni mwingi sana, ukitokeza hatari kubwa kwa afya ya wanawake. Kwa mfano, wanawake wa Brazili, walitoa mimba milioni nne mwaka uliopita. Ilibidi zaidi ya 400,000 kati yao kutafuta utibabu kwa sababu ya madhara yaliyotokana na utoaji-mimba. Katika Amerika ya Latini, karibu robo moja ya mimba zote hutolewa.
Ukivuka Atlantiki katika bara la Afrika, sheria ni kali pia. Majeraha na vifo ni kawaida, hasa miongoni mwa wanawake maskini wanaotafuta msaada wa madaktari wasio halali.
Kotekote katika Mashariki ya Kati, nchi nyingi zina sheria kali zilizoandikwa, lakini utoaji-mimba bado hutafutwa sana na kufanywa na wanawake wanaoweza kulipa fedha nyingi.
Sehemu kubwa ya Ulaya ya Magharibi huruhusu utoaji-mimba kwa kadiri fulani, nchi za Kiskandinavia zikitoa uhuru zaidi. Huduma ya Afya ya Kitaifa ya Uingereza imeweka rekodi ya utoaji-mimba tangu uhalalishwe katika 1967. Iliona kuongezeka maradufu kwa utoaji-mimba pamoja na ongezeko la kuzaliwa kwa watoto haramu, magonjwa ya kupitishwa kingono, umalaya, na matatizo mengi yanayohusiana na uzazi.
Ulaya ya Mashariki inapatwa na mabadiliko mengi kwa sasa, na ndivyo ilivyo na sheria za utoaji-mimba za huko. Katika ile iliyokuwa Muungano wa Sovieti, utoaji-mimba hukadiriwa kuwa milioni 11 kila mwaka, mojapo hesabu za juu zaidi ulimwenguni pote. Vizuia-mimba vikiwa havipatikani sana na hali za kiuchumi zikiwa mbaya, mwanamke wa kawaida katika eneo hilo anaweza kutoa mimba kutokea mara sita hadi tisa maishani mwake.
Katika Ulaya ya Mashariki yote, mwendo wa kawaida ni kulegeza sheria. Mfano unaotazamisha ni Romania, ambapo utawala uliopita ulipiga marufuku utoaji-mimba na vizuia-mimba ili kutia-moyo ongezeko la idadi ya watu. Wanawake walishurutishwa kuzaa angalau watoto wanne, na kufikia 1988, makao ya mayatima ya Romania yalikuwa yamejaa watoto walioachwa. Hivyo, tangu serikali ya kimapinduzi ya 1989 iondoe sheria hizo juu ya utoaji-mimba, mimba za watoto 3 kati ya 4 zinatolewa, uwiano wa juu zaidi wa Ulaya.
Esia ina hesabu kubwa zaidi ya utoaji-mimba. Jamhuri ya Watu wa Uchina, ikiwa na sera yao ya kuzaa mtoto mmoja na utoaji-mimba wa kulazimishwa, inaongoza katika orodha, ikiripoti utoaji-mimba milioni 14 kila mwaka. Katika Japan, wanawake hupamba sanamu ndogo-ndogo kwa aproni na vitu vya kuchezea wakikumbuka watoto wao ambao wametoa kabla ya kuzaliwa. Umma una wasiwasi sana juu ya tembe za kudhibiti uzazi, na utoaji-mimba ndio njia ya msingi ya kudhibiti uzazi.
Kotekote katika Esia, na hasa katika India, tekinolojia ya kitiba imetokeza hali yenye kufadhaisha kwa wanaotetea haki za wanawake. Njia kama ile ya kutoa maji ya mimba na utumizi wa sauti zinaweza kutumiwa ili kutambua jinsia ya mtoto mapema zaidi na zaidi mwanzoni mwa mimba. Utamaduni wa mashariki kwa muda mrefu umethamini wana kushinda mabinti. Kwa hiyo, katika sehemu ambazo ni rahisi kutambua jinsia ya mtoto na pia kutoa mimba, vijusi vya kike vinatolewa kwa wingi sana, jambo linalosababisha ukosefu wa usawaziko katika uwiano wa wanaume kwa wanawake. Sasa harakati ya kutetea wanawake iko katika hali ngumu kwa sababu ni kama wanadai haki ya wanawake ya kutoa kijusi cha kike.
Hisi za Mama
Kama ilivyo na taratibu nyinginezo za kitiba, utoaji-mimba huwa na hatari na uchungu wa kadiri fulani. Wakati wa mimba, mlango wa tumbo la uzazi hushikana sana ili mtoto awe salama. Kupanuliwa na kuingizwa kwa vitu humo ndani kwaweza kutokeza uchungu na kufadhaisha sana. Utoaji-mimba wa kuvutwa unaweza kuchukua dakika 30 hivi, wakati ambapo wanawake wengine wanaweza kuhisi uchungu wa kiasi hadi uchungu mwingi zaidi na kiharusi. Kwa utoaji-mimba wa kutumia chumvi, uzazi wa mapema unatokezwa, wakati mwingine kwa msaada wa prostaglandin, kitu fulani kinachochochea uzazi. Mibano ya utungu yaweza kuchukua saa nyingi au hata siku kadhaa na huenda yakawa yenye maumivu makali na yenye kumaliza mtu kihisia-moyo.
Madhara ya kwanza yanayotokana na utoaji-mimba yatia ndani kuvuja damu, jeraha au kupasuka kwa shingo ya mji wa mimba, kutobolewa kwa mji wa mimba, kugandamana kwa damu, matokeo ya dawa ya nusu-kaputi kwa mwili, kutetemeka kwa mwili, homa, ubaridi, na kutapika. Hatari ya kuambukizwa ugonjwa ni ya juu sana hasa ikiwa visehemu vya kijusi au kondo ya nyuma vimebaki ndani ya tumbo la uzazi. Utoaji-mimba usiokamilika ni kawaida, na huenda upasuaji ukahitajiwa ili kuondoa mnofu unaooza uliobaki nyuma au hata kuondolewa kwa mji wa mimba wote. Uchunguzi wa serikali katika United States, Uingereza, na ile iliyokuwa Chekoslovakia waonyesha kwamba utoaji-mimba waongeza sana uwezakano wa baadaye wa kuwa tasa, kupata mimba ya mrija wa falopia, kuharibika kwa mimba, uzazi wa kabla ya wakati, na kasoro za kuzaliwa.
Aliyekuwa Mkuu wa Afya wa U.S. C. Everett Koop alionelea kwamba hakuna mtu aliyekuwa amefanya “uchunguzi juu ya matokeo ya kihisia-moyo au hatia ya mwanamke ambaye amepata kutoa mimba na ambaye sasa anatamani sana kupata mtoto asiyeweza kumpata.”
Uchunguzi wa utoaji-mimba ungalipaswa kutia ndani pia kikundi cha vijana Wakristo waliosafi kiadili wanaobaki wakiwa bikira kwa sababu ya kustahi uhai na sheria za Mungu. Uchunguzi kama huo ungalionyesha kwamba vijana hawa Wakristo hufurahia uhusiano unaofaa zaidi, hujistahi zaidi, na wana amani ya akili yenye kudumu.
Hisi za Mtoto Ambaye Hajazaliwa
Mtoto ambaye hajazaliwa huhisi nini akiwa amewekwa kwa usalama katika ujoto wa tumbo la uzazi la mama yake na kisha kushambuliwa kwa ghafula na kwa nguvu nyingi? Tunaweza kuwazia tu, kwa sababu hatuwezi kusimuliwa jambo hilo na mtu aliyejionea.
Utoaji-mimba mwingi hufanywa katika majuma 12 ya kwanza ya uhai. Kufikia hatua hiyo, kijusi hicho kidogo hujizoeza kupumua na kumeza, na moyo wacho unapiga. Kinaweza kukunja vidole vya miguu yacho, kukunja ngumi, kujivingirisha katika ulimwengu wacho wa umaji-maji—na kuhisi uchungu.
Vijusi vingi hung’olewa kwa nguvu kutoka tumbo la uzazi na kuvutwa ndani ya chupa kwa kutumia mrija wa kuvuta hewa ndani wenye ncha. Utaratibu huo unaitwa kuvutwa nje. Kivutaji hicho chenye nguvu (kina nguvu mara 29 kushinda kisafishi cha nyumbani cha kuvuta hewa ndani) hurarua mwili huo mdogo vipande vipande. Watoto wengine hutolewa kwa upanuliwaji na kwa kukomba, kupitia kisu kilichopinda kinachosugua utando wa mji wa mimba, kikikata kijusi hicho vipande-vipande.
Vijusi vya majuma zaidi ya 16 vinaweza kufa kupitia njia ya utoaji-mimba wa chumvi au kutiwa sumu kwa chumvi. Sindano ndefu inachoma mfuko wa maji ya mimba, ikitoa baadhi ya umaji-umaji huo, na kuweka badala yao myeyusho mkali wa chumvi. Mtoto anapomeza na kupumua ndani, akijaza mapafu yake mororo na myeyusho huo wenye sumu, anatapa-tapa na kupinduka-pinduka. Matokeo yenye kuunguza ya sumu hiyo yachoma ngozi ya juu, yakiiacha ikiwa imechubuka na kukauka. Ubongo wake waweza kuanza kuvuja damu. Kifo chenye maumivu makali chaweza kutokea katika muda wa saa chache, ingawa mara kwa mara utungu uanzapo siku moja hivi baadaye, mtoto ambaye angali hai lakini anayekufa huzaliwa.
Ikiwa mtoto amekua sana kiasi cha kwamba hawezi kuuawa kwa njia hizo au zinazofanana na hizo, njia moja yabaki—upasuaji wa mji wa mimba, wenye kusudi tofauti, wa kukomesha uhai badala ya kuuokoa. Tumbo la mama hupasuliwa, na karibu sikuzote mtoto ambaye angali hai hutolewa. Huenda hata akalia. Lakini ni lazima aachwe afe. Wengine huuawa kimakusudi kwa kusongwa, kuingizwa ndani ya maji, na katika njia nyinginezo.
Hisi za Daktari
Kwa karne nyingi matabibu wametumia mambo yanayoelezwa katika kile kiapo kinachoheshimiwa sana cha Hipokrate, kinachosema hivi kwa sehemu: “Sitampa mtu yeyote dawa hatari, hata akiomba, wala sitatoa shauri kama hilo, na sitapatia mwanamke yeyote chombo hatari [cha kutoa-mimba], lakini nitafanya kazi yangu bila hatia na kwa staha.”
Ni magumu gani ya kiadili hukabili madaktari wanaokomesha uhai ndani ya tumbo la uzazi? Dkt. George Flesh ayaeleza hivi: “Utoaji-mimba wangu wa kwanza-kwanza, nikiwa anayepokea mazoezi maalum ya tiba na pia nikiwa katika mtaala wa juu wa kitiba, haukufadhaisha hisiamoyo zangu. . . . Nilianza kuhisi uchungu baada ya kutoa mamia ya mimba. . . . Kwa nini nilibadilika? Mapema katika kazi yangu, wenzi wa ndoa walinijia na kuomba utoaji-mimba. Kwa sababu shingo ya mji wa mimba ilishikana sana, nilishindwa kuipanua ili nitoe mimba hiyo. Nikamwuliza arudi katika muda wa juma moja, wakati ambapo shingo ya mji wa mimba ingekuwa nyororo zaidi. Wenzi hao walirudi na kuniambia kwamba walikuwa wamebadili maoni yao. Nilizalisha mtoto wao miezi saba baadaye.
“Miaka mingi baadaye, nilicheza na Jeffrey mchanga katika dimbwi la kuogelea la klabu ya tenisi ambapo wazazi wake nami tulikuwa wanachama. Alikuwa mwenye furaha na mwenye sura nzuri. Iliniogofya sana kufikiria kwamba ni jambo dogo tu lililonizuia nisikomeshe uhai wa Jeffrey. . . . Ninaamini kwamba kukata-kata katika visehemu-sehemu kijusi ambacho kimekua, kwa ajili tu ya ombi la mama, ni kitendo kilichopotoka ambacho jamii haipasi kukiruhusu.”
Mwuguzi mmoja aliyeacha kusaidia katika utoaji-mimba alisema hivi juu ya kazi yake katika kliniki ya utoaji-mimba: “Mojapo kazi yetu ilikuwa ni kuhesabu visehemu [vya mwili wa watoto]. . . . Msichana akienda nyumbani akiwa bado na visehemu vya mtoto ndani yake, matatizo makubwa yanaweza kutokea. Ningechukua visehemu hivyo na kuvichunguza kwa uangalifu ili nihakikishe kwamba kulikuwa na mikono miwili, miguu miwili, kiwiliwili, na kichwa. . . . Nina watoto wanne. . . . Kulikuwa na hitilafiano kubwa kati ya maisha yangu ya kikazi na maisha yangu binafsi ambalo nisingeweza kupatanisha. . . . Utoaji-mimba ni jambo gumu.”
[Picha katika ukurasa wa 7]
Katika Esia, ambako watoto wa kiume hupendelewa zaidi, madaktari hutoa maelfu ya vijusi vya kike
[Hisani]
Picha: Jean-Luc Bitton/Sipa Press
[Picha katika ukurasa wa 8]
Mwandishi wa habari katika maandamano ya kupinga utoaji-mimba akipiga picha kijusi cha majuma 20 kilichotolewa kihalali
[Hisani]
Picha: Nina Berman/Sipa Press
[Picha katika ukurasa wa 8]
Maandamano ya kutetea utoaji-mimba katika Washington, D.C., U.S.A.
[Hisani]
Picha: Rose Marston/Sipa Press
[Picha katika ukurasa wa 9]
Katika United States, wanawake 4 kati ya 5 wanaotaka kutoa mimba ni waseja