Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 11/22 kur. 11-14
  • Mambo Hakika ya Krismasi, Ista, na Halowini

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mambo Hakika ya Krismasi, Ista, na Halowini
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Hakuna Kuchanganya Kweli na Uwongo
  • Je! Ni Ista—au Astarte?
  • Halowini—Usiku wa Kale Wenye Hofu Kuu
  • Biblia Inasema Nini Kuhusu Ista?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Shughuli za Baada ya Masomo
    Shule na Mashahidi wa Yehova
  • Sikukuu
    Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko
  • Sherehe Ambazo Zinamchukiza Mungu
    “Jitunzeni Katika Upendo wa Mungu”
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 11/22 kur. 11-14

Mambo Hakika ya Krismasi, Ista, na Halowini

BIBLIA huonyesha kwamba Yesu alikuwa mwenye miaka 33 1/2 alipotundikwa mapema katika masika ya mwaka 33 W.K., wakati wa Sikukuu ya Kupitwa ya Kiyahudi. Kwa kuhesabu kurudi nyuma, hiyo yamaanisha kwamba yeye alizaliwa mapema katika vuli ya mwaka.

Sherehe ya Roma ya kipagani ya Saturnalia, siku ya kuzaliwa kwa Jua lisiloshindwa, ilikuwa miezi mitatu baada ya hapo. Sherehe ya kuzaliwa kwa Yesu ilisukumwaje mbele hadi Desemba 25, ili kuifanya ilingane kwa njia ya kukufuru na sherehe ya kipagani ya siku ya kuzaliwa kwa jua?

Zile siku fupi wakati wote za Desemba zilitokeza mbabaiko wa kishirikina miongoni mwa waabudu-jua hao, waliohofu kwamba mungu wao alikuwa akifa. Waliwasha mishumaa na kuwasha mioto mikubwa ili kusaidia kuhuisha kiabudiwa hicho kilichokuwa kikiugua. Hilo lilionekana kana kwamba lilifanya kazi. Kufuatia katikati ya kipindi cha kipupwe cha Desemba 21, mungu-jua alionekana kupata nguvu yake tena siku zilipoendelea kuwa ndefu zaidi.

“Desemba ulikuwa mwezi mkuu wa sherehe za kipagani, na Des. 25 ilikuwa kilele cha sherehe za kipupwe,” laeleza gazeti Church Christmas Tab. “Watu fulani huamini kwamba askofu wa Roma alichagua Des. 25 kuwa tarehe ya kuzaliwa kwa Kristo ili ‘kutakasa’ sherehe za kipagani. Kile kilichotokea kilikuwa mchanganyiko usiofaa wa sherehe za kipagani na za Kikristo ambazo ulimwengu sasa huita Krismasi.” Makala hiyo yakiri hivi: “Neno ‘Krismasi’ halionekani katika Biblia. Na Andiko halitoi idhini yoyote ya kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu.”7

Si ajabu kwamba mwanatheolojia Tertullian alilalamika hivi: “Sisi, ambao hatujui juu ya Sabato, miezi mipya na sherehe nyinginezo, ambazo wakati mmoja zilikubaliwa na Mungu, Saturnalia [na karamu nyinginezo za kipagani] sasa huzoewa, zawadi hupelekwa huku na kule, . . . na michezo na karamu husherehekewa kwa vigelegele.”8

Papa Gregory 1 aliendeleza mwendo huo wenye kuchafua. Kulingana na gazeti Natural History, “badala ya kujaribu kuondolea mbali desturi na itikadi za watu, maagizo ya papa yalikuwa, wazitumie. Ikiwa kikundi cha watu huabudu mti, badala ya kuukata, wauweke wakfu kwa Kristo na kuwaruhusu waendeleze ibada yao.”

Hakuna Kuchanganya Kweli na Uwongo

Je! mwongozo huo wa kuridhiana ulikuwa na kibali cha kimungu? Angalia onyo la Mungu kwa watu wake waliokuwa tayari kuingia katika Kanaani ya kipagani: “Ujiangalie, . . . usije ukauliza habari za miungu yao, ukisema, Mataifa haya waitumikiaje miungu yao? nami nifanye vivyo. Usimtende kama haya BWANA [Yehova, NW], Mungu wako; kwani kila yaliyo machukizo kwa BWANA [Yehova, NW], ayachukiayo yeye, wameifanyia miungu yao.” (Kumbukumbu la Torati 12:30, 31) Onyo hilohilo limerudiwa katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo: “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari [kielezi-chini, Shetani, NW]? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?”—2 Wakorintho 6:14, 15.

Nini ambacho Mungu huona kuwa chenye kuchukiza sana juu ya miungu hiyo bandia na ibada yayo? Saturni alikuwa mungu-jua wa Waroma aliyeheshimiwa katika sikukuu ya Saturnalia. Je! yeye alistahili? Simon Schama, profesa wa historia katika Chuo Kikuu cha Harvard, amwita “mwenye karamu za kula, kunywa na utukutu wa aina nyingineyo.” Gazeti Lear’s laita sikukuu hiyo “karamu ya mvinyo iliyo mashuhuri zaidi katika ulimwengu wa kale.”

Ibada ya kidhehebu ya mungu-jua Mithra ilienea katika Asia. Kulingana na mwanaanthropolojia Gabriel Seabrook, yeye alikuwa “mungu wa vita, aliyetupa mishale yenye kuangamiza uhai na maradhi yasiyotibika kwa maadui wake kwenye uwanja wa vita.”

Ibada ya jua miongoni mwa Waazteki ilikuwa yenye umwagaji damu hasa. Gazeti Natural History laeleza kwamba “isipokuwa wahanga watolewe dhabihu kwa miungu ya jua, uhai wote—kutia ule wa miungu—ungekufa.”

Baada ya kupitia asili ya sherehe hii (ona sanduku chini), labda hutashangaa kwamba wachawi na waabudu-Shetani bado huipa staha Desemba 25. Gazeti San Francisco Chronicle la Desemba 21, 1991, lanukuu mchawi aliye mwandikaji mashuhuri wa kipagani kuwa akisema: “Ni mojawapo sikukuu zenye kutaka jitihada sana. Hatupati lepe la usingizi usiku wote.” Mshiriki wa kikundi kiitwacho Ibada ya Mungu-Mke alisema: “Sisi hufanya sherehe fulani. . . . Washiriki wa makasisi wetu hufanya mwigizo wa kifumbo juu ya kuzaliwa kwa mtoto jua.”

Je! Mungu au Mwanae atakubali staha hiyo, ambayo ni ibada ya miungu bandia?

Je! Ni Ista—au Astarte?

Sherehe za sikukuu za familia hii zaanza mapema asubuhi waamkapo kusalimu machweo ya jua kwa hofu yenye kicho. Watoto wamevaa nguo mpya zilizo bora zaidi, kutia na kofia mpya. Sherehe hiyo yatia ndani mifano ya sungura, vikapu vilivyojaa mayai yaliyotiwa rangi maridadi, na vitumbua moto vyenye alama ya msalaba. Lazima iwe ni Ista. Au sivyo?

Wakati wa masika ulikuwa mtakatifu kwa waabudu-ngono wa Foinike. Kijimungu-kike chao cha uzazi, Astarte, au Ishtari (Afrodito kwa Wagiriki), alikuwa na mayai na sungura kuwa mifano yake. Alikuwa na kiu sana cha damu na cha ngono isiyo ya adili. Sanamu zake zilimwonyesha kwa njia mbalimbali akiwa na viungo vya uzazi vilivyopigwa chuku mno akiwa na yai mkononi na sungura kando yake. Umalaya mtakatifu ulikuwa sehemu ya ibada yake. Katika Kanaani, kijimungu-kike cha ngono kilionyeshwa kuwa mke wa Baali. Yeye alistahiwa kwa karamu za ngono zenye ulevi, waabudu wakiamini kwamba kufanya ngono kulisaidia kuleta mwamko kamili na kujamiiana kwa Baali na mkewe. Kulingana na kitabu Recent Discoveries in Bible Lands, “hakuna nchi nyingineyo ambayo ina idadi kubwa hivyo ya sanamu za kijimungu-kike cha uzazi kilicho uchi, baadhi yazo zikiwa za aibu sana.”

Chini ya kumbukumbu zake katika Carthage, vyombo vyenye rangi yenye kung’aa vilipatikana vikiwa na mifupa ya watoto wadogo iliyoungua. Wazazi wao, kwa kawaida wakiwa watu wa maisha ya hali ya juu, walitafuta kupata baraka ya miungu juu ya utajiri na uvutano wao. Baadhi ya vyombo hivyo vilipatikana vikiwa na mabaki ya watoto kadhaa wa umri mbalimbali, labda wa kutoka familia moja.

Kutazama sanduku lililo juu kutaonyesha jinsi mifano ya kisasa ya sherehe hizo za kale ilivyo mifanyizo hafifu. Hata jina Ista si tofauti sana na jina la kale la kipagani. Je! hiyo basi ndiyo njia ya kustahi Mwana wa Mungu aliye mtakatifu?

Halowini—Usiku wa Kale Wenye Hofu Kuu

Ni usiku wa mwisho wa Oktoba. Kwa nuru ya mwezi, kikundi kidogo cha watu wenye vinyago chaenda nyumba kwa nyumba kikitoa matakwa yacho kwa vitisho vikubwa. Taa zenye vichwa vyenye sura zilizokunjwa zilizotengenezwa kwa maboga zalinda milango fulani zikiangaza kwa mishumaa inayowaka—iliyofanyizwa kwa mafuta ya binadamu. Milango mingineyo yatiririka damu ya binadamu. Huo ni usiku wa Samhaini, bwana wa wafu wa Waselti.

Labda hakuna sherehe nyingine iliyobadilishwa kuwa ya “Kikristo” ambayo Shetani hujistahi mwenyewe sana na kukumbuka wafuasi wake waliokufa vitani. Mwandishi J. Garnier adokeza kwamba sherehe za kuteseka na kifo zarudi nyuma hadi kwenye uharibifu wa kale wa wafuasi wake wote wa kibinadamu, kutia na wana-mivyauso wa malaika walioasi, wakati wa lile Furiko. Tamaduni mbalimbali ulimwenguni pote zina sherehe za wafu, “zinazosherehekewa na wote katika au karibu na siku ileile ambayo, kulingana na masimulizi ya Kimusa, ile Gharika ilitukia, yaani, siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili—ule mwezi ambao karibu unalingana na Novemba wetu.”—The Worship of the Dead, cha J. Garnier.

Madruidi (aina ya wachawi) walihusika pia. Mnamo Oktoba 31, Samhaini ilisemwa kuwa iliachilia roho za wafu zijumuike na walio hai. Madruidi walizurura barabarani wakiwa na taa, na walipofika kwenye nyumba, walidai pesa kuwa toleo kwa ajili ya Shetani.

Halowini ni siku kuu ya sherehe za kishetani. “Hiyo ni sikukuu ya kidini katika ulimwengu wa wafu, waabudu-shetani wakitoa dhabihu na wachawi wakisherehekea kwa ukimya kwa kutoa sala nyingi au milo kwa ajili ya wafu,” kulingana na makala ya USA Today. Hiyo ilinukuu mchawi wa Washington Bryan Jordan kuwa akisema, “[Wakristo] hawang’amui, lakini wanasherehekea sikukuu yetu pamoja nasi. . . . Tunafurahi.”

Wazazi, je, mwataka watoto wenu waige sherehe hizo zenye uovu?

[Sanduku katika ukurasa wa 12]

Mifano ya Krismasi

Mti wa Krismasi “hauhusiani hata kidogo na sherehe za Krismasi na wahusiana sana na kule kuendelea kupitia maelfu ya miaka ya sherehe za kipagani za nuru ya kipupwe na kuzaliwa upya.” (The Boston Herald) “Miti yenye vipambo vidogo vining’iniavyo juu yayo ilikuwa sehemu ya sherehe hizo za kipagani kwa karne nyingi.”—Church Christmas Tab.

Kijiti holi kilipendwa sana na Waselti “ili kufanya zimwi wa nyumba wawe na utaratibu wakati wa kipindi cha katikati ya kipupwe. . . . Kingeweza kukinza uovu, kusaidia katika kubashiri ndoto, kilinde nyumba isipigwe na umeme.”—Beautiful British Columbia.

Mmea misotoo “ulikuja kutoka kwa Madruidi katika Uingereza walioutumia katika ibada isiyo ya kawaida inayohusiana na nguvu za kishetani na za kishirikina.”—Church Christmas Tab.

Mnamo Desemba 25 “Wamithra walisherehekea kuzaliwa kwa Mithra . . . Hakuna uthibitisho wowote wa kibiblia kuwa Desemba 25 ilikuwa siku ya Kuzaliwa kwa Yesu.”—Isaac Asimov.

Kupeana Zawadi kulikuwa jambo la kawaida la Saturnalia. “Kwenye sherehe hii ulitazamiwa kutoa zawadi kwa marafiki wako wote.”—Ancient Italy and Modern Religion.

Ile nyota “iliyo juu ya mti iliabudiwa katika Mashariki kuwa mfano wa usafi, uzuri, na amani miaka 5,000 kabla ya kuzaliwa kwa Kristo.”—United Church Herald.

Mshumaa “hautokani . . . na mahali patakatifu pa Kikristo. Tuliutoa kutoka altari ya mapema zaidi, mti wa oki uliotumiwa na Madruidi.”—United Church Herald.

Baba Krismasi aliibwa “kutoka ngano za kale za Ujerumani: ‘Thor alikuwa mwanamume mwenye umri mkubwa, mwenye furaha na urafiki, mnene na mwenye ndevu ndefu nyeupe. Yeye aliendesha kigari cha kukokotwa na farasi na ilisemwa kuwa aliishi katika Northland . . . Aliutumia moto, rangi yake ilikuwa nyekundu. Mahali pa moto katika kila nyumba palikuwa patakatifu kwake, na ilisemekana kuwa alishuka chini hadi ndani yapo kupitia dohani.”—United Church Herald.

[Sanduku katika ukurasa wa 13]

Sherehe za Masika

Ista ilikuwa “pale mwanzoni sherehe ya masika katika kustahi kijimungu-kike cha Ujerumani cha nuru na masika kiitwacho katika Kiingereza cha kale kuwa Istre.” (The Westminster Dictionary of the Bible) “Hakuna jambo lolote katika Agano Jipya linaloonyesha kwamba sherehe hiyo ya Ista ilifanywa.”—Encyclopædia Britannica.

Sungura “alikuwa mwandamani wa kijimungu-kike cha Ujerumani kiitwacho Ostara.”—Funk & Wagnalls Standard Dictionary of Folklore, Mythology and Legend.

Mayai “yalisemekana kuwa yalitiwa rangi na kuliwa kwenye sherehe za masika katika Misri, Uajemi, Ugiriki, na Roma ya kale.”—Celebrations.

Kofia ya Ista mwanzoni “ilikuwa shada la maua au majani. Ule mviringo au taji ilionyesha jua lililo mviringo na mwendo walo mbinguni ulioleta kurudi kwa masika.” Mavazi mapya ya Ista yalisitawi kwa sababu “ilionwa kuwa kukosa adabu na hivyo bahati mbaya kusalimu kijimungu-kike cha Masika cha Skandinavia, au Istre, katika chochote isipokuwa nguo mpya, kwa kuwa hicho kijimungu-kike kilikuwa kikitoa nguo mpya duniani.”—The Giant Book of Superstitions.

Vitumbua Moto vyenye alama ya msalaba: “Kama Wagiriki, Waroma walikula mkate uliotiwa alama ya msalaba . . . kwenye dhabihu za umma.” Zililiwa na Wajerumani wapagani kama staha kwa Ista.—Encyclopædia Britannica.

Maombi ya kucha kwa jua yafananisha sherehe “zilizofanywa katika masika katikati kukaribisha jua na uwezo walo mkuu wa kuleta uhai mpya kwa vitu vyote vikuavyo.”—Celebrations.

[Sanduku katika ukurasa wa 14]

Mashina Yenye Kutisha ya Halowini

Vifuniko vya usoni na mwilini: “Waselti waliandaa chakula, vinywaji na mambo mengine kwa roho halafu wakawadanganya ili waondoke kwa kuvaa vifuniko vya usoni na mwilini na kupiga miguu kwenye mipaka ya kijiji.”

Mioto Mikubwa ilikuwa “‘mioto mikubwa’ kihalisi” ambapo “makuhani walijaribu kutuliza mungu-jua kwa kutoa dhabihu za wanyama, na mara nyingi, watu pia.” (The Tampa Tribune) “Kwa kutazama jinsi wahanga walivyokufa, Madruidi walitafuta ubashiri wa wakati ujao.”—Beaumont Enterprise.

Udanganyo au mapendezi: “Kilio cha Madruidi kililingana na ‘Udanganyo au Mapendezi’ ya kisasa.”—Central Coast Parent.

Hadithi zenye kutisha: “Zile sherehe za Madruidi za umwagaji damu zaendelezwa kwa kuwakazia vijana juu ya mazimwi na roho. . . . Karamu za Halowini na kusimulia hadithi zenye kutisha pia zina vyanzo katika nyakati za Madruidi wakati roho waliaminiwa kuwa walivinjari barani.”—The Tampa Tribune.

Vijapokuwa vyanzo vya kipagani vya sikukuu hizo, watu fulani hawatapendezwa na wazo la kuwanyima watoto wao furaha ya sherehe za kisiku-hizi. Kwa vyovyote, watoto wenye elimu wanajua nini juu ya Saturni, Astarte, na Samhaini wa kale? Watoto fulani wajua kidogo. Pia wajua kwamba hawataki kuwa na sehemu yoyote yazo.

[Picha katika ukurasa wa 12]

Mithra

Thor

[Hisani]

Mithra: Musée du Louvre, Paris

Thor: The Age of Fable cha T. Bulfinch, 1898

[Picha katika ukurasa wa 13]

Astarte

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 14]

Fuvu: Picha ya U.S. Forest Service

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki