Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 1/22 kur. 21-24
  • Kuishinda Miito Migumu ya Maisha Katika Asia ya Kusini

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuishinda Miito Migumu ya Maisha Katika Asia ya Kusini
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Walikataa Kufanya Upasuaji Bila Damu
  • Maamuzi Magumu ya Kufanya
  • Mwenzi Mpya, Mtihani Mpya wa Uaminifu-Maadili
  • Eneo Lenye Mwito Mgumu
  • Mwisho wa Uovu U Karibu
  • Elimu Ambayo Imeendelea Katika Maisha Yangu Yote
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2004
  • Ukweli wa Ufalme Wachanua Katika Sri Lanka
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Kuweka Wakfu Ofisi ya Tawi ya Sri Lanka
    2015 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Kushangilia Mavuno Katika India
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 1/22 kur. 21-24

Kuishinda Miito Migumu ya Maisha Katika Asia ya Kusini

POLEPOLE nilipopata fahamu, nilitambua kwamba mguu wangu wa kushoto ulikuwa umekufa ganzi isivyo kawaida. Niligeuza kichwa changu. Mpenzi wangu Henry alikuwa akifa. Lakini, huo haukuwa wakati wa kutamauka. Ilikuwa ni lazima nipigane—pigano la kudumisha uaminifu-maadili wangu kwa Mungu ambaye alikuwa ametupa mambo mengi sana.

Ilikuwa Mei 17, 1982. Mume wangu alikuwa mwangalizi asafiriye wa makutaniko yasemayo lugha ya Kitamil ya Mashahidi wa Yehova katika Sri Lanka. Tulikuwa tukitumikia kutaniko moja mbali na Kolombo, jiji kubwa zaidi. Tukiwa tumepanda baiskeli pamoja, kama vile wengi hufanya katika nchi hiyo, tulifunga safari fupi ya kuzuru Shahidi mmoja mwenzetu. Na kwa ghafula, bila kutazamiwa, lori lilitugonga kama nyoka aina ya fira.

Madaktari walipokata tamaa ya kumwokoa Henry, walielekeza uangalifu wao wote kwangu. Nijapodhoofika sana, ule uhitaji wa dharura wa kuwashauri juu ya azimio langu la kustahi sheria ya Yehova ya kuepuka damu ulijaza moyo wangu. (Matendo 15:28, 29) Ni lazima niwajulishe madaktari hao. Nilijikakamua kwa nguvu zote nilizokuwa nazo na kusema: “Tafadhali, nipeni karatasi ndogo.” Nikaandika itikadi zangu na kutia sahihi karatasi hiyo kwa shida sana. Basi pigano likaanza.

Nilipewa huduma ya kwanza. Ilikuwa wazi kabisa kwamba nilikuwa nimejeruhiwa vibaya sana. Azimio langu la kutenda nikiwa Mkristo wa kweli lilikuwa hangaiko langu kubwa wakati huo—huo haukuwa wakati wa kuhuzunika.

Walikataa Kufanya Upasuaji Bila Damu

Kwa siku tisa vita kuhusu utiaji-damu mishipani iliendelea—pigano langu la kuishi kwa kupatana na dhamiri yangu kwa kukataa damu, na pigano la madaktari la kunishawishi nikubali damu. Ingawa walikuwa na ustadi wa kuweza kupasua bila damu, wao walikataa tu kufanya hivyo. Lilikuwa ni jeraha kubwa walilohitaji kuangalia haraka sana.

Lakini haikuwa lazima nipigane vita hiyo nikiwa peke yangu. Yehova alikuwa pamoja nami kila dakika. Na udugu wa watu wa Yehova ulijaa hangaiko lenye upendo. Kolombo lilikuwa umbali wa kilometa 400. Dakt. Perrin Jayasekera, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alipanga ili ndugu yake wa kimwili ambaye alikuwa mpasuaji huko anilaze katika Hospitali Kuu ya Kolombo.

Ikichukua muda wa karibu saa 24, safari hiyo katika sehemu ya nyuma ya gari kwenye barabara zilizo mbaya ilionekana kuwa safari ndefu zaidi maishani mwangu. Lakini, moyo wangu ulijawa na shukrani kwa Yehova kwa ajili ya utunzi wake wenye upendo, kama alivyokuwa amefanya tangu nilipojifunza kweli katika nchi niliyotoka, India. Hata hivyo, sasa sikuwa na mtu wa ukoo kando yangu. Lakini kwanza ni nini kilinileta Sri Lanka?

Nilizaliwa na wazazi waliokuwa Wakatoliki wa Roma katika jimbo la Kerala, India. Tulisema lugha ya Kimalayalam. Kiingereza kilifundishwa shuleni. Ninafurahi kama nini kwamba nilitumia fursa hiyo kukifahamu vizuri! Sehemu hiyo ya India ina idadi kubwa ya watu wanaodai kuwa Wakristo. Husemwa kimapokeo kwamba mtume Tomaso alileta Ukristo Kerala katika karne ya kwanza. Iwe hali ilikuwaje, zaidi ya miaka 1,400 baadaye, wakati Wakatoliki wa Roma kutoka Ureno waliokuja kutwaa maeneo wakiongozwa na Vasco da Gama walipofika Kerala, walishangaa kupata wengi huko ambao tayari walimwamini Kristo.

Maamuzi Magumu ya Kufanya

Familia yetu ilipoanza kujifunza kweli zenye kunurisha kutoka katika Biblia kwa msaada wa Mashahidi wa Yehova, tamaa yangu ya asili ilikuwa ni kueleza kweli hizo kwa wale waliodai kuwa Wakristo katika jumuiya yetu. Kwa hiyo punde tu baada ya kujiweka wakfu na kubatizwa, nikawa painia, mhudumu wa wakati wote. Kufanya hivyo kulimaanisha kukataa ombi la kazi nzuri ajabu la kuwa mwalimu katika Jimbo letu la nyumbani. Kuwa na usalama mzuri kama huo unaotolewa na kazi kama hiyo yenye malipo ya uzee huwa mradi wa vijana wengi wa India, lakini kusudi langu la maisha lilikuwa limebadilika. Nilitaka usalama halisi, na huo waweza kupatikana tu chini ya mkono wenye ulinzi wa Yehova.

Miaka miwili baadaye, kukawa na mwito mwingine mpya. Je! ningependa kuhamia sehemu nyingine ya India kusaidia katika mahali ambapo kulikuwa na uhitaji mkubwa zaidi wa wahubiri? Hilo lilitokeza mwito wa kujifunza lugha mpya, Kitamil, na kusaidia watu kutoka malezi ya kidini yaliyo tofauti sana, wakati huu Wahindu. Naam, fursa ya kuonyesha uthamini wangu kwa Yehova ilifanya mabadiliko hayo yafae. Kutoa ushahidi kwa watu hao wenye uchangamfu na wenye urafiki kutoka malezi ya Kihindu kulileta shangwe kwelikweli. Walikuwa wakikubali haraka kwamba twakaribia mwisho wa Kali Yuga (Enzi Mbovu) na kwamba kuna jambo bora zaidi mbele ya watu wanaotenda kwa uadilifu sasa. Hata hivyo, kuwasaidia waone tofauti kati ya Ukristo wa kweli na yale waliyokuwa wameyaona kutoka Magharibi kulikuwa jambo gumu sana. Nilifungua Biblia yangu mara nyingi kama nini kwenye Mathayo 7:21-23: “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.” Mohandas Gandhi alisema jambo hilo vema: ‘Mimi nampenda Kristo, lakini nachukia Wakristo kwa sababu wao hawaishi kama Kristo alivyoishi.’

Wahindu wengi wanaona, kama nilivyokuwa nimeona, kwamba taarifa hiyo ilikuwa kweli. Na sasa wao waona pia kwamba Wahindu wengi wenzao wanatenda karibu sawa na watu wa Magharibi wanaodai kinafiki kuwa Wakristo. Lakini Mashahidi wa Yehova ni watu tofauti sana. Maelfu ya Wahindu wanaanza kutambua jambo hilo.

Mwenzi Mpya, Mtihani Mpya wa Uaminifu-Maadili

Miaka miwili na nusu ilipita. Kusanyiko la Mashahidi wa Yehova la “Habari Njema za Milele” lilikuwa likifanywa ulimwenguni pote katika 1963. Moja ya sehemu za kulifanya ilikuwa ni New Delhi, kaskazini mwa nchi. Huo ulikuwa mkusanyiko wenye kukumbukwa kama nini! Na huko nilikutana na Henry Abraham. Sote wawili tulikuwa tukitafuta mtu wa kushiriki maisha yetu yenye ujitoaji kwa Yehova. Miezi mitano baadaye tulioana.

Alikuwa amezoezwa katika Watchtower Bible School of Gilead katika Jimbo la New York na kisha akarudishwa nchi ya kwao Sri Lanka, ambako kulikuwa na uhitaji mkubwa sana. Nilitumaini kwamba angekubali kuhamia India ambako nilihisi kulikuwa na uhitaji mkubwa zaidi. Lakini sivyo. Alihitajiwa mahali alipokuwa. Kwa hiyo makao yangu yakawa kisiwa hiki kizuri cha Sri Lanka. Kwa furaha, Kitamil na Kiingereza ni zenye mafaa sana hapa. Kwa hiyo sikuhitaji kujifunza lugha nyingine—wakati huo. Tulifurahia pamoja miaka 18 ya utumishi kwa Yehova kabla msiba wa lile lori lenye kwenda kwa kasi kutupata.

Lakini sasa nilikuwa Kolombo, na pigano langu la kutoridhiana uaminifu-maadili wangu kwa kutiwa damu mishipani liliendelea. Sasa uhai wangu ulikuwa hatarini, si kwa sababu ya msimamo wangu juu ya suala la damu, bali kwa sababu ya tiba kukawizwa.

Mpasuaji wa kurekebisha mwili mwenye malezi ya Kibuddha na mpasuaji wa mifupa mwenye malezi ya Kihindu waliunganisha stadi zao katika kunitibu. Hesabu ya damu yangu (hemoglobini) sasa ilikuwa imepungua hadi karibu nne.

Wangekataje mguu kwenye paja nikiwa na damu kidogo hivyo? Azimio langu lilikuwa wazi, lakini je, wapasuaji hao wawili wangekubali kunipa msaada niliokuwa nimenyimwa hapo awali? Moyo wao mkuu wa kunisaidia kukabili ugumu huu mkuu bila kujaribu kunishurutisha kuridhiana dhamiri yangu ulikuwa wenye kutokeza sana. Nilipoteza mguu wangu, lakini uhai wangu uliokolewa, na sikuvunja uaminifu-maadili wangu kwa Yehova.

Bila mume niliyempenda sana, hali mpya kabisa katika maisha yangu ilikuwa inaanza. Kwanza kwa mikongojo, kisha kwa mguu bandia (baadaye, kwa fadhili ya ndugu na dada wengi, mguu huo ukabadilishwa na mguu bandia bora zaidi), niliweza kuendelea na huduma yangu. Polepole huzuni yangu ikapungua ikichukuliwa na utendaji.

Je! nirudi India na kuishi na watu wa ukoo wasioamini? Nilikumbuka sana kielelezo kizuri sana katika Biblia cha mjane aliyeitwa Ruthu. Nilitaka kuwa mahali ambapo ningeweza kumtumikia Yehova kwa njia bora zaidi nijapokuwa na uwezo uliopunguka. Sri Lanka ingali ni nyumbani.—Ruthu 1:16, 17.

Eneo Lenye Mwito Mgumu

Miaka hiyo 11 imepita haraka. Kumekuwa na “mengi ya kufanya katika kazi ya Bwana.” (1 Wakorintho 15:58, NW) Nilikuwa na shughuli katika huduma ya shambani katika Kolombo. Hapa pana watu wa kutoka malezi mbalimbali ya kidini—Wahindu, Waislamu, Wabuddha, Wakristo kwa jina tu, na wengine wengi. Miito migumu yaendelea.

Kila mwezi wachache miongoni mwetu hutumia mwisho-juma mmoja kuzuru mji mmoja kati ya miji iliyoko upande wa kusini ambayo bado haina vikundi vya Mashahidi wa Yehova. Watu wengi sana hujiita Wabuddha, na wanasema lugha ya Kisinhala. Kujifunza kusaidia watu hao kumekuwa jambo la maana sana kwangu.

Kama ilivyo na Wahindu katika India na kotekote Sri Lanka, Wabuddha wamekataa Biblia kwa sababu ya mwenendo wa wale wanaojiita Wakristo wa Magharibi. Lakini, kanuni zao za msingi za Kibuddha, ile Njia ya Kujumlisha Nane iliyo mashuhuri sana ya mawazo mazuri na mwenendo mzuri (itikadi, usemi, tendo, kuishi, jitihada, mawazo, na kutafakari kuzuri), ni hekima tu ya binadamu asiyekamilika zikilinganishwa na kanuni za kimungu zinazopatikana katika Biblia, ambazo nyingi zazo ziliandikwa karne nyingi kabla ya Siddhārtha Gautama.

Siddhārtha Gautama aliposema na Kalamas kama ilivyonukuliwa katika Kalama Sutta, yeye alisema hivi: “Usiamini kile ambacho kimeaminiwa kwa sababu imesemwa kwa kurudiwa-rudiwa; wala mapokeo.” Ni ajabu kama nini kwamba niwe na pendeleo la kuwakumbusha Wabuddha wengi wanyoofu kwamba mwongozo wowote ukitumiwa leo, hakuna mtu awezaye kuamini ile ngano ya mageuzi wala kukataa kuwapo kwa Muumba fulani.

Mwisho wa Uovu U Karibu

Mashahidi wa Yehova wana mambo mengi mazuri kutoka kwa Biblia ya kuambia watu hawa—juu ya kalpa vinasha, mwisho wa uovu, ambao umekaribia. Unabii wa Biblia uliotolewa miaka 1,900 iliyopita kuhusu mwisho huo wapatikana katika 2 Timotheo 3:1-5, 13. Tuna pendeleo pia la kuwaonyesha kwamba mahali pa kuokolewa katika nyakati hizi si dini za Magharibi wala za Mashariki bali, kama vile mistari 16 na 17 ya sura iyo hiyo ionyeshavyo, ni Neno la Yehova lililovuviwa, Biblia.

Ubuddha ni utafutaji wa mnurisho. Katika Biblia, muda mrefu kabla Siddhārtha Gautama kuanza utafutaji wake, chanzo cha kweli cha mateseko kilielezwa waziwazi. (Mwanzo 3:1-19) Uasi dhidi ya sheria yenye uadilifu katika mwanzo wa historia ya kibinadamu ulileta matokeo mabaya—ugonjwa na kifo, zilizoenea kwa wanadamu wote wenye dhambi. Wengi walikuwa na maswali yenye kutatanisha—kama vile katika Habakuki 1:3, NW: “Mbona wanifanya nione mambo yanayoumiza, na waendelea kutazama tu tatizo? Na kwa nini kuna mabaya na jeuri mbele yangu, na kwa nini ugomvi watokea, na kwa nini kuna bishano?” Ni Muumba mwenye huruma pekee awezaye kuandaa majibu ya maswali hayo na kutengeneza njia ya kurudisha kabisa yote yaliyopotezwa. Hata sasa, mamilioni ulimwenguni pote wananufaika kutokana na hekima yenye kutumika kutoka kwa Neno la Mungu. Na sasa Kisinhala, lugha kuu katika nchi hii, imekuwa mwito mwingine mgumu kwangu, kwa sababu katika lugha hiyo, naweza kusaidia wale wanaotafuta kwa unyoofu mnurisho niliopata miaka 37 iliyopita.

Mwito mwingine tena. Kwa kujengwa kwa ofisi mpya ya tawi na kitovu cha kutafsiri katika Sri Lanka, watu wengi zaidi wahitaji kuzoezwa. Polepole ninajifunza lugha mpya ya kompyuta ninaposaidia kazi katika Idara ya Hesabu katika ofisi yetu ya tawi.

Miaka yangu 33 ya kumtumikia Yehova imekuwa pindi ambayo ninatumaini itaendelea milele nikimtumikia. Wengi wamejiunga nasi katika utumishi wa Yehova katika miaka ambayo imepita, kutia ndani yule mpasuaji mwenye ustadi aliyepanga mpango wote wa kulazwa katika hospitali ya Kolombo na upasuaji uliohitajiwa. Sasa yeye vilevile ni Shahidi mwenzetu aliyejiweka wakfu kwa Yehova.

Yehova pamoja na familia ya watumishi wake hapa duniani wameniendeleza vizuri sana. Nimehisi mkono wake wenye utunzi ukinifunika, na najua kwamba upendo wake wenye uaminifu-mshikamanifu umeweka Henry kikiki katika kumbukumbu lake. Ni Yehova pekee awezaye kumleta mpenzi wangu kutoka mavumbini, na kuniruhusu nimsalimie mara nyingine tena, na kumwambia Henry miito yote migumu yenye kusisimua ambayo kizazi chetu kimetokeza na jinsi Yehova ametusaidia kuikabili.—Kama ilivyosimuliwa na Annama Abraham.

[Picha katika ukurasa wa 21]

Annama Abraham na mume wake, Henry

[Picha katika ukurasa wa 23]

Annama atoa ushahidi kwa wachunaji wa majani-chai wanaofanya kazi katika shamba la majani-chai nchini Sri Lanka

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki