Maisha Jijini Hufurahisha Kadiri Gani?
AINABINADAMU yenye kusumbuka katika majiji ya leo hutafuta furaha kwa njia kadhaa. Majiji kama vile Bombay, Bangkok, Monte Carlo, San Francisco, na Dallas hujaribu kuitoa. Hayo huiandaa kwa njia nyingi. Lakini je, majiji ya ulimwengu ni chanzo cha shangwe ya kudumu?
Ndoto kwa Kulinganisha na Uhalisi
Mapema katika karne hii, Hollywood lilikuja kuwa jiji maarufu la sinema ulimwenguni. Kwa hiyo huenda ikashangaza kujua kwamba India hutokeza labda sinema zipatazo 800 kwa mwaka.[2] “Watu wa India ni wazoefu wa sinema,” laandika gazeti la Ujerumani Geo, likiita uzoefu wao “karibu kuwa kama dini.” Hilo laongeza: “Hakuna mahali penginepo ambapo majumba ya sinema hutumika waziwazi kuwa ulimwengu wa badala kwa ajili ya mamilioni waliokutanika wanaopata mafanikio na utajiri, furaha na haki katika sinema tu.”[3]
Ingawa karibu nusu ya sinema za India hutokezwa katika Madras kwenye pwani ya mashariki, biashara yayo ya sinema ilipata mwanzo wayo kwenye pwani ya magharibi. Katika 1896, ndugu Wafaransa Auguste na Louis Lumière, wavumbuzi wa projekta ya kibiashara ya sinema, walionyesha sinema yao ya kwanza kwenye Hoteli ya Watson ya Bombay.[4]
Bombay lilikuwa kijiji kidogo katika 1534 wakati wafanya biashara Wareno walipokimiliki. Mfalme wa Uingereza Charles 2 alioa binti-mfalme Mreno katika 1661, na akapewa kijiji hicho kuwa zawadi ya ndoa. Katika 1668 kilikuja kuwa chini ya uthibiti wa East India Company, na upesi Bombay likawa bandari kuu la magharibi la India.[5]
Ensaiklopidia moja husema kwamba “uvutio wa asili wa Bombay haupitwi na ule wa jiji jinginelo katika eneo hilo.”[6] Kwa kufikiria uzuri walo na kupatana na ule ulimwengu wa kindoto wa sinema za India ambazo limesaidia kufanyiza—mchanganyiko wa muziki, dansi, na mapenzi—Bombay lapaswa kuwa jiji la shangwe.[7]
Lakini Bombay lina mojapo idadi ya watu iliyo kubwa zaidi ulimwenguni.[8] Hali za misongamano huharibu mazingira maridadi ya jiji hilo na haziletei furaha yale maelfu mengi ya watu wanaoishi katika mitaa ya hali ya chini “bila maji ya mfereji au vyoo” na ambao hulazimika kutumia “mito ya karibu na sehemu zilizo wazi kuwa vyoo.”—5000 Days to Save the Planet.[9]
Bombay pia lina dini kadhaa.[10] Lakini badala ya kuleta shangwe, kumekuwako ghasia mbaya za kidini katika India. Katika miaka miwili tu iliyopita, hizo zimesababisha mamia ya vifo katika Bombay pekee.[11]
Yote Yang’aayo Si Dhahabu
San Francisco pia ni jiji la uzuri wa asili. Hilo lajulikana kwa vilima vyalo, kwa mojapo bandari nzuri sana ya asili uliwenguni, na kwa madaraja yalo, kutia na lile la Golden Gate linaloenea kuanzia kiingilio hadi kwenye bandari. Wageni wengi hustaajabishwa nalo.[12]
Katika 1835 Yerba Buena lilianzishwa, na katika 1847 liliitwa jina jipya San Francisco. Mwaka mmoja baadaye, dhahabu ilipatikana karibu na hapo, na harakati za kutafuta dhahabu ya California zikaanza. Kile kilichokuwa kijiji cha mamia tu ya wakazi, upesi kikawa mji mkubwa wa mpakani. Lakini lilikuwa na matatizo yalo lenyewe, kama vile lile tetemeko la dunia lenye uharibifu mkubwa na moto wa 1906.[13]
Mtindo walo wa kimataifa huchangia umaarufu wa San Francisco. Gazeti The European lasema kwamba ndani yalo, lina “maisha mbalimbali yaliyo tofauti sana katika hali na sura pia.” Vikundi kadhaa vya kitaifa huwakilisha Ulaya na Asia, kama ile moja ya jumuiya kubwa zaidi ya Wachina nje ya Asia. Wakazi wenye kusema Kihispania huonyesha mwanzo wa jiji hilo kuwa Meksiko.[14]
Hivi karibuni, mamia kadhaa ya watalii wastadi walipiga kura kwa San Francisco kuwa “jiji bora sana,” wakisifu “mchanganyiko walo wa kipekee wa urafiki, uzuri na uvumilivu.”[15] Mwandikaji habari za magazeti alifafanua hivi: “Ikiwa kuna jambo moja linalopambanua California Kaskazini pamoja na lile jiji niishimo, ni ule uvumilivu wa tabia za kibinadamu za aina zote unaoshangaza na kugadhabisha watu katika sehemu nyinginezo za nchi.”[16]
Mara nyingi tabia zalo za kiajabu-ajabu zimefanyiza habari kuu magazetini. Katika miaka ya 1960 wengi walitazama kwa wasiwasi huku vijana wenye nywele ndefu zisizo nadhifu wakitoa heshima kwa “upendo” na “amani” kabla ya kuingia katika ile desturi ya kuchukiza ya madawa ya kulevya na ngono za ovyo-ovyo. Na jiji hilo lina mojawapo jumuiya kubwa zaidi za wagoni-jinsia-moja nchini.[17]
UKIMWI umekumba San Francisco vibaya sana. Gazeti la Ujerumani huita ugonjwa huo “tatizo kubwa zaidi” la jiji hilo tangu tetemeko la dunia na moto wa 1906, likiongeza kwamba “hali [yalo] ya furaha yaonekana kuwa imepotea milele.”[18] Jiji hilo lililo kando ya Golden Gate limelazimika kukabili ukweli mchungu: Ingawa mitindo-maisha ya “kidhahabu,” ilionekana kuwa yenye kutumainisha, hiyo imepoteza mng’ao wayo kwa sababu ya matatizo makubwa.
Wengi Zaidi Hupoteza Kuliko Wale Wanaoshinda
Monte Carlo, kwa muda mrefu pakiwa mahali pa kuchezea pa matajiri na jamii ya hali ya juu, ni makao ya mojawapo majumba ya kamari yaliyo maarufu zaidi ulimwenguni. Tangu lianzishwe katika 1861, jumba lalo la kamari limekuwa kituo maarufu cha watalii.[19] Majumba kadhaa ya kamari hushughulikia wale wanaohisi kwamba kushinda katika kamari ndiyo njia ya kupata furaha ya kudumu. Lakini watu wengi zaidi hupoteza katika kamari kuliko wale wanaoshinda.
Monte Carlo liko kwenye French Riviera katika nchi ya Monaco na ina eneo la kilometa mbili unusu za mraba. Monaco ilikaliwa na Waroma katika nyakati za kale. Katika 1297 ile familia tajiri ya Wagrimaldi kutoka Italia ilitwaa udhibiti wayo. Baada yayo kupoteza uhuru, kwanza kwa Uhispania na kisha kwa Ufaransa, nchi hiyo ilirudishwa chini ya Wagrimaldi katika 1814.[21]
Katika 1992, Rainier 3, mzao wa Wagrimaldi, alieleza hangaiko lake juu ya usalama wa raia zake. Baada ya kusema kwamba “asilimia arobaini ya meli za mafuta za ulimwengu hupitia Mediterenia,” yeye aliongeza: “[Bahari] hiyo ina uchafuzi wa mafuta ulio mara 150 zaidi ya Bahari ya Kaskazini. Asilimia 80 ya mifereji ya maji machafu inayopakana na bahari hii humwaga maji hayo baharini bila kuyasafisha.”[22]
Kujapokuwa matatizo, “hakuna mahali pengine pa upendezi,” lasema The European, “panapoweza kutokeza mara hiyo wazo la kusisimua na mchachao mwingi kwa kutajwa tu kwa jina.” Linalochangia wazo hilo ni majumba yalo ya kamari, majumba yalo ya hifadhi, kilabu chalo cha mashua za starehe, mashindano yalo ya magari—watu fulani husema hayo huwa mashindano makubwa zaidi na yaliyo maarufu zaidi—kutia na jumba lalo la muziki. Hata hivyo, si tamaduni tu zinazovutia matajiri Monte Carlo; faida zalo za kodi ni kubwa.[23]
Lakini, fedha na utamaduni haziwezi kuhakikisha furaha ya kudumu. Charles Wells ambaye ni Mwingereza, kwa kweli alishinda fedha zote za kamari katika 1891, lakini ajapopata ‘bahati njema,’ yeye mwishowe aliishilia gerezani.[24] Na katika jiji lijulikanalo kwa msisimuko wa mbio za magari na za mashua, yasikitisha kwamba, mke wa Mwana–Mfalme Rainier, Binti-Mfalme Grace, alikufa mnamo 1982 katika aksidenti ya gari na kwamba mume wa binti yao aliuawa katika aksidenti ya mashindano ya mashua katika 1990.[25]
Utamaduni Uliofanyizwa Katika United States
Ingawa Wanaulaya wengi ni wachambuzi juu ya utamaduni wa Amerika, yaonekana wanaiga sehemu kubwa ya utamaduni huo. Kwa kielelezo, wao walitazama kwa upendezi wakati maonyesho ya hila na kashfa za familia yalipoonyeshwa kwenye televisheni kwa miaka kadhaa katika mfululizo ulioitwa Dallas.[26] Gazeti la Ujerumani lilisifu mfululizo huo kwa ajili ya “kutosheleza uhitaji wa kihisiamoyo” na kutoa “hisia ya usalama, utumainifu, na hisia ya kujisikia.”[27]
Gazeti Time halikutoa sifa hivyo. Lilisema kwamba programu hiyo “iliinua uhitaji duni kuwa dini ya watu . . . Ilijulisha watazamaji juu ya miaka ya 1980 yenye Pupa, kwa kumfanya mtu wa Texas aliyetajirika kwa mafuta awe kitu cha kuabudiwa.”[28]
Sifa iliyopewa jiji hilo kwa ajili ya kipindi hicho cha televisheni haikaribii ile iliyodhaniwa na wakili na mfanya biashara John Bryan alipoanzisha kituo cha kibiashara katika 1841, labda akikiita kwa jina la George Dallas, aliyekuwa makamu wa rais wa U.S. Likiwa jiji la kifedha, usafiri, na utokezaji bidhaa—sehemu yenye kampuni nyingi za mafuta kuliko jiji jingine lolote la U.S.—“Big D” (Dallas) ni lenye utajiri kwelikweli.[29]
Mara nyingi utajiri hulinganishwa na furaha, kwa hiyo huenda watu wakaona Dallas kuwa jiji lenye shangwe. Hata hivyo, utajiri hauzuii mambo mabaya yasitokee. Dallas ndiko John F. Kennedy, rais wa 35 wa United States, aliuawa mnamo Novemba 22, 1963.[30]
Uhalifu wa jijini ni mojapo matatizo ya Dallas yanayoondolea watu furaha.[32] Tatizo jingine ni uhasama wa kijamii na kitamaduni. Katika Dallas, kama ilivyo katika kila jiji lenye jamii yenye watu wa rangi mbalimbali na utamaduni mbalimbali, sikuzote kuna uwezekano wa jeuri, kama vile ghasia za kijamii katika Los Angeles na ghasia za kidini katika Bombay zinavyoonyesha.
Laumizwa na Mafanikio Yalo Yenyewe
Kwa sababu ya mifereji yayo mingi, Bangkok lilikuwa likiitwa “Venice la Mashariki.” Sasa mahali pa mifereji yayo mingi pamechukuliwa na barabara, na ripoti moja yasema kwamba “mwendesha-gari wa kawaida hutumia siku kama 44 kwa mwaka akiwa katika milolongo ya magari.”[33]
Mfalme Rama 1 hakujua juu ya matatizo hayo alipogeuza kijiji kidogo kuwa jiji la kifalme katika 1782, akilipa jina jipya Krung Thep, linalomaanisha “Jiji la Malaika.” Baada ya kujengwa kwa Jumba Tukufu la Mfalme, sehemu nyingineyo ya jiji ilijengwa kulizunguka kupatana na itikadi ya Wathailand kwamba jumba la mfalme ndilo kitovu cha ulimwengu wote mzima. Wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, Bangkok liliharibiwa sana kwa mashambulizi ya mabomu. Lijapokuwa na jina hilo na mahekalu yalo mazuri, halikupata ulinzi wowote wa kimalaika.[34]
Ingawa liko karibu kilometa 30 kutoka Ghuba ya Siam, Bangkok lilifanywa kuwa bandari kwa sababu ya kule kuzoa taka daima katika Mto Chao Phraya unaopita kati ya jiji. Mara nyingi mto huo hufurika na kufurikia sehemu fulani za jiji, nyingine zazo zikiwa futi mbili tu juu ya usawa wa bahari. Hata hivyo, maji ya furiko sasa huelekezwa kwingineko kupitia mfereji mwingine, na hilo limeleta kitulizo fulani. Tatizo jingine ni kwamba maelfu ya visima vya kwenda chini sana vimefanya kiwango cha maji kishuke. Tangu 1984 jiji zima limekuwa likizama kwa kiwango cha inchi nne kwa mwaka.[35]
Ukuzi wa Bangkok kufikia watu zaidi ya milioni tano, pamoja na kiwango fulani cha ufanisi wa kiuchumi, zapasa kuwa sababu za furaha. Na kila mwaka mamilioni ya watalii huzuru jiji hilo na kutumia fedha zao humo. Lakini kwa sehemu fulani, hilo limefanywa na kuliharibia sifa yalo, kwani wageni wengi huvutiwa na ngono isiyo ghali inayopatikana kwa urahisi katika madanguro ya Bangkok. Kwa hiyo jiji hilo sasa lajulikana kuwa jiji maarufu la ashiki la Mashariki ya Mbali.[36]
Hata ile shangwe itokanayo na sherehe kama ile ya kusherehekea miaka mia mbili ya Bangkok—mwandamano wa watu wenye maua, maonyesho ya kihistoria, sherehe za kifalme, dansi za kitamaduni, na fataki—haiwezi kuondoa huzuni iliyo katika jiji hilo. Gazeti Newsweek lilisema kwamba Bangkok “laumizwa na mafanikio yalo lenyewe ya kiuchumi.”[37]
Kupata Shangwe Halisi
Kuna nini cha maana katika vile vitovu vya vitumbuizo vilivyo maarufu, kama vile vilivyoonyeshwa katika majiji yaliyo juu? Labda kuna raha ya muda, lakini si furaha ya kudumu. Leo, furaha ya kudumu yaweza kupatikana tu kwa msaada wa roho ya Mungu, ambayo shangwe ni tunda layo.—Wagalatia 5:22.
Kwa hiyo usijisumbue kutafuta shangwe, katika majumba ya sinema ya Bombay, majumba ya kamari ya Monte Carlo, mitindo-maisha ya kiajabu-ajabu katika San Francisco, utajiri mwingi wa Dallas, au madanguro ya Bangkok. Katika matoleo ya wakati ujao, tutaona mahali ambapo shangwe ya kudumu yaweza kupatikana.
[Picha katika ukurasa wa 25]
San Francisco, U.S.A.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Bombay, India
[Picha katika ukurasa wa 26]
Bangkok, Thailand