Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 1/8 kur. 7-10
  • Kuungua Nishati—Waweza Kuikabilije Hali?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuungua Nishati—Waweza Kuikabilije Hali?
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Njia ya Kupona
  • Kikundi Chenye Tegemezo la Kuwasiliana
  • Kubadili Maoni Yako
  • Kuungua Nishati—Ni Nani Aliye Hatarini na kwa Nini?
    Amkeni!—1995
  • Kuungua Nishati Ni Zamu Yako?
    Amkeni!—1995
  • Jinsi ya Kukabiliana na Uchovu Mwingi
    Amkeni!—2014
  • Ninaweza Kuepukaje Uchovu wa Kupita Kiasi?
    Vijana Huuliza
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 1/8 kur. 7-10

Kuungua Nishati—Waweza Kuikabilije Hali?

WAKILEMEWA na mkazo kutokana na wasiwasi na mahangaiko ya kila siku, wengi hujaribu kuondoa mvurugiko wao wa hisia kwa kunywa. Alkoholi, dawa ya kulevya itumiwayo mahali pengi zaidi leo, hutumiwa na wengi katika jaribio la kuepuka magumu makubwa. Wengine wametegemea dawa za kulevya ziandikiwazo wagonjwa mara nyingi ili kushughulikia wasiwasi wao. Hata hivyo wengine hufuatia dawa za kulevya zenye kugeuza akili, kama bangi, metamfetamini, na kokeni. Hata watoto wadogo wamejulikana kuwa wenye kutumia dawa za kulevya ili kuepuka magumu ya maisha. Yasemwa kwamba asilimia 95 ya vijana Wamarekani watakuwa wametumia kitu kimoja au zaidi cha haramu kabla ya kuhitimu kutoka shule ya sekondari.

Halafu kuna wale wajaribuo kuepuka mkazo wa kila siku kwa kufanya shamrashamra nyingi pamoja na rafiki zao au kusingizia ni wachangamfu hali wanahisi wameshuka moyo ndani. Au wao hutafuta shauku na wororo wa jinsia tofauti kwa sababu zisizofaa. Lakini kutumia njia za kuepa ili kushughulika na mkazo huongezea tu mvurugiko wa hisia. Watu wajaribupo kutohoa mkazo kwa alkoholi au vitu vingine vya kugeuza akili, wao huharakisha utaratibu wa kuungua nishati badala ya kuwasha upya nishati zao. Basi, waweza kufanya nini uhisipo nishati zilizo ndani yako zikiungua polepole?

Njia ya Kupona

Amkeni! halipendekezi matibabu wala dawa hususa. Hata hivyo, latokeza madokezo machache yenye msaada yaliyo na msingi wa kanuni za Biblia ambayo huenda yakakusaidia kuwasha upya kuni zinazozimika ndani yako. Dakt. Yutaka Ono, mkurugenzi kwenye Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Keio, apendekeza “K tatu” za kukabiliana na kuungua nishati. Aeleza hivi: “‘K tatu’ hizo zasimamia kudhibiti, kuwasiliana, na kutambua.”

Ili kushinda hisia za kuwa hoi, ni lazima uweze kuhisi unadhibiti hisia na mwenendo wako. Mvurugiko wa hisia utawalapo hisia-moyo zako kila siku na kulemea uwezo wako wa kutatua matatizo, ni rahisi kuamini kwamba mambo yamekushinda. Hata hivyo, usiketi kitako tu na kukaa ukifikiria-fikiria matatizo tu. Jaribu kutatua tatizo lako hatua kwa hatua. (Ona sanduku, ukurasa 8.) Usiahirishe. Kwa kule tu kuanzisha hatua zilizo chanya, utaanza kuhisi vizuri zaidi na kuwa unadhibiti mambo.

Jaribu kupunguza maudhiko yatokezayo hisia za ushinde. Mathalani, watu fulani huelekea kuudhiwa na kila kijambo maishani. Wao husisitizia njia fulani ya kufanya mambo na huudhika wengine wasipoifuata, au huenda wakavurugwa hisia na mapungukio yao wenyewe. “Usiwe na haki kupita kiasi,” mwanamume wa kale mwenye hekima alisema, “wala usijiongezee hekima mno; kwani kujiangamiza mwenyewe?” (Mhubiri 7:16) Ni jambo la hakika kwamba kushikilia viwango vilivyo juu mno na kuhisi daima huvitimizi kutaunguza nishati zako.

Shauri zaidi lenye msaada kutoka katika Biblia ni ‘kuwa mwenye kiasi katika kutembea pamoja na Mungu wako.’ (Mika 6:8, New World Translation) Kuwa na kiasi humaanisha mtu aijue mipaka yake au aweke “kadirio la kiasi juu ya uwezo wake mbalimbali.” Huenda hii ikamaanisha kusema hapana kwa madai ya kupita kiasi kazini.

Wale wajuao mipaka yao hukaribisha msaada. Meneja mmoja wa kike aliyekuwa ameungua nishati alisema kwamba ufunguo wa kuepuka hilo ni kuomba msaada. Na bado, kama vile asemavyo, “watu wengi huogopa kuomba msaada kwa sababu huenda wakaonwa ni kama wanashindwa kufanikiwa katika kazi yao.” Iwe ni kazi ya nyumbani, kazi ya shuleni, au kazi ya kimwili—lolote lile linalotisha kuunguza nishati zako—gawia wengine kazi yako uwezapo kufanya hivyo. Utashangaa kuona jinsi mambo yatimizwavyo bila wewe kusimamia kila kitu moja kwa moja.—Linganisha Kutoka 18:13-27.

Huenda ukahitaji pumziko fulani. Likizo ya kwenda mahali pengine yaweza kumsaidia sana mtu ambaye angeweza kuwa jeruhi wa kuungua nishati. Hata hivyo, ikiwa hali zako haziruhusu hilo, “ikiwa wewe wajua jinsi ya kujichangamsha, hiyo hutokeza tofauti,” asema mtafiti Ann McGee-Cooper. Kupumzika ili kubadili mwendo huenda hata kukaongezea matokeo ya kazi, kukichochea akili yako ufikiri kwa njia ya kubuni mambo. Aliloshauri Mfalme Sulemani miaka mingi iliyopita lingali la kweli: “Heri konzi moja pamoja na utulivu, kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kujilisha upepo.”—Mhubiri 4:6.

Kikundi Chenye Tegemezo la Kuwasiliana

“K” ya pili ambayo Dakt. Ono alitaja yahusisha kuwasiliana. Inapendeza kwamba ni mara haba wazima moto huungua nishati. Hii huenda ikawa ni kwa sababu, zaidi ya wao kufikiriwa kuwa ni mashujaa, wao huungamanishwa na kifungo thabiti cha usahibu. Kwa kuwa na kikundi chenye tegemezo cha kuegemea, mtu aweza kupata msaada kwao. Wewe waweza kupata wapi tegemezo lenye kufariji leo? Kikieleza njia za matabibu za kukabiliana na kuungua nishati, kitabu Moetsukishokogun (Dalili za Kuungua Nishati) chataarifu hivi: “Kwa madaktari, mtegemezaji wao wa hisia-moyo aliye na matokeo na afaaye zaidi ni familia yao, hasa mwenzi wao wa ndoa.” Kila mtu ahitaji mtu fulani wa kumweleza siri ya hisia zao za kibinafsi. Katika jambo hili la kuwasiliana, Biblia hutoa ushauri wenye kutumika. Huwatia moyo wenzi waliofunga ndoa wadumishe mashikamano yenye mahaba kwa mtu na mwenzake na kuwaambia wote wawe na marafiki wawezao kuwapa madokezo thabiti yenye kufanya kazi.—Mithali 5:18, 19; 11:14.

“Ni lazima tujenge mfumo wetu wenyewe wa tegemezo la marafiki wa karibu na familia,” lasema USA Today. Halafu laongezea hivi: “Ni lazima pia tujihisi huru kutumia mategemezo ya vitovu vyetu vya kidini na huduma za afya ya kiakili.” Kwa habari ya jinsi ya kupata msaada wa mategemezo ya kidini, Yakobo ndugu-nusu wa Yesu aliandika hivi: “Je, kuna yeyote mgonjwa miongoni mwenu? Na awaite kwake wanaume wazee zaidi wa kutaniko, na acheni wasali juu yake, wakimpaka mafuta katika jina la Yehova.” (Yakobo 5:14, NW) Wakristo walio na matatizo waweza kupata burudiko kwa kuongea na wazee wa makutaniko ya Mashahidi wa Yehova. Ingawa wazee si wataalamu katika kushughulikia kuungua nishati, tegemezo la kiroho watoalo ni la thamani kubwa sana.

Ingawa mfumo wa tegemezo la kibinadamu huenda ukatutia nishati mpya za siku nyingine, huenda zisitoshe sikuzote. Katika utangulizi wa kitabu chake, Helplessness, Martin E. P. Seligman alielekeza kwenye ujitegemeo uonwao katika nchi za Magharibi kuwa kisababishi cha ongezeko la mshuko wa moyo leo, na alitaja uhitaji wa kupata kusudi maishani. Ndipo akaonyesha kwamba “sharti moja lihitajikalo ili maisha yawe na kusudi ni kushikamana na kitu chenye uwezo mkubwa kuliko wewe.” Ingawa watu wengi leo hawachukui uhusiano wao na Mungu kwa uzito, kuwasiliana na Muumba—ambaye kwa hakika ‘ana uwezo mkubwa kuliko wewe’—kwaweza kukusaidia ukabiliane na hisia za kuwa hoi.

Mfalme Daudi, aliyekabili matatanisho mengi, aliwatia moyo hivi raia zake: “Enyi watu, mtumainini [Mungu] sikuzote, ifunueni [“mwageni,” NW] mioyo yenu mbele zake; Mungu ndiye kimbilio letu.” (Zaburi 62:8) Mungu yu tayari kutega sikio lake, hata kwa ‘kuugua kwetu kusikoweza kutamkwa.’ (Warumi 8:26) Kumwomba kwa moyo wenye bidii hutokeza amani iwezayo ‘kuhifadhi mioyo yetu na nia zetu’ dhidi ya kuungua nishati.—Wafilipi 4:6, 7.

Kubadili Maoni Yako

Mwisho, huenda badiliko likahitajiwa katika jinsi uionavyo hali yako. Kutambua, au kufahamu, ndiyo “K” ya mwisho ambayo Dakt. Ono adokeza kuwa njia ya kukabiliana na kuungua hisia. Tuwapo chini ya mkazo mwingi mno, sisi huelekea kufanya makadirio hasi juu ya kila kitu nasi hujitega wenyewe katika maoni ya kutazamia mabaya. Hata hivyo, ni lazima tuone mambo kihalisi. Changanua kama msingi upo au haupo wa huko kufikiri hasi. Je, tokeo litakuwa baya kwa kadiri ambayo wewe wahofu? Jaribu kutazama mambo kwa maoni mengine.

“Waweza kuanza kuchukua kwamba ikiwa umeungua nishati, labda ni kwa sababu wewe ni ‘mwema,’ si kwa sababu wewe ni ‘mbaya,’” lasema gazeti Parents. Kumbuka: Watu wa namna zile zenye elekeo la kuungua nishati wana viwango vya juu na hujali wengine. Jambo lenye msaada zaidi kwa jeruhi wa kuungua nishati ni neno la uthamini. Kutakuwa na tofauti kubwa kwa mama ikiwa mume na watoto wake watamka na kuonyesha uthamini kwa kazi yote ihusikayo katika kuendesha nyumba. Ikiwa meneja wa ngazi ya katikati aungua nishati kazini, elezo la uthamini na kupewa pongezi vyaweza kubadili mtazamo wake kwa matokeo mema.

Biblia huonyesha jinsi mke hodari hustahili kusifiwa: “Wanawe huondoka na kumwita heri; mumewe naye humsifu, na kusema, Binti za watu wengi wamefanya mema, lakini wewe umewapita wote.” (Mithali 31:10, 28, 29) Kwa kweli, “maneno yapendezayo ni kama sega la asali; ni tamu nafsini na afya mifupani.”—Mithali 16:24.

Shinzo, mzee Mkristo aliyetajwa katika makala ya kwanza, alipata nafuu nyingi kutokana na kuungua nishati zake. Ingawa alipokea usaidizi wa kitaalamu, kilichosaidia Shinzo zaidi kilikuwa sala zake kwa Yehova. Baada ya sala zake za kuomba msaada, alikuja kukutana na yule mzee aliyekuwa amejifunza kwanza Neno la Mungu pamoja naye. Mzee huyo, na pia wazee wenzake wengine, walimtegemeza kwa kusikiliza wasiwasi wake. Kutokana na toleo la mapema kidogo la jarida unalolisoma sasa, alisomewa na mke wake makala zilizohusu kushinda hisia-moyo hasi. (Oktoba 8, 1992) Pole kwa pole aling’amua alikuwa akijaribu kufanya kila kitu peke yake. Njia yake ya kuyaona yaliyokuwa yakitendeka kumzunguka ilianza kubadilika. Ingawa kwanza alihisi kwamba alikuwa katika handaki la mtamauko usio na kikomo, aliona upande ule mwingine nuru iliyozidi kuongezeka polepole mpaka hatimaye akatoka katika handaki lake.

Sawasawa na Shinzo, wewe pia waweza kuikabili hali ya kuungua nishati ukabili maisha tena.

[Sanduku katika ukurasa wa 8]

Njia 12 za Kuzuia Kuungua Nishati

MAMBO yanayofuata yana msingi wa machache kati ya madokezo yaliyotolewa na mtaalamu mmoja wa kikliniki wa kuuguza afya ya akili.

1. Dhibiti fikira zako, hisia, na mwenendo—sala ni msaada mkubwa.

2. Uanzapo kuwa na wasiwasi, badili kufikiri kwako kimakusudi kuwe kufikiri kwenye mafaa, kwenye mkataa wa kuazimia.

3. Ufadhaikapo, vuta hewa kwa kina kirefu na ujistareheshe kimakusudi.

4. Jaribu kuziona hali kwa maoni ya mtu yule mwingine ili uelewe jinsi mkazo huo umesitawi.

5. Kaza fikira juu ya mambo uthaminiyo katika wengine na uwasifu. Wape sifa iliyochumwa wala si kuwasifu-sifu isivyo kweli.

6. Tambua na ukandamize kufikiri hasi, kwenye uharibifu.

7. Jua jinsi ya kusema hapana wakati nishati na ratiba yako zitakapo hivyo.

8. Jitie katika mazoezi fulani ya kimwili kila siku—matembezi ya chapuchapu ni mema.

9. Tendea wengine kwa staha, ukitafuta kutokeza sifa zao zilizo bora.

10. Kaa na hali ya ucheshi na ung’ae uso.

11. Acha matatizo yako ya kazi mahali pa kazi.

12. Lililo la lazima lifanye leo—usiahirishe.

(Yamerekebishwa kutokana na “Dealing With Feelings, Beating Burnout” [Kushughulika na Hisia, Kushinda Kuungua Nishati], iliyotungwa na Ruth Dailey Grainger, American Journal of Nursing, Januari 1992.)

[Picha katika ukurasa wa 9]

Mara nyingi kuungua nishati humpiga mtu asiyeacha kujitahidi, mwenye kujibidiisha sana

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki