Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 5/22 kur. 22-23
  • Chapa Yako Sahihi Yako

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Chapa Yako Sahihi Yako
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Jinsi ya Kujipatia Chapa
  • Asili ya Chapa
  • Namna Chapa Zionekanavyo
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1995
  • Watu Wawili Walioadhimisha Ukumbusho wa Siku ya Kuzaliwa
    Kumsikiliza Mwalimu Mkuu
  • Ufalme Unaofananishwa na Mti Mkubwa
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
  • Je, Karamu Zote Zinampendeza Mungu?
    Jifunze Kutoka kwa Mwalimu Mkuu
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 5/22 kur. 22-23

Chapa Yako Sahihi Yako

NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA TAIWAN

“WEKA chapa yako hapa,” asema karani nyuma ya kaunta katika posta yenye shughuli nyingi katika Taipei, Taiwan.

“Eti niweke chapa yangu?” natamka kwa kushangaa kabisa. “Lakini samahani, mimi mgeni hapa. Sina chapa—sijui wamaanisha nini,” najaribu kueleza. “Kwani siwezi kutia sahihi tu ya jina langu?”

“Ndiyo, waweza, lakini mbona usitengenezeshe chapa yako?” ajibu huyo karani wa posta. “Halafu hutasumbuliwa tena.”

Nikishangaa chapa ni nini na mahali jina layo la ajabu limetoka, nafanya uchunguzi. Kutokana na kamusi yangu najifunza kwamba chapa ni muhuri au stampu ya kugongwa rasmi au alama yayo na kwamba neno “chapa” latokana na neno la Kihindi chāp, kumaanisha “stampu.”[1]

Jinsi ya Kujipatia Chapa

Kwanza, nitahitaji jina la Kichina.a Kwa mtu mgeni jina hilo mara nyingi huwa ni utohozi wa msikiko wa jina lake. Kwa kielelezo, “John Smith” huenda likawa “Shih Mi Sse” au “Shih Yueh Han.” Au naweza kumwomba rafiki Mchina anisaidie kuchagua jina. Labda atachagua moja aonalo lanifaa, lakini huenda likawa tofauti sana na jina langu halisi.

Hatua ifuatayo ni kuzuru duka la mchonga-chapa. Huko mimi nachagua kipande cha kifaa cha mchongo kutokana na vifaa vya namna nyingi vilivyopo. Halafu msanii achonga zile herufi za jadi za jina langu la Kichina juu ya chapa yangu.

Sasa mimi niko tayari na kifaa cha kufanyia kazi au kushughulikiwa kwenye ofisi ya posta, benki, au mahali pengine pa shughuli rasmi. Kwa shughuli fulani za kisheria, alama zenye kuachwa na chapa yangu ni lazima zisajiliwe kwenye Ofisi ya Usajili wa Nyumbani. Ikiwa ni kwa ajili ya shirika fulani, basi itasajiliwa kwenye nyumba ya mahakama.

Lakini nashangaa ni jinsi gani karani hujua kama chapa ni ya kweli au si ya kweli. Ili kujua na kuona jinsi chapa hutengenezwa hasa, namtembelea Lin Rongdeh, mtengeneza-chapa katika jiji la Kaohsiung, katika Taiwan ya kusini. Kulingana na Bw. Lin, watu wengi huamini kwamba hata chapa zilizochongelewa jina lilelile moja na mtengeneza-chapa yuleyule mmoja hazifanani kabisa. Ili achunguze kama chapa ni ya kweli, karani wa ofisi angekunja nusu ya ile alama, kwa kawaida akifanya hivyo kutoka pembe ya juu kulia hadi chini kushoto, na kuiweka juu ya alama ambayo tayari imo katika faili. Nusu zote mbili zapasa kulingana kabisa.

“Ingawa hivyo,” asema Bw. Lin, akielekeza kidole kwenye mashine iliyo katika duka lake, “siku hizi kuna mashine zichongazo chapa kwa kusaidiwa na kompyuta. Chapa zichongwazo hivyo zingeweza kufanana halisi.”

“Ni ajabu!” mimi najibu. “Lakini wewe hutengenezaje chapa kwa kompyuta?”

“Kwanza, mimi hupanga maandishi au kuchora katika karatasi yenye kupenywa na nuru ya kadiri au nafanyiza plastiki ya herufi za lile jina kwa namna ifaayo chapa,” aeleza Bw. Lin. “Halafu naiweka juu ya kichwa kimoja kinachozunguka cha ile mashine, nayo yasoma jina hilo kwa nuru ya leza. Wakati uohuo, juu ya kichwa cha pili kinachozunguka naikandamiza chapa itakayochongwa, kisha kiparuzo kidogo sana kinachodhibitiwa na ile nuru ya leza chaparuza ile chapa kufanyiza herufi nilizochora.”

Kwa kuwa njia hii ni ya gharama kidogo sana, kwa kawaida kila mshirika wa familia hutengenezesha chapa. Chapa hizo huwekwa tayari ndani ya nyumba zitumiwe na mtu yeyote anayepokea barua zilizosajiliwa au vitu vingine ambavyo vingetaka sahihi katika mabara ya Magharibi.

Asili ya Chapa

Utumizi wa kwanza ujulikanao wa chapa katika China ulikuwa katika mwaka 1324 K.W.K.[2] Lakini zilianza kupendwa na watu wengi wakati wa nasaba ya Chou (1122-256 K.W.K.) Nyakati hizo za mapema, badala ya chapa kutumiwa kama sahihi zilikuwa mara nyingi zikibebwa kwenye ukanda wa kiunoni, kuonyesha daraja au cheo au kuonyesha tu kwamba mtu alikuwa wa kuheshimika. Chapa iliwakilisha zaidi cheo cha mtu kuliko kuwakilisha mtu mwenyewe hasa. Kama ilivyo mara nyingi leo, chapa ilipokezwa mtu aliyefuata kushika cheo baada ya kustaafu au kufa kwa ofisa. Kabaila alipotaka mazungumzo na maliki, angetoa chapa yake ya jiwe la jedi kuthibitisha utambulisho wake.

Karatasi ilipovumbuliwa, polepole ile chapa ilikuja kuwakilisha sahihi. Ikaja kutumiwa mara nyingi zaidi hata na watu wa kawaida. Leo, kila mtu ana chapa, hata mkaaji wa kigeni kama mimi, na ni kwa kutumia chapa tu kwamba mshughulikiano wowote unaohusu sahihi ya mtu waweza kukamilishwa. Ingawa kirasmi sahihi ya kuandikwa yaweza pia kutumiwa, kwa watu walio wengi chapa ndiyo huhalalisha mambo. Zoea hili limeenea sehemu iliyo kubwa zaidi ya nchi za Mashariki, hivi kwamba Wajapani na Wakorea pia hutumia chapa.

Namna Chapa Zionekanavyo

Chapa yaweza kuwa ya mraba, ya mstatili, ya umbo-yai, au ya mviringo, au yaweza kuwa na maumbo mengine mengi sana.[3] Yaweza kuwa ndogo kufikia milimeta 3 kwa kipenyo au kubwa kufikia sentimeta 15 za mraba. Chapa yaweza kufanyizwa kwa jiwe la jedi, jiwesabuni, pembe ya mnyama, mwanzi, shaba-nyeupe, mti, au plastiki, ikitegemea matakwa na uwezo wa mnunuzi na pia ni kwa kusudi gani chapa itatumiwa. Ikiwa chapa itatumiwa mara haba sana na kwa mishughulikiano isiyo ya maana sana, mti au plastiki huenda vikatosha. Lakini ikiwa mwenyewe apanga kuitumia muda wote wa maisha yake, basi aweza kuchagua kitu chenye thamani na chenye kuvutia zaidi.

Kwa kielelezo, chapa rasmi ya Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania, tawi la Taiwan, imechongwa juu ya kipande cha ubao mgumu wenye urefu wa sentimeta 7.5, upana wa sentimeta 5, na unene wa sentimeta 2.5. Je! si hiyo ni “sahihi” ya kutatiza kwelikweli? Mara nyingi huenda hata karatasi yenyewe ya kutiwa sahihi ikawa ya ukubwa uohuo!

Chapa zilizo za kawaida zaidi ni vipande visivyochorwa kitu vya kifaa kilichochaguliwa kikiwa na jina lililochongwa kwa herufi za mwandiko wa Kichina sehemu ya chini iliyo ya ubapa. Mchongo juu ya shina au sehemu ya juu huongeza umaridadi na thamani ya ile chapa. Chapa fulani ni kazi za sanaa yenye madoido sana. (Ona picha katika ukurasa wa 23.) Kwa kawaida mwenyewe ataichukua chapa ikiwa ama katika mfuko wa ngozi ama katika kisanduku chenye kigawanyo kilicho na lahamu ya wino mwekundu kwenye mwisho mmoja. Nyakati fulani wenzi wawili waliofunga ndoa karibuni huwa na chapa zilizochongwa juu ya vipande viwili vilivyotolewa au kukatwa katika shina lilelile moja, tena zikiwa na maumbo yanayofanana—wazo la kimahaba hivi. Au kama vile ilivyo kuhusu zile chapa maridadi za jiwe jedi la manjano katika ukurasa wa 23, zile chapa tatu na minyororo zilichongwa zote pamoja kutokana na kipande kimoja cha jiwe.

Ikiisha kuchongwa, chapa huwa ndiyo sahihi halali ya mwenyewe au mwenye cheo, kwa hiyo ni lazima itunzwe sana sana. Ni lazima ilindwe isiibwe, kwa kuwa mwizi angeweza kuitumia kutia sahihi bandia katika hati, kutoa fedha benki, kupata fedha za hundi au mikataba kwa kuzitia sahihi, na kadhalika.

Nifanye nini nikipoteza chapa yangu? Kwanza, ni lazima niarifu ofisi ya posta, benki, na mashirika mengine yahusikayo ili yaweze kufuta chapa yangu. Bila shaka, ni lazima nifanye hivyo mara hiyo ili kuzuia utumizi usio halali wa chapa yangu. Halafu ni lazima chapa mpya itengenezwe. Ikiwa hiyo itachukua mahali pa chapa iliyosajiliwa, ni lazima nipite katika zile hatua za kuisajili tena, na ofisi zihusikazo ni lazima ziarifiwe juu ya chapa yangu mpya. Kwa hiyo, je, wafikiri kwamba kupoteza kadi ya kuazimia vitu ndilo jambo gumu zaidi kushughulikiwa? Mtu mwenye hekima ndiye hulinda chapa yake isipotee au kuibwa!

Katika nchi za Magharibi, ukusanyaji-stampu ni kipendezi cha watu wengi. Katika China watu wengi hukusanya chapa au alama ya chapa mbalimbali, halafu vitabu maalumu huchapishwa. Chapa fulani ni maridadi sana, kwa kuwa mtindo wa herufi na umbo, rangi, na muundo wa ile chapa hujumlika kutokeza sura ya kupendeza sana. Chapa ambazo wakati mmoja zilikuwa mali ya watu mashuhuri au wenye cheo au chapa za ukale ulio maarufu mara nyingi huwekwa katika mikusanyiko ya majumba ya hifadhi.

Kwa ulinganisho, mtu mmoja katika nchi za Magharibi achukuapo kalamu kutia sahihi hati fulani rasmi, labda kuna mtu fulani katika bara fulani la Mashariki anayetoa chapa yake pia, kuikandamiza mara chache juu ya kifinyo chenye rangi ya wino mwekundu, na kugongesha kwa uangalifu “sahihi” yake juu ya ule mstari wa vitonetone.

Lo, desturi tofautitofauti hufanya maisha yapendeze kama nini!

[Maelezo ya Chini]

a Ingawa chapa zenye majina ya lugha nyinginezo zaweza kutengenezwa, umaridadi wa chapa hutegemea ubuni wa mwandiko wayo wa Kichina.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kuzunguka mwendo- wa-saa: Alama ya chapa yenye wino mwekundu; chapa zenye mnyororo, zote zikiwa zimechongwa kutokana na kipande kimoja cha jiwe la jedi; mtengeneza- chapa akichonga umbo fulani; chapa iliyoandikwa shairi

Chapa kwa namna ya kasa

[Hisani]

Chapa: National Palace Museum, Taipei, Taiwan

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki