Krakatoa—Maangamizi Yaamkia Tena
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA INDONESIA
UFUO WA KARITA waonekana kuwa mahali penye amani. Hakuna chochote kinachodokeza masumbuko ya wakati uliopita. Huonekana kama kimbilio lenye utulivu katika Java, karibu kilometa 150 magharibi mwa jiji la Djakarta lililopo katika Mlangobahari wa Sunda, linalogawanya visiwa vya Indonesia vya Java na Sumatra. Umati na msongamano wa magari wa Djakarta waonekana mbali sana, na hali ya hewa imetulia na yenye kustarehesha. Nyumba za wenyeji zimesimama wima kando ya ufuo wa maji.[1]
Lakini jina hilo—Ufuo wa Karita—halionyeshi historia. “Karita” ni neno la Kiindonesia linalomaanisha “hadithi,” na mahali hapa, kama ilivyo na nyinginezo katika eneo hilo, ni mahali panapohusu hadithi za majonzi—zote zikitoka kwenye tukio moja lililolipuka kwa jeuri katika eneo hili na kufanya yahisiwe ulimwenguni pote.[2]
Ukitazama kule maji ya rangi ya samawati, yaliyotulia ya Mlangobahari wa Sunda kutoka Ufuo wa Karita, unaweza kuona kikundi cha visiwa vidogo. Kutoka kimojapo—Anak Krakatau (Mtoto wa Krakatoa)—moshi bado hufuka. Jina hilo lenye kuogofya linakumbusha “baba” yake mkali, Mlima Krakatoa, ambao ulipotelea chini ya maji ya Mlangobahari wa Sunda baada ya kulipuka wakati wa mlipuko mkubwa wa historia yote ya kisasa mnamo Agosti 27, 1883.[3]
Tukiwa kikundi cha watu 17 tuliondoka Ufuo wa Karita kutembelea kikundi cha kisiwa hicho. Tulikodi mashua ili tusafiri kilometa 40 kupitia mlangobahari huo. Kwa kuwa Java ilianza kufifia kwa mbali kwenye umande, nilitafakari jeuri ya wakati uliopita ya Krakatoa.
Historia ya Krakatoa Yenye Jeuri
Leo, Krakatoa hurejezea kikundi cha visiwa vinne: Rakata, Panjang, na Sertung, vilivyoanzisha Anak Krakatau hivi karibuni kikiwa katikati. Rakata kilikuwa kitovu cha utendaji wa volkeno. Kilikua kwa ukubwa sana karne zilizopita wakati vilele viwili vya volkeno vilipojitokeza kutoka karibu na bahari na polepole vikaungana na Rakata vikafanyiza Mlima Krakatoa wenye kuogofya sana. Kwa uzuri, yaonekana kwamba utendaji wote huu uliacha kisiwa hicho ukiwa.[4]
Ijapokuwa kuna ripoti za mlipuko wa kiasi katika 1680 ambao uliharibu mimea yote, kufikia 1883, Krakatoa ilijawa na usitawi wa mimea ya hari. Lakini kisiwa hicho kililipuka kwa sauti yenye ngurumo mnamo Mei 20, 1883, kikitokeza milipuko ya vijiwe vidogo, jivu, na mawingu ya mvuke. Mlipuko huo uliendelea hadi Juni na Julai. Kufikia katikati ya Agosti, mashimo yote matatu ya volkeno yalikuwa yanatokeza mivuke mingi sana, mavumbi, vijiwe vidogo, na majivu. Meli zilizokuwa zikipita kwenye mlangobahari zilihitaji kupitia mawe ya volkeno yaliyoambatana, ilhali jivu lilijaa kwenye orofa zazo.[5]
Tuliposafiri kupitia maji hayohayo, kitu pekee kilichokuwa kikirukia sehemu ya juu kilikuwa ni samaki panzi la bahari ambaye hakuweza kuruka wakati wote kwenye mashua. Ilikuwa vigumu kuwazia wakati ambapo huzuni nyingi na uharibifu ulikuwa kwenye maji haya tulivu. Lakini uharibifu mkubwa ulikuwa ndio unaanza tu.
Mwisho ulifika katika Agosti 26, wakati mlipuko baada ya mlipuko uliongezeka kuwa uvumi wenye kuendelea. Hatimaye, mnamo Agosti 27, milipuko mikubwa saa—11:30, 12:44, 4:02, na 4:52 asubuhi—ilitikisa volkeno.[6] Mlipuko wa tatu ukiwa mlipuko mkubwa zaidi katika historia ya kisasa, mkubwa sana kuliko ule uliokuwa Hiroshima na milipuko yoyote ya kiatomi. Kwa kweli, watu fulani husema kwamba ilikuwa na nguvu ya bomu za haidrojeni 100,000.[7] Ulisikika katika Australia, Myanmar, na Rodrigues, kisiwa kilichoko umbali wa kilometa 5,000 katika Bahari ya Hindi. Mawimbi ya kanieneo katika mzunguko wa hali-hewa ilizunguka dunia mara saba na nusu kabla ya kuishilia mbali. Ng’ambo ile ya Lango-Bahari la Uingereza mashua zilisukwasukwa na yale mawimbi ya bahari yaliyosababishwa na mlipuko huo.[8]
Wingu la jivu liliinuka hadi kiwango kilichokadiriwa kuwa kilometa 80 juu angani na kufunika eneo kubwa. Giza lilijaa eneo lote hilo kwa siku mbili na nusu.[9] The New York Times mnamo Agosti 30, 1883, likinukuu kampuni ya Lloyd ya London, lilionya meli zote ziepuke Mlangobahari wa Sunda. Ilikuwa hatari kusafiri baharini kwa sababu minara yote ya taa “haingeweza kuonekana.” Mavumbi ya volkeno yalifika juu angani, ambapo mawimbi ya hewa yaliyasambaza duniani kwa majuma mawili. Tokeo moja lilikuwa mwaka mmoja au miwili ya miinuko ya jua miangavu, mishuko-jua, mizingo ya jua, na mambo mengine ya ajabu ya anga.[10]
Uharibifu wa Uhai
Mlipuko huo ulisababisha mawimbi makubwa ya bahari, yaitwayo mikondo ya mawimbi, inayofika urefu wa meta 15 katika bahari ya wazi. Wimbi moja lilipofikia ghuba lililoendelea kuwa jembamba katika mji wa Java wa Merak, ukuta wenye kuendelea wa maji unaaminiwa kuwa ulifikia urefu wa meta 40. Ulianguka kwa kishindo kwenye mji, ukiuangamiza kabisa. Miji mingine katika pwani za Java na Sumatra zilipatwa na msiba huohuo. Watu wapatao 37,000 walizama kwa mikondo ya mawimbi siku hiyo. Meli moja ya vita ilipatikana imekwama kilometa 3 kwenye bara![11]
Ni nini hasa, kilichokuwa kimetokea? Krakatoa yenye kuogofya ilitoa takataka za kilometa 20 za mraba, zikichuja kila kitu kwenye shimo layo kubwa la chini. Shimo hilo tupu liliporomoka, na hivyo likitumbukiza theluthi mbili ya kisiwa baharini. Bara lililokuwa limesimama meta 300 juu ya usawa wa bahari lilizama hadi meta 300 chini ya usawa wa bahari. Ni nusu ya jiwe la volkeno lililo refu zaidi tu, Rakata, lililobaki.[12]
Kilichobakia Rakata, pamoja na visiwa vya Panjang na Sertung, kilifunikwa na jivu tupu, lililo moto. Uhai wote waaminiwa kuwa uliharibiwa. Uchunguzi ulipofanywa miezi tisa baadaye, ni buibui moja mdogo tu alipatikana akifuma utando.[13] Kwa miaka iliyofuata, Krakatoa ilikuja kuwa jambo la utafiti wa wanasayansi walipoandikisha hati ya kurudi kwa uhai kwa visiwa hivyo vitatu. Bara la karibu zaidi ambalo uhai ungerudi lilikuwa kilometa 40.[14]
Miaka ipatayo karibu 60 iliyopita, jiwe jipya la volkeno lilijitokeza nje ya bahari katikati ya visiwa vitatu. Mtoto huyu wa Krakatoa (Anak Krakatau) aliendelea kulipuka na kukua kadiri miaka ilivyoendelea kupita. Leo yu karibu meta 200 kwa urefu, kilometa 2 kwa upana—na mwenye nguvu sana![15] Ni mtoto huyu mwenye hasira kali tuliyemzuru kwanza.
Kutembelea Mtoto wa Krakatoa na Majirani
Tuliendelea hadi kwenye ukingo wa Anak Krakatau, tukiwa na ugumu fulani tulipanda kiholelaholela kutoka mashuani kwenye changarawe nyeusi nyangavu ya pwani. Safari ya mashariki ya kisiwa ilijawa na pori la miti-kasuarina, mingine ikiwa na mashina yanayofikia sentimeta 60 kipenyo. Kulikuwako na aina nyinginezo zenye kustaajabisha za mimea na maua. Aina mbalimbali za ndege ziliruka kwa wepesi kupitia miti, na popo walining’inia kifudifudi kwenye mti wa tini. Mijusi walikimbia harakaharaka chini ya mimea. Sehemu ya msitu ya kisiwa hicho ilikuwa na wadudu na vipepeo.
Hata hivyo, kuzaliwa upya kwa Anak Krakatau kumezuiliwa na milipuko mingi kwa miaka; mimea inafunika asilimia 5 tu ya kisiwa hicho.[16] Tulipojikokota kupitia majivu meusi ti yenye vina kuelekea kileleta cha volkeno, tuliona kwamba tayari namna mbalimbali za mimea zilikuwa zikianza kukalia mitelemko hii tambarare, ikitambaa juu hadi mlipuko mwingine utakapoiteremsha chini tena.
Mvuke ulikuwa unavuja kutoka kwenye mipasuko ya upande wa volkeno. Tukitazama chini kwenye mioto itokayo kandokando ya shimo la volkeno, tuliweza kujionea wenyewe msukosuko wa mtoto huyu mtundu. Hakukuwa vigumu kuwazia tabaka za miamba ya tektoniki zikisyagwa pamoja polepole chini ya Mlangobahari wa Sunda, zikilifanya eneo hili kuwa lenye nguvu ya volkeno ulimwenguni.[17]
Kupandwa upya kwa misitu kumeendelea kwenye visiwa vya karibu vya Sertung, Rakata, na Panjang, vinavyoizunguka Anak Krakatau. Hivyo havijalipuka tangu mlipuko usiosahaulika wa 1883. Kwa karibu zaidi ya karne moja, vimepona na kufanywa upya na kugeuzwa tena kuwa visiwa vyenye amani vyenye kustarehesha vikiwa na ukuzi wa hari. Kwa kweli, katika miaka 20 hadi 40 baada ya mlipuko, visiwa hivi tayari vilikuwa vinapandwa misitu upya na kukaliwa na namna-namna za ndege, mijusi-kafiri, nyoka, popo, na wadudu. Tangu wakati huo, uhai umeendelea kukua kwa haraka.[18]
Je! aina fulani za maisha ziliokoka joto kali zaidi na majivu yenye kunyesha ya Krakatoa? Wastadi wengi wa mimea na wa wanyama wanasadiki kwamba aina fulani za maisha hazikuokoka, ijapokuwa wengine wanatilia shaka uamuzi huo. Kwa ujumla wanafikiria kwamba ndege wenye kubeba mbegu na takataka kutoka mito yenye kufurika katika Sumatra na Java yamechangia kurudi kwa vitu vilivyo hai.[19]
Mashua yetu ilipoelekea nje ya maji tulivu ya rangi samawati katika mzunguko wa visiwa kwa ajili ya safari yetu ya kurudi Java, sikukosa kutafakari uwezo wa sayari yetu wa kujirekebisha. Dunia ikiachwa, yaweza kurudisha ubora wayo. Niliona hilo kuwa wazo lenye kufariji sana, hasa kwa kuona kweli mwanadamu anasababisha msiba wa sehemu za tufeni pote za sayari hii hivi sasa. Leo, mwanadamu anasababisha uharibifu wa polepole unaoleta ule msiba Mkubwa Sana wa Krakatoa. Lakini akikoma kusababisha msiba duniani—na atakoma—dunia itapona. Tulipokuwa tukipiga makasia kupitia mawimbi ya Mlangobahari wa Sunda yenye rangi ya samawati ya anga safi, nilitazama nyuma kwenye visiwa vya rangi ya chani-kiwiti vikiwa hai tena baada ya kuangamizwa kwa Krakatoa. Ndiyo, dunia yaweza kupona. Litakuwa jambo lenye kupendeza kama nini kuona jambo hilo likitendeka tufeni pote!—Isaya 35:1-7; Ufunuo 11:18.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Anak Krakatau kwa mbali