Farasi Walikuwa Maisha Yangu
Kwato ndogo sana zilijitokeza kwanza, zikifuatwa na kichwa kilicholalia miguu ya mbele. Mabega yalinitatiza kidogo, lakini sehemu iliyobaki ilitoka nje haraka sana. Mara kiungamwana kilipokatwa, farasi huyo wa kike alisimama, akilialia kwa furaha na akitaka sana kumwona mtoto wake.
HIYO ilikuwa tu mojapo zile nyakati nyingi ambapo ilinilazimu kuondoka kitandani usiku ili nisaidie “mama” aliyekuwa katika dhiki. Nilikubali kazi hiyo bila kulalamika. Waona, kufuga farasi wa aina bora kabisa kulikuwa pendezi langu kubwa.
Upendo wangu wa farasi ulianza mapema sana maishani mwangu. Nilianza kupanda farasi nilipokuwa na miaka sita. Nikiwa nimezaliwa katika mji wa Roncq, kaskazini mwa Ufaransa, nililelewa na wazazi Wakatoliki, walionipeleka katika shule ya bweni ya Katoliki kwa masomo yangu ya shule ya upili. Hakukuwa shule za kufunza kufuga farasi, kwa hiyo niliamua kuacha shule na kuanza kazi-maisha ya kufuga farasi. Nilianza kuzoezwa katika Chantilly, mji uliokuwa kaskazini mwa Paris uliojulikana sana kwa farasi wa aina bora kabisa. Huko nilitambua jinsi ulimwengu wa mashindano ya mbio za farasi ulivyokuwa na matakwa mengi na magumu mengi sana. Kwa nini matakwa mengi? Farasi wa mashindano ya mbio wanaweza kulinganishwa na wanariadha hodari—wanahitaji uangalifu wa daima.
Kuwazoeza Farasi wa Mashindano ya Mbio
Ule wakati mgumu wa mazoezi na matayarisho mara nyingi huanza wakati wa vuli wakati farasi wana umri wa miezi 18. Ni lazima wazoee mazingira yao mapya na kujifunza kuacha michezo yao mingi ya awali, na kuchukua kwa uzito kazi yao. Kwanza, ni lazima mzoezaji amzoeze farasi kutumia hatamu, jambo ambalo si rahisi.
Kufunga tu kamba ya matandiko ya farasi kwaweza kumfanya farasi arukeruke! Farasi huyo mchanga ni lazima afundishwe kuzoea tandiko, na hatimaye wakati waja wa farasi kupandwa kwa mara ya kwanza. Mpandaji wa kwanza mara nyingi huchaguliwa kutoka kwa wale wanaojizoeza kuwa wapandaji farasi wa mashindano ya mbio. Hivyo, wengi wao hupata kuangushwa chini kwa mara ya kwanza wakati huo! Kuwazoeza farasi huhitaji ustadi mwingi na saburi nyingi, pamoja na wepesi wa kutambua mambo. Kwa kweli, ikiwa mnyama huyo amefadhaishwa, huenda maisha yake yote ya mashindano ya mbio yakahatarishwa.
Mapema kila asubuhi, tulikuwa tukiwapeleka farasi nje kuwafundisha njia tofauti za mwendo—yaani kutembea, mwendo wa matiti, na mwendo wa taratibu—zote ambazo ni sehemu zinazohitajiwa za mazoezi. Anapozoezwa, ni lazima farasi abadilishe kwa mafanikio namna za mwendo kulingana na maagizo. Hata hivyo, mwendo wa kasi huruhusiwa mara kwa mara, jambo hilo likiruhusu farasi akimbie atakavyo kwa mwendo mfupi.
Mwishoni mwa asubuhi, tulirudi kwenye mabanda ili farasi wachanwe kwa uangalifu sana. Ishara zote za jasho ziliondolewa, na kwato wazo zilisafishwa kwa uangalifu.
Ikiwa farasi anafanya maendeleo mazuri, anaweza kuanza kushiriki katika mashindano ya mbio za farasi wa miaka miwili kufikia mwisho wa kipupwe. Kazi ya farasi wa aina bora kabisa mara nyingi huisha mwishoni mwa mwaka wake wa tatu au, ikizidi, mwaka wake wa nne. Hata hivyo, farasi wenye kuvuta vigari, huendelea na mashindano ya mbio hadi wafikie umri wa miaka minane.
Ndoto Zangu Zatimia
Kwa vile nilipendezwa hasa na kufuga farasi, nilianza kujizoeza katika shamba la kufuga farasi katika Normandy, kaskazini-magharibi mwa Ufaransa—eneo bora sana la kufuga farasi wa mashindano ya mbio kwa sababu ya hali yalo ya hewa na malisho yalo mabichi. Miezi kumi na minane baadaye nikawa mkurugenzi msaidizi wa Shamba la Kufuga Farasi la Bois-Roussel, lililokuwa kubwa zaidi katika Ulaya wakati huo, likiwa na farasi 300 wa kutunzwa na eneo la mamia ya hektari.
Katika Shamba la Kufuga Farasi la Bois-Roussel, nilikutana na mwanamke ambaye baadaye alikuja kuwa mke wangu; alikuwa akifanya kazi hapo akiwa karani. Sikujua jinsi jambo hilo lingekuja kushawishi maisha yangu. Waona, alifahamiana na Mashahidi wa Yehova na akaanza kunizungumzia juu yao. Sikupendezwa wakati huo.
Mkurugenzi aliposikia mipango yetu ya kuoana miezi michache ijayo, alituuliza kama tungesimamia shamba jingine la kufuga farasi ambalo alikuwa mmoja wa wamiliki. Hivyo, ndoto zangu kubwa zaidi zikatimia. Hapa nilikuwa mkurugenzi wa shamba mashuhuri sana la kufuga farasi nikiwa na miaka 24! Kuna wakurugenzi wachache sana wa mashamba ya kufuga farasi katika Ufaransa; kwa kawaida vyeo hivyo hupewa washiriki wa kikundi cha watu wanaohusika na mashindano ya mbio za farasi. Likiwa dogo kuliko Bois-Roussel, Shamba la Ufugaji linaloitwa La Louvière lilikuwa katika Normandy na kwangu hilo lilikuwa paradiso ndogo yenye hektari 100, likiwa na farasi karibu mia moja, tukihesabu farasi dume, wa kike, na watoto.
Kwa vile mkurugenzi wa kwanza angeendelea kukaa kwa majuma sita, mwenye shamba hilo alijitolea kutupeleka United States kwa muda huo. Tulizuru mashamba makubwa ya kufuga farasi ya Amerika ili kujifunza njia zao za uzalishaji na tukawasiliana na mashamba kadhaa ambako baadaye tungepeleka farasi zetu wa kike wazalishwe na farasi dume zao.
Maisha Katika Shamba la Kufuga Farasi
Maisha katika shamba la kufuga farasi yana shughuli nyingi sana lakini hayachoshi. Kwa kweli yalituridhisha sana, kwa sababu tuliona mambo ya asili wakati wote na tulikuwa na wanyama wazuri wenye afya wa kutunza. Asubuhi tuliamkia sauti nyororo ya farasi wakila nyasi mbichi. Jambo hilo lilinifurahisha kama nini!
Kazi katika shamba imegawanywa katika msimu wa kushika mimba na wa kuzaa, wa watoto kuachishwa kunyonya, na wa kuuza farasi wachanga wa aina bora kabisa. Farasi dume huteuliwa kwa uangalifu kwa msingi wa rekodi yao nzuri ya mashindano ya mbio, na pia ukoo wa uzazi na nasaba yake. Kila wakati majira ya kipupwe yanapokwisha farasi jike karibu 40 huzalishwa, na fedha zinazoweza kufikia dola (za U.S) mia moja elfu zaweza kulipwa ili farasi dume mwenye rekodi nzuri aweze kuzalisha. Kwa sababu ya mambo hayo, si vigumu kuelewa ni kwa nini utunzaji mwingi hutumiwa wakati wa kushika mimba na wa kuzaa.
Kwa tukio baya, aksidenti pia hutokea, na nyakati nyingine mtoto mchanga ni yatima tokea uzazi. Katika hali kama hiyo, tunakabili hali ngumu ya kushawishi farasi wa kike amtunze. Farasi huyo huzuiwa kwa muda wa saa 48 na wafanyakazi wa vibanda wanaobadilishana zamu usiku na mchana, wakati mtoto mdogo anapoletwa karibu ili kunyonya. Farasi huyo ni lazima ashikwe ili asimpige teke mtoto, kwa vile anaweza kumwua yatima huyo kwa urahisi sana. Mguu mmoja wa mbele wa farasi huyo ni lazima ushikwe kwenye tumbo na mdomo wake wa juu kufinywa ili kumzuia.
Hatimaye, farasi huyo huanza kuchoka, na mwishowe mafanikio hufuata anapokubali mtoto huyo. Mara nyingi mama huyo mpya humlinda sana hivi kwamba inakuwa vigumu hata kumkaribia mtoto huyo. Ni lazima uzazi huo uripotiwe mara hiyo katika Usajili wa Kitaifa wa Ufaransa, ambapo anaorodheshwa chini ya aina hususa ya kizazi chake.
Farasi na Watoto Wao
Siku chache baada ya kuzaa, farasi hao wa kike wakifuatwa na watoto wao, hupelekwa uwanjani. Na kama ilivyo na wanyama wengi wachanga, watoto huanza kurukaruka sana, wakicheza kwa shangwe kando ya mama zao na kupiga mateke pande zote. Ni furaha kama nini kuwatazama wakirukaruka, wakijiinua, na kujifingirisha katika nyasi! Wanapenda maji na hujibwaga wenyewe ndani kwa kuchachawa, huku wakichapa miguu muda huo wote.
Farasi hawapendi kukaa peke yao na huhisi uchovu kwa urahisi. Hata hivyo, farasi dume na wana-farasi wanaozoezwa ni lazima watenganishwe. Ikiwa farasi hawezi kuvumilia upweke, basi ni lazima mnyama mwenzi atafutwe. Ilitulazimu tumpe mmoja wa farasi zetu dume kondoo. Walisikilizana vizuri. Kwa kweli, kondoo huyo alikataa kumwacha farasi huyo mchana au usiku. Farasi mmoja bingwa wa mashindano ya mbio aliyeitwa Allez France alikuwa na mwenzi kondoo aliyeandamana naye hata kwenye sehemu za mashindano ya mbio—ingawa si katika mashindano ya mbio yenyewe!
Mwezi wa Agosti huleta wakati wa kuachishwa kunyonya, wakati wa huzuni kwa mama na watoto. Ni lazima watenganishwe na wasikubaliwe kuonana wala hata kusikia sauti ya mmoja na mwenzake. Watoto huonyesha huzuni yao kwa kulia nyakati zote kwa siku kadhaa, wakipoa baada ya hapo. Katika Januari 1 wa mwaka unaofuata kuzaliwa kwao, wanaitwa wanamwaka. Katika minada ya kila mwaka huko Deauville, bei ya farasi hao wa mwaka mmoja waweza kupita kwa urahisi dola (za U.S.) milioni moja.
Baadhi ya farasi waliozaliwa na kukuzwa katika shamba letu la kufuga farasi walifanikiwa katika mashindano yao ya mbio. Mmoja wa hao alikuwa High Echelon, aliyeshinda mashindano ya mbio ya Prix d’Amèrique katika 1979, akiwa bingwa wa dunia katika mbio ya mwendo wa matiti. Pia tulifuga farasi wengine wa aina bora kabisa walioshinda hesabu fulani za mashindano ya mbio mashuhuri.
Naletewa Kweli
Miezi kadhaa ilipita tukiwa kwenye shamba hilo jipya bila kutembelewa na Mashahidi wa Yehova. Kwa hiyo mke wangu akadokeza kwamba niandikie kundi la karibu zaidi ili tuulize mtu atutembelee. Siku chache baadaye, wenzi wa ndoa wakaja mlangoni petu. Mimi binafsi, sikuamini kwamba Biblia ilieleza kwa usahihi siku zetu. Mke wangu aliponiambia kwamba Ufalme wa Mungu ulikuwa umesimamishwa katika 1914, nilihisi hiyo ilikuwa tu ni fasiri ya Mashahidi. Sikuwa nimepata kuona tarehe hiyo katika Biblia.
Tulikuwa na mazungumzo marefu na wenzi hao, waliokuwa waeneza evanjeli wa wakati wote, na maelezo yao—hasa katika kitabu cha Danieli—yaliamsha kupendezwa kwangu, nami nikakubali funzo la Biblia. Hata hivyo, ilikuwa vigumu kupata nafasi ya kujifunza, kwa sababu nilikuwa nimejiingiza mno katika kazi yangu.
Wenzi hao walisafiri kilometa 25 kutuzuru na mara nyingi walikuwa wakirudi nyumbani bila kuongoza funzo letu la Biblia kwa sababu nilikuwa nimelazimika kubaki na farasi mgonjwa au kuchunga farasi aliyekuwa akizaa. Lakini nilipokuza uthamini wa uhitaji wa kutanguliza mapendezi ya Ufalme na uadilifu wa Mungu, nilichukua hatua za ‘kununua wakati’ wa kujifunza.—Waefeso 5:16; Mathayo 6:33.
Nakabiliwa na Uchaguzi
Tulianza kuhudhuria mikutano upesi, na miezi sita baadaye nilihudhuria Kusanyiko la Wilaya la “Enzi Kuu ya Kimungu” katika Annecy, kusini-mashariki mwa Ufaransa. Wakati wa mkusanyiko huo, nilianza kung’amua kwamba kazi yangu haikupatana na Biblia. Nilikuja kuelewa kanuni inayoelezwa katika Isaya 65:11, inayoonyesha wazi kwamba wale ‘wanaoandika meza kwa ajili ya [mungu wa] bahati’ hawawezi kupata upendeleo wa Mungu. Kwa kuwa tulikuwa tukifuga farasi wa mashindano ya mbio pekee, tulikuwa tukichangia kwa njia isiyo ya moja kwa moja ile biashara ya kamari. Dhamiri zetu hazingeturuhusu tubatizwe.
Wakati ulikuwa umefika wa kufanya uamuzi mzito. Je! ningeendelea na kazi yangu niliyoipenda sana au ningeweka wakfu maisha yangu kwa Yehova Mungu? Kwa vile mapenzi ya Mungu yalikuja kuwa ya maana zaidi maishani mwangu, nilizungumza jambo hilo na wale wamiliki wawili wa shamba hilo na kuandika barua ya kujiuzulu. Ilinibidi nikae mwaka mwingine mmoja nikingojea mtu wa kuchukua mahali pangu, lakini katika kusanyiko la mzunguko lililofuata, lililofanywa mnamo Septemba 1976 katika Gargenville (eneo la Paris), mke wangu nami tulibatizwa.
Katika ulimwengu wa wafuga farasi, watu wengi walikuja kujua uamuzi wangu. Nakumbuka hasa mpasuaji mmoja wa hospitali aliyekuja kuzuru shamba hilo. Alisema kwamba kwa maoni ya kiadili alielewa ni kwa nini nilifanya uamuzi huo. Akitazama huku na huku, alivutiwa na ufanisi wa shamba hilo la kufuga farasi—matuta ya maua yenye rangi za kupendeza, vijumba vya mbao katika vibanda vya farasi, na kilometa nyingi za ua safi nyeupe. Alinieleza kwamba kwa kutofautisha alikuwa ameshindwa kupata fedha za kutosha za kurekebisha na kupamba hospitali yake.
Sijapata kusikitika juu ya uamuzi wangu. Mke wangu nami tuliondoka Ufaransa mapema katika 1992 ili tutumikie katika eneo linalosema Kifaransa ambako uhitaji ulikuwa mkubwa zaidi wa wapiga mbiu ya Ufalme. Huko, nina pendeleo la kutumikia nikiwa mzee katika kundi la Mashahidi wa Yehova. Tunashiriki maoni ya mtume Paulo yaliyoelezwa katika Wafilipi 3:8: “Nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo.”
Mke wangu nami bado twapenda vitu vya asili na wanyama, hasa farasi. Tunatazamia siku ambapo uhusiano wa binadamu na wanyama hautategemea mapato ya ubinafsi.—Kama ilivyosimuliwa na Stephane Jesuspret.