Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 6/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Makasisi Wagoni-Jinsia-Moja
  • Aksidenti na Damu Yenye Viini vya UKIMWI
  • Kansa—Kombora Lililotegewa Wakati wa Kulipuka
  • Msaada kwa Wasiopata Usingizi wa Kutosha
  • Lulu za Kometi
  • Jeuri Dhidi ya Wanawake
  • Maelfu ya Mimea Yapuuzwa
  • Uwezo Mdogo Juu ya Maisha Zao Wenyewe
  • Tasbihi ya Video ya Kuweka Mfukoni
  • Mahali Baridi Zaidi Katika Ulimwengu Wote Mzima
  • Thamani ya Kuangalia Nje Dirishani
  • Vibaramwezi vya Kuongeza Akili
  • Uharamia wa Baharini Waongezeka
  • Nyotamkia Yagonga Sumbula!
    Amkeni!—1997
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1995
  • Ni Nini Kilicho Nyuma ya Sayari?
    Amkeni!—1999
  • Vimondo Hutoka Wapi?
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 6/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Makasisi Wagoni-Jinsia-Moja

Kwa miaka kadhaa baraza la Kanisa la Lutheri la Kievanjeli la Hannover, Ujerumani, limeruhusu wagoni-jinsia-moja watende kazi wakiwa washirika wa makasisi maadamu hawana mwenzi wa ugoni-jinsia-moja. Lakini kulingana na kichapo The Week in Germany, kuondolewa kwa mgoni-jinsia-moja aliye mtendaji ili asiwe katika wajibu wake mbalimbali wa kikasisi zaidi ya miaka mitatu iliyopita kumetokeza ubishi mwingi. Kulingana na The Week, wenye mamlaka katika Hannover hivi majuzi wameidhinisha dokezo lenye kutaarifu kwamba “mapasta na waandamani wao ambao ‘huishi katika uenzi wa ugoni-jinsia-moja’ wangestahili kuajiriwa kazi katika kanisa, kutia na katika upasta.”

Aksidenti na Damu Yenye Viini vya UKIMWI

Hivi majuzi Wizara ya Afya na Masilahi ya Japani iliomba hospitali zipeleke ripoti juu ya ni mara ngapi wafanyakazi wa kitiba hupatwa na aksidenti zinazohusiana na damu iliyoambukizwa virusi ya HIV. Lililotakwa kujulikana hasa ni aksidenti zilizotukia miaka kumi iliyopita. Kulingana na The Daily Yomiuri, zile hospitali 276 zilizojibu ziliripoti kwamba “jumla ya aksidenti kutokana na sindano ilikuwa 12,914, kukiwa na visa 2,997 vya kugusana na damu kiaksidenti.” Kati ya visa hivi, zaidi ya mia moja vilihusu damu yenye virusi ya HIV. Majeruhi wote wa aksidenti hizi wamepimwa wakaonekana hawana HIV, ile virusi isababishayo UKIMWI.

Kansa—Kombora Lililotegewa Wakati wa Kulipuka

Uchunguzi mmoja katika Australia uliofanywa na Wakf wa Kusaidia Wenye Matatizo ya Ngozi na Kansa katika Australia lilifunua kwamba kansa ya ngozi sasa ndiyo namna ya kansa ipatikanayo kwa wingi zaidi katika nchi hiyo. Yakadiriwa kwamba kila mwaka Waaustralia wapatao 1,000 hufa kutokana na kansa ya ngozi. Kulingana na The Daily Telegraph Mirror la Sydney, Australia, uchunguzi huo wasema kwamba “ule mtazamo wa kutojali ambao Waaustralia wengi wamekuwa nao wakati uliopita wa kutojikinga na jua umefanyiza kombora la kansa lililotegewa wakati wa kulipuka.” Walio wengi wa majeruhi wa leo ndio waliokuwa matineja wa miaka ya 1960, 1970, na 1980 waliokuwa wakijilaza ili watandikwe sana na jua.

Msaada kwa Wasiopata Usingizi wa Kutosha

Watafiti katika Shule ya Tiba ya Harvard wamekusanya orodha ya madokezo kwa ajili ya watu wenye matatizo mazito ya kulala usingizi. Kulingana na The Harvard Mental Health Letter, kikundi cha wagonjwa waliokuwa wamehitaji karibu dakika 80 ili kulala usingizi walipata maendeleo makubwa. Baada ya kujaribu utibabu huo kwa majuma kadhaa, “iliwachukua wastani wa dakika kumi na tisa tu ili kulala usingizi (punguzo la asilimia 75),” ndivyo yataarifu barua hiyo. Njia zilizopendekezwa zatia ndani hizi: Epuka kutumia muda wa zaidi ya saa saba kitandani; epuka kukaa ukiwa umelala kitandani muda wa zaidi ya saa moja kupita wastani wako wa wakati wa kulala; amka wakati uleule kila siku, kutia na miisho-juma; enda kulala wakati tu uhisipo usingizi; na usipolala usingizi katika muda wa dakika 20 baada ya kwenda kitandani, inuka ufanye jambo fulani la kustarehesha mpaka uhisi ukitaka kulala tena.

Lulu za Kometi

Kikundi cha vipande zaidi ya 20 vya kometi (nyota-mkia), ambavyo katika picha za darubini huonekana kama mkufu wa lulu, ziko katika mstari wa kugongana na sayari Sumbula, laripoti The Washington Post. Vipande vya kometi, ambavyo baadhi yavyo huenda vikawa vya kilometa tatu kutoka upande hadi upande, kwa ujumla huitwa Shoemaker-Levy 9, kupatana na jina la waliogundua kometi hiyo. Wanasayansi waamini kwamba ule mkufu wa kometi ulifanyizwa wakati kometi iliyo pekee ilipopasuliwa vipande-vipande na nguvu za uvutano ilipokuwa ikiruka karibu na Sumbula hivi majuzi. Ile migongano ya vipande vya kometi, ambayo ni tukio la mara chache kwa watazamaji wa kibinadamu, itatukia muda wa siku kadhaa mwishoni mwa Julai 1994. Ingawa mgongano utatokea upande wa nyuma wa Sumbula, mimweko ya nuru itakayotokea huenda ikaangaza miezi ya Sumbula na huenda ikaonekana kutoka kwenye Dunia kupitia darubini.

Jeuri Dhidi ya Wanawake

Uchunguzi mmoja wa hivi majuzi wafunua kwamba asilimia 51 ya wanawake Wakanada wenye umri wa miaka 16 au zaidi wametendwa jeuri na wanaume angalau mara moja katika maisha yao ya utu mzima, kulingana na The Globe and Mail. Hiyo yajumlika kuwa zaidi ya wanawake milioni tano. Gazeti hili la Kanada liliripoti kwamba karibu nusu ya wanawake waliohojiwa walisema washambulizi walitoka kati ya “marafiki-wavulana, waume, marafiki, washiriki wa familia au wanaume wengine wenye kufahamiana nao.” Asilimia kumi ya wanawake waliohojiwa walitendwa vibaya mwaka uliopita pekee, na karibu shambulio 1 kati ya 5 lilikuwa zito kutosha kusababisha jeraha la kimwili. Wanawake wengi waliripoti kusukumwa, kubambwa, kupigwa kikumbo, kupigwa kofi, kupigwa teke, kuumwa, au kuchapwa na waume zao au wanaume waliowaweka wawe wenzi wao wa kinyumba.

Maelfu ya Mimea Yapuuzwa

“Elfu kadhaa za namna za mimea zimetumiwa kuwa chakula cha kibinadamu katika historia, lakini sasa ni karibu 150 tu ambazo husitawishwa na ni namna tatu tu ambazo hugawa karibu asilimia 60 ya kalori na protini zitolewazo katika mimea,” lasema Shirika la Kilimo na Chakula la UM. Uchunguzi mbalimbali wa ukulima wa kimataifa wathibitisha jambo hili. Wanadamu hushikamana na vyakula vyao vikubwa walivyovizoea—mpunga (mchele), mahindi, na ngano—huku wakipuuza maelfu ya mimea mingine ya ulishaji ipatikanayo katika asili.

Uwezo Mdogo Juu ya Maisha Zao Wenyewe

Kujapokuwa na mabadiliko ya hivi majuzi yenye kupendelea tawala za kidemokrasi, asilimia 90 ya idadi ya watu wa ulimwengu leo hawana mamlaka ya kujichagulia mambo yatakayofanyiza hali za maisha zao. Hilo ni shauri lililokatwa na Human Development Report 1993, lililotolewa na Shirika la Maendeleo la UM (UNDP). Aliyekuwa msimamizi wa UNDP, William Draper, alisema katika dibaji moja ya ripoti hiyo kwamba kwa watu walio wengi maisha bado hufanyizwa na “jitihada ngumu [zinazoendelea] za kutafuta kufikia yale mahitaji ya kawaida ya maisha—ardhi, maji, kazi, nafasi ya kuishi na huduma za kijamii.” Ripoti hiyo yasema kwamba “mara nyingi makabila ya walio wachache, maskini, wakaaji wa mashambani, wanawake, na wasiojiweza mara nyingi hawana uwezo wa kubadili maisha zao.”

Tasbihi ya Video ya Kuweka Mfukoni

Padri mmoja Mkatoliki wa Italia amejipatia umiliki wa haki za kutumia Tasbihi ya video ya elektroni iliyo na muziki na sanamu za kidini. Kulingana na gazeti la kila siku Il Resto del Carlino la Bologna, kifaa hicho, ambacho hutumia nguvu za betri, ni “sahili na chenye kuchukulika kwa urahisi.” Kwa wale watakao kurudiarudia sala huku wakiendesha gari, kuna “adapta maalumu pia iwezayo kuunganishwa ndani ya kile kiunganisho cha gari cha kuwashia sigareti.” Mwamini aweza kuchagua sehemu ya Tasbihi atakayo kurudiarudia. Kwa kielelezo, kibonyezo cha “Ave Maria” huwezesha mtumizi aendelee hatua kwa hatua katika zile sehemu mbalimbali za sala, na maneno yayo huonyeshwa katika kiwambo. “Mtu akichoka kabla ya kumaliza sala zote,” lasema Il Resto del Carlino, aweza kufunga kifaa hicho na, kwa msaada wa kumbukumbu la elektroni, “aendelee kutoka mahali alipoachia kifunguliwapo tena.”

Mahali Baridi Zaidi Katika Ulimwengu Wote Mzima

Halijoto yenye baridi zaidi katika ulimwengu wote mzima ilipimwa hivi majuzi kuwa 0.000,000,000,28 kulingana na kipimo cha Kelvin. Halijoto hii ya chini kabisa ni kisehemu kidogo sana cha digrii moja juu ya sifuri halisi. Halijoto hii yenye baridi sana ilionwa wapi? Katika nchi ya Nordi ya Finland, kulingana na gazeti New Scandinavian Technology. Hata hivyo, watu walio wengi katika Finland hawakuwa na habari juu ya tukio hili, kwa sababu halijoto hiyo ya chini ilifikiwa kwa majaribio yasiyo ya asili katika Maabara ya Fizikia ya Halijoto ya Chini katika Chuo Kikuu cha Ufundi cha Helsinki. Wanasayansi hawajaweza kamwe kufikia sifuri halisi, ambayo yaelezwa katika New Scandinavian Technology kuwa “halijoto iliyo alama ya kutokuwapo utendaji wowote wa joto ndani ya atomi.”

Thamani ya Kuangalia Nje Dirishani

Kulingana na uchunguzi mmoja uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Michigan, Marekani, waajiriwa wawezao kuangalia nje dirishani hufanya kazi vizuri zaidi. Tofauti na imani ya wengi, kuwa mahali pa kuweza kuangalia nje si lazima kuendeleze kuota ndoto za mchana. Gazeti Business Week laripoti kwamba uchunguzi uliofanywa kwa watu 1,200 ulifunua kwamba “wafanyakazi wenye kuweza kuangalia ulimwengu wa nje wana idili nyingi zaidi kwa kazi zao, hawavurugiki sana, wana saburi zaidi, uwezo mzuri zaidi wa kukazia mambo fikira, na maradhi machache zaidi ya kimwili.” Tofauti na hivyo, wafanyakazi walio katika vijumba visivyo na madirisha wataelekea kuwa “wasiowaza sana na wenye kuudhika zaidi” nao hutatizika zaidi kukaza fikira kwenye jambo moja.

Vibaramwezi vya Kuongeza Akili

“Mauzo ya vibaramwezi [vichezeo] vya kuelimisha yanaongezeka sana huku wazazi wakinunua vitu vya mchezo tu kwa ajili ya mashindano ya wakati ujao,” lasema The Globe and Mail, gazeti la Kanada. Ripoti hiyo yaongeza kwamba wazazi fulani hata wanazuia watoto wao wasicheze na vibaramwezi ambavyo “huchezewa mradi vichezewe tu. Badala ya hivyo, wao wataka kila dakika ya mchezo ijawe na uwezekano wa kufundisha mambo ya ustadi.” Ingawa wengi waamini kwamba elekeo hili laweza kufanyiza watoto wenye akili ya juu zaidi na stadi zilizo nzuri zaidi, wataalamu fulani hawakubaliani na hilo. Wao wahisi kwamba kunyima watoto wakati wenye thamani wa kucheza bila kupangiwa mambo hususa kutakandamiza uwezo wao wa kubuni mambo “na kwamba hatimaye watajifunza mambo machache zaidi,” lasema gazeti hilo.

Uharamia wa Baharini Waongezeka

Shirika la Ubaharia wa Kimataifa lenye makao London, ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na uharamia wa baharini na wizi wa meli kwa kutumia silaha, laripoti kwamba uharamia wa baharini ‘umeongezeka sana katika miaka ya majuzi kwa idadi na pia kwa ukatili ambao mabaharia hutendwa.” Ingawa vilivyo vingi vya visa 400 vya uharamia ulioripotiwa vilitendeka katika Mlangobahari wa Malacca wa Kusini-Mashariki mwa Asia, maharamia wa baharini wanaoteaotea wakiambaa kwenye pwani ya magharibi ya Afrika na pwani ya kaskazini-mashariki ya Amerika Kusini. Uharamia wa baharini, laandika gazeti UN Chronicle, “watisha kuwa tatizo la ulimwenguni pote.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki