Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 1/8 kur. 5-6
  • Kuungua Nishati—Ni Nani Aliye Hatarini na kwa Nini?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuungua Nishati—Ni Nani Aliye Hatarini na kwa Nini?
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Majeruhi Waelekeao Kuungua Nishati
  • Kwa Nini Watu Huungua Nishati
  • Kuungua Nishati—Waweza Kuikabilije Hali?
    Amkeni!—1995
  • Kuungua Nishati Ni Zamu Yako?
    Amkeni!—1995
  • Jinsi ya Kukabiliana na Uchovu Mwingi
    Amkeni!—2014
  • Ninaweza Kuepukaje Uchovu wa Kupita Kiasi?
    Vijana Huuliza
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 1/8 kur. 5-6

Kuungua Nishati—Ni Nani Aliye Hatarini na kwa Nini?

JIWAZIE kuwa u mfanyakazi wa ofisini mwenye familia—au labda ndivyo ulivyo hasa. Kazi imerundamana juu ya dawati lako. Simu yalia-lia kwa madai ya wateja yaliyo mengi kiasi cha kutowezekana kuyatimiza. Msimamizi wako amechukizwa kwamba hutimizi kiwango chako cha kazi. Mwana wako yumo matatani shule. Mwalimu ataka kukuona mara hiyo. Vilio vyako vya msaada kutoka kwa mwenzi wako wa ndoa vyaonyeshwa ubaridi. Hali hiyo ionekanapo kama isiyodhibitiwa, mkazo wawa msononeko, ukifungulia njia ya kuungua nishati.

Je, kuungua nishati husababishwa na kufanya kazi kupita kiasi? Ann McGee-Cooper, mtafiti wa ubongo, alisema kwamba kuungua nishati ni “tokeo la kuishi bila usawaziko, katika mfululizo wa kazi isiyo na starehe.” Hata hivyo, kufanya kazi kupita kiasi sicho kisababishi pekee; chini ya msongo na hali hizohizo, wengine huungua nishati hali wengine hawaungui.

Majeruhi Waelekeao Kuungua Nishati

Sawa na vile kulivyo na watu wenye mwelekeo zaidi wa kuambukizwa na maradhi fulani, ndivyo kulivyo na namna fulani za watu wenye mwelekeo zaidi wa kuungua nishati. “Ili uungue nishati,” asema Elliot Aronson, profesa wa saikolojia ya kijamii kwenye Chuo Kikuu cha California, “ni lazima kwanza uwe umewaka moto.” Kwa hiyo wale walio na elekeo la kuungua huwa wamewaka moto kwa kuweka miradi na mawazo ya juu. Imesemwa kwamba wale waunguao nishati huwa mara nyingi watu bora zaidi wa kampuni.

Akitoa muhtasari wa vitabia vya nyutu za majeruhi wenye mwelekeo wa kuungua nishati, Profesa Fumiaki Inaoka wa Koleji ya Uuguzi ya Msalaba Mwekundu wa Kijapani, aliandika hivi katika kitabu, Moetsukishokogun (Dalili za Kuungua Nishati): “Wale walio na mbetuko wa kuungua nishati wana maelekeo yenye nguvu ya kuwa wenye huruma, wenye ubinadamu, wororo wa hisia, wenye kujitoa sana, na wenye kufuatia miradi kikamilifu. Hawana asili ya kufanya mambo kama mashine isiyo na hisia bali ‘wana asili ya ubinadamu,’ yaweza kusemwa.”

Alipoombwa asitawishe mtihani wa kupambanua wale walio na mwelekeo wa kuungua nishati, mtaalamu mmoja alisema kwamba badala ya hivyo kipimo hicho chapasa kutumiwa kama kiwango cha kuajiri kazi. “Kile ambacho kampuni zahitaji kufanya,” akasema, “ni kutafuta watu ambao hujali sana kwa kadiri ya kuweza kuungua nishati . . . halafu wasitawishe programu za kupambana na kuungua nishati.”

Walio rahisi sana kuungua nishati ni wale wahusikao katika huduma za ubinadamu, kama wafanyakazi wa huduma za kijamii, madaktari, wauguzi, na walimu. Wao hujaribu kwa hamu kubwa kusaidia watu, kujitolea kuboresha maisha za wengine, na huenda wakaungua nishati wang’amuapo kwamba hawafikii ile miradi waliyojiwekea ambayo nyakati nyingine huwa isiyofikika. Akina mama wenye kujali waweza pia kuungua nishati kwa sababu hiyohiyo.

Kwa Nini Watu Huungua Nishati

Uchunguzi uliofanywa miongoni mwa wauguzi ulifunua visababishi vitatu vinavyoongoza kwenye kuungua nishati. Kilichoonwa kwanza kilikuwa ni kiasi cha masumbuko ya kila siku yanayosababisha mvurugo. Kwa kielelezo, walio wengi kati ya wauguzi hao walilazimika kubeba madaraka mazito, kushughulikia magumu kuhusiana na wagonjwa, kujipatanisha na vifaa vipya, kukabili gharama zenye kupanda, na kuchukuliana na mtindo-maisha usio wa kawaida. “Masumbuko haya ya kila siku hufanyiza athari iliyo kubwa zaidi kuelekea kuungua kwa nishati zao,” chasema kitabu Moetsukishokogun. Matatizo yabakipo bila kutatuliwa, mvurugiko wa hisia hujazana tu na kuongoza kwenye kuungua nishati.

Kisababishi cha pili kilichoonwa kilikuwa ukosefu wa tegemezo, kutokuwa na mtu wa kumweleza siri. Hivyo, mama ajitengaye na akina mama wengine ataelekea zaidi kuungua nishati. Uchunguzi uliotajwa juu ulipata kwamba wauguzi waseja huelekea zaidi kuungua nishati kuliko wale waliofunga ndoa. Hata hivyo, kuwa katika ndoa kwaweza kuongezea masumbuko ya kila siku ikiwa hakuna uwasiliano wa wazi kati ya mume na mke. Hata kila mtu awapo nyumbani, huenda mtu akajikuta akiwa pweke kwa sababu familia yake imefyonzwa fikira katika kutazama televisheni.

Kisababishi cha tatu kilikuwa hisia za kuwa hoi. Mathalani, wauguzi huelekea zaidi kupatwa na hisia za kuwa hoi kuliko madaktari kwa sababu huenda ikawa wauguzi hawana mamlaka ya kubadili mambo. Wale walio katika umeneja wa ngazi ya katikati huenda wakaungua nishati wahisipo kwamba jitihada zao kubwa kabisa hazifui dafu. Kama vile meneja mmoja wa nishati za kibinadamu alivyosema, kuungua nishati hutokana na ‘kuvurugwa hisia kwa kujaribu kufanya jitihada kubwa bila kusikilizwa.’

Hisia za kuwa hoi katika wanadamu huchipuka katika udongo wa mitazamo isiyothamini na huzaa matunda ya kuungua nishati. Wake huungua nishati waume zao wasipotambua kwamba kupamba nyumba na kutunza watoto ni kazi nyingi. Mameneja wa ngazi ya katikati huungua nishati wakati mkubwa wa kazi apuuzapo kazi iliyofanywa vema na kuwaonea-onea kwa makosa madogo. “Jambo kuu ni kwamba sisi sote twahitaji kuthaminiwa kwa jitihada zetu na kutambuliwa,” lasema gazeti Parents, “na ikiwa twafanya kazi katika mahali pasipothawabisha jitihada zetu—pawe ni nyumba yetu au ofisi yetu—basi tutaelekea zaidi kuungua nishati.”

Kwa kupendeza, ingawa wauguzi hupatwa na asilimia za juu za kuungua nishati, wakunga hawaungui sana hivyo. Kwa jumla, kazi ya mkunga husaidia uhai wa watu wapya uingie ulimwenguni. Akina mama na akina baba huwashukuru kwa kazi yao. Watu wathaminiwapo, wao huhisi kwamba ni wenye mafaa na huhamasishwa.

Mara tu mtu ajuapo ni nani mwenye elekeo la kuungua nishati na kwa nini, huwa ni rahisi zaidi kushughulika na tatizo hilo. Makala inayofuata yaweza kusaidia majeruhi wa kuungua nishati wawe na mfikio uliosawazika kuelekea maisha.

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Kuungua nishati ni tokeo la mfululizo wa kazi isiyo na starehe

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki