Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 10/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ulaya Yaonywa Juu ya Vita vya Kikabila
  • Utumizi Mbaya wa Kileo Katika Australia
  • Jitihada za Amani za UM Zashindwa kwa Kukosa Fedha
  • Mwaka wa Chuki
  • Wanawake Wanaokosekana
  • Kiwango cha Kuzaa Kinachoshuka cha China
  • ‘Tatizo Kubwa la Afya Kufikia Mwaka 2000’
  • Hatari ya Takataka za Angani
  • Bishano la Japan Juu ya Bendera na Wimbo wa Taifa
  • Misiba ya Kinyukilia Yafunuliwa
  • Serikali ya Ulimwengu—Je! Umoja wa Mataifa Ndilo Jibu?
    Amkeni!—1993
  • Je! Ulimwengu Waweza Kuungana?
    Amkeni!—1993
  • Tisho la Nyukilia—Je! Limekwisha Hatimaye?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 10/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Ulaya Yaonywa Juu ya Vita vya Kikabila

“Watu waweza kugeuzwa kuwa mashine zenye kuchukia na kuua bila ugumu wowote mkubwa,” aonya José-María Mendiluce, mwakilishi maalumu wa balozi mkuu wa UM anayeshughulikia wakimbizi. Bwa. Mendiluce, aliyetumia miezi 19 akisimamia mpango wa UM unaoshughulikia wakimbizi katika ile iliyokuwa Yugoslavia, alisema kwamba ni “kosa lenye hatari kubwa sana” kuwaona Wabalkani kuwa “tofauti kimsingi na Wazungu wengine,” na akasema kwamba mapigano ya kikabila kama hayo yaweza kutokea kwa urahisi katika nchi nyinginezo za Ulaya. “Kile kinachotakiwa tu ni tatizo la kiuchumi na wanasiasa wachache wenye madharau wanaoweka lawama juu ya wahamiaji au watu maskini au watu ambao ni tofauti kwa njia fulani,” yeye akasema. Kulingana na ripoti ya The New York Times, Bwa. Mendiluce alisema vile ilivyo rahisi kwa viongozi kuchochea chuki “kwa kueneza uwongo katika vyombo vya habari na kuchochea uchokozi,” akikazia kwamba wale waliotia sahihi mikataba ya amani hawakubadili tabia zao, bali waliendelea “kuchukia na kuua.”

Utumizi Mbaya wa Kileo Katika Australia

Habari za kupendeza katika Australia ni kwamba kiasi cha kileo kinachotumiwa katika taifa lote kinashuka. Lakini habari mbaya ni kwamba utumizi mbaya wa kileo bado hugharimu taifa hilo dola bilioni 6 za Australia na maisha za watu 6,000 kwa mwaka,” lasema The Sydney Morning Herald. Ripoti ya hivi karibuni iitwayo Dimensions and Effects of Alcohol Abuse ilifunua kwamba asilimia 88 ya wanaume Waaustralia na asilimia 75 ya wanawake hunywa vileo, na ikaonyesha ongezeko la unywaji miongoni mwa wanawake na “karamu za unywaji” kati ya matineja kuwa tatizo kubwa linalostahili kutatuliwa.

Jitihada za Amani za UM Zashindwa kwa Kukosa Fedha

Gharama za UM za kudumisha amani zinatazamiwa kufikia dola bilioni 3.7 (za U.S.) mwaka huu. Hata hivyo, “kushindwa kwa mataifa yaliyo wanachama kulipa sehemu yao kunazusha shaka juu ya uwezo wa shirika hilo kugharimia shughuli za wakati ujao au kugharimia vya kutosha jitihada za amani zilizopo sasa,” lasema The New York Times. UM linapaswa kuyapa mataifa yanayosaidia katika jitihada za kuweka amani rudishio dogo la dola 1,000 kila mwezi kwa kila askari-jeshi aliyetumwa. Lakini miezi mingi imepita bila nchi zilizotuma majeshi kwa ajili ya jitihada za amani katika ile iliyokuwa Yugoslavia na katika Kambodia kupata rudishio la fedha. Kufikia mwisho wa Aprili, fedha za kudumisha amani ambazo hazijalipwa zilifikia dola bilioni 1.5, kukiwa na dola milioni 970 za ziada ambazo bado hazijalipwa kwa ajili ya bajeti ya kawaida. Serikali za nchi fulani zinazoendelea zimeondoa majeshi yazo au zikakataa kushiriki katika jitihada mpya za amani kwa sababu ya kukosa kupewa rudishio.

Mwaka wa Chuki

“Mwaka kama wa 1992 watoa umaana mpya kwa maswali fulani ya kale juu ya asili ya kibinadamu,” lasema gazeti Newsweek. “Migawanyiko hii—jirani dhidi ya jirani, kabila dhidi ya kabila, utaifa dhidi ya utaifa—ni mambo ambayo sikuzote tumeelekea kuwa nayo, na matukio ya mwaka huu yazusha shaka juu ya kama tunafanikiwa kuziba mapengo hayo.” Hilo lilisema hivi: “‘Chukia jirani yako’ yaonekana kuwa shime ya mwaka huu.” Mbona “chuki ya kibinadamu” ikaongezeka hivyo katika 1992? “Kutokujali sheria kabisa kumesababisha jeuri nyingi ya mwaka uliopita,” lasema Newsweek, kutia na “kuharibika ghafula kwa hali ya uchumi” kulikofuata kuanguka kwa Ukomunisti wa Sovieti. Zaidi ya hiyo kulikuwa na chuki za kijamii zilizochochewa na wenye mamlaka wa serikali. Je! suluhisho ni wadumishaji usalama wa kijeshi? “Kwa karibu miaka 20, majeshi ya U.M. yamekuwa katika Saiprasi, yakiamua jumuiya za Kigiriki na Kituruki. Wakiwa salama kwa kuwekewa ulinzi huo na U.M., hakuna upande wowote ambao umekuwa na mathumuni yoyote ya kupatana,” lajibu Newsweek.

Wanawake Wanaokosekana

Wanawake hupita wanaume katika idadi kwa uwiano wa 105 kwa 100 katika nchi zilizoendelea, kama vile Uingereza, Ufaransa, Uswisi, na United States. Lakini takwimu za UM zaonyesha kwamba katika Esia makumi ya mamilioni ya wanawake wanakosekana. Kwa kielelezo, Afghanistan na Bangladesh zina wanawake 94 tu kwa kila wanaume 100, India ina 93, na Pakistan ina 92 tu. Tarakimu rasmi za China zilionyesha wavulana 114 wa umri wa kati ya mwaka mmoja au miwili kwa kila wasichana 100. Kwa nini kuna tofauti hiyo? “Wastadi waelekeza kwenye ubaguzi wenye kuhatarisha uhai ambao ni lazima wanawake wavumilie, ukifanya nafasi zao za kuokoka ziwe ndogo kuliko za wanaume: utoaji-mimba na uuaji wa vitoto visichana, lishe isiyofaa na utunzi mbaya wa afya, kupata mimba nyingi na kazi ngumu ya jasho,” lasema The Wash-ington Post. Isitoshe, katika tamaduni fulani, wanaume wanaohesabu watu ama huwapuuza wanawake ama hawaruhusiwi kuzungumza na wanawake. Na baba fulani, wakiona haya kwamba wana binti wengi kuliko wana, husema uwongo juu ya jinsia ya watoto wao.

Kiwango cha Kuzaa Kinachoshuka cha China

Takwimu za 1992 zaonyesha viwango vya chini zaidi vya kuzaa vilivyopata kurekodiwa katika China—watoto 18.2 kwa kila watu 1,000, kushuka kutoka 23.33 katika 1987, laripoti The New York Times. Ingawa lengo hilo halikutarajiwa kutimizwa hadi kufikia mwaka 2010, hilo lilifikiwa “kwa sababu maofisa wa vyama na wa Serikali katika kila tabaka walitoa uangalifu zaidi kwa mpango wa uzazi na wakatumia njia zenye matokeo zaidi,” asema Peng Peiyun, waziri wa Tume ya Kupanga Uzazi ya Taifa. Katika mpango huo maofisa wenyeji walionwa kuwa na daraka la kibinafsi la kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa katika sehemu wanazosimamia na wangeweza kuadhibiwa wakishindwa kufanya hivyo. Katika visa vingi, hiyo ilimaanisha kufunga kwa sharti uzazi wa wanawake waliokuwa tayari na mtoto mmoja na kuwatoza fedha nyingi sana wale waliopata mtoto bila idhini. Wanakijiji wanaposhindwa kulipa fedha hizo, mali yao ama hutwaliwa ama kuharibiwa, na mara nyingi nyumba zao hubomolewa. Tayari wenyeji wa China wapatao bilioni 1.17 hufanyiza asilimia 22 ya idadi ya watu ulimwenguni.

‘Tatizo Kubwa la Afya Kufikia Mwaka 2000’

Maofisa wa afya wa Ufaransa wanatabiri kwamba “mchochota-ini wa aina ya C wenye kusedeka utakuwa tatizo kubwa la afya katika Ufaransa kufikia mwaka 2000.” Madondoo kutoka kwa ripoti ya tiba iliyotokea katika gazeti la Paris Le Monde yalisema kwamba tatizo hilo lina mambo mawili ya kawaida: ile “sehemu kubwa ambayo mitio ya damu mishipani huwa nayo katika kueneza virusi hiyo” na “usitawi mwingi hasa [wa virusi hiyo] katika hali yayo ya kusedeka.” Inakadiriwa kwamba sasa kati ya watu 500,000 na 2,000,000 katika Ufaransa wameambukizwa virusi hiyo na kwamba inaelekea asilimia 62 kati yao watapatwa na mchochota-ini wenye kusedeka, wakiwa katika hatari ya kupatwa na kunyauka kwa ini au kansa kwa muda wa kati ya miaka 10 hadi 30. Madaktari husema kwamba ingawa watu wengi walioambukizwa mchochota-ini C hawana dalili zozote, hali yao si nzuri.

Hatari ya Takataka za Angani

“Takataka za angani zinazidi kuwa tatizo kubwa kwa safari za angani,” laripoti Süddeutsche Zeitung. Mkutano wa Ulaya wa kwanza juu ya Takataka za Angani, uliofanywa Aprili katika Darmstadt, Ujerumani, ulizungumzia “suala la kile kinachopaswa kufanywa na eneo la takataka linalozidi kuongezeka linalofanyizwa na satelaiti zisizofanya kazi, vipande vilivyotumika vya roketi, au vifaa vilivyopotea katika safari za mapema za angani.” Inakadiriwa kwamba zaidi ya vyombo 7,000 vya ukubwa wa mpira wa tenisi au vikubwa zaidi vinazunguka dunia, kutia na vipande vidogo-vidogo zaidi ya 100,000. Safari za Urusi na za U.S. husababisha asilimia 95 ya takataka za angani. “Katika miaka ya hivi karibuni, vyombo vya angani vinavyosafiri nusura vigongane na takataka inayoelea kila mahali,” gazeti hilo likaongeza. “Utatuzi pekee ni kuzuia kabisa takataka na makubaliano ya kimataifa juu ya miradi ya kuruka angani katika wakati ujao ili safari za angani zisiwe na tisho la kuangamia katika mileani inayofuata.”

Bishano la Japan Juu ya Bendera na Wimbo wa Taifa

Rekodi zilizotolewa hivi karibuni katika Yamato, Japan, zaonyesha kwamba wakuu wa shule “walitekeleza amri ya Wizara ya Elimu juu ya kupandishwa kwa bendera ya taifa na kuimba wimbo wa taifa . . . , ujapokuwa upinzani mkali kutoka kwa walimu wa kawaida,” lasema Mainichi Daily News. “Suala la kutia ndani Hinomaru [bendera ya taifa] na Kimigayo [wimbo wa taifa] katika sherehe za shule limezusha bishano katika taifa lote kwa sababu ya kushirikishwa kwavyo na utukuzo wa taifa wenye kupita kiasi na ubeberu wa Japan katika wakati wa vita.” Kulingana na Asahi Evening News, wapinzani wanafungamanisha bendera na wimbo wa taifa na ibada ya maliki na kusema kwamba kuwalazimisha watoto kuimba wimbo wa taifa “kungekuwa ni kuwalazimisha wafuate fundisho hususa la kidini.” Haki za kikatiba za uhuru wa kidini na dhamiri zinavunjwa, wao wasema.

Misiba ya Kinyukilia Yafunuliwa

Habari mpya juu ya mahali palipokuwa na aksidenti mbaya zaidi ya nyukilia ulimwenguni zimetangazwa baada ya miaka mingi ya usiri, lasema gazeti la Paris International Herald Tribune. Katika harakati yayo ya kutengeneza silaha za nyukilia, ile iliyokuwa serikali ya Sovieti ilijenga kiwanda cha plutoni katika Milima ya Ural. Kuanzia mwanzo wa ujenzi wacho katika 1948 hadi 1951, takataka zenye nururishi zilitupwa tu ndani ya mito ya huko, ambayo pia ilitumiwa kwa ukulima na maji ya kunywa. Kisha, katika 1957, takataka fulani za nyukilia huko zililipuka, zikitoa kiasi kikubwa cha takataka zenye nururishi katika anga la dunia. Mkasa mwingine ulitukia katika 1967, wakati ziwa lililo karibu lililokuwa limetumiwa kuwa mahali pa kutupa takataka za nyukilia lilipokauka. Upepo ulisambaza takataka nururishi katika eneo kubwa. Wanasayansi wanaamini kwamba uchafuzi wa nururishi kutokana na mikasa hiyo mitatu iliathiri watu wapatao 450,000.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki