Je! Ufuatilie Masomo Zaidi au La?
NI ELIMU kiasi gani inayohitajiwa ili mtu apate riziki? Jibu latofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine. Yaonekana kwamba katika nchi nyingi kiwango cha masomo kinachohitajika ili ujitegemeze ni cha juu kuliko ilivyokuwa miaka michache iliyopita. Katika hali nyinginezo elimu ya chini inayokubaliwa na sheria haitoshi mtu kujiruzuku.
Hiyo ndiyo sababu inayofanya idadi inayoongezeka ya wahitimu warudi shuleni badala ya kwenda kazini. Kwa kweli, thawabu huonekana kuwa yenye kuvutia. The New York Times lataja ripoti ya Taasisi ya Sera ya Uchumi kwamba “wafanyakazi waliopata diploma za shule za sekondari walipata upungufu wa thamani ya mishahara yao kwa asilimia 7.4 kuanzia 1979 hadi 1987, huku mishahara ya wahitimu wanaume wa vyuo ikipanda kwa asilimia 7.”
Wahitimu wa chuo hupata digrii zinazowawezesha kupata kazi. William B. Johnston, mtafiti wa ngazi ya juu kwenye Taasisi ya Hudson, asema: “Digrii ya chuo, au hata uthibitisho wa kuwa mmoja alipitia chuo, imekuwa njia muhimu zaidi ya kupata kazi nchini.”
Kwa upande mwingine, ni lazima ikiriwe kwamba wahitimu wengi wa vyuo hutoa jasho ili kupata kazi, na si kwamba hawawezi kusimamishwa kazi. “Wengi wa marafiki wangu waliohitimu pamoja nami hawana kazi,” asema Karl mwenye miaka 22. Jim, mwenye miaka 55, alihitimu kwa kupata shahada ya mwanafunzi bora kutoka kwenye chuo kikuu fulani kilicho mashuhuri lakini alisimamishwa kazi mnamo Februari 1992. Diploma yake haikumsaidia asisimamishwe wala haikumsaidia apate kazi yenye kutegemeka. “Msingi wako wageuka kuwa dhaifu na usiotegemeka,” yeye asema.
Kama Jim, wahitimu wengi wa vyuo wamejikuta katika hali ambayo U.S.News & World Report laita “pargatori ya kazi za ofisi”—wachanga mno kuweza kustaafu, wenye umri mkubwa mno wasiweze kuajiriwa na kampuni nyingine.
Kwa hiyo, ingawa elimu ya chuo inaweza kuwa na faida, kwa wazi hiyo si suluhisho la matatizo yote. Wala hiyo si jambo pekee la kufuatwa. Herbert Kohl aandika katika The Question Is College: “Kuna watu wengi wenye mafanikio ambao hawakuenda vyuo na kuna kazi nyingi nzuri zisizohitaji digrii za vyuo.” Kwa kielelezo, shirika moja huajiri watu ambao hawakwenda vyuo kwa kazi ambazo mara nyingi hufanywa na wahitimu wa vyuo. Badala ya kutafuta wenye digrii, kampuni hiyo hutafuta waomba-kazi wanaoonyesha wana uwezo wa kufanikiwa. “Tupatapo tu mtu huyo,” asema msemaji, “twachukua kwamba twaweza ku[m]fundisha stadi fulani hususa za kazi.”
Naam, wengi wamejiruzuku vizuri na familia zao bila kuwa na digrii ya chuo. Wengine wao walichukua mitaala katika shule za kiufundi, au vyuo vya kijumuiya, kwa gharama ndogo sana kwa wakati na fedha.a Wengine wameanzisha biashara au utumishi bila aina yoyote ya mazoezi ya kipekee. Wakidumisha sifa ya kuwa watu wenye kutegemeka, wamefaulu kudumisha kazi zenye kutegemeka.
Maoni Yenye Usawaziko
Bila shaka, hakuna aina ya masomo—kutia ndani ya chuo au elimu yoyote ya ziada—inayohakikisha kwamba utafanikiwa. Na zaidi, Biblia yataja kwa usahihi kwamba “mandhari ya ulimwengu huu inabadilika.” (1 Wakorintho 7:31, New World Translation) Jambo linalohitajika sana leo huenda lisifae kesho.
Hivyo, mtu anayefikiria kufuatia elimu ya ziada atafanya vizuri kuchanganua kwa uangalifu faida zayo na hasara zayo. ‘Je! naweza kugharimia? Nitakuwa katika mazingira ya aina gani? Je! mitaala hiyo itanipa mazoezi yenye kutumika iwezayo kunisaidia kujitegemea? Je! itanisaidia kuandalia riziki kwa familia yangu hatimaye nikifunga ndoa?’ Wazazi wenye utegemezo mzuri waweza kuandaa shauri zuri kwa kupatana na daraka wanalopewa na Biblia. (Kumbukumbu la Torati 4:10; 6:4-9; 11:18-21; Mithali 4:1, 2) Kama unafikiria mafaa ya kifedha ya elimu ya ziada au jambo lolote jingine kulihusu, maneno ya Yesu yafaa: “Maana ni nani katika nyinyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kumalizia?”—Luka 14:28.
Kwa kweli, kufuatia elimu ya ziada ni uamuzi unaopaswa kufikiriwa kwa uzito. Nyakati zote Mkristo apaswa kuzingatia akilini maneno ya Yesu kwenye Mathayo 6:33: “Utafuteni kwanza ufalme wake, na haki [ya Baba yenu wa kimbingu] na hayo yote mtazidishiwa.” Miongoni mwa Wakristo wa kweli, wale wasiokuwa na elimu ya ziada hawadharauliwi au kutendewa kuwa watu wenye hali ya chini, wala wale wenye elimu ya ziada hawaondoshwi wala hawaonwi kuwa wenye kujichukulia sana. Mtume Paulo aliandika: “Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama na huanguka? Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha.”—Warumi 14:4.
Yesu alikuwa na maoni hayo yenye usawaziko. Hakuwadharau wale “wasio na elimu, wasio na maarifa,” wala hakukataa kumchagua Paulo aliyeelimika sana atimize kazi yenye nguvu ya kueneza evanjeli. (Matendo 4:13; 9:10-16) Kwa pande zote mbili ni lazima elimu isitukuzwe mno, kama itakavyoonyeshwa na makala ifuatayo.
[Maelezo ya Chini]
a Programu za elimu ya ziada hutofautiana mahali mahali. Shule, maktaba, na idara za kuajiri watu za serikali zaweza kukunufaisha katika kujua ni programu ipi inapatikana kwenu.
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Elimu ya Ziada
Mnara wa Mlinzi la Novemba 1, 1992, lilisema hivi kuhusu Mashahidi wa Yehova na huduma ya wakati wote: “Mwelekeo wa kawaida katika [nchi nyingi] ni kwamba kiwango cha kwenda shule kinachohitajiwa ili kuchuma mshahara wa kadiri sasa ni cha juu zaidi ya vile ilivyokuwa miaka michache iliyopita. . . . Ni vigumu kupata kazi zenye mishahara ya kadiri baada ya kukamilisha tu elimu ya chini zaidi inayotakwa na sheria . . .
“Ni nini kinachomaanishwa na ‘mishahara ya kadiri’? . . . Mishahara yao yaweza ikasemwa kuwa ‘kiasi kinachofaa,’ au ‘yenye kuridhisha,’ ikiwa kile wanachochuma chawaruhusu waishi maisha ya kadiri kikiwaachia wakati na nguvu za kutosha kuweza kutimiza huduma yao ya Kikristo.”
Kwa hiyo Mnara wa Mlinzi lilisema: “Kanuni [ngumu] hazipaswi kuwekwa ama kuunga mkono ama kupinga elimu ya ziada.”