Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 9/22 uku. 31
  • Matukio ya Ajabu na Yenye Kuogofya Chini ya Tundu la Ozoni

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Matukio ya Ajabu na Yenye Kuogofya Chini ya Tundu la Ozoni
  • Amkeni!—1993
  • Habari Zinazolingana
  • Je, Uogope Kupigwa na Jua?
    Amkeni!—2009
  • Angahewa Letu Linapoharibiwa
    Amkeni!—1994
  • Ewe Mpenda-jua— Linda Ngozi Yako!
    Amkeni!—1999
  • Linda Ngozi Yako!
    Amkeni!—2005
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 9/22 uku. 31

Matukio ya Ajabu na Yenye Kuogofya Chini ya Tundu la Ozoni

WALE wakazi 125,000 wa Punta Arenas, jiji la kusini zaidi la Chile, kwa muda mrefu wametoa mzaha kuhusu kuishi katika “mwisho wa ulimwengu.” Lakini matukio mengi yasiyo ya kawaida na yenye kuogofya katika mwaka uliopita yanafanya mzaha huo uwe halisi kabisa. Wanasayansi fulani wanaanza kufikiri kwamba kwaweza kuwa na “jambo jipya chini ya jua hapa.” Taarifa moja katika The Wall Street Journal, la Januari 12, 1993, yatoa mambo mengine ya ndani.

Felix Zamorano, mshiriki wa Kikundi cha Kuchunguza Hewa katika Chuo Kikuu cha Magallanes kilichoko huko, aripoti hivi: “Katika Oktoba, tuliorodhesha kiwango kidogo zaidi cha ozoni kilichopata kuorodheshwa. Kwa siku tatu tabaka ya ozoni ilikuwa karibu nusu ya kawaida na ikapungua chini ya viwango ambavyo huonwa kuwa hatari zaidi.” Athari za ongezeko la mnururisho wa kiukaurujuani kutoka kwenye tundu katika tabaka ya ozoni “zatia ndani kansa ya ngozi na mtoto wa jicho, pamoja na tatizo kwa mimea ya planktoni, ambayo ni msingi wa mfuatano wa ulishano,” Journal likasema.

Mwaka uliopita “nusu ya kundi la ng’ombe 1,200 za Radovan Vilicic walipofushwa na mchochota wa utando wa jicho hivi kwamba walikuwa wakigongana kama magari ya kugonganishwa katika mchezo, na ng’ombe watano wakawa na njaa kali kwa sababu hawangeweza kupata chakula chao.”

Taarifa ya Journal yaendelea kusema: “Jose Bahamonde asimulia hadithi kama hiyo. Shamba lake la mifugo, lililoko kilometa 125, kutoka hapa hutoa mandhari nzuri ajabu ya Mlango Bahari wa Magellan, lakini wengi wa kondoo zake 4,300 hawawezi kuuona, wala hawawezi kuona vitu vingine vilevile. Karibu asilimia 10 yao wanatibiwa kwa maambukizo ya macho, na 200 wa kundi lake wakawa vipofu mwaka uliopita.”

Mstadi wa ngozi Jaime Abarca abisha kwamba “jambo linalotendeka hapa ni jambo jipya kabisa ulimwenguni. Ni jambo lisilo la kawaida kama vile kuja kwa watu kutoka Mihiri.” Yeye hutibu wagonjwa wengi zaidi na zaidi wenye matatizo ya ngozi, kuchomwa na jua kumeongezeka sana, na kiwango cha visa vya aina mpya za kansa za ngozi zinazoitwa melanoma ambazo ni hatari hata zaidi kimeongezeka mara tano kuliko kawaida. Yeye mwenyewe asadiki kwamba kuna uhusiano wa hayo na mnururisho ulioongezeka wa kiukaurujuani.

Wakazi wa Punta Arenas wanalichukua kuwa tatizo kubwa. Duka moja la madawa liliuza vizuia-jua kwa asilimia 40 zaidi ya mwaka uliopita. Huduma ya simu huandaa habari za viwango vya kiukaurujuani. Vituo vitatu vya redio huzitangaza pia. Shule huwaambia wanafunzi wavae kofia kubwa, kizuia-jua na miwani ya jua. Katika duka moja, mauzo ya miwani ya jua yalipanda kwa asilimia 30. Na “mkulima wa hapo anajaribu kubuni miwani ya jua kwa ajili ya kondoo zake.”

Gavana Scarpa asema hivi: “Mimi sikatai mambo ya hakika. . . . Mnataka kufanya nini? Hatuwezi kuweka paa katika eneo hili lote.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki