Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 6/8 kur. 11-13
  • Nilijifunza Kuchukia Kile Nilichokuwa Nimependa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nilijifunza Kuchukia Kile Nilichokuwa Nimependa
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mpiganaji wa Mitaani
  • Mchezo Mkatili
  • Jinsi Nilivyojifunza Kuchukia Ndondi
  • Pendeleo Kubwa Zaidi
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1982
  • Nilipenda Jeuri
    Amkeni!—2012
  • Niliacha Kupiga Watu Barabarani Nikawa Mhudumu Mkristo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
  • Biblia Inabadili Maisha
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2010
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 6/8 kur. 11-13

Nilijifunza Kuchukia Kile Nilichokuwa Nimependa

Kupigana kulikuwa maisha yangu. Nilifurahia kuweza kumpiga ngumi mpinzani wangu kwa nguvu zangu zote na kumwona akianguka miguuni pangu. Nilisisimka kusimama kwenye jukwaa la ndondi na kumsikia mtangazaji akitaja jina langu kwa sauti nikiwa mshindi wa shindano hilo. Nilipenda ndondi! Hata hivyo, sasa wazo lenyewe la jeuri huniudhi mimi. Nimejifunza kuchukia jambo ambalo sasa naliita mchezo wenye jeuri wa ndondi.

KATIKA 1944, nilipokuwa na miaka saba, nilikuwa nikiishi Lares, Puerto Riko, nilikozaliwa. Ndipo nilipopata shtuko baya sana la kupoteza mama yangu katika kifo. Yeye alikufa kwa kansa alipokuwa na umri wa miaka 32. Uchungu huo ulishindwa kuvumilika muda mchache baadaye, nilipokuja kutoka shuleni na kumwona mwanamke akiketi kwenye paja la baba yangu. Akawa mama yangu wa kambo.

Akitambua kutompendelea kwake, mama yangu huyo wa kambo alinitendea mabaya. Basi nikatoroka nyumbani. Nilitorokea kwenye lori lililopakiwa makaa-mawe na machungwa na nikalala. Ulikuwa mshangao kama nini kujipata mwenyewe nikiwa kwenye jiji la San Juan, upande ule mwingine wa kisiwa!

Mpiganaji wa Mitaani

Niliishi kwenye mitaa ya San Juan kwa miezi minane. Vijana wengine walikuwa wakiniudhi daima. Hivyo nikaamua kwamba nitapigana ili niishi. Baada ya miezi minane polisi walinipata na wakanipeleka nyumbani. Sikuzoea wazo la kuishi na mama wa kambo nami nikatumia wakati wangu wote mitaani. Karibu kila siku, nilijiingiza kwenye pigano. Nilipofika umri wa miaka kumi, nilitoroka tena.

Baada ya majuma machache, polisi walinichukua tena. Wakati huu nilikataa kuwaambia jina langu na nilikotoka. Baada ya kushindwa kupata familia yangu, walinipeleka kwenye makao ya mayatima ya serikali katika jiji la Guaynabo. Huko ndiko nilikovalia glavu zangu za kwanza za ndondi. Ilikuwa huko pia kwamba kwa mara ya kwanza maishani mwangu, niliona jina Yehova kwenye ubao. Niliuliza juu yalo, nami nikaambiwa kwamba Yehova alikuwa Mungu wa Wayahudi. Sikusahau jina hilo kamwe.

Nilipofika umri wa miaka 15, nilitoka kwenye makao ya mayatima, na sikurudi tena kamwe. Ili nijitegemeze, nilianza kuuza magazeti. Hata hivyo, kila barabara ilikuwa ni eneo la muuzaji-magazeti hususa. Kulikuwa na namna moja tu ya kuanzisha njia yangu: kupigana! Na nilipigana.

Miaka miwili baadaye nilijiunga na Jeshi la Marekani nami nikapokea mazoezi ya msingi katika Arkansas, Marekani. Upesi nikawa mshiriki wa timu ya ndondi. Kisha nikahamishwa kwenda kwenye kikosi cha Utumishi wa Pekee. Wajibu wangu ulikuwa katika chumba cha mazoezi, na sajini aliyekuwa mkubwa wangu alikuwa mwalimu wa ndondi.

Mchezo Mkatili

Nilipata mazoezi ya jinsi ya kutumia ngumi zangu ili kuumiza wapinzani wangu. Nilizoezwa kupuuza urafiki katika jukwaa la ndondi. Kengele ilipolia, rafiki akaja kuwa adui wa kupigwa na hasa kushindwa.

Nilitaka kubaki kwenye jeshi, lakini sajini wangu aliniambia: “Staafu jeshini upesi uwezavyo. Uwe bondia wa kulipwa, na kwa miaka michache, nitakuona kwenye televisheni ukipigana ndondi katika jumba la mchezo la Madison Square Garden katika New York City.” Ilikuwa vigumu kuamini hilo! Mimi—mvulana maskini asiye na makao—niwe bondia mashuhuri?

Baada ya miaka miwili niliacha jeshi nami nikarudi Puerto Riko. Siku moja katika 1956, niliona tangazo la shindano la ndondi la watu wasiolipwa, la Golden Gloves. Niliingia shindano hilo nami nikawa bingwa katika uzani wa welter wa Golden Gloves katika Puerto Riko. Kisha nikasafirishwa kwa ndege hadi New York City ili nishiriki mashindano ya kitaifa ya Golden Gloves. Nilipigana hadi nusu-fainali, lakini sikuweza kupata ushindi wa ubingwa. Hata hivyo, upesi wasimamizi na wakufunzi waliotazamia kunichukua wakaanza kunitolea ahadi. Kwa hiyo nikakubali mwaliko wa kukaa New York City na kujizoeza kwa ajili ya kulipwa.

Katika 1958, nikawa bondia wa kulipwa. Na msimamizi wangu alisema kweli. Katika 1961, miaka mitano baada ya kuacha jeshi, nilionekana katika televisheni ya taifa, nikipigana ndondi katika Madison Square Garden. Mapigano yangu mengi yalifanyika katika jumba hilo maarufu la michezo.

Ngumi zangu zilimaliza kazi-maisha za mabondia kadhaa. Bondia mmoja kutoka Mexico alipoteza uwezo wake wa kuona kwa sababu ya ngumi zangu katili. Pigano jingine ambalo lilikuja kuwa mzigo mkubwa kwa dhamiri yangu lilikuwa lile shindano na bingwa wa uzani wa kati kutoka Jamhuri ya Dominika. Kabla ya pigano alizusha fujo kwamba nilikuwa mzito kwa kilo 0.5 kuliko yeye. Mwelekeo wake ukanikasirisha sana. Sikuwa nimepata kulalamika kamwe mpinzani alipokuwa mzito kuniliko kwa uzani mdogo hivyo. Nilimwambia: “Basi, jitayarishe kwa kuwa usiku huu nitakuua!” Nilipopanda jukwaa, gazeti moja liliandika kwamba “sura yangu ilikuwa ya kishetani.”[1] Kwa muda unaopungua dakika mbili, mtu huyo alianguka sakafuni akiwa amekosa fahamu. Sikio lake la ndani liliharibiwa vibaya hivi kwamba hakupigana ndondi tena kamwe.

Jinsi Nilivyojifunza Kuchukia Ndondi

Kujulikana kwangu sana kulivutia uangalifu wa urafiki wa wachezaji wengine na wanamuziki. Wakati mmoja hata Joe Louis, aliyekuwa bingwa wa uzani mzito, alitegemeza mojapo mapigano yangu. Nilisafiri sana, nikawa na magari mazuri, na nikafurahia vitu vingine vya kimwili. Hata hivyo, kama ilivyo na mabondia wengi, mafanikio yangu yalikuwa ya muda mfupi. Katika 1963, niliumizwa vibaya katika mapigano kadhaa nami singeweza kupigana tena.

Kufikia wakati huu nilisoma makala ya gazeti moja la habari kwamba bondia mashuhuri alikuja kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Baada ya kusoma makala hiyo, kwa sababu fulani, nilibaki na hisi ya kwamba dini ya Mashahidi wa Yehova ilikuwa ya matajiri tu.

Miaka michache iliyofuata, nilianza kupata matatizo ya kitiba. Nilipatwa pia na mshuko mbaya sana wa moyo. Pindi moja nilipokuwa nimeshuka moyo sana hivyo, nilijiwekea bunduki moyoni na nikajilipua. Risasi iligeuzwa upande mwingine na ubavu wangu, ikiokoa uhai wangu. Nilikuwa hai, lakini asiye na furaha hata kidogo na mgonjwa sana. Sikuwa na pesa tena, wala umaarufu, wala hakukuwa kupigana ndondi tena!

Kisha, siku moja mke wangu, Doris, aliniambia kuwa alikuwa akijifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova naye alitaka kuhudhuria mikutano kwenye Jumba la Ufalme. “Sijui, Doris,” nikasema. “Sisi ni watu maskini, na Mashahidi wa Yehova ni watu matajiri na wa maana.” Aliniambia hilo halikuwa kweli na kwamba Shahidi aliyekuwa anajifunza pamoja naye alikuwa anaishi kwenye ujirani wetu. Kwa hiyo nikakubali uamuzi wake wa kuhudhuria mikutano. Katika pindi moja nilipokuwa nikimngoja nje ya Jumba la Ufalme, Shahidi mmoja alinialika niingie. Nilikuwa nimevalia nguo chafu za kazini, lakini alinisihi-sihi. Nilikaribishwa ijapokuwa sura yangu. Hali ya urafiki ilinipendeza zaidi.

Upesi nikaanza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi. Nilijifunza kwamba Yehova si Mungu wa Wayahudi tu, kama vile nilivyokuwa nimeambiwa, bali kwamba yeye ni Mungu pekee wa kweli, Mweza Yote, Muumba wa vitu vyote. Nilijifunza pia kwamba Yehova Mungu huchukia jeuri. Kwenye Zaburi 11:5 (Habari Njema kwa Watu Wote) Biblia yasema: “Mwenyezi-Mungu huwapima waadilifu na waovu; huwachukia kabisa watu wakatili.” Basi nikaacha kabisa kila kitu kilichohusiana na ndondi. Kwanza nilijua jinsi ulivyokuwa mchezo wa jeuri. Baada ya kujifunza jinsi Mungu anavyouona, sikuwa na shaka kwamba ndondi ulikuwa mchezo mwovu sana na wenye jeuri. Ndiyo, nilijifunza kuchukia mchezo niliokuwa nimeupenda.

Pendeleo Kubwa Zaidi

Katika 1970, nilifanya uamuzi wa kuweka maisha yangu wakfu kwa Yehova. Doris nami tukabatizwa Oktoba ya mwaka huo. Tangu wakati huo nimefurahia pendeleo la kuwahubiria wengine. Nikiwa mhubiri wa wakati wote, nimekuwa na ushiriki wa kusaidia watu wapatao 40 kuwa waabudu wa Yehova.

Kwa kusikitisha, bado naumia kwa sababu ya majeraha niliyopata wakati wa miaka yangu ya jeuri. Nilipata mamia ya ngumi kichwani mwangu, ikisababisha kasoro za muda wote kwa ubongo wangu. Nina matatizo ya kuwa na kumbukumbu fupi na sehemu ya sikio langu la ndani, ikiathiri usawaziko wangu. Nikizungusha kichwa changu harakaharaka, naweza kuhisi kisuunzi. Pia, napaswa kutumia dawa kwa ukawaida kwa ajili ya matatizo yangu ya mshuko wa moyo. Hata hivyo, Wakristo wenzangu wanaelewa, nao wananisaidia kukabiliana na hali. Namshukuru Yehova sana kwa kunipa nguvu ya kushiriki kikawaida kutangaza jina na makusudi yake kwa wengine.

Nafurahia pendeleo kubwa zaidi ya yote—nalo ni, kuwa na uhusiano wa kibinafsi pamoja na Mungu Mweza Yote, Yehova. Nilipokuwa bondia, nilihuzunisha moyo wa Yehova na kila pigano. Sasa naweza kufanya moyo wake ufurahi. Nahisi kana kwamba alikuwa ananizungumzia binafsi anaposema: “Mwanangu, uwe na hekima na kunifurahisha moyo wangu; ili nipate kumjibu anilaumuye.”—Mithali 27:11.

Karibuni Yehova atakomesha kazi za Shetani, kutia ndani jeuri yote na wale wanaoitegemeza. Namshukuru Yehova kama nini kwa kunifundisha si kupenda yaliyo mazuri tu bali pia kuchukia yaliyo mabaya! Hayo yatia ndani kuchukia mchezo wa jeuri wa ndondi. (Zaburi 97:10)—Kama ilivyosimuliwa na Obdulio Nuñez.

[Picha katika ukurasa wa 13]

Obdulio Nuñez

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki