Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 2/22 kur. 16-19
  • Wenyeji wa Australia—Watu wa Kipekee

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wenyeji wa Australia—Watu wa Kipekee
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maisha ya Mapema Katika Australia
  • Muziki na Uwindaji
  • Michoro ya Wenyeji Hao
  • Lugha za Wenyeji Hao
  • Kuitikia Tumaini Zuri Ajabu
  • Upendo Wangu kwa Dunia Utatoshelezwa Milele
    Amkeni!—1998
  • Ile Didjeridu na Miziki Yayo Yenye Kuvutia
    Amkeni!—1997
  • Kuwatafuta Wanaostahili Katika Sehemu ya Mashambani ya Australia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
  • Je, Kweli Huu ni Mti?
    Amkeni!—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 2/22 kur. 16-19

Wenyeji wa Australia—Watu wa Kipekee

Na mleta habari za Amkeni! katika Australia

AUSTRALIA yaweza kusemwa kuwa nchi ya kipekee, ikiwa na kangaruu na koala wanaovutia sana na wenye kubeba watoto kwa mifuko iliyoko nje ya tumbo, huku koala wakiwa kule juu ya miti aina ya kalitusi. Lakini, wakazi wa awali ambao ni wenyeji wa nchi hiyo, ni watu wa kipekee hata kushinda nchi hiyo.

Walowezi wa kwanza kutoka Ulaya walipofika kuelekea mwisho wa karne ya 18, idadi ya wenyeji ilikadiriwa kuwa ipatayo 300,000.[3] Miaka 200 baadaye, hesabu ya watu iliyofanywa katika 1991 ilionyesha kwamba kulikuwa na wenyeji wachache zaidi ya 230,000 kati ya jumla ya idadi yote ya Waaustralia iliyokaribia milioni 17.[4]

Wakazi hao wa awali wa Australia walikuwa akina nani? Nao walitoka wapi? Ni kwa nini wao wasemwa kuwa watu wa kipekee? Na wengi wao sasa wanafurahia tumaini gani la wakati ujao?

Maisha ya Mapema Katika Australia

Wastadi wengi wa historia ya kibinadamu wanakubaliana kwamba wenyeji wa Australia hapo awali walitoka Asia. Huenda walikamilisha sehemu ya mwisho ya uhamiaji wao kwa kuelea kwa chelezo au mashua wakitoka Asia ya kusini-mashariki, wakitua ukingoni mwa pwani ya kaskazini mwa Australia.[5] “Hawakuwa watu wanaohama-hama sana,” akasema Malcolm D. Prentis katika kitabu chake A Study in Black and White, “bali walikuwa watu wenye kuhama-hama kidogo: yaani, walikuwa wakipiga kambi za muda katika sehemu tofauti-tofauti za eneo lao wanalolijua.”[6]

Wenyeji hao walikuwa watu wenye kuhifadhi mazingira sana na kuyatunza vizuri. Mwenyeji mmoja alieleza hivi: “Tulilima mashamba yetu, lakini kwa njia tofauti sana na watu weupe. Sisi tulijitahidi kuishi kulingana na hali ya ardhi; wao waliinyonya. Nilifundishwa kuwa mwenye kuhifadhi, si mwenye kuharibu.”[30]

Prentis aliandika hivi kwa kuunga mkono jambo hilo: “Hali njema ya mimea na wanyama pamoja na ya wenyeji hao ilishikamana: ufanisi kwa mtu mmoja ulikuwa ufanisi kwa mwingine. Na hilo lilikuwa kweli: kwa kielelezo, wingi wa kangaruu ulimaanisha chakula kingi kwa wenyeji lakini kuua kangaruu wengi mno hatimaye kungeathiri vibaya wenyeji hao.”[6]

Wenyeji hao walifanya vizuri kwa mambo mengine pia. Mstadi wa lugha R. M. W. Dixon alisema hivi katika kitabu chake The Languages of Australia: “Lakini, kwa habari ya kujipanga kijamii, ni Wazungu wanaoonekana kuwa watu wa kinyume sana wakilinganishwa na wenyeji wa Australia; makabila yote ya Australia yalikuwa na mifumo ya kiukoo iliyofafanuliwa vizuri ikiwa na sheria hususa za ndoa na ikiwa na daraka hususa la kila sherehe ya kijamii.”[7]

Muziki na Uwindaji

Jambo la kipekee kuhusu wenyeji hao ni ala ya muziki iitwayo didjeridu. Neno hilo lamaanisha kihalisi “filimbi-mvumo,” linaloeleza vizuri aina ya sauti ambayo ala hiyo ya muziki hutoa. Badala ya kuendeleza melodia ya muziki, didjeridu huandaa aina ya sauti nene ya kiume na mdundo katika sherehe za kidesturi na dansi za usiku ziitwazo korobori. Ala hiyo ya muziki humpa mwimbaji mdundo wa kichinichini akiwa na vijiti viwili vyenye kugongeshwa pamoja.

Didjeridu hutengenezwa kutokana na matawi ya miti yaliyo wazi ndani na yaliyoteuliwa kwa uangalifu. Urefu upendwao zaidi ni kutoka futi 3 hadi 5 lakini ala nyinginezo hufikia urefu wa futi 15. Mara nyingi sehemu moja ya mwisho huwekwa chini huku mwimbaji anayeketi akipuliza kupitia mwisho ule mwingine unaoshikiliwa mdomoni kwa mikono miwili.[8]

Kwa sababu sauti hiyo nzito iliyo nene ya ala hiyo huendelea daima, ni lazima mchezaji wayo aendelee kupuliza pumzi ndani ya ala hiyo wakati uo huo akipumua hewa safi kupitia pua yake bila kukatiza sauti ya muziki. Huu ni ustadi unaofanana na ule ambao ni lazima mwanamuziki achezaye ala ya muziki ya tiuba ajifunze. Ustadi huo huitwa na wachezaji wa ala za kupuliziwa pumzi, kupumua kwa kuendelea, na si rahisi kujifunza ustadi huo.[9]

Kwa ajili ya uwindaji, wenyeji hao walitumia vizuri kitu kingine ambacho ni cha kipekee—bumerang’i (gongo lililopindika). Ilitengenezwa kuwa silaha ya kuwinda na ya vita miongoni mwa wenyeji hao. Lakini kwa watalii wengi leo, hiyo imekuwa ishara nyingine maarufu ya Australia. Bumerang’i zijulikanazo sana ni silaha zenye kupinda ambazo humrudia mwenye kuzitupa zikitupwa vizuri. Hata hivyo, kuna aina nyinginezo ambazo si za kumrudia yule aliyezitupa. Hizo zaitwa kwa usahihi zaidi kilis, au fimbo za kuua.[29]

Michoro ya Wenyeji Hao

Kwanza, utamaduni wa wenyeji hao haukuwa na namna yoyote ya kuwasiliana kwa maandishi. Hivyo, Kevin Gilbert, mshairi na mchoraji mwenyeji, alieleza hivi: ‘Uchoraji ulikuwa njia nzuri zaidi ya kuwasiliana kwa wenyeji hao na ulikuwa ndio wa kueleweka ulimwenguni pote.’ Yeye alidai hivi: “Mchoro huwasilisha jambo vizuri zaidi na una maana zaidi kuliko maneno yanayoandikwa.”[11]

Kwa hiyo, kuwasiliana kwa michoro inayoonwa na miigizo kulikuja kushikamana sana na njia ya maisha ya wenyeji hao. Jambo hilo lilimaanisha kwamba michoro yao ilitumikia makusudi mawili: iliandaa njia ya kukazia uwasiliano wa mdomo, na vilevile ilitumika kuwa kikumbusha cha hadithi za historia, desturi na mambo ya kidini ya kabila hilo.

Kwa sababu nguo za kuchorea, karatasi, na vitu vingine kama hivyo havikuwako, wenyeji hao walichora juu ya miamba, mapango, na katika magome. Matumizi mengi ya rangi yafananayo na ardhi yaonwa sana katika michoro yao yote. Walitumia rangi zilizokuwa zikipatikana sana katika maeneo ambayo michoro hiyo ilichorwa. Rangi hizo zilitengenezwa kutokana na udongo.[12]

Jambo ambalo labda ni la kipekee kuhusiana na michoro yao ni kwamba karibu michoro yao yote ni ya madoa-doa na mistari. Hata mandhari za nyuma, ambazo kwanza zaweza kuonekana kuwa rangi moja, zaonyesha kigezo fulani cha madoa-doa mengi yenye rangi tofauti-tofauti.[14]

Wonyesho wa usanii wenye kichwa Marketing Aboriginal Art in the 1990s wasema kwamba katika miaka ya 1980 “Michoro ya Wenyeji hao . . . ilifanya maendeleo makubwa kutoka kuwa ‘michoro ya kitamaduni’ hadi kuwa ‘michoro ya kibiashara.’” Wengine wasema kwamba michoro hiyo yenye madoa-doa iliyo ya kiakrili inapendwa sana na wao husifu sana kuja kupendwa kwa michoro hiyo.[20]

Lugha za Wenyeji Hao

Kwa kawaida Waaustralia weupe huwa na maoni yasiyo sahihi juu ya lugha za wenyeji. Kwa kielelezo, wengine hudhani kwamba kulikuwa na lugha moja tu ya wenyeji hao na kwamba ilikuwa ya hali ya chini sana hivi kwamba ilifanyizwa tu kwa maguno na mikoromo michache. Lakini jambo hilo si kweli kabisa!

Kwa kweli, pindi moja kulikuwa na lugha zilizokadiriwa kuwa kati ya 200 hadi 250 za wenyeji hao. Hata hivyo, zaidi ya nusu ya lugha hizo zimepotelea mbali. Kufikia leo ni lugha karibu 50 pekee ambazo bado zatumiwa na vikundi 100 au zaidi vya wenyeji hao. Na hesabu ya lugha zinazosemwa na wenyeji wapatao 500 au zaidi sasa ni chini ya 20.[23]

Mbali na kuwa lugha ya hali ya chini sana, lugha inayosemwa na wenyeji hao imeendelea sana kisarufi. Katika kitabu chake The Languages of Australia, Profesa Dixon aandika: “Hakuna lugha yoyote, miongoni mwa zile lugha zipatazo 5,000 zinazosemwa ulimwenguni pote leo, iwezayo kusemwa kuwa ya ‘hali ya chini.’ Kila lugha ijulikanayo ina mfanyizo mgumu, hivi kwamba ufafanuzi tu wa mambo makuu ya sarufi yayo huhitaji mamia kadhaa ya kurasa; kila lugha ina maelfu ya misamiati inayotumika katika maisha ya kila siku.”[22]

Barry J. Blake aliandika akiwa na maoni ayo hayo kuhusu lugha za wenyeji hao: “Hizo ni njia za uwasiliano za hali ya juu sana, kila moja ikitoshea kueleza ono la wenyeji hao kama vile Kiingereza au Kifaransa ziwezavyo kueleza juu ya ono la Wazungu.”[24] Akiunga mkono kauli hiyo, mwandikaji wa gazeti mwenyeji Galarrwuy Yunupingu alieleza hivi: “Ni wazungu wachache sana wamewahi kujaribu kujifunza lugha yetu, na Kiingereza hakiwezi kueleza uhusiano wetu na bara hili la mababu wetu wa ukoo.”[25]

Katika karne ya 19, sehemu fulani za Biblia zilitafsiriwa katika lugha mbili za wenyeji hao. Gospeli ya Luka ilitafsiriwa katika lugha ya Kiawabakal na sehemu za Mwanzo, Kutoka, na Gospeli ya Mathayo zilitafsiriwa katika lugha ya Kinarrinyeri. Kwa kupendeza, tafsiri hizo zilitafsiri jina la Mungu Mweza Yote kuwa “Yehóa” na “Jehova,” kulingana na jinsi maneno ya lugha hiyo huandikwa.[27]

Leo, mkazo mkubwa zaidi umewekwa juu ya kurudisha lugha za wenyeji hao na kuonyesha thamani, ubora, na uzuri wa lugha hizo miongoni mwa Waaustralia ambao si wenyeji. Kwa hiyo, wengi sasa wanafurahi kujua kwamba Waziri wa Mambo ya Wenyeji wa Australia ameidhinisha kutokezwa kwa kamusi katika lugha 40 za wenyeji hao. Kamusi hizo zitatia ndani zile lugha zinazotumiwa sasa na vilevile lugha nyingi ambazo hazitumiwi sasa ambazo zitafanyiwa utafiti katika majumba ya vitu vya kale na vyanzo vingine vya habari za kihistoria.[26]

Kuitikia Tumaini Zuri Ajabu

Wazungu walipokuja Australia kuelekea mwisho wa karne ya 18, karibu waangamize kabisa wenyeji hao. Hata hivyo, siku hizi kuna miji kadhaa ya mashambani yenye idadi kubwa zaidi ya wenyeji hao, na bado kuna vijiji vyenye wenyeji hao pekee, hasa katika maeneo ya mbali. Mara nyingi watu hao hawana tumaini maishani. “Hatuwezi kufikiria tena mambo ya zamani,” akaandika mwenyeji fulani, “wala haturidhiki kwa hali za sasa.” Lakini akaongezea: “Kuna tumaini la wakati ujao kwa wengi wetu.”[30]

Sababu ya hiyo ni kwamba wakazi wengi wa awali wa Australia sasa wanafurahia kusoma katika Biblia—labda kwa lugha yao wenyewe—kwamba hivi karibuni maovu yatakwisha na kwamba dunia itapewa wale miongoni mwa binadamu watakaoitunza vizuri. (Zaburi 37:9-11, 29-34; Mithali 2:21, 22) Ufalme wa Mungu utatimiza hilo. Ufalme huo, ambao Yesu Kristo alitufunza tusali juu yao, ni serikali halisi ya kimbingu. (Mathayo 6:9, 10) Wenyeji wengi wanaume kwa wanawake sasa wanashughulika sana kueleza wengine juu ya baraka nzuri ajabu ambazo Ufalme wa Mungu utaletea jamii ya kibinadamu.—Ufunuo 21:3, 4.

Mwenyeji mmoja alieleza hivi juu ya wengi wa Waaustralia wenzake: “Wao huona kwamba maoni yanayokubaliwa na wazungu, wenyeji, na watu wengine wengi wa dunia ni yenye makosa. Ni maoni ya kwamba Australia ni mali ya wenyeji hao kwa sababu waliigundua kwanza au ni mali ya wazungu kwa sababu ya kuinyakua. Hayo yote si kweli. Hiyo ni mali ya Yehova Mungu kwa sababu aliiumba.”—Ufunuo 4:11.[30]

Kwa kweli Muumba wetu, Yehova Mungu, ndiye mwenye Australia pamoja na dunia yote nzima. Na kwa kutimiza sala ambayo Yesu alifundisha, Ufalme wa Mungu utakuja, na dunia yote itageuzwa kuwa paradiso ya duniani pote inayokaliwa na watu wa jamii zote na mataifa yote wanaompenda na kumtumikia Mungu wa kweli.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Didjeridu ni ala ya muziki ya kipekee kwa wenyeji wa Australia

[Picha katika ukurasa wa 17]

Wonyesho wa michoro ya wenyeji

[Hisani]

Kwa Hisani ya Australian Overseas Information Service

[Picha katika ukurasa wa 18]

Wenyeji wengi sasa wanatangazia wengine habari njema za Ufalme wa Mungu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki