Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 6/22 kur. 4-7
  • Kufanya Kazi kwa Bidii—Je! Kunahatarisha Afya Yako?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kufanya Kazi kwa Bidii—Je! Kunahatarisha Afya Yako?
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uchovu na Mshuko wa Moyo
  • Maisha ya Familia Yaharibiwa
  • Kuzeeka Lakini Bila Uradhi
  • Kuungua Nishati Ni Zamu Yako?
    Amkeni!—1995
  • Kuungua Nishati—Ni Nani Aliye Hatarini na kwa Nini?
    Amkeni!—1995
  • Kuungua Nishati—Waweza Kuikabilije Hali?
    Amkeni!—1995
  • Jinsi ya Kukabiliana na Uchovu Mwingi
    Amkeni!—2014
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 6/22 kur. 4-7

Kufanya Kazi kwa Bidii—Je! Kunahatarisha Afya Yako?

AKIANGUKIA gari lake, muuzaji mmoja wa bima mwenye umri wa makamo alitapika na kuzimia. Alikuwa bado anashikilia mfuko wake, ishara ya kazi yake. Akifanya kazi kwa kutii ile shime ya kampuni yake, “Sasa ndio wakati muhimu. Tumia kabisa nguvu zako kufikia asilimia 150 ya uwezo wayo,” alikuwa ameendesha gari lake kilometa zapata 3,000 katika mwezi ambao alizimia. Akafa siku nne baadaye.

Hicho si kisa cha pekee. “Mashujaa wa makampuni,” kama wanavyoitwa katika Japani, huhofu sana karoshi, au kifo kinachosababishwa na kufanya kazi nyingi kupita kiasi. Wakili mmoja wa sheria ambaye ni mtaalamu wa kesi kama hizo anakadiria kwamba kuna “angalau watu 30,000 wanaopatwa na karoshi katika Japani kila mwaka.” Si ajabu kwamba zaidi ya asilimia 40 ya wafanyakazi wa ofisi wa Japani waliochunguzwa karibuni walihofu uwezekano wa kifo kinachosababishwa na kufanya kazi nyingi kupita kiasi.

Ingawa ni vigumu kuthibitisha uhusiano uliopo kati ya kufanya kazi nyingi kupita kiasi na matatizo ya afya, familia za watu wanaopatwa na hali hizo hawana shaka. Kwa kweli, maneno “kifo kutokana na kufanya kazi nyingi kupita kiasi” yalibuniwa na familia zilizofiwa zilizokuwa zikidai ridhaa. “Kwa maoni ya kitiba,” asema Tetsunojo Uehata wa Taasisi ya Afya ya Umma katika Japani, “maneno hayo yanarejezea kifo au ulemavu unaotokana na ugonjwa wa ghafula wa ubongo, kufa kwa misuli ya moyo kwa sababu ya kufungwa kwa mishipa, au maradhi ya moyo yanayotokana na kazi nyingi mno inayoongezea msukumo mkubwa wa damu au mishipa ya arteri kunenepa na kuwa migumu.” Ripoti ya hivi karibuni ya Wizara ya Afya na Hali Njema ya Japani inaonya kwamba kazi ya baada ya saa za kawaida inayofanywa daima hufanya mtu asipate usingizi na hatimaye huongoza kwenye afya mbaya na ugonjwa.

Lakini, kama vile wavutaji sigareti huwa hawataki kukubali kwamba kuna hatari za kuvuta sigareti, na walevi hawataki kukubali hatari za ulevi, watu wanaofanya kazi nyingi kupita kiasi hawataki kukubali hatari za kufanya kazi kwa muda wa saa nyingi isivyo kawaida. Na kifo si hatari pekee iliyopo.

Uchovu na Mshuko wa Moyo

Ingawa baadhi ya watu wanaofanya kazi nyingi kupita kiasi hupatwa na ulemavu na kifo, wengine hupatwa na uchovu. “Uchovu hauna ufafanuzi hususa wa kitiba,” laeleza gazeti Fortune, “lakini dalili za kawaida zinazokubalika zinatia ndani kuchoka, kukosa furaha, kukosa kwenda kazini mara kwa mara, matatizo zaidi ya afya, na kutumia dawa za kulevya na kuwa mlevi.” Wachovu wengine huwa wakali, huku wengine wakianza kufanya makosa bila kujali. Hata hivyo, watu hupatwaje na hali ya uchovu wa kazi?

Kwa kawaida, si wale wanaoshindwa kupatana na hali au wenye masumbufu ya moyoni wanaopatwa na hali hiyo. Mara nyingi ni watu wanaojali sana kazi yao. Huenda wanajitahidi kuendelea katika mashindano makali au wanajitahidi kupata vyeo kazini. Wanafanya kazi kwa muda mrefu na kwa bidii, wakijaribu kudhibiti kabisa kazi yao. Lakini ujitoaji wao thabiti na kazi yao isiyokoma isipoleta uradhi na mafanikio yaliyotarajiwa, wanatamauka, wanahisi wamechoka, na kupatwa na hali ya uchovu wa kazi.

Matokeo ni nini? Katika Tokyo, huduma ya simu iitwayo Life Line, iliyoanzishwa kwa ajili ya watu ambao wangejiua, inapata simu nyingi zaidi na zaidi kutoka kwa wafanyakazi wenye umri wa makamo na wafanyakazi wa ofisi wenye umri mkubwa zaidi wanaofadhaika. Kati ya watu zaidi ya 25,000 waliojiua katika Japani mwaka 1986, asilimia 40 yenye kustaajabisha walikuwa katika miaka yao ya 40 na 50, na asilimia 70 yao walikuwa wanaume. “Ni kwa sababu kushuka moyo miongoni mwa wafanyakazi wenye umri wa makamo kunaongezeka,” aomboleza Hiroshi Inamura, profesa wa matatizo ya akili.

Kisha kuna lile linaloitwa fadhaiko la likizo. Dalili yalo ni nini? Kuudhika wakati wa likizo kwa kukosa kitu cha kufanya. Akisukumwa na tamaa kubwa ya kufanya kazi, dhamiri ya mtu anayejitoa kwa kazi humsumbua wakati anapokuwa likizoni. Akishindwa kupata amani ya akili, yeye hutembea huku na huku katika chumba chake kidogo kama mnyama katika kizimba. Jumatatu inapofika, basi aenda ofisini, akiwa amefarijika.

Aina fulani ya pekee ya mshuko wa moyo inayofanya wafanyakazi wenye umri wa makamo wamwone daktari ni ule unaoitwa eti ugonjwa wa kuogopa nyumbani. Wafanyakazi wachovu hukaa katika mikahawa au mabaa baada ya kazi. Hatimaye, wao huacha kuenda nyumbani kabisa. Ni kwa nini wao huogopa kurudi nyumbani? Ingawa sababu moja yaweza kuwa ni wenzi wa ndoa wasiowahurumia, “wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii sana na wakapoteza uwezo wa kupatana na hali iliyo nje ya mahali pa kazi, hata katika visa vingi kwa familia zao wenyewe,” asema Dakt. Toru Sekiya, anayeandaa “Mfumo wa Hospitali ya Usiku” kwa wagonjwa kama hao.

Maisha ya Familia Yaharibiwa

Huenda mtu anayefanya kazi nyingi kupita kiasi asiwe ndiye anayeumia sana. Ugonjwa wa kufanya kazi nyingi kupita kiasi “mara nyingi huwa ni tatizo zaidi kwa wale wanaoishi na mtu anayefanya kazi nyingi kupita kiasi,” laonelea gazeti Entrepreneur. Maisha ya mwenzi wa ndoa yaweza kugeuka kuwa maisha yenye hofu. Mwenzi anayefanya kazi nyingi kupita kiasi “tayari amepata kitu cha maana zaidi maishani mwake,” lasema gazeti The Bulletin la Sydney, Australia, na “si rahisi sikuzote kukubali kuwa wa pili.” Ni nini hutendeka katika ndoa kama hiyo?

Chukua kisa cha Larry, Mwamerika aliyeajiriwa na kampuni ya Japani katika United States. Alifanya kazi nyingi za baada ya kazi bila kulipwa, akiongezea mazao ya kiwanda hicho kwa asilimia 234. Mafanikio na furaha? “Kichaa!” akataja mke wake mahakamani alipokuwa akimtaliki mume wake.

Kisa kingine kilichokuwa kibaya hata zaidi kilikuwa cha ofisa mmoja wa biashara wa Japani aliyekuwa akienda kazini saa kumi na moja asubuhi na hakuwa akirudi nyumbani kabla ya saa tatu usiku. Mke wake akaanza kunywa pombe kupita kiasi. Siku moja, walipokuwa wakigombana juu ya unywaji pombe wa mke wake, mtu huyo alimnyonga mkewe. Hakimu alimpata na hatia ya kuua na akasema: “Ukiwa umejitoa kabisa kwa kazi yako, hukutambua upweke wa mke wako na hukujitahidi kumpa sababu za kufurahia maisha.”

Kunyonga mwenzi wa ndoa ni kitendo kinachopita kiasi, lakini kufanya kazi nyingi kupita kiasi kunaweza kuharibu familia katika njia nyinginezo. Mume akiwapo nyumbani siku za Jumapili, huenda akaketi tu kutazama televisheni inayoonyesha programu ya michezo anayopenda zaidi na kusinzia alasiri nzima. Waume hao hawang’amui jinsi wamepuuza pande fulani za maisha. Wakiwa wamelemewa na kazi yao, wanapuuza kitu chenye thamani zaidi maishani, familia yao. Wakipuuza uhitaji wa kuwasiliana na familia, wanafuata mwendo ambao unaongoza kwenye ustaafu ulio wa upweke.

Kuzeeka Lakini Bila Uradhi

Kitabu At Work kilitahadharisha hivi kwenye utangulizi wacho: “Katika jamii yetu, . . . ufungamano kati ya kazi, kujistahi na cheo katika jamii ni wenye nguvu sana hivi kwamba wakati wa kustaafu, wengine huona ikiwa vigumu sana kujipatanisha na maisha bila kazi yao ya zamani.” Ni lazima wale wanaoifanya kazi iwe jambo kuu maishani mwao wajiulize swali hili: ‘Nitabaki na nini nikipoteza kazi yangu?’ Kumbuka, mtu anapostaafu, maisha yake huenda yakahusisha familia na jumuiya yake.

Wale ambao wamepuuza uhitaji wa kuwasiliana na familia na majirani zao hawana uhakika wa mambo ya kusema nao baada ya kustaafu. “Wanavuna matokeo ya kutofikiria kitu kingine ila kazi, ama sivyo?” asema mshauri mwenye ujuzi wa wenzi wa ndoa walio na umri wa makamo katika Japani. “Maisha zao zilikosa hali ya kushirikiana na watu wengine, nao walifikiria kwamba wana uhusiano mzuri na familia eti kwa sababu tu walikuwa wakiandaa riziki. Hata hivyo, wanapostaafu, wanapata kwamba hali ni kama zimebadilika.”

Miaka hiyo yote 30 au 40 ya kazi ngumu, eti kwa ajili ya familia yaweza kuwa na matokeo mabaya. Ni jambo la kuhuzunisha kama nini ikiwa baada ya miaka mingi ya kazi ngumu, wale waliokuwa waandaaji wa riziki wanaonwa na familia zao kuwa “takataka za viwanda” na nureochiba (matawi yenye unyevu yaliyoanguka). Msemo huo wa mwisho hutumiwa katika Japani kueleza juu ya waume waliostaafu ambao hawana kitu cha kufanya ila kukaa tu na wake zao siku nzima. Hivyo wanafananishwa na matawi yenye unyevu yanayokwama kwenye ufagio na hayawezi kuondolewa, yakiwa tu masumbufu.

Ukifikiria hatari zote zinazohusika, ni kawaida tu kuuliza, Kufanya kazi kwa bidii kunaweza kunufaishaje kwelikweli? Je! kuna kazi inayoleta uradhi halisi? Makala yetu inayofuata katika mfululizo huu itajibu maswali hayo.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Onyo la Wakati Unaofaa

“Ikiwa mume hupoteza hamu ya kula, hapati usingizi, hukataa kuongea, basi anaonyesha ishara za kutaabika. Mwambie ajaribu kupata furaha katika mambo mengine mbali na kazi na ajaribu kushirikiana na watu asiofanya kazi nao katika kampuni moja.”—Dakt. Toru Sekiya, Kliniki ya Mfumo wa Neva ya Sekiya, Tokyo, Japani.

“Ninapenda kufanya kazi kwa muda wa saa nyingi, lakini ikiwa ni lazima upoteze mke au familia ukifanya hivyo, basi unafanya mambo kwa njia isiyofaa. Hakuna raha katika kutumia pesa ukiwa peke yako.”—Mary Kay Ash, msimamizi wa kampuni ya marashi ya Mary Kay Cosmetics.

[Picha katika ukurasa wa 5]

Uchovu wa kazi wakati mwingine huongoza kwenye matatizo makubwa

[Picha katika ukurasa wa 7]

Vichwa vya familia wanaofanya kazi nyingi kupita kiasi mara nyingi huharibu maisha za wale wanaopaswa kuwa karibu nao zaidi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki