Je! Ulimwengu Waweza Kuungana?
‘Mara nyingi sana, mchukie jirani yako ulionekana kuwa usemi wa 1992.’
HILO lilikuwa kadirio la Newsweek. Gazeti hilo liliongeza: “Migawanyiko hiyo—jirani dhidi ya jirani, rangi dhidi ya rangi, taifa dhidi ya taifa—ni jambo ambalo tumeelekea kuwa nalo sikuzote, na matukio ya mwaka huu yanazusha shaka juu ya kama kuna nafuu yoyote katika kuziba mapengo hayo.”[1]
Hivi karibuni, mazingiwa ya kijeshi, machinjo, na unajisi katika ile iliyokuwa Yugoslavia yamekuwa vichwa vya habari ulimwenguni pote. Katika Bosnia na Herzegovina pekee, watu wapatao 150,000 wameuawa au hawajulikani waliko. Na karibu 1,500,000 wamehamishwa kutoka makao yao.[2] Je! wewe wasema kwamba matukio hayo yenye msiba hayangeweza kamwe kutukia katika ujirani wako?
Ofisa wa UM José-María Mendiluce alionya hivi: “Watu waweza kugeuzwa kuwa mashine zenye kuchukia na kuua bila ugumu wowote mkubwa. . . . Kuna mtazamo katika Magharibi kwamba vita inapiganwa vikali kwa saa tatu kutoka Venice kwa sababu tu Wabalkan kwa msingi ni tofauti na Wazungu wengine. Hilo ni kosa lenye hatari.”[3]
Muungano wa Sovieti ulipotanguka katika 1991, jeuri ya kikabila ilifuata upesi. Watu wapatao 1,500 waliuawa, na karibu 80,000 wakakosa makao katika ile iliyokuwa jamhuri ya Georgia ya Sovieti. Mamia ya watu walikufa, na maelfu walikosa makao kwa mapigano katika Moldova. Uhai umepotezwa pia katika mapambano kati ya Armenia na Azerbaijan, pamoja na jamhuri nyinginezo za ile iliyokuwa Sovieti.[4]
Jamhuri iliyo kubwa zaidi ya zote katika ile iliyokuwa Sovieti ni Urusi. Hata huko vikundi vingi vya kikabila vyatafuta kuanzisha jamhuri zao wenyewe zilizo huru. Hivyo, The European liliripoti hivi katika kiangazi hiki: “Muungano wa Urusi wakabili mvunjiko.” Gazeti hilo lilisema: “Katika majuma machache yaliyopita, maeneo matatu yamepiga kura ya kujitangaza yenyewe kuwa jamhuri . . . Mengine matatu yalionyesha juma hili lililopita kwamba yatafuata hatua hiyo.”[5]
Nchi tofauti-tofauti zikifanyizwa, unaweza kung’ang’ana na majina usiyofahamu, kama vile Kaliningrad, Tatarstan, Stavropolye, Chechnya, Vologda, Sverdlovsk, Bashkortostan, Yakutiya, na Primorye.[6] Je! jambo hili halionekani sawa na lile lililotukia katika ile iliyokuwa Yugoslavia—ambapo Serbia, Croatia, na Slovenia zimeundwa na ambapo bado nchi nyinginezo huenda zikatokezwa?
Katibu wa serikali wa U.S. Warren Christopher alizungumza juu ya “kutokea kwa mapambano ya kikabila, kidini na kimaeneo yaliyokuwa yamezuiwa kwa muda mrefu” na akauliza: “Tusipopata njia fulani ya vikundi tofauti vya kikabila kuweza kuishi pamoja katika nchi moja, tutakuwa na nchi ngapi?” Alisema kwamba kutakuwa na maelfu.[7]
Migawanyiko Kila Mahali
Unaamini kulikuwako mapambano mangapi ya kikabila, kidini, na kimaeneo yaliyoendelea mapema mwaka huu? Je! ungesema 4, 7, 9, 13, labda hata 15? Katika Februari, The New York Times liliorodhesha jumbla ya 48! Huenda televisheni haikuandaa picha za maiti zenye kujaa damu na watoto wenye hofu kuu kutoka kwa mapambano hayo yote 48, lakini je, hilo lafanya msiba huo kutokuwa halisi kwa wahusika?[8]
Ni kama hakuna hata pembe moja ya tufe ambapo uwezekano wa kupigana haupo. Katika Nigeria, ambapo vikundi vya kikabila 200 hivi vipo, kuna lile tisho la vita ya wenyewe kwa wenyewe. “Pambano kama hilo,” gazeti Time likaripoti, “lingeweza kugongesha vikundi vikubwa vitatu vya kikabila—Hausa, Ibo na Yoruba—kimoja dhidi ya kingine.” Liliongezea hivi: “Kama vile wachunguzi wengine wanavyoliona, Nigeria yaweza kugeuka kuwa kama Yugoslavia.”[9]
Nchi ya Afrika Magharibi ya Liberia imeharibiwa vivyo hivyo na jeuri ya kikabila. Kiongozi mmoja wa wapiganaji wa kuvizia alipata tegemezo kutoka kwa makabila ya Gio na Mano ili kumpindua rais, ambaye alikuwa wa kikundi cha kabila la Krahn. Zaidi ya watu 20,000 waliuawa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, na mamia ya maelfu waliondoshwa mahali pao.[10]
Katika Afrika Kusini, weupe na weusi wanashindana kwa kung’ang’ania uongozi wa kisiasa. Lakini kupigana huko si tu kwa mweusi dhidi ya mweupe. Mwaka uliopita pekee, watu wapatao 3,000 waliuawa katika mapigano kati ya vikundi vya weusi vyenye kuzozana.[11]
Katika Somalia watu wapatao 300,000 walikufa na milioni moja waliachwa bila makao wakati vita ya kiukoo iligeuka kuwa ya wenyewe kwa wenyewe.[12] Katika Burundi na Rwanda, mapigano ya kikabila kati ya Wahutu na Watutsi yametokeza maelfu ya vifo katika miaka ya karibuni.[13]
Kupigana kwaonekana kana kwamba hakuishi kati ya Wayahudi na Waarabu katika Israel, kati ya Wahindu na Waislamu katika India, na kati ya Waprotestanti na Wakatoliki katika Ailandi. Jeuri ya kirangi pia ilifoka mwaka uliopita katika Los Angeles, Kalifornia, ikiangamiza maisha zaidi ya 40. Kokote ambako watu wa rangi, mataifa, au dini mbalimbali wanaishi pamoja karibu-karibu, mara nyingi mapambano makali hutokea.[14]
Je! wanadamu waweza kutatua mashaka haya ya ugomvi wa kikabila?
Jitihada za Mapatano za Wanadamu
Kwa kielelezo, fikiria lililopata jitihada katika ile iliyokuwa Yugoslavia na ile iliyokuwa Muungano wa Sovieti. Katika 1929, Yugoslavia iliundwa katika jaribio la kuunganisha vi-kundi mbalimbali vya kikabila vinavyoishi katika kusini-mashariki mwa Ulaya viwe nchi moja. Muungano wa Sovieti pia uliundwa vivyo hivyo kwa kuleta pamoja watu wa rangi, dini na mataifa mbalimbali. Kwa miongo mingi nchi hizo mbili zilikuwa na serikali kuu zenye nguvu zilizowaunganisha, na hatimaye ilionekana kama raia zao wamejifunza kuishi pamoja.
“Ramani ya kikabila ya Bosnia kabla ya vita, na vilevile Yugoslavia kabla ya vita, ilikuwa kama ngozi ya chui wa Amerika,” akaeleza Mserbia mwenye kuongoza. “Watu hao walikuwa mchanganyiko usiochangulika.” Kwa kweli, karibu asilimia 15 ya ndoa katika Yugoslavia zilikuwa kati ya watu wa vikundi mbalimbali vya kikabila.[15] Hali kama hiyo ya kuonekana kuwa kuna umoja ilikuwa imekuwapo kwa kuchanganyika kwa vikundi vya kikabila katika Muungano wa Sovieti.
Hivyo, shtuko lilikuwa kubwa wakati, baada ya miongo mingi ya amani iliyo wazi, jeuri ya kikabila ilifoka. Leo, kama vile mwandikaji mmoja wa magazeti alivyoandika, watu sasa “huweka ramani ya namna Yugoslavia ilivyokuwa kwa kuigawanya kirangi, kidini na kitaifa.”[16] Kwa nini, wakati serikali hizo zenye nguvu zilipoanguka, nchi hizo ziligawanyika?
Mambo Yanayosababisha
Kiasili watu hawachukii watu wa kikundi kingine cha kikabila. Kama vile wimbo mmoja wenye kupendwa sana ulivyosema wakati mmoja, unahitaji ‘kufunzwa kwa uangalifu kabla haijawa kuchelewa mno, kabla hujawa na umri wa miaka sita au saba au minane, kuchukia watu wote ambao watu wa ukoo wako wanawachukia.’[17] Wimbo huo ulirejezea wenzi wachanga waliooana ambao kwa wazi wana tofauti kubwa za kirangi. Hata hivyo, kulingana na mstadi wa afya ya kiakili Zarka Kovac, watu katika ile iliyokuwa Yugoslavia “ni adimu kuwa na tofauti zozote za kimwili.” Ingawa hivyo, jeuri ni nyingi sana. “Unamkatakata mtu uliyemuua ili usimtambue ndugu yako,” Kovac akasema.[18]
Kwa wazi, chuki hiyo ya kirangi na ya kikabila si asili ya kibinadamu. Watu wamefundishwa kwa uangalifu na waeneza propaganda pamoja na watu wa ukoo ambao wanakumbuka ukatili wa zamani. Ni nani achocheaye yote hayo? Akijaribu kuelewa maogofyo ya vita, mwanabiashara mmoja kutoka Sarajevo alichochewa kukata kauli hivi: “Baada ya mwaka wa vita ya Bosnia naamini kwamba ni Shetani aichocheaye. Hiki ni kichaa kabisa.”[19]
Ijapokuwa wengi hawaamini kuwapo kwa Shetani Ibilisi, Biblia yaonyesha wazi kuwapo kwa mtu asiyeonekana mwenye uwezo kupita wa kibinadamu, ambaye anaathiri vibaya tabia ya ainabinadamu. (Mathayo 4:1-11; Yohana 12:31) Unapofikiri juu ya jambo hilo—juu ya ubaguzi, chuki, na jeuri zenye upumbavu—labda utakubali kwamba Biblia haikisii inaposema hivi: “[Yule] aitwaye Ibilisi na Shetani . . . audanganyaye ulimwengu wote.”—Ufunuo 12:9; 1 Yohana 5:19.
Mwanga wa Tumaini
Tunapofikiria msukosuko wa ulimwengu wa karibuni, ile ndoto ya ainabinadamu yenye muungano yaonekana kuwa mbali kuliko wakati mwingine wowote. Mashindano ya kitaifa na kikabila yatisha kuwapo kwa mwanadamu kuliko wakati mwingine wowote. Hata hivyo, miongoni mwa giza hili la tufeni, mwanga wa tumaini wang’aa pe. Wakati wa kiangazi cha 1993, kikundi cha watu kutoka vikundi vya kikabila vyenye kupigana walionyesha muungano sawa ambao umewaruhusu kushinda ugomvi wa kikabila na kufanya kazi pamoja kwa upendo na umoja.
Jambo lililo kinyume ni kwamba muungano huo waletwa na jambo hasa linalogawanya ainabinadamu—dini. Gazeti Time liliripoti: “Ukichunguza ukabila wowote wenye ugomvi, au utaifa, kwa kawaida utapata chini yake kiini cha kidini . . . Chuki za kidini huwa za kikatili na zisizo na huruma na zisizo na mpaka.”[20] Juu ya mambo hayohayo, India Today lilisema: “Dini imekuwa jina ambalo uhalifu mwingi mkatili umetendwa. . . . Hiyo hutokeza jeuri kubwa ajabu na ni nguvu yenye kuangamiza sana.”[21]
Kwelikweli, kwa kawaida dini imekuwa sehemu ya tatizo hilo, si utatuzi. Lakini kikundi hiki kimoja cha kidini kilichotajwa juu—kikundi chenye watu wengi—kimeonyesha kwamba dini yaweza kuunganisha watu, si kugawanya. Ni nani walio katika kikundi hiki? Na kwa nini wamefurahia mafanikio makubwa ajabu ilhali wengine wameshindwa? Ili kupata jibu twakukaribisha usome makala zifuatazo. Kufanya hivyo kwaweza kukupa mtazamo mpya wa wakati ujao wa ainabinadamu.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Makaburi katika Bosnia. Haley/Sipa Press