Ile Didjeridu na Miziki Yayo Yenye Kuvutia
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA
NJOO nasi kwenye sherehe ya Wenyeji wa Australia katika Eneo la Kaskazini la Australia, si mbali sana kutoka Darwin, jiji lalo kuu. Badala ya kufanywa zikiwa kitangulizi cha vita vya kikabila, sherehe nyingi za leo hufanyiwa hasa watalii. Tutahudhuria sherehe ya aina hiyo.
Wachezaji, ambao miili yao imepakwa rangi nyangavu, wamesimama tuli wakingojea muziki utoe ishara ya kuanza kucheza dansi. Ghafula muziki waanza, na utulivu wa jioni yenye giza ya sehemu za mashambani za Australia waangua kwa muziki wenye nguvu wenye kudundadunda. Mwambatanisho zaidi waandaliwa kwa kupigapiga vijiti—vijiti viwili vyagonganishwa kwa kupatana na muziki unaochezwa kwenye didjeridu.
Si watu wengi nje ya Australia wamesikia didjeridu, ala hii ya muziki ambayo ni ya Wenyeji wa Australia pekee. Kwa kawaida hiyo hutengenezwa kwa tawi lililofanyizwa uwazi la mti uitwao eucalyptus, na urefu ufaao ni kutoka meta moja hadi moja na nusu. Mwanamuziki hukaa ardhini kando ya sehemu ya kuchezea, akipuliza didjeridu yake—ala ionekanayo kuwa sahili lakini yenye kuvutia.
Sauti ya Kipekee
Ingawa didjeridu hutokeza sauti ileile—hiyo imefafanuliwa kwa kufaa kuwa “tarumbeta ya mvumo”—yaweza kufanyiza ulinganifu wa mwendo na mitetemo ya sauti iliyo tata. Dakika moja ina sauti moja pekee, dakika ifuatayo, yaweza kujaa nguvu na hisia, kama kikundi kamili cha wapiga muziki.
Kabla ya Wanaulaya kuja Australia miaka ipatayo 200 iliyopita, didjeridu ilijulikana kwa Wenyeji hao wa Australia tu ambao walizunguka-zunguka sehemu za kaskazini za kontinenti hiyo iliyo kisiwa. Kwenye sherehe, hiyo iliandaa mwambatanisho wa kimuziki kwa dansi zilizorudiarudia hekaya za Wenyeji hao wa Australia zinazohusu uumbaji. Kwa wakati huo, wale waliocheza didjeridu kwa ustadi waliheshimiwa sana, na hata leo mchezaji stadi huonwa kuwa mshiriki wa kabila mwenye kuheshimiwa sana.
Wachezaji stadi mara nyingi huongezea miigizo ya sauti za wanyama na ndege kwenye sauti za msingi za didjeridu. Kicheko cha kookaburra; kilio cha mbwa mwitu wa Australia au dingo; mlio mwororo wa hua; na sauti nyinginezo nyingi huwa sehemu zenye ustadi za uigizaji wao.
The New Grove Dictionary of Music and Musicians husema hivi kuhusu mchezaji wa didjeridu: “Miongoni mwa sifa zake mna utumizi sahihi na wepesi wa kutumia ulimi, udhibiti mzuri sana wa upumuaji, ufungaji mkamilifu wa midomo mwishoni wa mrija na kumbukumbu bora sana la muziki. . . . Ingawa hana tekinolojia na vifaa, na hafahamu dhana ya ala ya mdomo, filimbi, ala aina ya slide, au matundu ya filimbi, [Mwenyeji wa Australia] hata hivyo amebadili kifaa sahili kuwa ala ya muziki ya mwanamuziki stadi sana kupitia kutumia mawazo ya kimuziki na stadi za kimwili za hali ya juu.”
Bila shaka sehemu yenye kutazamisha zaidi ya didjeridu ni sauti yayo yenye kuendelea, au mvumo. Mchezaji hutoa wazo la kuwa na uwezo usio na mwisho wa pafu, kwa kuwa huenda kusiwe na kupumzika katika muziki kufikia muda wa dakika kumi kwa wakati mmoja.
Kutengeneza Didjeridu
Kwa jicho lililozoezwa, fundi mwenyeji huvinjari kichaka akitafuta mti mgumu, hasa eucalyptus. Ingawa mbao laini zaidi zaweza kutumiwa, mbao ngumu hutokeza kadiri ya sauti iliyo bora. Mti huo wahitaji kutafutwa karibu na vichuguu vya mchwa kwa sababu mchwa ndio wahandisi wa didjeridu. Wao hufanyiza uwazi katika matawi yatumiwayo kwa ala hii ya muziki.
Baada ya tawi kuchaguliwa, hilo hukatwa kwa urefu upendwao. Urefu uliochaguliwa huamua kadiri ya sauti ya ala itakayotengenezwa. Kisha gome huambuliwa, sehemu laini ya nje huondolewa ili kuzuia kupasuka, na sehemu ya ndani yatolewa ili kufanyiza uwazi. Ikiwa sehemu ya ndani imeliwa vya kutosha na mchwa, yapasa kuwezekana kubingirisha sarafu kubwa kiasi kupitia uwazi huo. Hatua ifuatayo ni urembeshaji, ambao waweza kuvutia sana. Lakini bado didjeridu haiko tayari kuchezwa.
Ngozi inayozunguka kinywa cha mchezaji yaweza kuwashwa na kujifuta kila wakati kwenye mbao hiyo. Kwa hiyo nta ya nyuki huzungushwa kwenye tundu la didjeridu, ikiacha ulaini ambao hautawasha ngozi ya mchezaji. Hata hivyo, leo didjeridu nyingi hutengenezwa viwandani, mara nyingi kutokana na mbao laini. Lakini didjeridu za kutengenezwa viwandani kwa kawaida ni za hali ya chini zikilinganishwa na mbao ya kipekee na ubora wa sauti wa mbao ngumu ya asili.
Kwa hiyo, sherehe inapomalizika na jioni yetu ya kitropiki chini ya nyota kumalizika, hatuoni didjeridu kuwa tu jambo la kuvuta udadisi. Kwa kweli, muundo wa muziki usiotoweka wa didjeridu ni sifa kwa wenyeji wapenda muziki wa nchi ya Australia.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Didjeridu yaweza kupakwa rangi mbalimbali
[Picha katika ukurasa wa 25]
Sherehe ya Wenyeji wa Australia
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Ukurasa wa 24-25 Wenyeji wa Australia: Kwa Hisani ya Australian Northern Territory Tourist Commission