Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w92 5/1 kur. 3-5
  • 1914-Mwaka Ulioshtua Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • 1914-Mwaka Ulioshtua Ulimwengu
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kwa Ghafula, Katika Agosti
  • Ingemalizika Kabla ya Krismasi Kufika?
  • Badiliko Kubwa
  • Ufalme wa Mungu Huanza Kutawala Katikati ya Adui Zake
    Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele
  • Sarajevo—Kutoka 1914 Hadi 1994
    Amkeni!—1994
  • Ambayo 1914 Ungemaanisha Kwako Wewe
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
  • Maana Halisi ya 1914
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
w92 5/1 kur. 3-5

1914-Mwaka Ulioshtua Ulimwengu

“Ile Vita Kubwa ya 1914-18 huwa kama ukanda wa bara ulioteketezwa unaotenga wakati huo na wetu. Kwa kuangamiza maisha mengi sana . . . , kwa kuharibu imani, kubadili mawazo, na kuacha majeraha yasiyoponyeka ya utamausho, ilifanyiza pengo kubwa la halisi na la akili pia kati ya mihula miwili.”—Kutoka kitabu The Proud Tower—A Portrait of the World Before the War 1890-1914, cha Barbara Tekman.

“Karibu iwe—lakini si kikamili bado—sehemu ya historia, kwani maelfu mengi ya watu waliokuwa wachanga mwanzoni mwa karne hii ya ishirini ya maana sana wangali hai.”—Kutoka kitabu 1914, cha Lin MacDonald, kilichotangazwa kwa chapa katika 1987.

KWA nini tupendezwe na mwaka 1914? ‘Ni wakati ujao unaonihangaisha,’ huenda ukasema, ‘si wakati uliopita.’ Kukiwa na matatizo kama vile uchafuzi wa duniani pote, kuvunjika kwa maisha ya familia, ongezeko katika uhalifu, ugonjwa wa akili, na ukosefu wa kazi za kuajiriwa, wakati ujao wa mwanadamu huenda ukaonekana kuwa unakosa tumaini. Hata hivyo, wengi ambao wamechunguza umaana wa 1914, walipata msingi wa tumaini katika wakati ujao ulio bora zaidi.

Kwa miongo kadhaa Mnara wa Mlinzi limeeleza kwamba katika 1914 ainabinadamu waliona ule uitwao “mwanzo wa maumivu makali ya ghafula ya taabu.” Usemi huo hufanyiza sehemu ya unabii mkubwa wa Yesu Kristo juu ya matukio ambayo yangetangulia mwisho wa mfumo mbovu wa mwanadamu.—Mathayo 24:7, 8, New World Translation of the Holy Scriptures.

Leo, asilimia ndogo ya ainabinadamu ingali yaweza kukumbuka matukio yenye kutazamisha ya 1914. Je! kizazi hicho cha wazee-wazee kitapita kabla ya Mungu kuokoa dunia kutoka uharibifu? Sivyo kulingana na unabii wa Biblia. “Myaonapo hayo yote,” Yesu akaahidi, “tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni. Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia.”—Mathayo 24:33, 34.

Ili kuthamini ni kwa nini mwaka 1914 una umaana wa kihistoria kama huo, fikiria hali ya ulimwengu mpaka kufikia katikati ya 1914. Kabla ya wakati huo, watawala kama vile Maliki Nicholas wa Urusi, Maliki Vilhelm wa Ujerumani, na Maliki Frantsi Yozef wa Austria-Hangari walitumia uwezo mwingi. Kila mmoja wa wanaume hao angeweza kuwakusanya wanaume wa vita zaidi ya milioni nne na kuwatuma vitani. Lakini babu zao walikuwa wametia sahihi ule ulioitwa Mpatano Mtakatifu, wakipiga mbiu kwamba Mungu alikuwa amewachagua watawale sehemu tofauti za “taifa la Kikristo” moja kubwa.

Kulingana na The Encyclopœdia Britannica, hati hiyo “iliathiri kwa nguvu mwendo wa mapatano ya Ulaya katika karne ya 19.” Ilitumiwa kupinga harakati za kidemokrasi na kupendelea ile iliyoitwa eti haki ya kimungu ya wafalme. “Sisi Wafalme Wakristo,” Maliki Vilhelm akamwandikia Maliki Nicholas, “tuna wajibu mmoja mtakatifu, tuliopewa na Mbingu, huo ni kutegemeza ile kanuni ya [haki ya kimungu ya wafalme].” Je! hilo lilimaanisha kwamba wafalme wa Ulaya walihusika kwa njia fulani na Ufalme wa Mungu? (Linganisha 1 Wakorintho 4:8.) Na vipi makanisa yaliyowategemeza wafalme hao? Je! kudai kwao Ukristo kulikuwa kwa kweli? Jibu la maswali hayo lilikuwa wazi katika miaka iliyofuata 1914 moja kwa moja.

Kwa Ghafula, Katika Agosti

“Masika na kiangazi cha 1914 katika Ulaya kilionyesha hali ya utulivu isiyo ya kawaida,” akaandika waziri wa serikali Mwingereza Winston Churchill. Watu kwa ujumla walikuwa na matazamio mazuri juu ya wakati ujao. “Ulimwengu wa 1914 ulijawa na tumaini na ahadi,” asema Louis Snyder katika kitabu chake World War I.

Kweli, kwa miaka kadhaa kulikuwako ushindani mwingi kati ya Ujerumani na Uingereza. Hata hivyo, kama mwanahistoria G. P. Gooch aelezavyo katika kitabu chake Under Six Reigns: “Haikuelekea sana kwamba kungekuwa pigano katika Ulaya mwaka wa 1914 kama ilivyoelekea kuwako katika 1911, 1912 au 1913 . . . Uhusiano kati ya serikali hizo mbili ulikuwa afadhali zaidi ya jinsi ulivyokuwa kwa miaka kadhaa.” Kulingana na Winston Churchill, mshiriki wa bunge la Uingereza la 1914: “Ujerumani ilionekana kuwa na nia kama yetu ya kuazimia kuwa na amani.”

Hata hivyo, baada ya uuaji katika Sarajevo wa mwanamfalme mrithi wa Milki ya Austria-Hangari katika Juni 28, 1914, matazamio ya wakati ujao yakawa mabaya. Mwezi mmoja baadaye, Maliki Franz Josef alitangaza vita dhidi ya Serbia na akaamuru majeshi yake yashambulie ufalme huo. Wakati huo huo, usiku wa Agosti 3, 1914, kwa amri ya Maliki Vilhelm, jeshi kubwa la Kijerumani lilishambulia kwa ghafula ufalme wa Ubelgiji na kupigana likielekea Ufaransa. Siku iliyofuata Uingereza ilitangaza vita dhidi ya Ujerumani. Naye Maliki Nicholas, alikuwa ameamuru kukusanywa kwa jeshi kubwa la Urusi ili lipigane vita dhidi ya Ujerumani na Austria-Hangari. Ule Mpatano Mtakatifu ulikuwa umeshindwa kuwazuia wafalme wa Ulaya wasiingize bara hilo katika mauaji ya bure ya kuchinjana wenyewe kwa wenyewe. Lakini mishtuo mikubwa zaidi bado ingekuja.

Ingemalizika Kabla ya Krismasi Kufika?

Kutokea kwa vita hakukuzima matazamio mazuri ya watu. Wengi waliamini kwamba vita ingetokeza ulimwengu bora zaidi, na makundi mengi ya watu kotekote Ulaya yalikusanyika kuonyesha kuunga kwao mkono vita hiyo. “Hakuna yeyote katika 1914,” aandika A. J. P. Taylor katika kitabu chake The Stuggle for Mastery in Europe—1848-1918, “aliyefikiria kwa uzito hatari ya vita isipokuwa kijeshi. . . . Hakuna aliyetazamia msiba mkuu wa kijamii.” Badala ya hiyo, wengi walitoa unabii kwamba vita hiyo ingeisha baada ya miezi michache.

Ingawa hivyo, muda mrefu kabla ya watu wa Ulaya kuweza kusherehekea Krismasi yao ya 1914, mgogoro wenye umwagaji mwingi wa damu ulikuwa umetokea katika mahandaki yenye kufuatana urefu wa zaidi ya kilometa 700 kutoka Uswisi upande wa kusini hadi pwani ya Ubelgiji upande wa kaskazini. Hilo liliitwa Jeshi la Mbele la Magharibi, na mtungaji Mjerumani Herbert Selzbak alilitaja katika maandishi yake ya kila siku yaliyofanywa siku ya mwisho ya 1914. Maandishi hayo husomwa hivi: “Vita hii mbaya sana yazidi kuendelea, na hali kila mtu alifikiri mwanzoni kwamba ingeisha katika majuma machache, sasa mwisho hauonekani.” Wakati ule ule, katika sehemu nyinginezo za Ulaya, mapigano yenye umwagaji mwingi wa damu yali-endelea kati ya majeshi ya Urusi, Ujerumani, Austria-Hangari, na Serbia. Vita hiyo ilienea upesi kupita Ulaya, na mapigano yaliendelea baharini na katika Afrika, Mashariki ya Kati, na visiwa vya Pasifiki.

Miaka minne baadaye Ulaya ilikuwa imeharibika kabisa. Ujerumani, Urusi, na Austria-Hangari kila moja ilipoteza kati ya wanajeshi milioni moja na milioni mbili. Urusi ilikuwa imepoteza hata umaliki wayo katika mapinduzi ya Bolsheviki ya 1917. Huo ulikuwa mshtuo ulioje kwa wafalme wa Ulaya na makasisi wao wenye kuwaunga mkono! Wanahistoria wa ki-siku-hizi wangali wakionyesha mshangao. Katika kitabu chake Royal Sunset, Gordon Brook-Shepherd auliza hivi: “Ilikuwaje kwamba watawala, waliokuwa mara nyingi na uhusiano wa ukoo wa damu au wa ndoa na wote wenye kujitoa kabisa ili kuhifadhi umaliki, walijiruhusu wenyewe wahusike katika mauaji ya bure ya ukoo yaliyowafutilia mbali wengi wao wasiwepo tena na kuacha waokokaji wote wakiwa wamedhoofika?”

Jamhuri ya Ufaransa pia ilipoteza zaidi ya wanajeshi milioni moja, na Milki ya Uingereza, ambayo umaliki wayo ulikuwa tayari umedhoofika muda mrefu kabla ya vita hiyo, ilipoteza zaidi ya 900,000. Kwa ujumla, zaidi ya wanajeshi milioni 9 walikufa, na milioni 21 zaidi kujeruhiwa. Kuhusu raia waliokufa, The World Book Encyclopedia hutaarifu hivi: “Hakuna yeyote ajuaye ni raia wangapi waliokufa kwa sababu ya ugonjwa, njaa, na sababu nyinginezo zinazohusika na vita. Wanahistoria wengine huamini kwamba idadi ya raia waliokufa ilikuwa sawa na ile ya wanajeshi.” Mafua ya Kihispania yenye kuambukiza ya 1918 yaliua watu 21,000,000 wengine kotekote duniani.

Badiliko Kubwa

Ulimwengu haukuwa kamwe jinsi ulivyokuwa kabla ya ile Vita Kubwa, kama ilivyoitwa wakati huo. Kwa kuwa makanisa mengi ya Jumuiya ya Wakristo yalikuwa yameshiriki kwa bidii katika vita hiyo, waokokaji wengi waliotamauka waliacha dini na kupendelea kutokuamini kuwako kwa Mungu. Wengine waligeukia ufuatiaji wa mali za kimwili na anasa. Kulingana na Profesa Modris Eksteins katika kitabu chake Rites of Spring, miaka ya 1920 “ilishuhudia upendo wa anasa na upendo wa binafsi kwa kadiri yenye kutokeza.”

“Vita hiyo,” aeleza Profesa Eksteins, “ilishambulia viwango vya adili.” Watu kutoka pande zote mbili walikuwa wamefundishwa na viongozi wa kidini, kijeshi, na kisiasa waone uuaji wa watu wengi kuwa jambo jema kiadili. Hilo, akiri Esteins, “lilikuwa tu shambulio lenye kukosa hisia zaidi dhidi ya utaratibu wa kiadili uliodai kuwa na msingi katika elimu ya maadili ya Kiyahudi na Kikristo.” “Katika Jeshi la Mbele la Magharibi,” yeye aongeza, “nyumba za makahaba zilikuwa sehemu za kawaida za kambi za kijeshi . . . Huko nyumbani wanawake na wanaume pia wakawa wenye kukosa maadili. Umalaya uliongezeka kwa ajabu sana.”

Kwa kweli, 1914 ulibadili mambo mengi. Haukuwa umetokeza ulimwengu bora zaidi, na vita hiyo haikuthibitika kuwa “vita yenye kukomesha vita vyote,” kama watu wengi walivyokuwa wametumaini. Badala ya hiyo, kama mwanahistoria Barbara Tekman aoneleavyo: “Mawazo makuu na misisimko iliyokuwako hadi 1914 ilipotea polepole kwa sababu ya utamausho mwingi.”

Hata hivyo, wengine walioshuhudia msiba wa 1914 hawakushangazwa na matukio ya mwaka huo. Kwa kweli, kabla ya vita hiyo kutokea, walikuwa wakitazamia “wakati mbaya sana wa taabu.” Wao walikuwa nani? Na wao walijua nini ambalo wengine hawakujua?

[Sanduku katika ukurasa wa 5]

Matazamio Mazuri ya Uingereza Katika 1914

“Kwa muda wa karibu karne moja hakukuwa na adui yeyote katika bahari zinazozunguka kisiwa chetu. . . . Ilikuwa vigumu hata kuwazia uwezekano wa tisho kwa pwani hizi zenye amani. . . . London haikupata kamwe kuwa na furaha na ufanisi mwingi jinsi hiyo. Hakukupata kamwe kuwa na mengi sana yaliyostahili kufanywa, na kuonwa, na kusikiwa jinsi hiyo. Wala wazee wala vijana hawakuwa wakishuku hata kidogo kwamba lile walilokuwa wakishuhudia, katika majira hayo ya 1914 yasiyo na kifani, lilikuwa kwa kweli, mwisho wa muhula.”—Before the Lamps Went Out, cha Geoffrey Markus.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki