Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 10/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Watoto wa Mitaani Watoroka Kutendwa Vibaya
  • Watu Wasahaulifu
  • Kwa Nini Mstari Wako Husonga Polepole
  • Kutendwa Vibaya na Makasisi Katika Afrika
  • Wahubiri Wabeba Bunduki
  • Watoto Wachanga Wanahitaji Kuguswa
  • Kutupa Mbwa wa Kisasa
  • Watoto—Iweni Watendaji!
  • Wahasiriwa wa Biashara ya Ngono
  • Je, Tuelekeze Nuru Kwenye Goti ili Kupunguza Uchovu wa Safari?
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1996
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1994
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2003
  • Kuzuia Nyumbani
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 10/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Watoto wa Mitaani Watoroka Kutendwa Vibaya

“Asilimia 90 ya watoto wa mitaani wanatoka katika familia fulani. Karibu asilimia 90 [ya watoto hawa wa mitaani] hushambuliwa na wazazi wao na kwa hiyo hutoroka, wakijihusisha na uhalifu, dawa za kulevya, na ngono,” asema Enza Mattar, mratibu wa shirika la Regional Center for Attention to Mistreated Children (Crami). Mattar, ambaye alinukuliwa na gazeti la habari la Brazili O Estado de S. Paulo, ashauri wataalamu wa kitiba na walimu wawe macho kuona dalili za kutendwa vibaya, kutia ndani “mabadiliko ya ghafula katika mwenendo, kujitenga, na alama mwilini.” Kuingilia jambo hili kwaweza kuwa muhimu, kwa kuwa ni asilimia 5 pekee ya kesi zinazoshughulikiwa na Crami ndizo huhusisha watoto ambao huomba walindwe. Mara nyingi wazazi wenye kutenda watoto vibaya hukataa msaada. Kwa nini? Msimamizi wa Crami João Roberto Scomparim asema hivi: “Wazazi wanaowashambulia kijeuri watoto wao wanarudia kufanya mambo ambayo wao wenyewe walifanyiwa walipokuwa wachanga, nao wanaamini kwamba wanaelimisha watoto wao.”

Watu Wasahaulifu

Katika uchunguzi wa Italia uliohusisha watu wazima 1,600, asilimia 77 walisema kwamba wao husahau-sahau mambo, lasema gazeti la habari La Repubblica. Katika mwaka uliopita zaidi ya thuluthi moja walisahau uadhimisho mkubwa katika mwaka uliotangulia. Kwa kuongezea, asilimia 42 walikuwa wakisahau kwa ukawaida mahali walipoegesha gari lao, zaidi ya asilimia 30 walisahau funguo za nyumba zao, zaidi ya asilimia 25 walisahau kibeti chao, na asilimia 1.2 hata walisahau jina lao wenyewe na jina la familia. Kwa upande mwingine, asilimia 28 ya Waitalia wanasema kwamba bado wanakumbuka angalau shairi moja walilokariri shuleni. Unaweza kuboreshaje kumbukumbu lako? Mwanasaikolojia mmoja apendekeza kuhusianisha kitu cha kukumbukwa na kitu kingine, kuandika mambo katika kitabu cha kumbukumbu, na kuzoeza akili yako kwa kukariri nambari za simu, tuni, na hata nambari za leseni.

Kwa Nini Mstari Wako Husonga Polepole

Ikionekana kwamba sikuzote unajipata katika mstari unaosonga polepole zaidi wakati wa kufanya ununuzi, yaweza kuwa ni hali ya uwezekano inayotokea tu. Kama lisemavyo gazeti la habari la Ujerumani Die Zeit, uwezekano wa kusonga kwa haraka kwa mistari miwili iliyo karibu nawe ni 2 kati ya 3. Kadiri kunavyokuwa na mistari mingi, ndivyo uwezekano huwa mdogo. Watafiti wamepata kwamba jambo linalowaudhi watu zaidi si kungoja, badala yake “ni kuona kwamba wanapoteza wakati.” Ili watu wasiudhike wanapongojea lifti, hoteli fulani zimeweka vioo kwenye ukumbi. Hili huwapa watu jambo la kufanya—kuchana nywele zao au kurekebisha tai zao. Pia inasaidia kujulisha watu muda unaobaki wa kungoja. Hivyo, mifumo fulani ya magari-moshi ya chini ya ardhi huonyesha matangazo yanayoonyesha ni dakika ngapi zinazosalia kabla ya gari-moshi linalofuata kuondoka.

Kutendwa Vibaya na Makasisi Katika Afrika

Gazeti Catholic International laripoti kwamba “kesi za kutendwa vibaya kingono na makasisi zimeanza kutokea katika Afrika.” Ili kuzuia kutendwa vibaya huko, maaskofu fulani Wakatoliki wanapendekeza kwamba uchunguzi na mazoezi zaidi yafanyiwe watu wawezao kuwa wanasemina. Mambo mengine yanayowahangaisha maaskofu wa Kiafrika ni mwenendo mbaya wa makasisi unaohusisha “matumizi mabaya ya vileo, na kujihusisha na mambo yasiyofaa au yasiyopatana na hali na wito wa kikasisi, kama vile biashara, siasa.” Kwa nini mambo haya yamejulikana hivi karibuni tu? Gazeti Catholic International lajibu likisema “uhuru zaidi ambao vyombo vya habari vimepata na kulegezwa kwa udhibiti wa Kanisa juu ya vyombo vya habari,” likiongezea kwamba “majaribio ya hapo mwanzoni ya wenye mamlaka fulani wa Kanisa katika sehemu fulani ya Afrika ya kuzuia habari zisizofaa . . . yameshindwa.”

Wahubiri Wabeba Bunduki

Katika jimbo la Kentucky, Marekani, hivi karibuni sheria ya jimbo hilo ilifanyiwa marekebisho ili kuruhusu mapasta wabebe bunduki zilizofichwa wakiwa kanisani ikiwa wana leseni ya kubeba silaha zilizofichwa, laripoti shirika la habari la Reuters. Hapo awali, mapasta waliopewa leseni ya kubeba silaha hatari zilizofichwa hawangeweza kufanya hivyo katika sehemu za ibada katika jimbo hilo. Katika mwaka wa 1997, makanisa fulani ya Kentucky yaliibiwa michango yao kwa kutumia bunduki. Ingawa hakuna mtu aliyejeruhiwa, “wahudumu na makasisi wa makanisa ya mashambani walishawishi watunga-sheria wa jimbo kuwaruhusu wabebe bunduki zilizofichwa,” yasema ripoti hiyo. Hata hivyo, si makasisi wote wanaounga mkono badiliko hili. Nancy Jo Kemper, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Makanisa la Kentucky, aliuliza hivi: “Twaweza kuwatarajiaje watoto wetu wajue kwamba bunduki hazitaweza kutatua matatizo ikiwa wanaona hata wahudumu, wanaopaswa kuwa wawakilishi wa amani na upatanisho, wakibeba silaha zinazoweza kuua?”

Watoto Wachanga Wanahitaji Kuguswa

“Watoto wanaolelewa bila kukumbatiwa kikawaida au kupapaswa . . . wana viwango vya juu sana vya homoni za mkazo,” kulingana na uchunguzi ulioripotiwa katika gazeti la habari la Toronto Star. Watafiti hao wanaamini kwamba kutenganishwa na mama au kupuuzwa utotoni “kwaweza kutokeza madhara ya muda mrefu katika kujifunza na kumbukumbu.” Mwanasayansi wa Shule ya Kitiba ya Harvard Mary Carlson alizidi kusema kwamba vijana ambao familia ziliwaingiza kwenye “sehemu za kutunzia watoto zisizofaa walikuwa na viwango vya homoni visivyo vya kawaida katika siku za juma lakini si katika mwisho-juma watoto walipokuwa nyumbani.” Utafiti huu watoa uthibitisho zaidi kwamba kugusa kwa uanana na upendo mwingi ni mambo ya maana kwa watoto wetu.

Kutupa Mbwa wa Kisasa

Makao ya wanyama ya Australia yanajaa mbwa ambao hawapendwi tena, lasema gazeti la habari la Melbourne Herald Sun. Ripoti hiyo yasema kwamba “mbwa waitwao malamute wa Alaska ndio wametupwa kwa idadi kubwa zaidi hivi karibuni.” Wenye mbwa hao huwatupa kwa sababu hawapendwi tena au wamekua wakubwa sana hivi kwamba hawapendezi. Shirika la kutetea masilahi ya wanyama la Royal Society for Prevention of Cruelty to Animals (RSPCA) latarajia kwamba mbwa aina ya Dalmatian ndio watakaofuata kutupwa, wakati aina hii ambayo imependwa sana baada ya kuonyeshwa kwenye sinema hivi karibuni, itakapoacha kuwa ya kisasa. Mkuu wa shirika la RSPCA Richard Hunter asema kwamba kutupa mbwa wa kisasa si jambo jipya. Jambo hili lilitukia katika miaka ya 1970 kwa mbwa wa Afghan; na katika miaka ya 1980, kwa mbwa wa kulinda kondoo wa Uingereza. Kwa kusikitisha imebidi mbwa wengi walioachwa wauawe. Shirika la RSPCA lahimiza watu wateue mbwa kwa kutegemea tabia na mtindo-maisha wa mwenye mbwa badala ya kufuatilia mtindo.

Watoto—Iweni Watendaji!

Ripoti moja katika gazeti la bidhaa la Ujerumani Test yasema kwamba ukosefu wa utendaji kwa watoto wanaotazama sana televisheni huathiri utambuzi, na kupatana kwa misuli, ukiongeza uwezekano wa kupatwa na aksidenti. Uchunguzi wa kimwili wa watoto wanaoingia shuleni katika Ujerumani ulifunua kwamba kufikia asilimia 30 walikuwa wanene kupita kiasi, kufikia asilimia 40 walikuwa na matatizo ya kupatana kwa misuli, na kufikia asilimia 60 walikuwa na matatizo ya mkao. Ili kuwafanya watoto wawe watendaji, walimu Wajerumani wa michezo, usalama, na wa mambo ya barabarani wamebuni mchezo wa sanduku wenye diski, mipira, na vitu vingine vya kuchezea ili watoto wafurahie huku wakiwa watendaji kimwili.

Wahasiriwa wa Biashara ya Ngono

Tangazo moja la biashara katika gazeti la habari la Ukrainia lasema hivi: “Wasichana: Wapaswa kuwa waseja na warembo sana. Wenye umri mchanga na warefu. Twawaalika mtumike mkiwa waonyeshaji mitindo, makarani, wacheza-dansi, wanasarakasi.” Hili ni tangazo la kawaida sana la wafanya-biashara wa ngono ili kuwaingiza kwenye ukahaba wanawake wachanga wasio na habari, laripoti The New York Times. Kila mwaka, maelfu ya wanawake wa Ukrainia na Urusi husafiri ng’ambo katika matumaini ya kuboresha hali yao ya kifedha. Lakini wanapowasili ng’ambo, “wakubwa” wao wahalifu huwanyang’anya vyeti vyao vya kusafiria na kulazimishwa kufanya kazi katika madanguro. Kukataa kwaweza kumaanisha kupigwa, kubakwa, na kuuawa kikatili. Mwanasaikolojia wa Ukrainia Lyudmilla Biryuk, ambaye ameshauri wanawake waliotoroka utumwa huo, asema: “Unataka kuwaambia watoto hawa kwamba jambo likionekana kuwa zuri sana, mara nyingi si zuri.”

Je, Tuelekeze Nuru Kwenye Goti ili Kupunguza Uchovu wa Safari?

Mpaka sasa, sikuzote imedhaniwa kwamba saa ya kiasili ya binadamu huongozwa na chembe zilizo katika retina jicho. Hata hivyo, uchunguzi mpya waonyesha kwamba wanadamu wana chembe zinazogundua kwa urahisi nuru kwenye sehemu nyingine za mwili mbali na jicho, laripoti gazeti la habari la Kifaransa Le Quotidien du médecin. Katika majaribio yaliyofanywa na watafiti Marekani, wajitoleaji fulani waliwekwa kwenye nuru nyangavu iliyopitishwa kwenye neli ya fumwale za kioo iliyofungwa nyuma ya goti, huku wengine ambao vilevile walikuwa na vifaa hivyo, hawakupitishiwa nuru. Hakuna mjitoleaji yeyote aliyejua kabisa ni nani aliyekuwa akipokea tiba ya nuru. Saa za mwili za asili zilipimwa kwa kutegemea hali joto ya mwili na viwango vya homoni ziitwazo melatonin. Pia likiripoti juu ya uchunguzi huo, International Herald Tribune lasema kwamba mifuatano inayotukia kwa muda wa saa 24 ya wale waliowekewa nuru “ilivurugwa kwa muda upatao saa tatu.” Bado haijajulikana namna jambo hili linavyotokea. Lakini matokeo yangeweza kutumiwa kwa kupendeza katika kutibu uchovu wa kusafiri kwa ndege, mshuko-moyo wa pindi kwa pindi, na matatizo ya usingizi.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki