Kuutazama Ulimwengu
Kutotumaini Serikali
“Watu sehemu zote za ulimwengu wanapoteza imani katika mfumo,” ndivyo lilivyodai The Washington Post majuzi, likiongeza kwamba, “Kila mahali, watu hawapendi kusikia serikali ikitajwa.” Likieleza juu ya kura za kutafuta maoni ya umma katika miaka ya majuzi, gazeti hilo lilisema hivi: “Kuanzia Kanada hadi Japani na sehemu za hapo katikati, nyakati fulani raia wengi mno wanaambia waomba-maoni kwamba serikali ya nchi yao haiwezi kutumainiwa, kwamba uchumi wa taifa lao karibu uangamie na kwamba mambo yatazidi tu kuwa mabaya, si mazuri.” Kwa kielelezo, katika Ufaransa asilimia kama 60 ya wale walioombwa maoni walitarajia mambo yazidi kuwa mabaya wakati ujao, hali idadi inayokaribia kulingana na hiyo walionyesha kutoridhika na jinsi nchi isimamiwavyo. Katika Italia karibu asilimia 75 walihisi kwamba Serikali haikuwa ikifanya kazi vizuri kama miaka mitano au kumi iliyopita. Katika Kanada zaidi ya nusu walihisi kwamba kizazi kifuatacho kingekuwa katika hali mbaya hata zaidi ya kiuchumi kuliko chao wenyewe.
Nguvu ya Dawa za Kutuliza Akili Tu Bila Kuponya
Watafiti wa kitiba wameshikilia kwa muda mrefu kwamba karibu theluthi moja ya wagonjwa huelekea kuonyesha nafuu fulani walipopewa dawa ya kutuliza akili tu bila kuponya. Hata hivyo, uchunguzi mpya umeonyesha kwamba dawa za kutuliza akili tu bila kuponya zaweza kuwa na tokeo lenye nguvu zaidi. The New York Times liliripoti hivi majuzi kwamba wanasayansi kwenye La Jolla, Kalifornia, U.S.A., walichunguza wagonjwa karibu 7,000 waliokuwa wamepewa matibabu mapya ya kujaribia tu ambayo baadaye yalionekana kuwa bila mafaa yoyote ya kitiba. Uchunguzi huo ulionyesha kwamba theluthi mbili za wagonjwa walipata nafuu, angalau kwa muda, huku matibabu hayo yakiwa na matokeo juu yao. Ingawa huenda ikawa kwamba katika visa fulani utumizi wa dawa za kutuliza akili tu bila kuponya waweza kuleta nafuu halisi ya kimwili, wanasayansi wanatahadharisha kwamba nyakati fulani huonyesha tamaa ya mgonjwa mwenyewe ya kumpendeza tabibu kwa kuripoti kwamba amepata nafuu. Hivyo, watafiti fulani wataja uchunguzi huo kuwa sababu ya kufanya majaribio makali zaidi juu ya dawa zilizo mpya.
Kunusa Ili Kupata Penye Kuvuja
Kuvuja kwa mafuta katika vishimo vidogo vya mabomba yaliyofunikwa ardhini huenda kusitangazwe sana kama mapasuko ya mabomba na mimwagiko mikubwa ya mafuta, lakini bado kuvuja kudogo huko hugharimu shughuli ya viwanda mamilioni ya dola kila mwaka na kusababisha “uchafuzi uliofichika, usioonekana,” laripoti gazeti National Geographic. Shirika moja la Kanada limepata utatuzi usio wa kawaida kwa hilo tatizo—wao huwatumia mbwa, mbwa-watafutaji wa aina ya Labrador, kunusa ni wapi penye vishimo vidogo kama sindano vinavyovuja katika mabomba yenye mafuta, gesi ya kiasili, na kemikali. Kwanza, kemikali yenye kunuka sana hunyunyizwa katika sehemu fulani ya bomba lishukiwalo kuvuja. Kisha mbwa huingia kazini. Geographic laripoti hivi: “Wao waweza kunusa kemikali inayoponyoka katika mabomba yaliyofunikwa na ardhi kina cha meta 5. Katika bwawa moja lenye matope la Louisiana [hao] mbwa walisimama juu ya mashua zilizo ndogo na kuigundua harufu kutoka kwenye mabomba ya kemikali yenye kuvuja yakiwa meta 1.8 chini ya maji na meta 1.5 chini ya ardhi.” Hilo gazeti laongezea hivi: “Hao mbwa huwa wakingoja zamu za kuitwa ulimwenguni pote.”
Miungu ya Mvua Yakatisha Tamaa
Kwa kukabiliwa na ukavu mkali, serikali ya jimbo la Andhra Pradesh katika kusini-mashariki mwa India hivi majuzi iligeukia mbinu isiyo ya kawaida ili kuleta mvua. Kulingana na gazeti India Today, serikali ya jimbo ilitafuta msaada wa “sherehe ya kale ya kusihi miungu ya mvua kwa sherehe ya kutumia maandishi matakatifu ya Veda.” Aliwaza hivi Waziri wa Idara ya Majaliwa: “Mungu atatuokoa.” Makuhani kutoka mahekalu 50 yaliyochaguliwa walifanya hizo desturi za kiibada kwa siku 11. Tokeo likawa nini? India Today laripoti hivi: “Ni wazi kwamba miungu haikupendezwa. . . . Kwa kuwa dini imeshindwa, sasa Serikali imeamua kutegemea ile njia ya kisayansi. Imechukua hatua za kufanyiza mvua-bandia” katika jaribio la kunyunyiza kemikali juu ya mawingu ili yadondoshe mvua.
Mridhiano Juu ya Mridhiano
Walutheri katika United States na pia Wamethodisti katika Uingereza wameshughulikia suala la ugoni-jinsia-moja hivi majuzi. Katika Uingereza, Kongamano la Wamethodisti lilifikia uamuzi usioeleweka vizuri. Waliamua kutoagiza rasmi wanaume na wanawake wagoni-jinsia-moja kuwa wahudumu; hata hivyo, wakati huohuo walitangaza kwamba kanisa “hutambua, huimarisha na kusherehekea ushiriki na huduma ya wanawake na wanaume wagoni-jinsia-moja katika Kanisa.” Katika United States, kikundi fulani cha Kanisa la Kilutheri kilitoa ripoti yenye kurasa 21 iliyokusudiwa kupelekewa mapasta 19,000 wa kanisa ili watoe maoni yao. Kulingana na Shirika la Habari la Associated Press, hiyo ripoti yashikilia kwamba Biblia huunga mkono ndoa za wagoni-jinsia-moja. Vilevile hiyo ripoti yadai kwamba kupiga punyeto “kwa ujumla kwafaa na ni kwenye afya.” Katika ushikilio wa maoni hayo na katika dai hilo, ripoti hiyo yapinga msimamo wa Biblia katika mambo hayo.—Warumi 1:26, 27; 1 Wakorintho 6:9, 10; Wakolosai 3:6, 7.
Biashara ya Tumbaku Yasitawi Katika Urusi
Biashara ya tumbaku inavuma katika Urusi na maeneo mengine yaliyokuwa ya Sovieti, laripoti gazeti la Maclean’s la Kanada. Kuna wavutaji karibu milioni 70 katika ule uliokuwa Muungano wa Sovieti, au yapata asilimia 25 ya idadi ya watu, nao humaliza sigareti bilioni 350 kwa mwaka. Na kwa kuwa sheria za Sovieti zilizokuwa zikikataza utangazaji wa sigareti hapo kwanza hazitumiki tena, mashirika ya tumbaku ya Magharibi yametia mafuriko ya matangazo ya bidhaa zao katika vyombo vya habari—redio, televisheni, magazeti, na mbao za matangazo. Ingawa aina za sigareti za Magharibi zaweza kugharimu kuanzia mara mbili hadi nne kwa kulinganisha na aina za kienyeji, mara nyingi ndizo hutafutwa na watu ili ziwe ishara yao ya umashuhuri. Lasema hivi Maclean’s: “Takwimu za serikali zaonyesha kwamba Warusi wapatao 500,000 hupatwa kila mwaka na kansa ya mapafu na magonjwa mengine yanayohusiana na uvutaji.”
Hospitali Yenye Magurudumu
Hospitali isiyo ya kawaida imekuwa ikisaidia wagonjwa katika India: gari-moshi ambalo huitwa “Lifeline Express.” Gari-moshi hilo lenye kuendeshwa na madaktari wa kujitolea ni “kama tu hospitali yenye magurudumu,” laripoti gazeti Asiaweek. Gari-moshi hilo hupiga mwendo kuingia katika vijiji na kusimama kuanzia mwezi mmoja hadi mwezi-mmoja-na-nusu, likiwapa madaktari-wapasuaji wakati wa kutibu angalau wagonjwa 600 kabla halijaenda kijiji kifuatacho. Hospitali hiyo ya kuhamahama huendeshwa na kikundi kisichojitafutia faida ambacho chaitwa Shirika la Impact India, na kufikia sasa limesaidia watu wapatao 400,000. Zelma Lazarus wa Impact India aripoti hivi: “Mradi huu umevuvumka ukapita kiasi kifaacho. Nchi nyinginezo sasa zinatuomba tuanzishe mfumo wa hospitali kama hiyo ya kuhamahama.”
Kuhesabu Ni Wangapi Wanaoelekea Helo
Wabaptisti wa Kusini wa Alabama, U.S.A., waliingia motoni hivi majuzi walipochapisha kadirio rasmi lenye kudokeza kwamba asilimia 46.1 ya idadi ya watu wa jimbo hilo huenda wakaingia katika helo ya Kibaptisti. Ripoti yao, iliyochapishwa katika The Birmingham News, ilitoa maelezo juu ya kila kata ya jimbo hilo, ikiorodhesha asilimia za hesabu ya “wasiookoka” katika kila kata. Kulingana na Shirika la Habari la Associated Press, jambo tu walilofanya Wabaptisti ni kupunguza tarakimu za idadi ya washirika wa kanisa kutoka idadi ya watu wa kila kata, kisha wakatumia “hesabu ya siri” kuamua idadi ya watu wa kutoka dini nyinginezo ambao wao waliwafikiria pia yaelekea watakwenda mbinguni. Ripoti yao ilichambuliwa vikali na wasomaji wa The Birmingham News. Mmoja aliandika hivi: “Ni kimbelembele kisicho na kifani kutafuta njia ya kuhesabu idadi ya wasiookoka.”
Mambo ya Kujenga Husaidia Kuendeleza Mtu Kuwa Mwenye Afya
“Mkazo mkali sana na matatizo ya kihisia-moyo hupunguza kinga ya mwili, hali shangwe na raha huchochea mfumo wa kukinga mwili na viini na kuitia nguvu kinga ya mwili kuelekea ugonjwa.” Hivyo ndivyo gazeti la Kijerumani Nassauische Neue Presse litoavyo muhtasari wa uthibitisho uliokusanywa na sayansi mpya ya kuchunguza matokeo ambayo hali ya akilini huleta juu ya mfumo wa kinga za mwili. Mavutano mabaya kazini au nyumbani hudhoofisha kinga ya mwili. Kwa upande mwingine, kulingana na Dakt. Anton Mayr, aliye profesa na mchunguzi wa viini vidogo sana, kuwa na hisia-moyo zifaazo na kupatwa na mambo yafaayo kuna matokeo ya kutia nguvu. Hivi ni baadhi ya vielelezo alivyotaja: “Imani, tumaini, upendo, tumainio, usalama, uwasiliano, kichocheo kifaacho maishani, tafrija—na nia ya kuishi na kuwa mwenye afya.”
Ufisadi na Ungamo
Waandikaji Waitalia wawili, kwa kujifanya ni wanasiasa au wanabiashara, waliomba mapadri wengi Wakatoliki wawaondolee dhambi za ufisadi. Halafu wakachapisha mambo ambayo mapadri hao waliwaambia katika lile ungamo. Laripoti hivi gazeti La Repubblica: “Kanisa laona kwamba [hao waandikaji] wamekufuru, na tayari wameshambuliwa na labda wakaondoshwa katika ushirika kwa kutenda jambo hilo.” Lakini gazeti hilo laongezea kwamba maungamo bandia hayo “yaonyesha vurugu halisi, kutostahili, na kujitia katika anasa kwa sehemu kubwa ya wale mapadri Waitalia 36,000, ambao huonekana mara nyingi wakipendezwa na ngono kuliko dhambi dhidi ya jamii ya watu.” Pino Nicotri, mmoja wa hao waandikaji, alipata kwamba kati ya wale mapadri 49 ambao yeye ‘aliwaungamia,’ ni mmoja tu aliyekataa kumwondolea dhambi na kumwambia aripoti uhalifu wake kwa wenye mamlaka. La Repubblica lilitoa elezo hili: “Kwa habari ya wale wengine, ama rushwa si dhambi, ama ni kazi-bure kuendea hakimu, kwa kuwa jambo la maana ni msamaha kutoka kwa Mungu.”
Idadi Kubwa Hupata Nafuu
“Hali ya Brazili imebadilika miaka ya majuzi. Zaidi ya kuwa njia ya kupitiwa na wachuuzi wa dawa za kuondoa maumivu za aina ya kasumba, nchi hiyo imekuwa pia mtumiaji na mtengenezaji wa dawa hizo,” aeleza Arthur Guerra de Andrade, mtaalamu ahusikaye na uzoelevu wa kutumia vileo na dawa za kulevya. Kulingana na O Estado de S. Paulo, utumizi mbaya wa dawa “huathiri asilimia 6 hadi 8 ya idadi ya watu.” Kwa kuongezea, “miongoni mwa vijana wa miaka 12 hadi 16, asilimia 90 wametumia kileo angalau mara moja.” Andrade aongezea hivi: “Hesabu ya watu waonekanao kuwa na matatizo ya kimwili na ya kimawazo kwa sababu ya kileo imeongezeka kwa asilimia 50 katika miaka kumi iliyopita.” Zaidi ya hilo, “karibu asilimia 25 ya aksidenti za kazini ambazo hutukia katika Brazili zahusiana na utumizi mbaya wa dawa, hasa kileo.” Ingawa hivyo, tukigeukia upande mzuri, Brazili “ni moja ya nchi zilizo na visa vingi zaidi ulimwenguni vya kupata nafuu—asilimia 60 hadi 80 ya wafanyakazi walio wazoelevu wa kileo.”