Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 7/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Vijana Wakataa Dini Zilizopangwa Kitengenezo
  • Vyumba Hatari
  • Maisha Magumu kwa Wafanyakazi wa Farao
  • Madubwana Wabadilishwa
  • Ugonjwa wa Chaga na Kutiwa Damu Mishipani
  • Ujumbe wa Faksi kwa Mungu?
  • Uchafuzi wa Umeme
  • Roma Bila Papa?
  • Wanajimu Wakosea Tena
  • Kupumua Hewa Hatari
  • Jinsi Wazungu Hutumia Wakati Wao
  • Ugumu wa Kulisha Majiji
    Amkeni!—2005
  • Mamilioni ya Uhai Yakitokomea Moshini
    Amkeni!—1995
  • Majiji Makubwa Yanasongwa Pumzi Polepole
    Amkeni!—1994
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 7/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Vijana Wakataa Dini Zilizopangwa Kitengenezo

Vijana wa Kanada wanapeleka ujumbe wenye kufanya viongozi wa kidini wafikiri sana: Makasisi wameshindwa kuwa walimu wa Neno la Mungu. Uchunguzi wa kitaifa uliofanywa karibuni unafunua kwamba vijana wachache sana wanaunga mkono dini zilizopangwa kitengenezo kuliko wakati mwingine wowote. Ni asilimia 10 tu wanaamini kwamba kujihusisha na kikundi cha kidini ni muhimu maishani mwao. Lakini, “zaidi ya asilimia 80 huendea dini zilizopangwa kitengenezo kwa ajili ya sherehe zinazohusika na kuzaliwa, ndoa, na kifo,” laripoti gazeti The Toronto Star. Kwa kupendeza, asilimia 80 pia inaamini katika kuwapo kwa Mungu, huku asilimia 60 wakiamini katika uhai baada ya kifo. “Vijana wanaelekea sana kuvutwa na marika, vyombo vya habari, sinema na muziki zinazopendwa zaidi kuliko kuvutiwa na makasisi,” laongeza gazeti Star. Ni kikundi kidogo tu cha vijana kinachoweza kutafuta mwelekezo kutoka kwa viongozi wa kanisa kwa mambo muhimu ya maisha.

Vyumba Hatari

“Moshi wa tumbako katika mazingira husababisha vifo vingi zaidi kuliko kichafuzi chochote kinachofanyizwa na binadamu,” asema Dakt. Michael Popkiss, ofisa wa tiba ya afya wa Cape Town, Afrika Kusini. Alikuwa akiitikia kwa karatasi iliyogawanywa na Taasisi ya Tumbako ya Kusini mwa Afrika iliyodai kwamba kutopata hewa safi ndiko tatizo. Dakt. Popkiss alieleza kwamba “moshi wa tumbako kwa kawaida huwa mwingi mno katika majengo kuliko kiwango kinachotakikana cha hewa safi” na waweza kutokeza kansa ya mapafu na maradhi ya moyo, na vilevile ukuzi wenye kasoro wa mapafu katika watoto. Alisema kwamba hakuna njia ya kuweza kusafisha hewa wala kuchuja hewa katika jengo ili lisiwe kabisa na moshi wa sigareti. Aliongezea hivi: “Njia inayotumika zaidi ya kuweka hewa ikiwa safi ni kwa kukomesha kutumia vichafuzi vya hewa kwenye vianzo vyavyo.”

Maisha Magumu kwa Wafanyakazi wa Farao

Uchunguzi wa karibuni wa mifupa ya wale waliofanya kazi kwa piramidi, makaburi, na mahekalu ya Farao unaonyesha kwamba waliugua utapiamlo (ukosefu wa lishe bora), walikuwa na maradhi mengi, na kufanyishwa kazi kupita kiasi. Wengi wa wafanyakazi hao walikuwa na ugonjwa wa yabisi kavu, asema Azza Sarry el-Din, mstadi wa elimu ya binadamu. Uchunguzi wake pia ulifunua kwamba wafanyakazi hao walivumilia kazi ngumu. “Uti wao wa mgongo ulipindika kwa sababu ya kubeba mizigo mizito,” na “kuna kufura kwa mifupa, kunakotokeza hali isiyostarehesha,” yeye amalizia. Uthibitisho wa kuwapo kwa magonjwa hayo ulipatikana kwa kuchunguza mafuvu ya vichwa, uti wa migongo, na mifupa midogo ya vidole vya mikono na miguu zilizofukuliwa kutoka makaburi yaliyokuwa karibu. Hata hivyo, magonjwa hayo hayakuonekana katika mabaki yaliyopatikana kwenye makaburi ya watu wa hali ya juu. Wastadi wa elimu ya binadamu wanakadiria kwamba tarajio la maisha ya wafanyakazi lilikuwa katikati ya eneo la miaka 18 hadi 40, huku wale wenye maisha ya hali ya juu waliishi miaka yapata 50 hadi 70.

Madubwana Wabadilishwa

Watekaji watu nyara na majambazi wamebadilisha madubwana katika hofu kuu za watoto Wabrazili. Kulingana na Veja, mtafiti “Lenise Maria Duarte Lacerda alitambua orodha inayoshtua ya ogofyo jingi. Hangaiko lililotajwa na wengi wa watoto hao waliohojiwa, wenye umri wa miaka 7 hadi 11, lilikuwa kushambuliwa, ujeuri, kutekwa nyara, na wevi wachanga.” Kwa sababu wala polisi wala wazazi hawawezi kuwahakikishia ulinzi, “mtoto anapoteza lile wazo la yule shujaa ambalo amesitawisha akilini,” aongezea. Daktari wa watoto Dakt. José Henrique Goulart da Graça asema hivi juu ya matokeo: “Ugonjwa mkuu wa watoto leo ni hofu. Watoto wengi huuonyesha kwa magonjwa ya akili, kama kuumwa na kichwa, ugonjwa wa pumu, kuhara, na gastriki.”

Ugonjwa wa Chaga na Kutiwa Damu Mishipani

Wabrazili 20,000 huambukizwa na ugonjwa wa chaga kila mwaka. Lakini, João Carlos Dias, msimamizi wa Shirika la Taifa la Afya, asema hivi katika Globo Ciência: “Hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi kwa sababu ya uhamaji mwingi wa watu wa mashambani kwenda miji mikubwa, ugonjwa huo waweza kuenea mijini.” Kwa sababu vijidudu vya ugonjwa huo ‘vinaweza kukaa katika kiungo chochote, kutia ndani moyo, hatimaye mgonjwa aweza kufa kutokana na kushindwa kwa moyo kufanya kazi.’ Linapoelezea kwamba ni watu 8,000 tu huambukizwa kutokana na kuumwa na mdudu, gazeti hilo laongezea hivi: “Njia nyingine ya ambukizo inayotokea mara nyingi ni kupitia kutiwa damu mishipani. Inakadiriwa kwamba visa vipya 12,000 [vya ugonjwa huo] hutokea kila mwaka kutokana na (akina mama wanaopitishia watoto ugonjwa) kupitia damu au kwa kutiwa damu mishipani.”

Ujumbe wa Faksi kwa Mungu?

Je! Mungu anaweza kufikiwa kwa faksi? Bezeq, kampuni ya simu ya Israeli, kwa wazi inafikiria hivyo. Katika Januari, Bezeq ilianzisha huduma inayowezesha watu kumpelekea Mungu ujumbe kupitia nambari fulani za faksi katika Jerusalem, laripoti International Herald Tribune. Wanapopokea faksi hiyo, mfanyakazi wa faksi hufunga ujumbe huo na kuupeleka uingizwe ndani ya mashimo ya Ukuta wa Magharibi, unaoaminiwa kuwa masalio ya hekalu la Yehova lililoharibiwa na majeshi ya Roma katika 70 W.K. Kulingana na Tribune, zoea la kuweka sala zilizoandikwa katika nyufa za ukuta huo ni “kipimo cha bahati nzuri” linalofanywa na waabudu wanaotafuta msaada wa Mungu katika kutafuta mwenzi wa ndoa, afya bora zaidi, na miradi mingine. Katika siku ya kwanza ya huduma ya faksi, jumbe 60 zilifika.

Uchafuzi wa Umeme

Waastronomia wanahangaika sana kwa sababu umeme kutoka mijini huangaza anga la usiku, jambo linalozuia jitihada za kuchunguza nyota. Kama ilivyoripotiwa katika International Herald Tribune, Alan MacRobert, mhariri mshiriki wa gazeti Sky and Telescope, alionelea hivi: “Ule utukufu mkuu, uwezo mwingi sana wa anga la usiku lenye giza ambalo limejaa nyota ulikuwa sehemu ya ono la binadamu katika historia yote. Sasa katika nchi zilizositawi, haujulikani kabisa.” Likiitikia mikazo kutoka kwenye mitambo ya kuangalia anga, jiji la Tucson, Arizona, U.S.A. lilibadili taa 14,000 zalo za barabarani kutoka kwa taa za hidrajiri hadi taa za natiri zenye vishiko vyenye kuelekeza nuru chini.

Roma Bila Papa?

Kulingana na John Paul 2, mapapa ni waandamizi wa Petro, na kiti chao kiko Roma kwa sababu, kama ilivyothibitishwa na “mapokeo ya zamani zaidi” ya kanisa, inasemekana kwamba mtume huyo aliuawa huko. Hata hivyo, papa alisababisha mazungumzo mengi aliposema kwamba “kwa sababu ya hali ya nyakati au kwa ajili ya sababu zao hasa wenyewe, inawezekana kwa Maaskofu wa Roma kuweka kwa muda makao yao katika sehemu nyinginezo badala ya Jiji la Milele.” Je! makao ya papa yataondolewa kwa muda yaende mahali pengine? Kuna wengine wanaoliona kuwa tukio ambalo “litaleta mabadiliko makubwa katika utamaduni wetu wote,” lakini watu wengi wanaamini kwamba mambo ya desturi yana nguvu sana na kwamba kiti cha papa hakitahamishwa. “Ni Mtakatifu mwingine kama Petro atalazimika kuja ili kuhamisha kiti cha papa,” asema mwalimu wa sheria ya kanisa, Carlo Cardia, ambaye hata hivyo, anatambua kwamba “chaguo la Roma halina msingi wa kitheolojia.”

Wanajimu Wakosea Tena

Mapema katika 1992, Shirika la Utafiti la Kisayansi katika Parasayansi nchini Ujerumani lilikusanya matabiri karibu 50 ya wanajimu kutoka ulimwenguni pote, wakichanganua matokeo ya mwishoni mwa mwaka. Shirika hilo lilikuwa limefanya vivyo hivyo katika 1991. (Ona Amkeni! la Juni 8, 1992, ukurasa 29, Kiingereza.) Je! matabiri hayo yalikuwa sahihi zaidi kuliko yale ya 1991? Hayakuwa sahihi hata kidogo. “Huku matabiri yasiyo wazi ya 1991 yakipata angalau utimizo kidogo,” laripoti Süddeutsche Zeitung, “wakati huu matabiri hayo hata hayakuwa na utabiri uliotimizwa kabisa.” Matabiri ya mwaka wa 1992 yalitia ndani kuchaguliwa tena kwa George Bush na kuharibiwa kwa Ikulu ya Rais wa Amerika kwa moto. Likitazamia mbele kwenye 1993, shirika hilo hata lilifanya utabiri walo: “Wanajimu watakosea sana tena mwaka ujao.”

Kupumua Hewa Hatari

Kutoka Buenos Aires hadi Beijing, kutoka Seoul hadi Calcutta na Cairo, hewa katika majiji makubwa zaidi ya ulimwengu inakuwa hatari zaidi na zaidi kupumua. Likitaja ripoti moja iliyotolewa na Programu ya Mazingira ya UM na Shirika la Afya Ulimwenguni, gazeti la Ufaransa Le Figaro lasema kwamba kiwango cha sumu kinachoendelea kuongezeka cha uchafuzi wa hewa (kama vile kaboni monoksaidi, salfa dioksidi, ozoni, na risasi) kwa wazi kinaharibu afya ya watu wanaoishi katika sehemu za miji mikubwa na kinaweza hata kuhusianishwa na kifo cha mapema cha baadhi ya wakazi wa jijini. Ikitegemea uchunguzi wa miaka 15 kwa majiji 20, ripoti hiyo ya pamoja yaonya kwamba hatua za dharura zichukuliwe sasa ili kupunguza uchafuzi na kulinda afya ya wakazi wa mijini. Umoja wa Mataifa linakadiria kwamba kufikia mwaka wa 2000, karibu nusu ya wanadamu watakuwa wakiishi katika sehemu za mijini.

Jinsi Wazungu Hutumia Wakati Wao

Ili kupata habari juu ya maisha ya kila siku katika Ulaya, zaidi ya watu 9,700 katika nchi 20 walihojiwa mwishoni mwa 1991 na kikundi cha waandishi wa habari cha Information et Publicité. Je! utendaji wa kila siku hutofautiana jinsi gani katika nchi moja na nyingine? Süddeutsche Zeitung laripoti kwamba Wagiriki huenda kulala kama wamechelewa mno kuliko wengine (saa 6:40 za usiku), lakini Wahangari ni miongoni mwa watu wanaoamka mapema zaidi (saa 11:45 alfajiri). Wailandi na watu wa Luxembuorg hulala zaidi ya wengi. Wacheki, Waslovaki, na Waswisi hawapendelei sana TV, wakiitazama muda wa saa mbili tu kila siku, na huku katika Uingereza “televisheni hutazamwa kwa karibu muda wa saa nne kila siku.” Katika Swedeni, zaidi ya muda wa saa tano kila siku hutumiwa katika kusoma au kusikiliza redio, huku watu wa Denmark wakifurahia muda wa saa moja na nusu ya wakati wa burudisho kila siku kwenye sinema, jumba la michezo, au mambo yanayofanana na hayo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki