Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g01 9/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—2001
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Watumwa” Katika Meli za Kisasa
  • “Siri za Maumbile” Zinatokomea
  • Karatasi Zingali Zinatumiwa
  • Hatari ya Magenge ya Uhalifu
  • Takataka Zimejaa Angani
  • Uhaba wa Makazi Unazidi
  • Je, Ustadi wa Kuiba Mifukoni Unatokomea?
  • Wazazi Wawe Madereva Wazuri
  • “Mmea Mkubwa Zaidi Ulimwenguni”
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1993
  • Kujitahidi Kumaliza Uhalifu
    Amkeni!—1996
  • Ofisi Isiyotumia Karatasi
    Amkeni!—1999
  • Je! Wanadamu Wanaweza Kuleta Amani na Usalama Wenye Kudumu?
    Amani na Usalama wa Kweli—Wewe Unaweza Kuupataje?
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2001
g01 9/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

“Watumwa” Katika Meli za Kisasa

“Makumi ya maelfu ya mabaharia katika meli za kibiashara wanatendewa kama watumwa,” lasema gazeti la International Herald Tribune. Ripoti iliyoandikwa na Tume ya Kimataifa ya Usafiri wa Meli ilifunua kwamba mabaharia hao “wanafanya kazi katika mazingira hatari na kwa saa nyingi, hawalipwi mishahara, hawapati chakula cha kutosha, wanabakwa na kupigwa.” Mabaharia wa meli fulani wanaolalamika au kuomba msaada kwa vyama vya wafanyakazi wanaweza kutupwa baharini au kuandikwa kwenye orodha ya wale watakaoadhibiwa. Wengi wa wahasiriwa wa huo “utumwa wa kisasa” wanatoka hasa katika nchi zinazositawi. Kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi katika nchi zao, wengi wao hawana njia nyingine yoyote ya kupata riziki. Mwandishi wa ripoti hiyo anasema kwamba ndiyo sababu “wanakandamizwa, . . . wanadanganywa na kutopewa haki yao.”

“Siri za Maumbile” Zinatokomea

“Shirika la UM linakadiria kwamba asilimia 90 hivi ya lugha za ulimwengu zitatoweka katika karne ijayo na hivyo habari muhimu kuhusu maumbile zitatoweka pia,” yasema ripoti ya Shirika la Habari la Uingereza. Kwa kawaida lugha za kienyeji huwa na desturi, nyimbo, na hadithi zenye masomo muhimu kuhusu mazingira na wanyama, ambazo zimepitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Kwa mfano, kwa muda mrefu, Waturkana wanaoishi kaskazini-magharibi mwa Kenya wamekuwa wakichunguza tabia za ndege fulani ili kutabiri wakati wa mvua kunyesha. Jambo hilo linawasaidia kujua wakati wa kupanda. Ujuzi mwingi sana uliopitishwa kutoka vizazi vingi utapotea endapo lugha yao itatoweka. Tayari, lugha 234 za kienyeji zimetoweka, na lugha 2,500 ziko karibu sana kutoweka. “Siri za maumbile, zilizo katika nyimbo, hadithi, na sanaa za wenyeji, huenda zikatoweka milele,” yasema ripoti ya UM, ambayo inaonya kwamba jambo hilo ni hatari kwa ukuzaji wa mazao.

Karatasi Zingali Zinatumiwa

Zaidi ya miaka 25 iliyopita, ilitabiriwa kwamba matumizi ya karatasi yangepungua huku kompyuta zikizidi kutumiwa maofisini kuhifadhi habari. Lakini bado karatasi zinatumiwa kwa wingi. Gazeti Vancouver Sun lasema kwamba, mnamo mwaka wa 1999 Wakanada walitumia kiasi cha karatasi kinachozidi kiasi kilichotumiwa mwaka wa 1992 kwa asilimia 25 katika kunakili na kutuma faksi. Hiyo yamaanisha kwamba kwa ujumla “kila Mkanada, kutia ndani watoto, alitumia kilogramu 30 za karatasi kila mwaka.” Uchunguzi mmoja wa wafanyakazi wa ofisini ulionyesha kwamba ijapokuwa watu husoma habari kwanza kwenye kompyuta, bado wanapenda kuchapisha habari hiyo kwenye karatasi. Hata wale walio na kompyuta ndogo za kibinafsi wanafanya vivyo hivyo, lasema gazeti la Sun. Watoto wanatumia kiasi kikubwa sana cha karatasi, wao hupenda kuchapisha kila kitu wanachochora au kuona kwenye kompyuta.

Hatari ya Magenge ya Uhalifu

“Magenge ya uhalifu ulimwenguni pote yanahatarisha sana usalama wa watu wa kawaida kuliko vita.” Shirika la habari la Agence France-Presses linasema kwamba hoja hiyo ilitolewa hivi karibuni katika mkutano mmoja kuhusu uhalifu wa kimataifa. Akihutubia mkutano huo uliofanywa Tokyo, Pino Arlacchi, Msaidizi wa Katibu-Mkuu katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Kupambana na Uhalifu, alisema hivi: “Uhalifu ulimwenguni pote umefikia kiwango na hali ambayo raia na serikali haziwezi kuvumilia tena.” Alisema kwamba uuzaji wa wanadamu ndio uhalifu unaoongezeka kasi sana kuliko uhalifu mwingine wowote. Wanawake na watoto wapatao milioni moja wanasafirishwa kisiri na kuuzwa kwa faida kubwa na magenge ya uhalifu. Bunmei Ibuki, aliyekuwa kiongozi wa kisiasa wa mashirika ya polisi nchini Japani alisema, “hakuna nchi yoyote inayoweza kupambana na uhalifu wa kimataifa wa magenge ikiwa peke yake.” “Ndiyo sababu majimbo au ulimwengu wote unahitaji kufanya juu chini ili kupambana na tatizo hilo.”

Takataka Zimejaa Angani

Wanadamu wametupa takataka nyingi angani tangu walipoanza kusafiri huko miaka 40 hivi iliyopita. Kulingana na gazeti la The News la Mexico City, roketi zipatazo 4,000 zimerushwa angani, na sasa “kuna zaidi ya vitu 23,000 angani, kila kimoja ni kikubwa kushinda mpira wa kriketi.” Vitu 6,000 kati yake ni “takataka,” na vina uzito wa tani 1,800 kwa ujumla. Vitu vilivyo angani vimegongana na kutokeza vifusi vidogo-vidogo 100,000 hivi. Ijapokuwa vifusi hivyo si hatari kwa dunia, ni hatari sana kwa usafiri wa angani kwa sababu vinasafiri kwa mwendo wa kasi. Kipande kidogo sana cha chuma kinachosafiri kwa mwendo wa kilometa 50,000 kwa saa kinaweza kuvunja dirisha la kituo cha angani, kinaweza kutoboa betri inayotumia nishati ya jua, au kutoboa mavazi ya mwanaanga anayezunguka angani. “Shirika la NASA linatengeneza Kifaa cha Orion, ambacho kitafagia takataka zote angani,” lasema gazeti la The News. “Lengo ni kusambaratisha takataka hizo kwa miale ya leza, . . . ili ziingie katika anga la juu la Dunia ambamo zinaweza kuungua bila kudhuru dunia.”

Uhaba wa Makazi Unazidi

“Mnamo mwaka wa 1948 katika Azimio la Haki za Binadamu, shirika la UM lilisema kwamba kila mtu ana haki ya kuwa na makazi yafaayo, lakini sasa baada ya miaka 50 na zaidi, haki ya kuwa na makazi salama haijatimizwa bado,” lasema Shirika la Habari la Uingereza. Ripoti ya hivi karibuni ya UM inakadiria kwamba watu milioni 100 kote ulimwenguni hawana makazi—kutia ndani zaidi ya watoto milioni 30—na inaonya kwamba hali hiyo inazidi kuwa mbaya. Shirika la UM linasema kwamba hali hiyo inazidi kuwa mbaya katika nchi zinazositawi kwa sababu ya kuongezeka kwa miji. Kwa kuongezea, watu wapatao milioni 600 katika Asia Kusini-mashariki na katika Afrika, wanaishi katika mabanda machafu yaliyosongamana na yasiyokuwa na maji. Nchi tajiri zinakabili tatizo hilohilo. Nchini Marekani, watu wapatao 700,000 wanaishi barabarani. Katika sehemu fulani za Ulaya Magharibi, watu 12 kati ya watu 1,000 hawana makazi.

Je, Ustadi wa Kuiba Mifukoni Unatokomea?

“Ustadi wa kuiba mifukoni unatokomea huko Osaka,” Japani, kwa sababu “vijana hawapendezwi tena na tabia hiyo,” laripoti gazeti la Asahi Evening News. Afisa mmoja wa polisi katika jimbo hilo anasema kwamba ili kuwa mwizi stadi wa mifukoni mtu anahitaji kujizoeza kwa miaka kadhaa. Yaonekana kwamba vijana wahalifu wanapendelea njia rahisi za kuiba. Kwa mfano, visa vya unyakuzi wa pochi vinaongezeka. Thuluthi ya washukiwa waliokamatwa mwaka uliopita kwa sababu ya kuiba mifukoni katika Jimbo la Osaka walikuwa na umri wa miaka 60 au zaidi. Mshukiwa mzee zaidi, mwanamume mwenye umri wa miaka 78, alikamatwa kwa mara ya 12 alipokuwa akijaribu kuiba kifuko cha miwani kutoka kwa mkoba wa mwanamke mmoja mzee. Mpelelezi mmoja alisema kwamba “mzee huyo haoni vizuri kwa hiyo alichukua kifuko cha miwani huku akidhani ni pochi.”

Wazazi Wawe Madereva Wazuri

“Wazazi wanahitaji kutambua kwamba wanaigwa na watoto wao wanapojifunza udereva kabla ya kupata leseni,” asema Susan Ferguson wa Taasisi ya Bima ya Usalama wa Barabarani. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti New Scientist, Susan na wafanyakazi wenzake walichunguza rekodi za aksidenti za familia 140,000 za Marekani, na kulinganisha rekodi za wazazi na watoto wao wenye umri wa kati ya miaka 18 na 21. Watoto wa wazazi waliohusika katika aksidenti tatu au zaidi za gari katika muda wa miaka mitano walikuwa na uwezekano wa asilimia 22 wa kupata aksidenti kuliko watoto wa wazazi ambao hawakupata aksidenti. Ndivyo ilivyo pia kuhusiana na kukiuka sheria za barabarani kama vile kwenda kasi mno au kupuuza taa za kuongoza magari. Katika visa hivyo, uwezekano wa watoto kuiga wazazi wao ulikuwa asilimia 38. “Wazazi wanapaswa kuwa vielelezo bora,” asema Jane Eason wa Shirika la Uingereza la Kuzuia Aksidenti. “Watu wanapaswa kufundishwa umuhimu wa usalama wa barabarani wakiwa wangali wachanga.”

“Mmea Mkubwa Zaidi Ulimwenguni”

“Kuvu iitwayo Armillaria ostoyae inayosambaa katika misitu isiyokauka katika mashariki mwa Oregon, ndiyo mmea mkubwa zaidi ulimwenguni,” lasema gazeti la National Wildlife. “Kuvu hiyo imeishi kwa angalau miaka 2,400 na imefunika eneo lenye ukubwa unaozidi ekari 2,200—au viwanja 1,700 hivi vya soka, ndivyo wanavyosema wanasayansi wa Idara ya Misitu ya Marekani, waliogundua kuvu hiyo.” Kuvu hiyo inakua ardhini, na mara nyingi inaenea polepole kutoka mti mmoja hadi mwingine kupitia mizizi. Lakini kuvu hiyo ina “madhara,” wasema wataalamu wa misitu. Gazeti hilo laripoti kwamba “kuvu aina ya Armillaria inasababisha ugonjwa wa mizizi unaoangamiza miti.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki