Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 11/8 kur. 3-9
  • Sarajevo—Kutoka 1914 Hadi 1994

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sarajevo—Kutoka 1914 Hadi 1994
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Yugoslavia na Vita ya Ulimwengu 1
  • Yugoslavia na Vita ya Ulimwengu 2
  • Risasi Zile Zilizobadili Ulimwengu
  • Majaribio ya Kueleza 1914
  • Makosa Yaliyoanzisha Vita vya Ulimwengu
    Amkeni!—2009
  • 1914-Mwaka Ulioshtua Ulimwengu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Ufalme wa Mungu Huanza Kutawala Katikati ya Adui Zake
    Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele
  • 1914 Ni Historia Tu? Au Una Matokeo Juu Yako?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 11/8 kur. 3-9

Sarajevo—Kutoka 1914 Hadi 1994

NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA SWEDEN

Miaka 80 imepita tangu mipigo hiyo yenye msiba mnamo Juni 28, 1914, katika Sarajevo. Mipigo hiyo iliua Dyuki-mkuu Francis Ferdinand na mkeye, Dyuki-mkuu wa kike Sophie, na kisha uhasama kati ya Austria-Hungaria na Serbia ukaongezeka kuwa Vita ya Ulimwengu 1. Kati ya wanaume vijana milioni 65 waliopelekwa kwenye nyanja-vita, karibu milioni 9 hawakurudi kamwe. Kutia ndani majeruhi wa kiraia, jumla ya watu milioni 21 waliuawa. Wengine bado huongea kwamba katika Agosti 1914 ndio wakati ambapo “ulimwengu ulipatwa na kichaa.”

MARA nyingine tena mwangwi wa mipigo hiyo umekuwa ukiendelea kotekote Sarajevo. Na si katika Sarajevo tu bali pia katika jamhuri sita za muungano wa zamani wa Yugoslavia.a Kile kitabu Jugoslavien—Ett land i upplösning (Yugoslavia—Nchi Inayosambaratika) chataarifu: “Ni vita ya kiraia ambayo jirani hupigana na jirani. Madukuduku yenye kudumu na mitazamo ya udadisi yamekua kuwa chuki. Chuki hiyo imeongoza kwenye mapigano na mapigano kwenye mauaji mengi zaidi na uharibifu zaidi. Ni kama duara la uhalifu ama, mzunguko wenye kuongezeka wa chuki, udadisi, na mauaji.”

Mapigano yalipozuka katika Yugoslavia mnamo Juni 1991, haishangazi kwamba watu wengi walikumbuka ile mipigo iliyofyatuliwa katika Sarajevo mnamo Juni 1914. Je, mzozano mpya huu ungeongoza kwenye matokeo yenye maangamizi kama yale yale? Je, amani katika Ulaya ingehatarishwa? Je, programu hiyo ya “usafishaji wa kikabila” (mauaji ya kimakusudi na kufukuzwa kwa vikundi vya kijamii, kisiasa, ama kitamaduni) ingeweza kusambaa hadi sehemu nyingine za ulimwengu? Msongo wa kimataifa umewekwa ili kujaribu kukomesha mapigano. Lakini ni nini hasa kisababishi cha matatizo katika iliyokuwa Yugoslavia? Je, matukio ya hivi karibuni katika Sarajevo yana uhusiano wowote na yale mauaji ya Dyuki-mkuu katika 1914?

Yugoslavia na Vita ya Ulimwengu 1

Mizozano hiyo si mipya. Mwanzoni mwa karne hii, Peninsula ya Balkani ilisemwa kuwa “pembe isiyotulia ya Ulaya.” Jugoslavien—Ett land i upplösning husema: “Ni suala la kusambaratika kwa muungano ambapo wasiwasi umekuwa ukikua kwa muda mrefu. Kwa hakika, mizozano hiyo ilikuwepo tayari zilipoundwa Falme za Serbia, Kroatia na Slovenia [jina la awali la Yugoslavia] mwishoni mwa Vita ya Ulimwengu 1.” Historia fulani itatusaidia kuona jinsi mizozano ya kisiku-hizi ihusianavyo kwa Vita ya Ulimwengu 1.

Historia hutuambia kwamba wakati wa kuuawa kwa Francis Ferdinand mnamo 1914, nchi za Kislavi za Kusini za Slovenia, Kroatia, na Bosnia na Herzegovina zilikuwa mikoa katika Milki ya Austria-Hungaria. Kwa upande ule mwingine, Serbia ilikuwa ufalme ulio huru na ulikuwa umekuwa hivyo tangu 1878, ikiungwa mkono sana na Urusi. Hata hivyo, Waserbia wengi waliishi katika mikoa iliyotawaliwa na Austria-Hungaria, na hivyo basi Waserbia walitaka Austria-Hungaria maeneo yote iliyotwaa katika Peninsula ya Balkani. Hata ingawa mizozano ilikuweko baina ya Kroatia na Serbia, waliungamana katika takwa moja: kuwaondoa watawala wa kigeni wenye kuwachukiza. Wanautaifa waliota juu ya kuungamanisha Waslavu wa Kusini wote wawe ufalme mmoja. Katika kuunda jimbo kama hilo lililo huru, Waserbia walikuwa na athari kubwa zaidi.

Katika wakati huo maliki mtawala, Francis Joseph, alikuwa na umri wa miaka 84. Muda mfupi baadaye Dyuki-mkuu Francis Ferdinand angekuwa maliki mpya. Wanautaifa Waserbia walimwona Francis Ferdinand kama kipingamizi cha utimizo wa ndoto yao ya ufalme wa Kislavi wa Kusini.

Wanafunzi fulani vijana katika Serbia walipagawa na dhana ya ufalme huru wa Kislavi wa Kusini na walikuwa na hiari ya kufia hilo. Vijana kadhaa walichaguliwa kutekeleza mauaji ya Dyuki-mkuu huyo. Walipewa silaha na wakazoezwa na kikundi cha wanautaifa cha siri cha Kiserbia kiitwacho Mkono Mweusi. Wawili wa vijana hao walifanya majaribio ya kuua Dyuki-mkuu, na mmoja wao akafaulu. Jina lake lilikuwa Gavrilo Princip. Alikuwa na umri wa miaka 19.

Uuaji huu ulitimiza makusudi ya watekelezi. Vita ya ulimwengu ya kwanza ilipoisha, utawala wa kifalme wa Austria-Hungaria ulikuwa umevunjwa, na Serbia ingaliweza kuongoza katika kuungamanisha Waslavu ili kuunda ufalme. Mnamo 1918 ufalme huo ukaja kujulikana kama Ufalme wa Waserbia, Wakroatia, na Wasloveni. Katika 1929 jina likabadilishwa kuwa Yugoslavia. Hata hivyo, vikundi viwili hivyo vilipokuwa havihitaji tena kuungamana katika uadui wao wa kishirika dhidi ya Austria-Hungaria, ikawa wazi kwamba kulikuwa na tofauti kati ya vikundi vyenyewe. Kuna idadi ya karibu vikundi 20 tofauti, lugha nne rasmi na nyingine kadhaa ndogo, alfabeti mbili tofauti (Kiroma na Kisirili), na dini kubwa tatu—Katoliki, Uislamu, na Orthodoksi ya Waserbia. Dini huendelea kuwa kisababishi kikubwa cha migawanyiko. Kwa maneno mengine, kulikuwa na visababishi vingi vya kudumu vyenye kugawanya katika Serikali mpya hiyo.

Yugoslavia na Vita ya Ulimwengu 2

Wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, Ujerumani ilivamia Yugoslavia, na, kulingana na kitabu The Yugoslav Auschwitz and the Vatican, “zaidi ya watu 200,000, wengi wao Waorthodoksi Waserbia, kwa utaratibu waliuawa kimakusudi” na Wakatoliki Wakroatia waliokuwa wakishirikiana na Wanazi. Hata hivyo, Josip Tito Mkroatia, pamoja na washirika wake Wakomunisti na kwa ushirikiano wa Waingereza na Wamarekani aliweza kuwashinda Wajerumani. Vita ilipoisha, bila kupingwa akawa kiongozi wa nchi hiyo naye akatawala kwa mabavu. Alikuwa mwanamume mwenye kujitegemea. Hata Stalin hangeweza kumlazimisha kupatanisha Yugoslavia na sehemu ile nyingine ya mataifa ya Ukomunisti.

Wengi kutoka Yugoslavia hiyo ya zamani wamesema hivi: ‘Isingalikuwa Tito, muungano ungalisambaratika mapema zaidi. Yeye peke yake alikuwa na uwezo na mamlaka yaliyohitajika kuunganisha.’ Hilo limethibitika kuwa kweli. Ilikuwa baada ya kifo cha Tito mnamo 1980 kwamba mizozano ilichacha tena, ikiongezeka hadi kufyatuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe katika 1991.

Risasi Zile Zilizobadili Ulimwengu

Katika kitabu chake Thunder at Twilight—Vienna 1913/1914, mtungaji Frederic Morton aliandika kuhusu mauaji ya kukusudia ya Francis Ferdinand: “Ile risasi iliyojitoma kooni mwake iliashiria mpigo wa mwanzo katika mauaji maangamivu ambayo mwanadamu alikuwa hajawahi kuyaona. Ilianzisha michocheo iliyoongoza kwenye Vita ya Ulimwengu 2. . . . Vingi vya visababishi vya yote yale tuyaonayo leo vikasababishwa kando kando ya Danube ule mwaka na nusu uliotangulia kufyatuliwa kwa bastola kichwani mwa Dyuki-mkuu.”—Italiki ni zetu.

Matukio ya majuzi katika iliyokuwa Yugoslavia siyo tu yaliyo “visababishi vya yote yale tuyaonayo” viwezavyo kufuatiliwa nyuma hadi 1914. Mwanahistoria Edmond Taylor aeleza jambo ambalo wanahistoria wengi hukubali: “Kufyatuka kwa Vita ya Ulimwengu 1 kulifungulia karne ya ishirini ‘Wakati wa Taabu’ . . . Vurugu zote za nusu karne iliyokwisha zimeanzia moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kurudi nyuma kwenye 1914.”

Jitihada zimefanywa ili kueleza kwa nini mipigo katika Sarajevo ilikuwa na matokeo yenye msiba hivyo. Ingewezekanaje mipigo miwili kutoka kwa “kijana wa shule” kuwasha moto ulimwengu wote na kuanzisha kipindi cha jeuri, mchafuko, na mzinduko ambacho kimeendelea mpaka hivi leo?

Majaribio ya Kueleza 1914

Katika kitabu chake Thunder at Twilight—Vienna 1913/1914, mtungaji ajitahidi kueleza kisababishi kwa kuelekeza kwa kile alichokiita “ule uwezo mpya” ulioathiri mataifa katika 1914. Huo “uwezo,” asema, kwa kweli vilikuwa visababishi kadhaa vilivyotenda kwa umoja. Zile sauti chache za akili timamu zilizopaazwa zilimezwa na vilio vilivyoendelea daima vya vita. Kujitayarisha kivita kwa nchi moja kulihamasisha zile nyingine kufanya hivyo. Mamlaka ilihamishwa kutoka kwa daraja la watawala hadi kwa majenerali. Watu wengi pia katika vita walipata fursa ya kupata “uvinjari mkuu wa kitaifa” na hivyo basi kuyapa kisogo maisha ya kila siku yenye kuchosha. Baadaye, ofisa mmoja aliandika hivi: “Kama watu wanaotarajia faraja kutoka kwa ngurumo ya radi wakati wa ari ya kiangazi, ndivyo kizazi cha 1914 kilivyoamini faraja ambayo vita ingeweza kuleta.” Mtungaji Mjerumani Hermann Hesse alisema ingenufaisha watu zaidi kuwaamsha kutoka kwa “amani isiyopendeza ya kikabaila.” Mshinda tuzo la Nobeli mtungaji Thomas Mann alisema kuwa vita ni “utakasaji, uwekaji huru, tumaini kubwa sana.” Hata Winston Churchill, akiwa amelewa wazo la vita, aliandika hivi: “Matayarisho ya Vita yana msisimuko wa kunichukiza sana. Mimi nasali kwa Mungu ili anisamehe kwa hali hizo za ugeugeu wa msisimuko wenye hofu.”

Ni kwa sababu ya huu “uwezo mpya” kwamba tamasha zenye hamasa zilionekana kotekote Ulaya wanajeshi walipoelekea vitani. Vitawi vibichi vilibandikwa katika kofia zao, maua ya waridi yaliangikwa kwa matita kuzunguka mizinga, okestra zilicheza, wake wa nyumbani walipunga kwa vitambaa vya mkono kutoka kwenye madirisha yao, na watoto wenye shangwe walikimbia sambamba na wanajeshi. Ilikuwa kana kwamba watu walisherehekea na kushangilia kufika kwa vita. Vita ya ulimwengu iliwapata ikiwa shamrashamra.

Huu ni muhtasari wa baadhi ya yale Morton, aliyenukuliwa mbeleni, aliyaita “uwezo mpya” unaopaswa kutusaidia kuelewa kiini cha vita ya ulimwengu ya kwanza. Lakini “uwezo” huu ulitoka wapi? Mwanahistoria Barbara Tuchman aliandika kwamba jamii ya kiviwanda ilimpa mwanadamu uwezo mbalimbali ulio mpya na misongo mipya. Hakika, “jamii . . . ilikuwa . . . ikipasuka kwa mivutano mipya na nguvu zilizorundamana.” Stefan Zweig, kijana mwenye akili kutoka Vienna wakati ule, aliandika hivi: “Siwezi kueleza vingine kuliko kwa kani hii ya ziada, tokeo lenye msiba la nishati nyingi zilizorundamana kwa miaka arobaini ya amani na sasa zimetafuta kipenyo cha kutokea.” Yale maelezo “Siwezi kueleza vingine” hudokeza kwamba yeye mwenyewe huona ugumu wa kueleza. Katika dibaji kwa kitabu chake Thunder at Twilight, Morton aandika: “Kwa nini hilo lilitokea wakati huo na huko tu? Na jinsi gani? . . . Je, kuna kigezo cha kitendawili hicho?”

Naam, wengi wanaojitahidi kueleza 1914 huhisi kwamba sababu za kimsingi hakika si rahisi kuzielewa. Kwa nini vita haikudhibitiwa iwe ya vikundi vilivyohusika moja kwa moja? Kwa nini ikasambaa kuwa vita ya ulimwengu? Kwa nini ilikuwa ni ya pekee sana na yenye kuangamiza? Ni nini hasa uwezo mgeni huu ulioshika mwanadamu katika vuli ya 1914? Makala yetu ifuatayo, ukurasa 10, itazungumzia jibu la Biblia kwa maswali haya.

[Maelezo ya Chini]

a Yugoslavia humaanisha “Bara la Waslavu wa Kusini.” Ni jamhuri za Bosnia na Herzegovina, Kroatia, Makedonia, Montenegro, Serbia, na Slovenia.

[Blabu katika ukurasa wa 6]

“Kama watu wanaotarajia faraja kutoka kwa ngurumo ya radi wakati wa ari ya kiangazi, ndivyo kizazi cha 1914 kilivyoamini faraja ambayo vita ingeweza kuleta.”—Ernest U. Cormons, Mjumbe wa ubalozi wa Austria

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

1914

Biblia ilitoa unabii juu ya yale matukio yenye msiba ambayo yametukia tangu 1914

“Akatoka farasi mwingine, mwekundu sana, na yeye aliyempanda alipewa kuiondoa amani katika nchi, ili watu wauane, naye akapewa upanga mkubwa. Na alipoifungua muhuri ya tatu, nikamsikia yule wa tatu mwenye uhai akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi mweusi, na yeye aliyempanda ana mizani mkononi mwake. Nikasikia kama sauti katikati ya hao wenye uhai wanne, ikisema, Kibaba cha ngano kwa nusu rupia, na vibaba vitatu vya shayiri kwa nusu rupia, wala usiyadhuru mafuta wala divai. Na alipoifungua muhuri ya nne, nikasikia sauti ya yule mwenye uhai wa nne akisema, Njoo! Nikaona, na tazama, farasi wa rangi ya kijivujivu, na yeye aliyempanda jina lake ni Mauti, na Kuzimu [“Hadesi,” New World Translation] akafuatana naye. Nao wakapewa mamlaka juu ya robo ya nchi, waue kwa upanga na kwa njaa na kwa tauni na kwa hayawani wa nchi.” Ufunuo 6:4-8 (Ona pia Luka 21:10-26; 2 Timotheo 3:1-5.)

“Vita Kubwa ya 1914-18 yajitanda kama ukanda wa ardhi ulionyauka uliobainisha wakati huo kutoka kwa wetu. Kwa kufyeka uhai wa watu wengi ambao wangalikuwa watendaji kwa miaka iliyofuata, kwa kuharibu itikadi, kubadili mawazo, na kuacha vidonda visivyopona vya mzinduko, ilikuza mwanya mkuu wa kimwili na pia wa kisaikolojia kati ya mihula miwili.”—Dibaji kwa The Proud Tower, na Barbara W. Tuchman.

“Miaka minne iliyofuata [1914] ilikuwa, kama Graham Wallas alivyoandika, ‘miaka minne ya jitihada iliyo kali na ya ujasiri mwingi zaidi iliyopata kufanywa na jamii ya binadamu.’ Jitihada hiyo ilipoisha, ndoto na idili zihusuzo 1914 zilianza kudidimia polepole chini ya tungamo la bahari ya mzinduko mkubwa sana. Kwa gharama ambayo ubinadamu ulikuwa umeilipa, faida kuu uliyoipata ilikuwa kutambua mipaka yayo yenyewe kwa njia yenye maumivu.”—Maneno ya baadaye katika kichapo hichohicho.

[Hisani]

The Bettmann Archive

The Trustees of the Imperial War Museum, London

National Archives of Canada, P.A. 40136

[Ramani katika ukurasa wa 7]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Ulaya Kama Ilivyokuwa—Agosti 1914

1. Uingereza na Ireland 2. Ufaransa 3. Hispania

4. Milki ya Ujerumani 5. Uswisi 6. Italia

7. Urusi 8. Austria-Hungaria

9. Rumania 10. Bulgaria 11. Serbia

12. Montenegro 13. Albania 14. Ugiriki

[Picha katika ukurasa wa 5]

Gavrilo Princip

[Picha katika ukurasa wa 6]

Wajerumani wakipokea maua wakielekea vitani

[Hisani]

The Bettmann Archive

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

Culver Pictures

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki